SALA ZA KISIASA!

MAKALA HII ILICHAPISHWA KWENYE GAZETI LA TANZANIA DAIMA JUMAPILI 2005.

JE, NI VYAMA VYOTE VITAOMBEWA SALA NA VIONGOZI WA DINI ZA KIKRISTU?

Kuomba ni jambo jema na kila mja analazimika kuomba kwa muumba wake. Hata na majambazi wana sala yao wanayoiomba kabla ya kwenda kuvamia na kufanya mauaji. Wanajeshi wanaokwenda vitani wakijua vita ni kutoa uhai na kuharibu mali, wanaomba pia kwa muumba wao kabla ya kuanza vita. Machangudoa na Malaya wanaokwenda kinyume na maadili nao wana sala yao kabla ya kuanza kazi zao za kuuza miili yao na kawaida hawa ni kati ya watu wanaotoa sadaka kubwa kule makanisani!

Siku chache kabla ya mikutano ya chama cha mapinduzi ya kumtafuta mgombea wa urais, viongozi wa dini za Kikristu, walikutana Jangwani, Dar-es-Salaam kuiombea mikutano hiyo ya CCM. Sala hiyo ilikuwa na lengo la kuomba Mungu, awasaidie wanaCCM, kumchagua kiongozi bora, na si bora kwa CCM tu bali bora kwa Taifa zima la Tanzania. Kwa maneno mengine ilikuwa sala ya kuomba apatikane rais bora wa Tanzania, kutoka CCM!

Kusali na kuomba ni kitu cha kawaida. Tunachokihoji hapa si kusali wala kukiombea chama, tunachokihoji ni kule kukiombea chama kimoja wakati nchi yetu ina vyama vingi vya siasa. Tunachokihoji ni viongozi wa dini wenye dhamana ya kuwaongoza waumini wenye maoni tofauti, vyama tofauti, makabila tofauti, kuwalazimisha waumini wao kukipenda chama kimoja cha siasa. Tunachokihoji ni viongozi wa dini za Kikristu kutumia jukwaa la sala na kuligeuza jukwaa la siasa na kampeni! Tunachokihoji ni hii ndoa ya siasa na dini, na hasa dini moja, katika nchi yenye dini nyingi, kufunga ndoa na chama kimoja cha siasa, wakati nchi ina vyama vingi vya siasa. Hiki ndicho tunachokihoji. Huu ndio wasiwasi wetu mkubwa!

“Mnaposali, msifanye kama wanafiki. Wao hupenda kusimama na kusali katika masinagogi, na katika pembe za njia ili watu wawaone. Kweli nawambieni, hao wamekwisha pata tuzo lao. Lakini wewe unaposali, ingia chumbani mwako, na ukisha funga mlango, Sali kwa Baba yako asiyeonekana. Naye Baba yako aonaye yaliyofichika atakutuza. Mnaposali, msipayuke maneno kama watu wasiomjua Mungu. Wao hudhani kwamba Mungu atawasikiliza ati kwa sababu ya maneno mengi, Msiwe kama wao. Baba yenu anajua mnayoyahitaji hata kabla ya kumwomba” (Matayo 6:5-8).

Sala ya Jangwani, ilikuwa kinyume na maelekezo ya Bwana Yesu, kuhusu kusali na kuomba. Badala ya kusali makanisani kwao kwa maficho, viongozi hawa walikusanyana kwenye viwanja vya Jangwani! Ilikuwa sala ya maneno mengi na kupayuka sawa na sala ya watu wasiomjua Mungu. Je, Baba yetu aliye Mbinguni, hajui kwamba tunamhitaji Kiongozi bora? Awe wa CHADEMA, TLP, CUF au CCM?

Jambo la pili ni kwamba sala yenyewe ilivyoendeshwa ni kana kwamba viongozi hawa na waumini wao waliokusanyika kuomba walikuwa wakiomba Mungu, awapatie rais bora kutoka CCM! Hii ilijionyesha wazi kwenye maombi yaliyotolewa na kila Askofu kutoka madhehebu mbalimbali. Sala ya Askofu Kilaini, ilikuwa ya wazi kuliko za wengine. Alisali akielekeza moja kwa moja kwa CCM. Hata kama kwa uchambuzi wake, kwa vile yeye ni msomi na mtu mwenye akili nyingi, ameshatabiri ushindi wa CCM, si busara yeye kama kiongozi wa dini kuonyesha hilo wazi wazi. Nchi ambayo inaongozwa kwa demokrasia ya vyama vingi kiongozi wa nchi huchaguliwa kwa kura ya siri na wala si kwa sala na uchambuzi wa mtu binafsi!

Ingekuwa sala ya kuombea uchaguzi mkuu, au sala ya kuviombea vyama vyote vichague wagombea bora, hakuna ambaye angehoji. Sasa ni lazima tuhoji. Hizi dalili za dini moja kuunga mkono chama kimoja cha siasa ni hatari sana. Ni ugonjwa unaohitaji dawa ya haraka, vinginevyo utalitafuna taifa letu kama mdudu asiyeonekana! Sala za namna hii ni lazima zilaaniwe na kila Mtanzania anayelitakia mema taifa letu!

Rwanda, kabla ya vita vya maangamizi vya 1994, maaskofu wa Kanisa katoliki, walikuwa wakiunga mkono chama tawala. Wengine walikuwa kwenye Kamati kuu na halmashauri kuu ya chama hicho. Matokeo yake sote tunayajua. Maaskofu wanne, waliuawa na jeshi la RPF. Mapadre na watawa walishiriki katika mauaji. Kwa vile chama tawala walichokuwa wakikiunga mkono kilikuwa hatarini kuondoka madarakani, ilibidi wakitetee kwa nguvu zote.

Ukishaunga mkono kitu wazi wazi, na hasa chama cha kisiasa, inakuwa vigumu kuweka mipaka. Inakuwa vigumu kujipangia ushiriki hadi wapi. Unakuwa mkereketwa, mfurukutwa na ngangali. Mtu akikigusa chama hicho anakuwa amekugusa na wewe. Mtu akikipinga chama hicho anakuwa amekupinga na wewe.

CUF, walifanya uchaguzi wao. Hatukusikia viongozi wa dini za Kikristu wakikusanya waumini kuombea uchaguzi wa CUF. Je, viongozi hawa wataitisha sala kuombea uchaguzi wa CHADEMA, NCCR-Mageuzi, UDP na vyama vingine? Ili hii iwe jadi yetu kwamba vyama vya siasa vinapowachagua viongozi wa kuwania kiti cha urais, sala za waumini mbali mbali zinafanyika kwenye majukwaa ya wazi kama lile la Jangwani?

Tujuavyo, si waumini wote wa dini za Kikristu ni wapenzi wa CCM. Baadhi wanaipenda CCM, na baadhi wanavipenda vyama vingine. Kitendo cha viongozi wao kuonyesha wazi wazi kwamba wanakipenda chama Fulani – yaani chama cha CCM, ni kuleta mgawanyiko katika dini zao. Mgawanyiko huu hauwezi kuishia kwenye dini zao tu, ni lazima usambae nchi nzima. Hakuna machafuko mabaya kama ya kidini. Mara nyingi kwenye machafuko ya kidini watu hawatumii akili zao bali huongozwa na imani. Hii ni hatari zaidi. Mtu akianza kutetea hoja zake kwa kutumia imani ya dini, anakuwa kipofu. Anakuwa hana tena uwezo wa kutambua ukweli na uongo. Anaweza kubeba bomu la kujimaliza yeye na maadui zake. Tunayasikia haya yakitokea katika nchi mbali mbali. Si kwamba yalianza ghafla, yalianza pole pole kama yanavyoanza hapa kwetu kwa hizi sala zisizokuwa na mpangilio wala vision ya mbali.

Tunajua jinsi serikali ya CCM, inavyoyasaidia mashirika ya kidini. Tunajua misamaha ya ushuru inayotolewa kwa mashirika ya dini, Tunajua jinsi serikali ya CCM, inavyotoa uhuru mwingi kwa viongozi wa dini. Wanapata heshima kama VIP, na kupendelewa kwa mambo mengi. Lakini kwa vile wao ni viongozi wa watu wote wa Tanzania, si busara kuonyesha mapenzi yao wazi kwa chama kimoja. Ni nani amewaambia kwamba CUF, ikiingia madarakani, au CHADEMA, TLP, NCCR-Mageuzi na vingine, upendeleo wanaoupata kutoka serikalini utasitishwa?

Ni bora viongozi hawa wafanye kazi yao. Wafundishe neno la Mungu. Wachochee maadili bora katika jamii. Mambo ya siasa wawachie wanasiasa. Muumini ambaye amefundishwa maadili mema ni lazima atakuwa mwanasiasa bora. Kwa vile hatuna wanasiasa bora, maana yake ni kwamba viongozi wetu wa dini hawajafanya kazi yao vizuri.

Tunawaomba sana viongozi wetu wa dini za Kikristu, swala la siasa, wasilifanye ni agenda ya kidini. Kama wanakipenda chama cha mapinduzi, wakipende moyoni mwao, wasianzishe ushawishi wa wazi unaoweza kuzua balaa kubwa katika taifa letu.

Na
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment