UHAKIKI WA KITABU: HAINI
1.
Rekodi za Kibibliografia.
Jina la kitabu
kinachohahikiwa hapa ni HAINI, Kimeandikwa na Adam Shafi. Mchapishaji wa kitabu
hiki ni Sasa Sema Publications Chapa ya Longhorn Publishers na amekipatia namba ifuatayo katika
sekwensia ya vitabu duniani (ISBN): 978 9966 49 766 8. Kitabu kina kurasa 272 .
Na anayekihakiki sasa hivi katika safu hii ni mimi Padri Privatus Karugendo.
II. Utangulizi
Haini ni riwaya ya
kubuni inayochukua tukio la kihistoria la kuuawa kwa kiongozi mmoja wa Kiafrika
mwaka 1972. Baada ya mauaji Hamza, kijana mwandishi wa habari, anakamatwa kwa
kutuhumiwa kuwa haini, hasa kutokana na uhusiano wake wa karibu na Hamduni,
ambaye amempiga risasi na kumwua Kigogo huyo, kiongozi wa nchi. Sehemu kubwa ya
riwaya hii inasimuliwa gerezani ambako Hamza pamoja na wengine waliosombwa na
kurundikwa huko gerezani wanateswa, kuthakilishwa na kutendewa unyama wa kila
namna.
Pamoja na tukio hili la
Uhaini, riwaya hii inachunguza matatizo ya kisiasa, kijamii na kiuchumi ya nchi
za Kiafrika baada ya uhuru chini ya
mifumo ya utawala inayojali tu maslahi ya wachache. Ni riwaya inayogusa hisia
na kuchochea hasira na uchungu rohoni, hata hivyo ina ucheshi na viliwazo,
mfano mwandishi anapoandika hivi: “ Alinyanyuliwa akatupwa nje na baada ya
kutua juu ya ile sakafu tu wakammwagia ndoo nzima ya maji kumfufua arudi tena
duniani. Walipomwona anazindukana wakaanza tena, ‘sasa utasema”.
Riwaya hii imeandikwa na
Adam Shafi, mwandishi mkongwe. Mbali na riwaya hii ameandika vitabu vingine vitatu,
vyote vikiwa ni riwaya: Kasri ya Mwinyi Fuad ( ambacho kimetafsiriwa kwa lugha za Kifaransa, Kijerumani na Kirusi);
Kuli na Vuta nikuvute ( ambacho kilimpatia tuzo ya mwandishi bora nchini
Tanzania mwaka 1998). Sasa hivi yuko mbioni anaandika kitabu kingine cha
kusisimua Mbali na Nyumbani, kama alivyonielezea tulipokutana katikati mwa Jiji
la Dar-es-Salaam: “ Ninaandika juu ya maisha yangu, ujana wangu, harakati za
kutafuta elimu na mpango wa kuzamia kupitia Misri kwenda Ujerumani kutafuta
maisha na baadaye kurudi hapa Tanzania kuendeleza mapambano ya maisha hadi leo
hii”. Alieleza Mzee Adam Shafi.
Ukiongea naye, mbali na
hekima na busara zilizotulia kwenye kichwa chake ambacho sasa kimejaa mvi,
utaburudika na utaalamu wake wa lugha ya Kiswahili, anaongea Kiswahili sanifu,
hata akiongea Kingereza na Kijerumani matamshi yake yanaonyesha kwamba yeye ni
mtaalamu wa lugha hizo.
Adam Shafi alizaliwa
mjini Zanzibar mwaka 1940. Baada ya elimu yake ya shule ya msingi alijiunga na
Chuo cha Ualimu cha Seyyid Khalifa ( sasa Chuo cha Ualimu cha Nkrumah) mwaka
1957 hadi mwaka 1960. Alipata Diploma ya Juu katika fani ya Siasa na Uchumi
katika Chuo cha Fritz Heckert, katika iliyokuwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya
Ujerumani mwaka 1963. Alipata mafunzo ya uandishi wa habari mjini Prague,
nchini Czechoslovakia 9 sasa Jamhuri ya Czech) mwaka 1964 hadi mwaka 1965,
nchini Sweden mwaka 1982 na nchini Marekani mwaka 1983. Adam Shafi alikuwa
mwenyekiti wa Umoja wa Waandishi wa Vitabu Tanzania (UWAVITA) kuanzia 1998 hadi
2002. Alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa Baraza la Maendeleo ya Vitabu Tanzania
(BAMVITA) mwaka 2002. Sasa hivi amestaafu na kuendelea na kazi zake za uandishi
binafsi.
III. Mazingira
yanayokizunguka kitabu
Kabla sijaanza uchambuzi wa kitabu hiki cha Haini, ni bora nielezee mazingira yanayokizunguka kitabu hiki. Sina uhakika kama kitabu hiki kinauzwa Tanzania Bara. Kitabu hili kilichapishwa mara ya kwanza 2003 na mara ya pili 2010, kule nchini Kenya. Mimi nimepata bahati ya kukipata mwaka wa 2010, nilipokwenda Zanzibar wakati wa Uchaguzi Mkuu nikiwa Mwangalizi huru wa TEMCO. Nilipoingia kwenye duka la vitabu pale Darajani, nilikikuta kitabu hiki, ingawa bei yake ilikuwa juu kidogo, shilingi elfu kumi na tano ukilinganisha na vitabu vya riwaya tulivyozoea kununua huku bara, sikukiacha. Nilikinunua na kuanza kukisoma.
Adam Shafi, aliniambia
kwamba aliamua kukichapisha kitabu chake Kenya, baada ya mizengwe ya wachapishaji wa Tanzania. Labda waliogopa
kuchapisha kitabu cha Haini? Ni wazi unahitaji ushupavu wa pekee kukichapisha
kitabu hiki, hata mimi mwenye nilisitia kukifanyia uhakiki, nilikisoma 2010, ninakifanyia uhakiki 2012!
Ni riwaya iliyosheheni ukweli ambao
wengi wetu hatupendi kuusikia na tukifikia hatua ya kufilisika kimawazo, ukweli
kama huu kwenye riwaya hii ni lazima
tuupatie jina la uchochezi!
Mwandishi
anasema riwaya hii inachukua tukio la kihistoria, la kuuawa kwa Kiongozi kwenye
nchi za Afrika. Hapendi kuitaja nchi hiyo na kiongozi huyo. Lakini kwa makusudi
au kwa bahati mbaya anasahau kuficha majina ya Pemba, Unguja, Darajani na
mengine mengi. Mwisho wake, hata kama msomaji ni zezeta ni lazima atagundua
kwamba nchi inayoongolewa hapa ni
Zanzibar, na kiongozi aliyeuawa mwaka 1972, si mwingine zaidi ya
Marehemu Rais Karume.
IV. Muhtasari wa
Kitabu
Unaweza kufanya
Muhtasari wa Kitabu hiki kwa maneno machache: Baada ya kifo cha kigogo, au kwa
maneno mengine Kiongozi wa nchi hii isiyotajwa jina na mwandishi, waliokamatwa,
wakawekwa ndani, wakateswa na hatimaye baadhi yao wakahukumiwa kunyongwa si waliopanga njama za mauaji. Riwaya inaonyesha
na kuweka wazi kwama Kigogo, aliuawa na watu wake mwenyewe, rafiki na ndugu
zake waliokuwa wakimzunguka kila siku ya Mungu. Hawa walikuwa na uchu wa
madaraka, walitaka Kigogo, aondoke ili
wao waingie madarakani, baada ya mipango yao kushindwa, maana nchi hii
ilikuwa na nguvu nyingine kutoka nje ambazo zisingeruhusu madaraka kuchukuliwa
kwa mtutu wa bunduki, waliona waihadae dunia kwa kuwakamata “washukiwa bandia”
na kuwaweka gerezani.
Riwaya hii, inatufumbua
macho kwamba Haini si Haini. Wale
waliopaswa kuitwa Haini kule Zanzibar, walibaki huru na kuendelea kula maisha.
Wanyonge na watu baki ndio walikamatwa na kubambikizwa jina hili la Haini.
Mfano mzuri ni Hamza,
huyu ni mwandishi wa habari. Alikamatwa kwa vile alikuwa ni rafiki wa Hamduni,
kijana aliyetekeleza mauaji. Hivyo Hamza na wengine wengi waliokamatwa,
hawakuwa na habari za mpango wa mauaji, bali wenye mpango, ambao ndio waliokuwa
serikalini, walitaka kuwakamata watu, kuwatesa hadi waungame kitendo cha mauaji.
Maungamo yao, yalikuwa salama kwa kikundi kizima kilichotekeleza mauaji.
Riwaya inaelezea
jinsi baadhi watu walivyokamatwa hata
kabla ya kufahamu kilichotokea. Ukurasa wa 7 hadi wa 14 unaelezea jinsi Hamza
alivyokamatwa na kupelekwa Gerezani. Kule alikumbana na mateso ya kutisha.
Asilimia kubwa ya riwaya
ni maisha ya gerezani. Ingawa mwandishi anajitahidi kuficha jina la nchi,
lakini majina ya gereza yanamsaliti kiasi mtu anagundua kwamba hizi ni gereza
za Zanzibar ambazo hazitofautiani na zile za Tanzania bara. Ukatili na unyama
ambao hadi leo hii unaendelea kwenye magereza zote nchini.
“Baada ya siku mbili
mwili wa Sururu ulivunda, unanyekenya nyekenyeke, unatoja rojo ya usaha.
Mgongoni mlifanya mashata ya damu na usaha juu ya misirimbo ya michapo mikali
ya fimbo na viboko iliyomzonga mdawari mgongoni kuzungukia mbavuni mpaka
tumboni, kama miraba ya pundamilia, kwake kulala kulikuwa ni shida na kukaa pia
ni shida, na yote hayo yalimletea mitonesho mikali. Uso ulikuwa umemjaa,
umetutumka machoni na mashavuni na domo nalo limeumuka damu bado zinamtoka
kwenye lile pengo alilong’olewa meno. Na usoni ndevu zake zilikuwa zikiota kwa
haraka, zikashikana na damu iliyokauka zikawa kama vigaga” (Uk wa 21).
Ukatili unaosimuliwa
kwenye riwaya unatisha. Je mwandishi
alionja maisha ya gereza au ni kubuni tu? Ni mateso ya kinyama ambayo kuna
ushahidi kwamba mateso hayo ni chakula cha kila siku kwenye magereza yetu mbaya
zaidi kwa Haini, anayekisiwa kutoa roho ya Kigogo: “Alimwangalia jinsi
anavyohaha, pumzi juu juu, akawaza watu wale walikompeleka Hamza usiku kucha
wakamrudisha akiwa na hali ile, si wa
dunia hii wa ahera. Aliwaza jinsi binadamu anavyoweza kukosa huruma kwa
binadamu mwenzake, akajifanya yeye ni
binadamu zaidi kuliko binadamu
wengine, akajiweka karibu na Mungu akajipa uwezo wa kuua na kuhuisha” (Uk wa
67)
Mbali na mateso, mbinu
nyingine nyingi zilitumika ili kuwafanya waungame mauaji, wajinga walianguka
kwenye mtego na hao ndio mwisho wa
mwisho walihukumiwa kunyongwa. Welevu kama Hamza, ambao walijua fika hakufanya
kitu walikwepa mitego hiyo: “ Sisi tunajua kwamba wewe huhusiki lakini ombi
letu ni kukutaka ukubali. Ujidai kama vile umo na unawajua wengine. Tuna orodha
ya majina hapa tutakupa, na wote hao tumeshawatungia hadithi kuthibitisha vipi wanahusika”
(Uk 82). Hamza alikataa ushawishi huo,
lakini wao waliendelea kumshawishi “ Hamza usiwe na wasiwasi. Wapo wenzako
waliokwishakubali watakuwa mashahidi
halafu tutawachilia. Unasemaje, utajiunga na kundi hilo? Tena wao hivi sasa tumewaweka pazuri. Wanakula
pilau, chai ya maziwa, mikate, siagi, jam, al-hasil wako burean, alieleza
Kanali Mapepe” (Uk 82). Pamoja na yote hayo, Hamza, alijua hakufanya kitu.
Alivumilia mateso yote na kukataa kuungama kitu ambacho hakufanya.
Wafungwa wengine
walijaribu kutoroka, lakini walikamatwa na kurudishwa gerezani au wengine
kupotezwa kabisa. Wafungwa wengine walijua kabisa kwamba wameingizwa tu ili
kufunika ya wakubwa: “ Sikiliza Kuchi. Haya mambo kuna wenyewe wanaoyajua.
Wanayajua utando mpaka ukoko. Kuna wenyewe waliyoyapanga” Alisema Haramia, “
Wenyewe gani?” aliuliza Kuchi
“Wakubwa! Wakubwa
wenyewe ndio waliyoyapanga haya’
“Unataka kuniambia
kwamba Kigogo kauliwa na wakubwa wenzake?”
“ Sasa tena!” alitia
mkazo Haramia
“Vipi?” aliuliza Kuchi
“ Wewe Kuchi hebu kaa
ufikiri. Silaha zimeibiwa kutoka kwenye ghala ya kutunzia silaha wiki nzima
kabla ya siku ya mauaji. Wakubwa wakijua hayo na hakuna lolote walilolifanya”
alisema Haramia.( Uk 158).
Ili kuonyesha kwamba
mauaji yalipangwa na wakubwa, mwandishi anatuingiza kwenye tafakuri ya bure: “
Ile siku ya maziko yake. Kigogo alizikwa
kwa heshima zote alizostahiki mtu kama yeye na haukupita muda mrefu mrithi wake
akatawazwa. Kanali Bunju ( ambaye ndiye anayeongoza mateso ya wangungwa wa
Uhaini) akajikuta kiti kile amekikosa
amekikalia mwingine..... Kigogo ameuawa na hakuna mwingine yeyote aliyestahili
kiti chake isipokuwa yeye, leo kiti hicho anakikalia mtu mwingie, siye yeye..”
( Uk 161).
Baada ya Kigogo, kuuawa,
wakubwa walihakikisha wale wauaji wote wanauawa ili wasijetoa ushahidi wa
kuwaingiza kwenye kesi. Hivyo hawa wote waliosombwa na kutupwa gerezani
hawakuwa na ushahidi wa kujinasua zaidi ya kukubali au kukataa ushawishi wa
gerezani.
Kesi ya Uhaini ilipoanza
kusikilizwa, wale waliokataa kudanganywa ili wakubali waliendelea kusimama
kidete kupinga kukamatwa kwao: “ Katika maelezo yangu hayo nimeeleza wazi wazi
kwamba mimi sielewi, chochote, wala sihusiki kwa namna yoyote na mpango wa
uhaini. Nimekuwa msimamo huo hata baada ya kuhojiwa mara sita katika hali ya
vitisho na mateso makubwa, nikilazimishwa nikubali khusika na uhaini kwa
kucharazwa kwa mipweke na mpera, kutimbwa kwa mateke ya watu waliovaa viatu
vizito vya kijeshi, na kuning’inizwa kwenye kitanzi mpaka choo kibichi
kikanitoka” ( Uk 248).
Mwandishi anaonyesha
jinsi kesi ya uhaini ilivyoendeshwa kwa sheria na kufuata haki. Wale wote
waliokataa kudanganywa ili wakubali kutenda kosa waliachiwa huru. Wale tisa
waliokubali na kupata maisha mazuri gerezani kwa ahadi ya wakubwa kwamba kesi
ikifika wao watakuwa mashahidi, hao ndo kibao kiliwageukia. Kwa kukubali wao
wenyewe, hukumu ilipitishwa kwamba walikuwa na hatia. Hivyo watu tisa ndo walipatikana na makosa ya mpango wa
kifo cha Kigogo.
Kwa maoni ya mwandishi
ni kwamba wale waliopanga njama za kifo cha Kigogo, walibaki huru hadi leo hii.
Waliokamatwa, kuteswa na kufungwa zaidi ya miaka miwili na hatimaye baadhi yao
kupata hukumu ya kifo, ni watu wasiokuwa na hatia. Bahati mbaya riwaya inafikia
mwisho bila kufahamu kama kweli hao watu tisa walinyongwa au walikata rufaa? Je
historia ya Zanzibar inasema nini kuhusiana na kesi hii ya uhaini? Kuna haja ya
kuichimba sasa ili kulinganisha ukweli wa riwaya hii na ukweli wa historia..
V. TATHIMINI YA KITABU.
Nianze kwa kumpongeza
Adam Shafi, kwa kazi hii nzuri sana aliyoiandika. Kusema kweli hadithi hii
inaburudisha, inasikitisha na kufikirisha. Ni hadithi yenye kuchekesha pia.
Pili nimpongeze mwandishi kwa kuthubutu kuandika mambo haya ambayo wengi
wangeogopa kuyaandika. Inahitaji moyo wa
ushupavu kuandika riwaya inayofichua ukweli uliofichika, kwamba wale waliopanga
mbinu na njama za mauaji ya Kigogo, walibaki huru wakati walikamatwa watu
wanyonge wasiokuwa na sauti.
Tatu, ni kumpongeza kwa
matumizi ya Kiswahili sanifu na kama ilivyo kawaida yake anapoandika kuiacha
ile harufu ya mvuto mzuri wa lugha kiasi kwamba msomaji anatambua pasipo na
shaka kwamba mwandishi ni mtu wa visiwani.
Nne, ni uhodari wake wa kutengeneza maumbo na
kufanikiwa kutoa picha halisi ya kile anachotaka kuelezea. Kwa mtu anayeifahamu
Zanzibar, akisoma kitabu cha haini, anajiona kama yuko Zanzibar vile: “ Hamza
alijikuta peke yake ameibuka kutoka katika vichochoro vyembamba vya Malindi na
kuchomozea katia barabara kuu ya Darajani.. Mtaa wa Darajani ulikuwa umepumbaa
kwa kukosa ule uhai wake wa kawaida saa kama zile, saa ambazo kwa kawaida, watu
baada ya kusali Swala ya Magharibi, hujitandaza ovyo ovyo vibarazani, wengine
wakipiga gumzo kwenye mabao ya wauza kahawa wakibwia mafunda ya kahawa chungu
iliyochemka bara bara.” (Uk 2)
Tano, mwandishi
amefanikiwa kuelezea hali ya uchumi ya wakati huo na ugumu wa maisha: “ Sasa
Khadija akaanza kufikiri. Ataupata wapi mchele
na siku yao ya ukoo bado haikufika. Hapo duka la ukoo ukienda, kama siku
yako haikufika hata ukilia machozi ya damu mchele huupati. Ataupata wapi mkate.
Watu huanza kujipanga foleni ya mkate tokea usiku na hukesha hapo hapo kusubiri mkate wa asubuhi. Hata hivyo
huo mkate wenyewe kuupata ni bahati nasibu tu. Wakati mwingine hiyo foleni huvurugika
watu wakakanyagana na kutiana kabari wakakaribia kuuana” ( 146).
Sita, Mwandishi
anatufunulia uaminifu na uvumilivu wa wanawake wa Zanzibar. Sura yote ya Kumi na nne, inaonyesha uaminifu wa Khadija
juu ya mme wake Hamza, aliyekuwa
amekamatwa uhaini kusweka gerezani. Pamoja na ugumu wa maisha na vishawishi
vingi kutoka kwa wakubwa wa Serikalini, Khadija akiwawakilisha wanawake wengine
wa Zanzibar na labda hata wa Tanzania bara, alibaki mwaminifu kwa miaka yote
ambayo mme wake alikuwa kifungoni. Hili ni jambo la kupongezwa, maana kuna
baadhi ya waandishi ambao daima wanaonyesha kuwa mwanamke ni dhaifu na hawezi
kupambana na maisha magumu na yenye vishawishi.
Saba, ni uhodari wa
kuficha jina la nchi na Kiongozi. Hapa kuna utata kidogo. Mtu anaweza kujiuliza
ni kwa nini mwandishi alificha jina la nchi na kiongozi, lakini riwaya nzima
inaonyesha wazi kwamba nchi yenyewe ni Zanzibar na kiongozi aliyeuawa ni
Marehemu Rais Karume. Je, angetaja jina utamu wa riwaya ungepungua? Au labda ni
ushauri kutoka kwa wachapishaji na watu walioupitia muswada huu? Waliogopa
riwaya isilete uchochezi au labda mwandishi kuingia matatani? Inashangaza
kidogo na inahitaji majibu. Ni matumaini yangu kwamba baada ya kusoma uhakiki
huu mwandishi atatoa majibu.
VI. HITIMISHO.
Ni wazi ningependa
kuwashauri wasomaji wangu kukinunua kitabu hiki na kukisoma ingawa sina uhakika
kitabu hiki kinapatikana Tanzania bara. Mimi nilikitafuta siku nyingi na
hatimaye kufanikiwa kukipata kule Zanzibar. Pamoja na ukweli kwamba bei ya
kitabu hiki ni kubwa, ni muhimu kukinunua na kujisomea yale tunayoyajua na
tusiyoyajua.
Kama nilivyosema hapo
juu, kuna haja mwandishi akaelezea lengo lake la kuficha jina la nchi na
kiongozi aliyeuawa, wakati riwaya nzima inaonyesha bila kificho. Akitoa toleo
jingine, ni bora kuyakweka majina, ili watu wakapata ukweli na uhondo wa
historia na riwaya yenyewe.
Pia mwandishi anaweza
kufanya jitihada binafsi kuhakikisha kitabu chake kinauzwa Tanzania Bara.
Sitaki kuamini kwamba alikuwa akiwaandikia wa Zanzibari peke yao. Mauaji ya Kigogo yaliligusa taifa
zima la Tanzania; sote tuwe macho maana tukio kama hilo laweza kutokea tena na
mtego wa panya ukawaingiza waliyemo na wasiokuwemo. Wanaotenda kitendo wanabaki
huru na kuendelea na maisha, wanakamatwa dagaa, Nyangumi na papa wanaendelea
kuelea.
Na,
Padri Privatus
Karugendo.
0 comments:
Post a Comment