MWANA MAMA PROFESA
ANNA KAJUMULO TIBAIJUKA.
Leo katika safu yetu ya Mwana Mama, tunawaletea Mheshimiwa Profesa Anna Kajumulo Tibaijuka. Lengo la
safu hii ni kuandika habari za mwana mama ambaye ametoa mchango mkubwa katika
taifa letu lakini habari zake hazijulikani. Ni kutokana na mfumo dume ambao
daima unatoa nafasi kwa wanaume kuliko wanawake ndiyo maana historia yetu
inaandikwa kana kwamba wanaume peke yao ndo wameishi na kuiendesha historia
hiyo.
Ni wazi habari juu ya Profesa Anna Kajumulo Tibaijuka, zimeandikwa sana.
Hivyo huyu si mlengwa wa safu hii! Hata hivyo na mimi siandiki juu ya Anna
Tibaijuka Profesa wa uchumi wa Cho Kikuu cha Dar-es-Salaam, najua mengi
yameandikwa juu yake. Pia siandiki juu ya Anna Tibaijuka, aliyefanya kazi Umoja
wa mataifa, ni wazi mengi yameandikwa juu yake na wala hakuna tena haja ya
kuandika zaidi. Siwezi kusema ninaandika juu ya Anna Tibaijuka Mbunge, mjumbe
wa NEC wa CCM, au waziri wa Ardhi Nyumba na makazi; kwa nafasi aliyo nayo sasa
hivi habari zake zinaandikwa kila gazeti
na mitandao mbali mbali.
Katika safu hii ya Mwana Mama, naandika juu ya Profesa Anna Kajumulo
Tibaijuka, mwanzilishi wa BAWATA. Ni wazi kwa vile shirika hili lilifutwa na
serikali, ilikuwa vigumu kuandika juu yake, lakini ukweli unabaki kwamba
mchango wa muda mfupi wa shirika hili hautafutika. Shirika hili lililojulikana kama Baraza la
Wanawake Tanzania, lilianzishwa kwenye miaka ya tisini likiwa na lengo la
kuwaunganisha wanawake wa Tanzania; kuwakomboa wanawake kutokana na mfumo dume uliojikita
katika jamii yetu; kuwawezesha wanawake kielimu na kiuchumi. Shirika hili
lililenga kuwaunganisha wanawake bila kuangalia itikadi zao za vyama vya siasa,
dini zao na makabila yao. Mwenyekiti wa kwanza wa shirika hili alikuwa Profesa
Anna Kajumulo Tibaijuka; mwanamke shupavu anayejisimamia na si mwepesi wa kuyumbishwa.
Kwa muda mfupi BAWATA, ilisambaa kama kimbunga na kuenea Tanzania nzima.
Akiwa mchumi wa masuala ya kilimo, Mama Anna Tibaijuka, alishafanya utafiti
na kugundua matatizo yanayokwaza maendeleo ya wanawake wa Tanzania. Akagundua
kwamba mgawanyiko uliopo kwenye makundi ya wanawake unadhoofisha nguvu zao na
jitihada zao za kuleta maendeleo. Akajipanga kuinua maisha ya wanawake hawa
kupitia umoja wao ndani ya shirika la BAWATA. Kama shirika hili lingeendelea
leo hii tusingekuwa tunaongelea viti maalumu; wanawake wangekuwa wanapambana
sambamba na wanaume kuingia Bungeni.
BAWATA, ilieleweka haraka kwa wanawake wa kawaida vijijini na kwa wanawake waliopenda umoja. Wakati
kulikuwa na vyama vya wanawake vya siasa, dini na makundi ya wasomi, BAWATA
ililenga kuwaunganisha wanawake wote; na dalili za ukombozi zilianza kuonekana,
maana Waswahili wanasema “ Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu”. Umoja wa
wanawake waliopigania Uhuru wa taifa letu, ulikuwa bado kwenye kumbukumbu za
wengi, na hasa viongozi (Wanaume) waliokuwa madarakani, walijua vizuri nguvu za
umoja wa wanawake. Baada ya uhuru umoja huu wa wanawake ulisambaratishwa kwa
kuwatenga wanawake kwa kuunda vikundi mbali mbali.
BAWATA, ilionyesha nia ya kufufua umoja na nguvu ya wanawake. Kwa wanaume
wasiojiamini, waliona tishio la BAWATA. Bahati mbaya au nzuri, BAWATA iliibuka
wakati wa vyama vingi vya siasa na kuelekea uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi
wa 1995. Wenye uchu wa madaraka na hasa wanaume wanaofikiri walizaliwa
kuitawala Tanzania, waliogopa umoja huu wa wanawake. Wangependa kuwaona
wanawake wametengana kuliko kuungana. Woga ukatanda nchi nzima kwamba BAWATA,
itajiingiza kwenye siasa na labda kuunga mkono vyama vya upinzani. Hivyo
Serikali ikahakikisha shirika hilo linafutwa!
Profesa Anna Kajumulo Tibaijuka, ninayemwandika katika safu hii ya Mwana
Mama, alisimama imara kuitetea BAWATA yake. Hakukubali kuonewa, hakukubali kuyumbishwa
na hakukubali vitisho. Alitetea hoja ya kuanzishwa BAWATA na taifa zima
lilimuelewa. Hata hivyo 1994, serikali iliamua kuifuta BAWATA. Profesa Anna
Kajumulo Tibaijuka na wenzake wakakimbilia mahakamani kutetea haki yao huko.
Kesi ilichukua muda mrefu, baada ya miaka 12, BAWATA iliibwaga Serikali mahakamani.
Watu wote wanaopenda haki katika taifa letu, walimpongeza Profesa Isa Shivji,
kwa kupambana hadi kufanikisha haki ya BAWATA kupatikana. Hata hivyo malengo ya
wenye uchu wa madaraka yalishafanikiwa na wanawake wakatengwa vikundi vikundi
kiasi ni vigumu kuwaunganisha tena.
Sina uhakika, baada ya kushinda kesi BAWATA, iliendelea na shughuli zake na wala hili si lengo la makala hii kwa
leo. Hoja yangu ya leo, ni Mwana Mama aliyeanzisha shirika la kuwaunganisha
wanawake wa Tanzania, akashirikiana na wenzake kuliunda na kulisimika,
likasambaa nchi nzima, lakini serikali ikaliogopa na kulifuta. Mwana Mama huyo,
akapambana mahakamani na kushinda kesi. Hoja yangu ni kuandika juu ya Mwana
Mama shupavu, mwana mama anayejisimamia, mwana mama asiyeyumbishwa, mwana mama
mwenye mtizamo wa umoja na uzalendo, Mwana Mama Profesa Anna Kajumulo
Tibaijuka.
Baada ya kufutwa BAWATA na baadaye kidogo kifo cha mme wake, kilichomgusa
kwa kiasi kikubwa na kuiumiza familia yake wengi walifikiri huo ungekuwa mwisho
wa mwanamke huyu machachari, lakini Mwana Mama huyu alipaa hadi anga za
kimataifa, hadi kuingia kwenye siasa za hapa nchini na kufanya kazi ndani ya
mfumo wa serikali iliyofuta shirika lake la BAWATA! Ni namna gani anaweza
kufanya kazi ndani ya mfumo huo ni swali la kujiuliza!
Hivyo twaweza kusema kuna sura mbili za Profesa Anna Kajumulo Tibaijuka?
Sura ya kwanza ikiwakilisha mwana mama msomi, mpambanaji, shupavu,
asiyeyumbishwa na mtetezi wa wanyonge na sura ya pili ikimwakilisha Profesa
Anna Kajumulo Tibaijuka, mwana mama wa kimataifa, mwanasiasa , mbunge na
waziri?
Nilipokutana naye mwezi wa tatu mwaka huu, alizikataa sura mbili za
Anna Tibaijuka. Binafsi nilisifia sura
ya Anna Tibaijuka wa BAWATA. Kwa
mshangao aliniuliza “ Unafikiri sasa
hivi mimi ni dhaifu?” aliendelea: “ Mimi ni Yule Yule wa BAWATA, ni Yule Yule asiyeyumbishwa,
ni Yule Yule mtetezi wa wanyonge, mpambanaji na mzalendo.. tofauti ni muda na
nyakati tofauti na matatizo tofauti, lakini mtu bado ni Yule Yule na msimamo ni
ule ule wa haki na wajibu..”.
Nikashuhudia maneno yake wakati wa Kigoda cha tano cha Mwalimu Nyerere.
Wakati viongozi wa serikali walisusia tamasha hilo linalofanyika kila mwaka, kwa kisingizio kwamba Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam
kina tabia mbaya ya kuwazomea viongozi wa serikali, Profesa Anna Kajumulo
Tibaijuka , alikuwa kiongozi pekee wa serikali aliyehudhuria na kusimama
jukwaani kutoa hoja zake kwa kujiamini. Mada yenyewe ilikuwa nyeti: Juu ya
kilimo na suala zima la umiliki ardhi katika nchi za Afrika. Ingawa idadi kubwa
ya wachangiaji walikuwa na msimamo wa kilimo cha wakulima wadogo wadogo na
Profesa Anna Tibaijula, alilijua hilo, bado alisimama kidete kutetea sera za
serikali za kuendeleza kilimo kwa kutumia makampuni makubwa ya uwekezaji. Hakukwepa kuelezea mpango mzima wa kutoa
ardhi kwa wawekezaji. Bila kupinga moja kwa moja kilimo cha wakulima wadogo
wadogo, alijenga hoja kwamba sasa hivi watanzania wanakimbilia mijini na
kufikia 2025, Jiji la Dar-es-Salaam litakuwa na watu zaidi ya milioni 10, na
itakuwa hivyo kwenye miji mingine. Bila kuangalia mbali na kuendelea na kilimo
cha wakulima wadogo wadogo tutakwama mbeleni. Hakuna aliyemzomea, alishangiliwa
hadi anamaliza hotuba yake.
Tumeshuhudia pia bungeni, wakati Mawaziri wanafanya mbinu za kuchomoa hoja
binafsi za wabunge wa upinzani na kuhakikisha hazijadiliwi bungeni, Profesa
Anna Kajumulo Tibaijuka anapambana na hoja hizo. Si mtu anayeogopa hoja na
mawazo tofauti. Pia jitihada zake za kuhakikisha haki inatendeka katika
umilikaji wa ardhi ndani ya taifa letu ni ushuhuda wa kutosha kwamba Profesa
Anna Tibaijuka wa BAWATA bado ni Yule
Yule. Na bila kumung’unya maneno, huyu ana sifa zote za kuandikwa kwenye safu
yetu ya Mwana Mama.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
+255 754 633122
1 comments:
Tunashukuru sana father kwa kutuandikia juu ya watu muhimu sana wenye mchango mkubwa sana kwenye taifa letu na hasa wa mama,kiukweli huyu mama ana mchango mkubwa sana kwenye taifa letu na anasifa zote nzuri kwa nchi hii hasa katika kipindi hiki ambacho watu wengi wamepoteza imani kwa viongozi wao,mama huyu ni mchapakazi,anayesimamia haki na sheria,hasiye yumbishwa na tamaa na ni mtetezi wa wanyonge,jasiri na msema kweli,mama huyu ni mffano kwa viongozi wengi hapa nchini,naomba viongozi waige mfano wake,pia watanzania naomba sana tuthamini michango yao na kiukweli tuwape nguvu watu muhimu na wanao onyesha juhudi za kweli za ukombozi wa taifa letu,tuache ushabiki usio kuwa na maana,wale wanao stahili pongezi na support yetu kama mama huyu tuwape nguvu ili waweze kulifikisha taifa hili mbali sana.
Post a Comment