UHAKIKI WA KITABU: “ In the belly of Dar-es-salaam”
1. Rekodi za Kibikiogarafia
Jina la
kitabu kinachohakikiwa hapa ni “In the belly of Dar-es-salaam” na kimetungwa
na Elieshi Lema. Mchapishaji wa kitabu
hiki ni E&D Vision Publishing na amekipa namba ifuatayo katika sekwensia ya
vitabu duniani (ISBN) 978-9987-521-74-6.Kimechapishwa mwaka 2011 kikiwa na
kurasa 185. Na anayekihakiki sasa hivi katika
safu hii ni mimi Padri Privatus
Karugendo.
II. Utangulizi
Hii ni hadithi ya kubuni .Mwandishi wa
hadithi hii Mama Elieshi Lema, ni mwandishi mahiri .Siku chache
zilizopita, nilifanya uhakiki wa vitabu vyake vya watoto. Vitabu vya Freshi na
Maisha, vinaonyesha ubunifu wa Mama huyu wa kufikisha ujumbe mzito kwa watoto.
Kitabu chake cha “Parched Earth”, ambacho nacho nilikifanyia uhakiki ni
ushuhuda mwingine wa kuonyesha kwamba mwandishi huyu ana mbinu si za kufikisha
ujumbe kwa watoto peke yao bali na kwa wakubwa pia!
Hadithi yake ya “ In the belly of Dar-es-salaam” akimaanisha “Ndani mwa
tumbo la Dar-es-Salaam” inachokoza mawazo, inamfanya mtu kutafakari na
kujiuliza maswali mengi juu ya maisha yake na juu ya uhusiano wake na jamii
inayomzunguka. Hii ni hadithi ya watoto
kama nyingine ambazo Mama Elishi amekuwa akiwaandikia watoto wa Kitanzania,
lakini mfumo wake wa uandishi unabaki ni ule wa kutumia hadithi za watoto
kufikishwa ujumbe mzito kwa watu wazima wanaosababisha “Tumbo la Dar-es-Salaam”
liwe na vitu vingi; vizuri na vibaya, matajiri na masikini, matabaka ya watu na
mengine mengi ya kulijaza tumbo likawa kubwa hadi kuvimbewa. Hadithi yenyewe
ina sura 15. Katika aya zifuatazo nitatoa muhtasari na tathmini yake, lakini
baada ya kudokeza mazingira yanayokizunguka kitabu hiki.
III. Mazingira yanayokizunguka kitabu
Kitabu hiki kimeandikwa kwa lugha ya
Kiingereza, kitu kinachoongeza mvuto wa kitabu na hadithi yenyewe. Ukweli ni
kwamba mpaka sasa hapa Tanzania tuna vitabu vichache vya hadithi za Kingereza
vilioandikwa na watanzania wenyewe. Inavutia kuona Mtanzania, anavyoweza
kuandika hadithi inayohusu maisha ya Kitanzania kwa Kingereza. Huu ni mchango
mkubwa katika kukuza na kuendeleza lugha hii ya kingeni ambayo ni lugha ya
kimataifa na inaongoza katika kijiji cha Utandawazi. Na wala huku si kupiga
vita Kiswahili, bali ni kuiendeleza lugha hii katika jamii ya Kitanzania
.Mwandishi wa riwaya hii ya Kingereza, ameandika riwaya nyingi kwa lugha ya
Kiswahili. Jambo la msingi ni kuzipatia nafasi lugha zote na hasa lugha kuu,
mfano lugha ya taifa na lugha za kimataifa kama kingereza Mfano, mimi nimeisoma
riwaya hii kwa Kingereza, lakini sasa ninafanya uhakiki wake kwa Kiswahili.
Hata mtu ambaye hafahamu Kingereza, kwa kusoma uhakiki huu, anaweza kupata
ujumbe wa riwaya hiyo – ingawa ingekuwa bora zaidi mtu kuisoma riwaya yenyewe
kwa lugha iliyoandikwa.
Kitabu hiki kimeandikwa chini ya Mradi wa vitabu vya watoto Tanzania (CBP).
Tangia mwaka 2008, Mradi huu wa vitabu vya watoto kwa kusaidiwa na “ The Burt
Award for African Literature” umekuwa ukisaidia waaandishi wanaoandika hadithi
za Kiingereza, kuandika na kuchapisha vitabu vyao. Lengo likiwa ni kukuza lugha
hii ya Kiingereza katika shule za msingi na sekondari. Kawaida waandishi
wanashindanishwa na kuibuka na washindi watatu. Tuzo inatolewa kwa washindi
watatu. Kwa vigezo vya majaji ambavyo hatuna ruhusa ya kuviingilia, hadidhi hii
ya “In the belly of Dar-es-Salaam” ilipata tuzo ya mshindi wa tatu.
Riwaya hii imesheheni yale yasiyofundishwa
popote, imesheheni yale ambayo kwa kawaida kila mtu anaachiwa kuongelea
apendavyo. Wale wanaofanikiwa kuongelea vizuri, wanafanikiwa kuvuka – wenye
bahati mbaya wanazama au wanaendelea kuogelea bila kufikia mwisho.
Bahati mbaya wale wanaoogelea hadi mwisho, hawako
tayari kuelezea uzoefu wao na kutoa mbinu walizozitumia kufanikiwa. Walio wengi
inakuwa ni kujaribu hili na kuacha lile, ni mchezo wa pata potea. Haitoshi
kumwambia mtoto asizini, haitoshi kuwazuia vijana kufanya mapenzi, bila
kuwapatia mwongozo na uzoefu wa kupambana na nafsi zao, bila mwongozo wa maisha ya kiroho ya kuweza kuweka kando mvuto
wa kimwili na kuangalia ndani ya nafsi ya mtu, heshima ya mtu, furaha ya mtu,
mema na mabaya ya mtu. Maana uzuri wa mtu si umbo lake, bali ni yale ya ndani
yanayomfanya kuwa mtu, ni matendo yake yanayomtofautisha na wanyama wengine.
Riwaya hii inafumua na kuelezea yale yote
yanayotendeka ndani ya Jiji kubwa la Dar-es-salaam. Matatizo ya watoto wa
mitaani, maisha magumu ya watu wa kipato cha chini. Umoja na mshikamano wa
watoto wanaoishi ndani ya Jiji la Dar-es-salaamKijana. Riwaya hii pia
inaonyesha wazi umuhimu wa sokoo Kuu la Kariakoo, ambalo mwandishi analiita
“Mama”.Ni soko la uhai, vijana wanaendesha maisha yao kwa kufanya biashara
kwenye soko ili na wengine soko hili ni nyumba ya kulala na sehemu ya kuleta
matumaini katika maisha yao.
Mwandishi anaonyesha wazi kwamba watoto wa mitaani
wanaofanikiwa kupata kipato kidogo wanapanga vyumba maeneo ya karibu na
Kariakoo, kama vile Kigogo na Bonde la Msimbazi. Bahati mbaya au nzuri riwaya
iliandikwa kabla ya mfuliko ya mwaka jana. Vinginevyo angeonyesha kwenye riwaya
yake jinsi ilivyo dhamb ya mauti
kuwahamisha watu kutoka bonde la Msimbazi na kuwapeleka mbali na “Mama” yao.
Soko kuu la Kariakoo. Hawa walitegemea kuendesha maisha yao kutegemea Soko kuu
la Kariakoo kama tunavyoelezwa maisha ya Sara na wenzeka kwenye riwaya hii,
sasa kule Mabwepande wataweza kumpata “Mama” mwingine? Wataweza kusafiri kila
siku kuja Kariakoo na kurudi Mabwepande?
Riwaya ya “In the Belly of Dar-es-salaam” inaelezea matatizo ya siku kwa
siku yanayowakuta vijana wetu. Kwa
upande mwingine inavunja tabia ya kuyafunika matatizo na kujenga utamaduni wa
unafiki. Baada ya maelezo haya sasa tuone kitabu chenyewe kwa muhtasari.
IV. Muhtasari wa Kitabu.
Riwaya hii ya “In the
Belly of Dar-es-salaam” ni kama mwendelezo wa Riwaya nyingine ya Mwandishi Elieshi,
ya Safari ya Prospa. Hivyo ili mtu aifaidi vizuri riwaya hii ni bora kuanza
kusoma kitabu cha Safari ya Prospa, ndipo apate mtiririko wote. Katika riwaya
ya Safari ya Pospa, kijana Prospa anajitosa kwenye ulimwengu wa ujasusi na
kuamua kwenda Dar-es-Salaam, kumtafuta Merisho, mpwa wake aliyetoweka nyumbani
kwa mazingira ya kutatanisha.
Katika safari ya Prospa
ya kutoka Moshi kwenda Dar, njiani anakutana na Sara. Wanaambatana hadi
Dar-es-Salaam, Zanzibar. Prospar, anaamua kurudi nyumbani, lakini Sara anaamua
kubaki Dar-es-Salaam ili “kutafuta maisha”. Riwaya hii ya “In the Belly of
Dar-es-salaam, inahusu maisha ya mtaani ya Sara na wenzake akina Mansa kutoka
Kibaha, Ali kutoka Lushoto na Kaleb kutoka Mtwara. Wote hawa wanakutana kwenye
mitaa ya Dar-es-Salaam, wakiwa wanakimbia umasikini wa vijijini. Wakiwa ndani
ya jiji, wanakutana na maisha magumu na kutisha, wanalala wengi kwenye chumba
kimoja, wanatembea juani na wakati mwingine kulala barazani. Wakati vijana hawa
wakipata taabu na mateso, maisha ya
anasa na starehe yanaendelea ndani ya jiji la Dar-es-Salaam. Swali kuba
linabaki juu ya mgawanyo wa rasilimali za taifa letu. Kwa nini wengine waishi
maisha ya peponi wakati wengine wanaishi maisha sawa na ya jehanamu?
Mwandishi anatumia
riwaya hii kuelezea yale yanayotendeka ndani ya jiji la Dar-es-Salaam; watu
kuishi kwenye makundi ya kikabila,
Wamakonde wana kikundi chao na biashara zao, Waha wana kikundi chao na biashara
zao, wasambaa wana vikundi vyao na biashara zao (uk 47). Hata watoto wa mitaani,
wanaokimbia vijijini kuja Dar-es-Salaam kutafuta maisha, wanajikuta kwenye
makundi haya ya kikabila.
Mwandisi anatumia riwaya
kutuchorea vizuri maisha ya watoto wa mitaani; maisha magumu, kulala kwenye
baraza, kulala kwenye muziki, kupigana na kulindana na wakati mwingine kujenga
mshikamano mkubwa. Kinachojitokeza hapa ni kwamba watoto wa mitaani ndani ya
jiji la Dar-es-Salaam ni jamii ya aina yake ni jamii ambayo inaacha maswali
magumu juu ya umakini wa serikali kushughulika na huduma za kijamii na kuwajali
watoto.
Mwandishi anaonyesha
jinsi wasichana wanavyojiingiza kwenye biashara ya kujiuza na wakati mwingine
kufanya kazi za kudhalilishwa. Baadhi ya wasichana waliojiuza walifanya hivyo ili waweze kupata fedha ya kuwatumia mama
zao na bibi zao waliobaki vijiji wakiwalelea watoto wao. Wengi wao wanafanya
kazi hii ya kujiuza bila kikomo hadi pale wanapoanza kuugua na kupelekwa
nyumbani kwao vijijini ili wafe kwa
amani (Uk 84).
Mwandishi anaonyesha
umahiri wake wa uandishi pale anapoibatiza “Kariakoo” jina la mama. Kwamba
Kariakoo, ndo uhai wa watu wenye kipato cha chini ndani ya jiji la
Dar-es-Salaam. Kwamba Kariakoo ni mama wa wanyonge. Hapa anamwaga sifa za mama
ambazo wengi wetu tunazijua: huruma,
kuvumilia na kujali. Kariakoo inamjali kila mtu: Ni kituo cha biashara ambacho
kila mtu anapata riziki yake. Kariakoo inamkumbatia na kumlinda kila mtu, hata
Wachina wanatoka kule kwao na kuja kutafuta maisha ndani ya Kariakoo; wanauza
maua na mambo mengine mengi ambayo hata watanzania wangeweza kuuza. Lakini mama
Kariakoo anawalinda na kuwatunza (uk 145 – 149).
Kama kawaida ya
mwandishi, ya kutoegemea mabaya peke yake , bado anaamini pamoja na ubaya ulio
ndani ya tumbo la Dar-es-Salaam, bado kuna watu wazuri wenye kujali, wenye roho
kama ya Mama Kariakoo. Mpenzi wa Sara, ambaye ni baba mwenye familia,
anaonekana kuwa tofauti. Anampenda Sara, si kwa kumtumia tu bali anampatia hata
mtaji wa kuanzisha biashara. Ni bahati mbaya kwamba riwaya hii inakwisha wakati
ndo imeanza; wasomaji wangependa kujua kilichotokea baada ya upasuaji
anaofanyiwa Sara, ili kurekebisha macho yake. Huyu mpenzi wa Sara, anajitolea
kulipa gharama za matibabu bila masharti yoyote yale. Kumbe dunia hii, na
Tanzania yetu ina watu wema na wabaya! Wasomaji wangependa kujua uhusiano huu
wa Sara na mshikaji wake unaishia wapi? Je Sara, atamkubali Mansa, kijana
wanaoishi na kuendesha maisha magumu? Au ataendelea na uhusiano na mshikaji
ambaye alimpatia mtaji na kumtibisha, lakini ana mke mwingine.
Mwandishi Elieshi,
amebobea kwenye ushauri wa mahusiano. Vitabu vyake vyote anajaribu kuwafundisha
vijana juu ya mahusiano ya mtu na mtu, na hasa mahusiano ya mwanamke na
mwanamume. Tunamsikia Rose, kwenye riwaya hii akisema: “ Mwanaume ninayeishi
naye ni mwema kwangu. Ila nina mashaka kama kuna penzi kati yetu. Yeye
alihitaji mwanamke na mimi nilihitaji rafiki.....Sina uhakika wa kitakachotokea
endapo nitatumbukia kwenye penzi na mwanaume mwingine” (tafsiri ni yangu). (Uk
166).
Maana yake ni nini?
Kwamba kuna watu wanaoingia kwenye mahusiano kwa kusukumwa na mazingira fulani;
upweke, umasikini au makazi. Mazingira yakibadilika, au mtu akakutana mtu
anayemvutia na kuwa na penzi zito, basi mahusiano ya mwanzo yanapotea! Haya
yanatokea mitaani miongoni mwa watoto wanaoishi maisha hatarishi mitaani, lakini
yanatokea kwenye jamii yetu ndani ya tumbo la Dar-es-Salaam. Ni wito wa
mwandishi kwetu sote kuwa na utamaduni wa kujenga upendo imara kwenye familia
zetu.
V. Tathmini ya Kitabu.
Baada ya kuona muhtasari
huu sasa tufanye tathmini ya kazi hii
aliyoifanya Mama Elieshi Lema. Awali ya yote lazima niseme kwamba , kwa
kuangalia hadhira anayoikusudia, kitabu hiki kinasisimua sana na kutoa
mafundisho katika jamii yetu na hasa kuhusu uhusiano wa mtu na mtu na maisha ya
watoto wanaoishi maisha magumu ndani ya jiji la Dar-es-Salaam.
Changamoto anayoitoa
Mama Elieshi Lema, katika riwaya hii ni swali la kawaida: Kwa nini tunaendelea
kuwa na watoto wa mitaani? Hali hii itakwisha lini? Je serikali inaona ukweli
huu wa watoto wa mitaani? Kama anavyosema Kaleb kwenye riwaya kwamba Mawaziri
wanaishi kwenye ulimwengu wao na wako juu sawa na ndege inayopaa angani na
wakati mwingine inakuwa vigumu kuwaona kwa macho ya kawaida (uk 54)
Lengo la riwaya hii
kufuatana na matakwa ya Mradi wa vitabu vya watoto, ni kuwasaidia vijana wa
shule za msingi na sekondari kusoma riwaya za Kiingereza na kwa njia hii
kujifunza kingereza. Tofauti na waandishi wengine walioshiriki zoezi hili ka
kuandika riwaya za watoto kwa lugha ya kingereza , Elieshi, hakuandika riwaya
ya kufikirika, amejikita kwa mambo yanayotokea kwenye jamii. Hivyo riwaya yake
inafanya kazi mbili kwa wakati mmoja. Inawasaidia watoto kujifunza lugha ya
Kiingereza, lakini pia inawasaidia watoto kujifunza mambo yanayotokea katika
jamii yetu na hasa yale yanayowahusu watoto wenyewe kama vile maisha ya watoto
wanaoishi maisha hatarishi. Maisha ya kuishi mitaani, maisha ya kuishi maisha
mgumu ya kupanga chumba kimoja watu wengi, ni hali inayoweza kumtokea kila
kijana hapa Tanzania. Hivyo kuyasoma kwenye riwaya, hata kama ni ya kubuni,
inasaidia, maana mwandishi anatwambia alifanya utafiti kwenye maeneo ya Kigogo
na sehemu nyingine ambazo watoto wanaishi kwenye mazingira hatarishi; ni muhimu
kuisoma riwaya hii.
Mama Elieshi Lema, ameonyesha mfano mzuri wa
kutuandikia riwaya ya “In the belly of Dar-es-salaam”. Ni bora kila mzazi
angemnunulia mtoto wake kitabu hiki. Kama wazazi hawana nafasi ya kuongea na watoto wao, riwaya hii
itaongea badala yao. Si lengo langu kukipigia debe kitabu hiki, bali ni
kuupigia debe ujumbe mzito ulio katika riwaya hii iliyotukuka.
VI. Hitimisho
Kwa kuhitimisha basi, kwa upande mmoja, nawashauri
watanzania kukisoma kitabu hiki ili waweze kujionea wenyewe uhondo uliomo
ndani. Lakini kwa upande mwingine namwomba mwandishi wa kitabu hiki kufanya
jambo moja la ziada, nalo ni kushirikiana na waandishi na wachapishaji wa
vitabu na watu wengine wanaojali umuhimu wa vitabu katika jamii, kubuni mbinu
za kuwashawishi watanzania kujenga utamaduni wa kujisomea. Bila mbinu hizi,
uandishi wa vitabu na ujumbe wake utakuwa sawa na kupigia ngoma kwenye maji!
Na,
Padri Privatus Karugendo.
0 comments:
Post a Comment