Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) Mkoa wa Mara, Esther BulayaMWANA MAMA MHESHIMIWA ESTER AMOS BULAYA.

Katika safu yetu ya Mwana Mama, leo tunawaletea Mheshimiwa Ester Bulaya mbunge wa viti maalumu kundi la vijana wa chama cha mapinduzi mkoa wa Mara. Kama kawaida yetu hatuandiki juu ya maisha binafsi juu ya Ester Bulaya, hayo tunawaachia watu wengine. Sisi tunamwangalia Mwana Mama Ester Bulaya na mchango wake katika taifa letu la Tanzania. Pia tunajua wazi kwamba mengi yameandikwa juu ya Mheshimiwa Ester Bulaya: hata hivyo  tumeamua kuandika juu yake kwa kuamini yanayoandikwa juu yake ni ya kisiasa na mara nyingi yenye ushabiki wa chama chake cha CCM. Sisi tunamwandika mama huyu kwa jicho tofauti na ndiyo maana tunaamini ana sifa za kuingia kwenye safu iliyoanzishwa kwa lengo la kuandika habari za mama wanaotoa mchango mkubwa katika taifa letu, lakini habari zao haziandikwi na wala hazijulikani.
Sifa kuu aliyonayo Mheshimiwa Ester Bulaya, ni kupigania haki za vijana bila kuangalia itikadi zao za vyama, dini wala kabila zao. Yeye amejipanga kupigania haki za vijana wa Tanzania; Mwana mama  huyu ni miongoni mwa vijana wachache wanaoona ukweli kwamba hatima ya uhai wa Tanzania, iko mikononi mwa vijana.  Huyu ni miongoni mwa vijana wachache wanaoona ukweli kwamba vijana wa Tanzania wakiuungana na kufanya kazi kwa pamoja, hata kama watakuwa na itikadi tofauti za vyama, wataweza kulijenga taifa lenye maendeleo na lenye kujiamini . Hivyo amekuwa mstari wa mbele kushirikiana na vijana wote, na hasa wanasiasa wenzake, wabunge wenzake bila kujali wanatoka chama gani cha siasa.
Msimamo wake huo wa kushirikiana na vijana wa vyama vya upinzani, umemwingiza matatani ndani ya chama chake. Chama chake cha CCM, kinamwangalia kwa jicho la tahadhari na baadhi wakifikiri ni Mwana mama huyu ni msaliti. Yeye mwenyewe anasema kwa kujiamini: “Nipo bungeni kuwawakilisha vijana na niko tayari kupoteza hata uhai wangu kwa kulitetea taifa langu hata kama nitaonekana msaliti katika chama changu kwa kukemea maovu,”
Wakati CCM, wakimtilia shaka Ester Bulaya na kumkosoa kushirikiana na wapinzani, kuna wanaomchukulia Mheshimiwa Bulaya, kuwa ni mwoga: Anaona nusu tu ya ukweli, haitoshi kushirikiana na vyama upinzani. Muhimu ni kutambua kuwa CCM si baba wala mama, na wala CCM si Tanzania! Kwa maana kwamba CCM, itapita kama vitakavyopita vyama vyote  vya siasa. Tanzania itabaki! Hivyo kitu muhimu ni Tanzania. Ukweli huu Mheshimiwa Ester Bulaya anauona nusu nusu! Maana kuna wakati naye anakumbwa na wimbi kubwa la kukitukuza na kukishangilia chama chake hata bila kutafakari na kuchucha uzito wa hoja inayokuwa jukwaani. Siku atakapobahatika kuuona ukweli huu mzima, huyu atakuwa miongoni mwa vijana wa kulivusha Taifa letu kuelekea maendeleo na utulivu wa kisiasa.
Mheshimiwa Ester Bulaya, alizaliwa Ilala Dar-es-Salaam, tarehe 3 Machi 1980. akiwa darasa la sita, baba yake mzazi Amos Bulaya aliyekuwa askari wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wa cheo cha meja katika kambi ya Pangawe, Morogoro alifariki dunia na akiwa kidato cha pili, mama yake Hadija Ismail alifariki dunia pia.  Hivyo alilelewa na baba yake mdogo Paul Bulaya (Ofisa wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) ambaye alimsomesha hadi alipomaliza elimu yake ya sekondari na chuo. Yawezekana hali ya kujiamini na kujisimamia, hali ya kuwapenda vijana na watoto na kupenda kuwasaidia, imejengwa na hali ya kuwapoteza wazazi wake akiwa binti mdogo? Hili ni swali la kumuuliza wakati wa kufanya naye mahojiano.
Mheshimiwa Ester Bulaya, alisoma shule ya msingi ya Kurasini Dar-es-Salaam na Sekondari ya Makongo. Baada ya kumaliza elimu ya sekondari, alijiunga na chuo cha Uandishi wa habari cha Morogoro na kujipatia Diploma  ya Uandishi wa habari. Alifanya kazi kwenye gazeti la Uhuru mwaka 2002 mpaka 2008, alipopata nafasi ya kwenda Amerika kusoma masomo ya Uongozi.
Alipoingia Bungeni, amekuwa sauti ya vijana na watoto. Tumemsikia mara nyingi akitetea haki za vijana na watoto. Pia anapigania haki ya mtoto wa kike na kuamini njia ya kumkomboa mtoto wa kike ni kumpatia elimu. Tulisikia kwenye vyombo vya habari jinsi alivyojitolea kumsomesha mtoto Penina Wayoga, hadi kidato cha sita, baada ya binti huyu kuuonyesha kufanya vizuri kidato cha nne.
Tunasikia jinsi Mheshimiwa Ester Bulaya, anavyowahamasisha vijana wa Mkoa wa Mara, kushirikiana kupitia mchezo wa mpira wa miguu. Mbinu hii, wameitumia wanasiasa wengi wenye kuona mbali. Kwa kucheza pamoja vijana wanashirikiana na kutoa tofauti miongoni mwao. Mashindano ya mpira anayoyaendesha Mheshimiwa Ester Bulaya, hayana itikadi ya kisiasa na wala hayaangalii imani ya vijana hawa. Ni michezo ya vijana, ambao kwa kucheza pamoja, kwa kushindana, wanajenga mahusiano na uelewa mpana wa kutofautiana kwa mawazo, kutofautiana kwa misimamo, lakini kushirikiana kuijenga Tanzania moja.
Kama anavyosema yeye mwenyewe: “Maendeleo hayaji kama hushirikiani na vijana katika uamuzi na utekelezaji, vijana wote bila kujali itikadi za vyama wanapaswa kuungana kukemea maovu na kupandikiza mbegu mpya ya ushindi na maendeleo ya nchi yetu,”
Tumesikia jinsi Mheshimiwa Ester, anavyotoa misaada kwa vijana na hasa katika jimbo lake la Bunda. Misaada hii imekuwa tishio kwa wale wanaotaka kugombea ubunge katika jimbo hilo. Bila kuingia kwa ndani nia na lengo lake la kutoa misaada, ni wazi kwamba umoja anaoujenga kupitia misaada yake hiyo ambayo kwa kiasi kikubwa inawaunganisha vijana, ni mchango mkubwa utakaobaki na kudumu hata kama yeye hatafanikiwa kugombea na kupita kama mbunge wa jimbo hilo. Kwa vile anaamini kuwekeza kwa vijana, ni mtu muhimu ambaye hata bila kuchaguliwa kuwa mbunge anaweza kuendelea kuchangia kulijenga taifa letu. Si lazima mtu awe mbunge ndo achangie maendeleo. Lakini ikitokea akafanikiwa kurudi bungeni kwa kupigania na kuchaguliwa kama mbunge wa jimbo, wananchi wa Bunda watakuwa wamempata mwakilishi mzuri.
 Kipaji cha uongozi cha Mheshimiwa Ester Bulaya kilijionyesha wakati akiwa darasa la kwanza alipoteuliwa kuwa kiongozi wa darasa hali ambayo iliendelea hadi akiwa darasa la saba katika shule ya msingi Kurasini, jijini Dar es Salaam. Pia akiwa shule ya sekondari Makongo aliteuliwa  kuwa kiranja jambo ambalo liliwafurahisha hata ndugu zake hasa baba yake mdogo ambaye ndiye alikuwa akiishi naye kwa wakati huo. Mnamo mwaka 2000 alijiunga na Chuo cha Uandishi wa Habari cha Morogoro, (MSJ) kuchukua Diploma ya uandishi wa habari ambako pia alikuwa Waziri wa Maendeleo ya jamii na Michezo.
Jina la Esther lilianza kuonekana kwenye vyombo vya habari mwanzoni mwa miaka ya 2000 alipokuwa mwandishi katika kampuni ya Uhuru Publications Ltd inayochapisha magazeti ya Uhuru na Mzalendo.
Esther aliyeingia bungeni baada ya kushinda nafasi za uwakilishi wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) na ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Utekelezaji katika jumuiya hiyo anasema kazi kubwa anayofanya ni kushirikisha vijana katika kujiletea maendeleo yao.
Huyo ndiye Mwana Mama Ester Bulaya, Mheshimiwa Mbunge, mwandishi wa habari, mpambanaji na mwanaharakati.
Na,
Padri Privatus  Karugendo,
+255 754 633122.0 comments:

Post a Comment