UHAKIKI WA KITABU: MERCHANT
POLITICS AND THE MOCKERY OF MULTIPARTY POLITICS IN TANZANIA
1. Rekodi za Kibibliografia.
Jina la kitabu kinachohahikiwa hapa ni MERCHANT POLITICS AND THE MOCKERY OF
MULTIPARTY POLITICS IN TANZANIA, Kimeandikwa na Lawrence I.M Kilimwiko.
Mchapishaji wa kitabu hiki ni Konrad
Adenauer Stiftung na amekipatia namba ifuatayo katika sekwensia ya vitabu
duniani (ISBN): 978- 9987- 716-01-2. Kitabu kina kurasa 116 . Na anayekihakiki
sasa hivi katika safu hii ni mimi Padri Privatus Karugendo.
II. Utangulizi
Kitabu hiki kilizinduliwa mwezi wa pili Jijini Dar-es-Salaam
na bahati nzuri mchambuzi wa kitabu hiki alikuwa miongoni mwa watu waliopata
mwaliko wa kuhudhuria sherehe za uzinduzi huo. Majadiliano yaliyofuata baada ya
uzinduzi wa kitabu hiki yamechangia kwa kiasi kikubwa uchambuzi huu
ninaoufanya. Hapa na pale nimezingatia maoni na michango ya washiriki mbali
mbali. Pia baadhi ya majibu ya maswali
kutoka kwa mwandishi wa kitabu hiki yaliyoulizwa wakati wa uzinduzi yameingizwa
kwenye uchambuzi huu kwa namna moja ama
nyingine.
Kitabu hiki kinakuja wakati wake. Tunapoandika
Katiba mpya na tunaelekea uchaguzi wa 2015, ni muhimu kuanza kutafakari juu ya
siasa yetu na mfumo tunaoutumia katika siasa za Tanzania. Bwana Lawrence Kilimwiko, ametuchokoza na
kutuelekeza katika mjadala huu. Ni imani yangu kwamba kitabu hiki kitaleta
mchango mkubwa na hasa kama jitihada itafanyika kukitafsiri kitabu hiki kutoka
lugha ya kigeni.
Kitabu hiki kimeandikwa kwa kimombo, na labda
ndiyo hiyo dhihaka yenyewe inayoongelewa katika kitabu hiki? Mtu ambaye
analenga kusahihisha mwenendo wa siasa ndani ya nchi ambayo lugha yake kuu ni Kiswahili
na kuamua kuandika kwa lugha ya kigeni, si tu kwamba inashangaza, bali ni
dhihaka. Mwandishi anasisitiza kwamba tunafanya mambo kwa kushinikizwa na
wafadhili, na yeye anaandika kwa lugha ya kigeni dalili ya wazi kwamba naye
anashinikizwa na wafadhili kwa kuandika lugha wanayoifahamu wao? Ukombozi
kamili na kufanya mambo sahihi ni pamoja na kuitumia lugha ya taifa. Mtu anayetumia
lugha za wengine kujieleza na “kusambaza” ujumbe kwenye jamii, si mtu huru! Kwa
Kiswahili cha kawaida, kitabu hiki kinaitwa Biashara ya Siasa na Dhihaka
ya Vyama vingi Tanzania. Hoja ya
mwandishi ni kwamba badala ya Tanzania kuwa na mfumo wa siasa wa vyama vingi
kutokana na uhitaji wake kama ilivyo katika nchi zilizoendelea, mfumo uliopo
kwa sasa hivi ni wa kisheria zaidi. Na kwamba kutokana na kushinikizwa na
wafadhili kuachana na mfumo wa chama kimoja, kulibuniwa vyama bandia huku vile
vilivyoanzishwa kwa nia njema vikisongwa na vizingiti vingi katika kuviendesha.
Hivyo badala ya kuwa na vyama vilivyoanzishwa kutokana na uhitaji iwake katika
jamii, kumekuwepo na vyama bandia vilivyougeuza mfuo wa vyama vingi badala ya
kuwa huria kuwa holela na dhihaka mbele ya
dunia yetu ya leo.
Mwandishi anakumbusha historia ya Tanzania na
vyama vingi. Kwamba CCM, ilikuwa imegoma kukumbatia mfumo wa vyama vingi.
Lakini baada ya shinikizo la wafadhili, ilibadilisha msimamo wake na kuelekeza
nguvu zote kwa mfumo wa vyama vingi. Hata hivyo hili lilifanyika shingo upande
na Chama cha Mapinduzi kupitia Serikali
kilibuni mbinu ambazo kutokana na historia ya nyuma, vyama vipya
visingeweza kufua dafu mbele yake; Sheria ilitungwa ya kuvitaka vyama
visajiliwe lakini siyo CCM ambacho kilisajiliwa pasipo kufuata masharti kwa
vyama vingine. CCM pia ilijinyakulia rasilimali zote zilizokuwa zimekusanywa na
watanzania wote ikiwemo vitega uchumi, majengo na hata viwanja vya michezo
mikoani kote.
Kwa kuogopa wafanyabiashara wakubwa kujiunga na
vyama vingine vya siasa, CCM ililegeza masharti yake ya chama cha wakulima na
wafanyakazi na kufungua milango yake kwa kila mtu hata mijizi, matapeli,
mawakala wa ubepari, ukabaila na hata wale wasiokuwa na maadili wala uzalendo.
Matokeo yake ikawa ni kwa chama hicho maarufu
barani Afrika kutekwa nyara na genge la mijizi,
na kwa mkakati kasi ya ajabu uongozi wa CCM ukawa mikononi mwa watu
wasiokuwa wajamaa, wazalendo na wala waadilifu. Siasa ya ujamaa na kujitegemea
ikageuzwa kibao na kuwa siasa ya kujimegea, kubinafsisha mali za vijiji na
kupora ardhi, wanyama pori na rasilmali nyingine.
Mwandishi anasisitiza hoja yake kwa kutoa mfano
kwamba kuibuka kwa CHADEMA kama chama kimbilio la wanyonge ni ishara tosha ya
pale CCM ya vibopa ilipojifikisha na kuifanya siasa ya vyama vingi kugeuka
dhihaka tupu. Mfumo huria wa kisiasa nchini umegeuka kuwa mfumo holela.
Kitabu hiki kimeandikwa ili kuibua fikra mpya
kuhusu mfumo mzuri wa kuendesha siasa za vyama vingi vinavyotokana na makundi
ya wanachama wenye msimamo, itikadi na falsafa moja ya wanaokusanyika kwa hiari
yao na siyo sheria kama ilivyo sasa.
Lawrence Musanguka Kilimwiko, ni mwandishi mkongwe
ambaye amefanya kazi ya uandishi wa habari zaidi ya miaka 30 akiandika juu ya
masuala ya siasa. Ameandika vitabu vingi vikiwemo: Media Power and Politics in
Tanzania (2009), The Fourth Estate in Tanzania (2002), The Spokesperson: A
Media User Friendly Guide (2004) na Biashara ya Dini, Siasa na Ufisadi.
Lawrence Kilimwiko, alisomea uandishi wa habari
kule India, pia alisomea mahusiano ya kimataifa kwenye chuo kikuu cha
Jahawaharlal India na amesoma Sayansi ya siasa na uongozi Chuo kikuu cha Dar-es-Salaam.
III. Mazingira yanayokizunguka kitabu
Kabla sijaanza uchambuzi wa kitabu hiki cha Biashara ya Siasa na
Dhihaka ya Vyama vingi Tanzania , ni
bora nielezee mazingira yanayokizunguka kitabu hiki. Kwanza nikubali kwamba
jambo hili la kuandika kitabu juu ya mwenendo wa siasa, si la kawaida hapa
Tanzania. Tumekuwa tukisoma vitabu vinavyojadili mwenendo wa siasa katika
mataifa mengine na hasa yale yaliyoendelea. Hivyo kazi hii si ya kawaida.
Lakini pia kuna ukweli kwamba leo hii taifa letu linapitia katika
wakati mgumu kwa vile tulifanya kosa kubwa la kuifanya siasa kuwa biashara.
Tatizo la biashara ni kwamba bidhaa ikikaa sokoni, ni lazima wanunuzi waje na
daima mwenye dau kubwa ndo anafanikiwa
kuondoka na bidhaa sokoni.
Na tabia ya biashara ni ushindani, ni mbinu na ujanja. Ikibidi kwenye
biashara ni lazima kuhakikisha anayekuzibia njia unamwondosha. Haya ndiyo
tunayoyashuhudia sasa hivi katika taifa letu. Haya matukio ya kuwateka watu,
kuwapiga na kuwaumiza, ni dalili kwamba kuna watu wanaoziba njia za
wafanyabiashara wa siasa.
Siasa ikifanywa biashara, inapoteza maana yake. Ndani ya siasa tunapata
wawakilishi wa wananchi. Kwa maana kwamba wananchi wanamchagua mmoja wao kuwawakilisha
katika vyombo vya kutunga sheria na kuitawala nchi. Kwa maana nyingine ni
kwamba kama ingebidi, wananchi wangelazimika kutumia njia zozote zile
kumshawishi mtu wanayempenda ili akubali kuwawakilisha. La kushangaza ni kwamba
katika biashara ya siasa, mwakilishi ndiye anafanya mbinu za ushawishi hata
kutumia fedha ili wananchi wamchague na kumtuma kuwawakilishia. Hii ni kinyume
kabisa na kwa vyovyote ni dhihaka!
Kitabu hiki kinaandikwa wakati tunatengeneza katiba mpya na tunaelekea
kwenye uchaguzi mkuu wa 2015. Ni wakati ambapo Chama tawala tayari kinaona
nguvu mpya ya vyama vya upinzani na nguvu mpya ya vijana ambao kwa kiasi
kikubwa hawaeleweki vizuri, lakini upepo wa kutumia fedha kwa kila hatua, ni
dalili tosha kwamba chama ambacho kitakuwa kimefanikiwa vizuri kufanya biashara
ya siasa kinaweza kuibuka mshindi, maana fedha ni sabuni ya roho kama wasemavyo
Waswahili.
Vyovyote vile, uwe upinzani au chama
tawala, bila fedha ni vigumu kuupata uongozi ndani ya vyama au ndani ya
serikali. Maana yake ni nini? Kwa upande mkubwa wenye fedha ni wazee na wazee
hawa ndo wanataka wabaki madarakani kwa njia zozote zile.
Mazingira mengine yanayokizunguka kitabu hiki
ni kwamba sasa hivi kila kitu kimekuwa
biashara; siasa ni biashara, elimu ni biashara hata na afya ni biashara. Kwa
vile siasa ni biashara kuna uwezekano mkubwa kumpata kiongozi asiyekuwa na
uwezo, wa kuongoza na kufikiri, lakini ana uwezo wa fedha. Badala ya kutawaliwa
na fikira, tunatawaliwa na fedha. Na kwa vile elimu imekuwa ni biashara,
tumeanza kupata matokeo yanayofanana na biashara, badala ya kupata elimu bora
na nzuri kwa ukombozi wa watanzania tunapata elimu mchoko na watoto wetu wanaendelea
kuwa wajinga. Matokeo ya mtihani wa mwaka huu yameonyesha kabisa
ninachokielezea. Na kwa vile afya imegeuzwa kuwa biashara, watu wanaweza
kuingiza hadi dawa bandia au zile zilizokwisha muda wake.
Kwa kifupi ni kwamba Biashara ya siasa, imebadilisha kabisa mwelekeo
wa taifa letu. Haya ndiyo mambo
yanayokizunguka kitabu hiki na kwa njia moja ama nyingine haya ndiyo
yaliyomsukuma mwandishi kuandika kitabu hiki.
IV. Muhtasari wa Kitabu
Mwandishi amekigawa
kitabu katika sura saba ambazo zinaongelea; sheria zinazoongoza uanzishwaji wa
vyama vingi vya siasa, matumizi na ushawishi wa fedha katika siasa za Tanzania,
mabadiliko yaliyoingiza siasa katika biashara, biashara ya siasa kutawala siasa
za Tanzania, na pia anaangalia njia mbali mbali ambazo zinaweza kuuinua
upinzani hadi kufikia kuishika dola.
Mwandishi anakwenda
mbali na kuangalia biashara ya siasa kuanzia miaka ya 80, akiunganisha siasa
hizi na ujio wa soko huria na kile kilichokuja kujulikana kama Azimio la
Zanzibar. Siasa hizi zilizoingia Tanzania, kwenye miaka ya 80, silifutilia
mbali uwezekano wa mtu maskini, hata kama ana akili nzuri kushiriki kwenye
uongozi wa taifa letu la Tanzania.
Mwandishi, katika kitabu
chake anakwenda zaidi kuandika na kusema kwamba, inakuwa shida kwa mwananchi wa
kawaida kuchaguliwa kuongoza, maana hawezi kuwa na fedha za kununua uongozi.
Kilimwiko, anajadili
hoja ya Uzawa, iliyoibuliwa na Mchungaji Chritopher Mtikila ya Uzawa na :
“Walalahoi” , (Gabacholi) Wahindi, na kuonyesha kwamba mali nyingi ya Tanzania
iko mikononi mwa Wahindi. Ukweli kwamba Mtikila, alisikilizwa na kuzoa
washabiki wengi ilikuwa ni dalili ya wazi kabisa kwamba ufa kati ya walionacho
wasiokuwanacho ulikuwa unapanuka sana.
Mwandishi anaifananisha CCM
na mnyama mkubwa aina ya mjusi “Dinosaur”. Mnyama huyu alikuwa mkubwa kuliko
wanyama wote hapa duniani, lakini sasa ametoweka kabisa. Na la kushangaza ni
kwamba mnyama huyu alikuwa anaishi hapa Tanzania. Kwa vile CCM imejiingiza
katika biashara ya siasa na kukubali kutawaliwa na kuongozwa na fedha badala ya
itikadi, fikra, sera na kuijenga nchi, mwisho wake unaweza kuwa kama wa mnyama
mkubwa “Dinosaur” aliyepotea kwenye uso wa dunia.
Kilimwiko anamalizia
kitabu chake kwa kugusia vyama vya upinzani na hasa Chadema na CUF. Anaonyesha
jinsi vyama hivi vilivyopitia vipindi vigumu, pamoja na jitihada za kuonyesha
kwamba vyama hivi ni vibaya, lakini bado hadi leo hii vyama hivi vinaendelea
kuishi na kusonga mbele. CUF, kilibatizwa kwamba ni chama cha Wapemba na
kilikuwa kikiendeshwa na fedha za Waislamu wenye itikadi kali. Sifa hizi
zililenga kukimaliza chama hiki, lakini ilishindikana. Nacho Chadema,
kilibatizwa jina la kuwa ni chama cha matajiri, wakristu na wachaga. Hata hivyo
chama hiki kinaendelea kupanuka na kukubalika kwenye jamii ya watanzania.
V. TATHIMINI YA KITABU.
Nianze kwa kumpongeza ndugu yetu Lawrence Kilimwiko, kwa kuandika
kitabu hiki cha aina yake juu ya siasa za Tanzania. Kitabu hiki ni cha kwanza
kuandikwa juu ya siasa kiasi kinaweza kumsaidia mtu yeyote yule awe mgeni au
mwenyeji, kuona Tanzania tumetoka wapi, tuko wapi na tunakwenda wapi kama mambo
yataachwa kwenda kama yanavyokwenda hivi sasa.
Pili, Kilimwiko, ametoa changamoto kwa watanzania wote na hasa
waandishi wa habari kuyachambua maisha yetu ya kila siku ili yatusaidie
kujipima, kujisahihisha na kusonga mbele. Kitabu ni kati ya njia zinazosaidia
jamii kujiona.
Tatu, mwandishi amefanikiwa kufunua ubovu ulio katika mifumo yetu ya
utawala na jinsi fedha inavyoongoza na kuweka mbali fikra na maadili bora, bila
yeye kuonyesha ushabiki wa aina yoyote ile.
Nne, mwandishi amefanikiwa kuionyesha dhihaka ya vyama vya siasa katika
Taifa letu la Tanzania; na ukweli kwamba kama vyama vyote vinaweza kuwa na
uwanja wa ushindani ulio sawa, hakuna chama ambacho kingekuwa kinajizolea
ushindi wote. Pamoja na matumizi ya fedha, bado chama cha CCM kinabebwa na
dola.
VI. HITIMISHO.
Kama kawaida yangu ya uchambuzi wa vitabu,
ningependa kuwashauri watanzania kukisoma kitabu hiki ambacho kwa kiasi kikubwa
kimechambua siasa za Tanzania na vyama vya siasa.
Kwa upande wa mwandishi ni kumuomba kufanya
jitihadi kubwa kukitafsiri kitabu hiki katika lugha ya taifa. Kama nilivyosema
hapo mwanzoni, ni kwamba inashangaza mtu ambaye anatoa changamoto ya siasa za
Tanzania, yeye mwenyewe anaandika kwa lugha ya kigeni. Hoja yake kubwa ni
kwamba kosa kubwa la taifa letu ni kufanya na kutenda kwa maelekezo ya wafadhili
wa nchi za nje. Kosa hili ambalo analielezea kwa ufasaha mkubwa ndani ya kitabu
chake analifanya yeye mwenyewe! Tunaweza kusema Kilimwiko, aliandika kwa lugha
ya Kizungu kwa vile kazi yake ya kuandika imechangiwa fedha na shirika la nje?
Kama jibu ni kweli basi naye anasukumwa na wa nje kuandika juu ya siasa za
Tanzania.
Inawezekana kabisa tukatoweka kama taifa na
kutokomea kusikojulikana kama alivyotokomea mnyama mkubwa aina “Dinosaur” kama hatufanyi jitihada za kutosha
kuitumia lugha yetu. Rais wa China, aliyeitembelea Tanzania juzi, alitumia
lugha yake kulihutubia Taifa la Tanzania, na watafsiri wakafanya kazi yao.
Haina maana kwamba Rais huyu hafahamu Kizungu, ila ni ile hali ya kujivunia
lugha yake. Lakini Rais wetu Mheshimiwa Dkt Jakaya Kikwete, alitumia Kizungu
kujibu hotuba ya Rais wa China. Hii inaonyesha wazi kwamba hata kama tunapinga
kutawaliwa na Wazungu, ukweli ni kwamba wanaendelea kututawala na watatutawala
milele yote kama hatufanyi jitihada za kujinasua kuanzia kutumia lugha zetu
badala kuzishabikia lugha zao.
Na,
Padri Privatus Karugendo
+255 754 633122
0 comments:
Post a Comment