MTWARA KUCHLE 2MTWARA KUCHELE 2
Makala iliyopita ya Mtwara Kuchele, ni matokeo ya utafiti uliofanywa na mwandishi wa safu hii akishirikiana na Mtandao wa Madeni na Maendeleo (TCDD) kama sehemu ya mafunzo ya ushawishi na utetezi yaliyofanyika tarehe 10-13 Septemba 2013 kwa wanachama wake 30 waliotoka kwenye mikoa ya Mbeya, Iringa, Ruvuma, Mtwara, Lindi, Mara, Kigoma, Mwanza, Pwani, Dar es Salaam na Tabora ilifanya utafiti kwenye manispaa ya Mtwara Mikindani juu ya ukweli kuhusu sakata la mradi wa Gesi Mtwara lilitokea kuanzia tarehe 17 Mei 2013. Mafunzo haya yalifanyika kwenye ukumbi wa Lutheran Centre Mtwara na mwandishi wa makala hii alishiriki kuendesha mafunzo hayo.
TCDD ilifanya mahojiano na watu 257 kwenye kata 7 kati ya 15 za Manispaa ya Mtwara Mikindani, ambao kati yao walikuwa Viongozi wa ngazi ya mkoa 4Viongozi wa ngazi ya wilaya 6 Madiwani 10Viongozi wa serikali za mitaa 46Wananchi wa kawaida 193.
Wote waliohojiwa,  waliomba majina yao yasitajwe, kwa kuogopa kichapo na mateso ya Gwantanamo. Mzee mmoja alituelezea kwamba:
Tambiko maalumu walilolifanya baadhi ya wazee wa mila, wananchi wa Mtwara kwa kushirikisha viongozi wa dini na makundi ya jamii mara baada ya madhila ya May 23 mwaka huu ni kiashiria cha kutokukubaliana na mazingira ya utekelezaji wa mradi wa Gesi  licha ya manufaa kwa taifa yanayoelezwa na viongozi”
Mzee huyu aliyekuwa anazungumza kwa kujiamini, aliendelea kutuelimisha juu ya vurugu zilizojitokeza Mtwara, kwa kauli mbiu ya “ Haitoki”, kwamba:
“Kwa namna yoyote ile ridhaa ya wananchi katika utekelezaji wa miradi inayolenga kutumia raslimali iliyolindwa kwa miongo kadhaa na vizazi vya jamii ya eneo ambapo mradi unakusudiwa kutekelezwa ni muhimu na vyema kuheshimiwa ili kuhakikisha kwamba laana za vizazi hivyo hazijengwi katika kizazi kinachofuata ndivyo imani za asili zinavyotambuliwa
“Hii inadhihirishwa na hatua zinazochukuliwa na jamii hizo hasa katika kutekeleza matambiko ambapo heshima maalumu kwa wafu waliotangulia mbele za haki na kuzikwa kwenye maeneo ambako miradi inafanyika hupewa nafasi ya kuhamisha makaburi kama sehemu muhimu ya kutekeleza imani na matambiko.”
Ikumbukwe awali lilishatolewa tamko kutoka Msimbati kwa bibi Samoe Mtiti (106) kuwa ikiwa serikali itaendelea kulazimisha mchakato wa gesi bila kusikiliza hoja za wananchi angegeuza gesi kuwa maji, hatua ambayo ililazimu mbinu mbalimbali za kumshawishi bi Samoe zifanyike ili hali hiyo isijitokeze. Wakazi wa Mtwara, wanaamini nguvu za  Bibi Mtiti, kwamba ana uwezo wa kubadili gesi kuwa maji, na akitaka gesi isitoke, haiwezi kutoka!
Imani hii kwa Bibi Samoe Mtiti, inaonyesha wazi jinsi suala zima la Gesi, halijaelezwa vizuri. Watu hawana elimu juu ya Gesi na matumizi yake. Kama bado wanaamini Gesi inaweza kubadilika kwa nguvu za miujiza ikawa maji, bado kuna kazi kubwa. Serikali ina wajibu mkubwa wa kuwaelimisha watu wa Mtwara. Kutumia jeshi kuwapiga na kuwanyamazisha si njia sahihi ya kuleta mabadiliko na maendeleo. Kinachohitajika ni kuwasiliza, kujadiliana nao, kuwashirikisha na kuwaelimisha.
Kuna habari za kuaminika kwamba Januari 24, 2013 gari lenye namba za usajili T609 BXG la mtu mmoja anayedhaniwa kuwa ni ofisa wa idara nyeti liliteketezwa kwa moto na wananchi wa Msimbati kwa kile kinachoelezwa kuwa lilifika kumteka bi Somoe ambaye kijijini hapo anajulikana kama mkuu wa kaya. Wako tayari kumlinda bibi huyu kwa gharama yoyote ile, kwa vile wanaamini ana nguvu za kutenda miujiza.
Mzee, tuliyeongea naye, alikuwa anajaribu kutufafanulia umuhimu wa ushirikishwaji. Kwamba serikali haikuzingatia hili, na watu wa Mtwara hawakushirikishwa juu ya uchimbaji wa gesi, kwani raslimali gesi sasa inazungumzwa kama bidhaa haramu kama ilivyo bangi kwenye vyombo vya dola! Ukitamka suala la gesi kwa wanamtwara wanakuona kama vile umetumwa kuwadodosa ili uwachomee utambi kwenye jeshi na hatimaye wapelekwe Gwantanamo kuteswa; hiki ni kituo cha Jeshi cha Nalyendele, ambacho kimebatizwa jina la Gwantanamo, kutokana na vitendo vya mateso vinavyoendelea kwenye kituo hicho.
Wananchi wanaolizungumzia suala la gesi  kwa tahadhari wanatamka bayana kuwa vyombo vya  usalama  vinavyoshughulikia ukusanyaji wa taarifa havikujipa kazi ngumu kujua hasa kwa nini wananchi wanashinikiza  gesi haitoki bila kujali imani, vyama na hali zao. Kiongozi wa serikali za mtaa tuliyeongea naye wakti wa utafiti huu alituelezea kwamba:
“Hili lilichukuliwa kama ajenda ya kisiasa na watoa taarifa ngazi za juu na ndiyo sababu katika mazungumzo ya viongozi wa ngazi ya kitaifa wanaliona kama lilikuwa la kisiasa kumbe hii ni ajenda ya wana-Mtwara imezingatia zaidi maslahi na ustawi wa wana Mtwara na ni matokeo ya maumivu ya muda mrefu kucheleweshwa kwenye safari ya kufikia maendeleo ya kweli”. Na kuongezea kwamba:
“Hivyo maamuzi ya matumizi ya nguvu ndiyo yakachochea zaidi ufa wa mahusiano baina ya serikali na wananchi  hadi sasa ambapo kama mtu anafanya utafiti atabaini kuwa kati ya watu kumi unaokutana nao ni nadra kukutana na mtu anayesifia matunda tarajiwa ya miradi ya gesi kwa Mkoa wa Mtwara huku wengi zaidi wakilaumu mazingira ya utekelezaji mradi huo”
 Serikali bado inatumia nguvu kubwa kuhakikisha inazima sauti za watu wa Mtwara. Hii inadhihirishwa na tukio la Septemba 12,2013 katika Kijiji cha Shole –Mtwara. Wanajeshi walitembeza kipigo kwenye kijiji hicho na baadhi ya watu waliumizwa vibaya kwa  taarifa kwamba kulikuwa na vipeperushi vya kuwazuia watu kushiriki mapokezi ya Mwenge wa uhuru.
Mapokezi mabaya ya mwenge katika wilaya ya Mtwara yanadhihirisha kuwepo kinyongo miongoni mwa wananchi ambapo ililazimu kutumika mbinu za kuwaruhusu wanafunzi kuvaa nguo za nyumbani ili isionekane kwamba Mwenge unapokelewa na wanafunzi  peke yao, hata hivyo mbinu hii  haikusaidia kuficha hasira za wananchi.
Baada ya kichapo cha Kijiji cha Shole, diwani mmoja wa CCM alitwambia kwamba:
“Matumizi ya nguvu kubwa za dola katika masuala yanayohitaji utashi wa watu ni kiashiria kuwa kuna pengo la mahusiano baina ya serikali na wananchi na hivyo kuhitaji chombo kingine kuunganisha makundi yanayotofautiana ”
Kulingana na maelezo ya wananchi, kwa sasa chombo kinachopewa nafasi katika kuunganisha mahusiano baina ya wananchi na mamlaka ya serikali ni mijadala ya pamoja ikihusisha asasi za kiraia ili kurejesha mawasiliano na kuaminiana ambako kumetoweka.
Wananchi wa Mtwara wanasema ukimya uliopo sasa si kwamba ni utulivu na amani bali ni utulivu pasipo amani, na wananchi wanafanya hivi kupisha udhalilishaji na manyanyaso ya matumizi makubwa ya nguvu za dola.
Kimsingi tangu kutolewa agizo la kutoitishwa mikutano ya wazi inayojumuisha watu kwenye maeneo ya wazi, Mtwara imekuwa kisiwa kwa muda sasa kutokana na wananchi kutopata fursa ya kukutanika kujadili maendeleo ya mkoa wao.
“Hivi sasa  msimu wa korosho umeanza lakini hatuwezi kukubaliwa kuitisha mikutano ya kujadiliana juu ya maslahi ya wakulima wa korosho kutokana na agizo hilo na kwamba ukifanya mkusanyiko wowote utakuwa umevunja amri halali ya serikali” . Alituelezea kiongozi mmoja wa serikali za mitaa.
Utekelezaji wa kamata kamata ya watuhumiwa wa vurugu za Mei 23 ulioendeshwa kwa usiri mkubwa na nyakati za usiku kwa kutumia wanajeshi, umetajwa pia kufanywa kwa uonevu mkubwa  kwa sababu hata wale  ambao hawakuwepo mazingira ya tukio kubebwa kwa chuki na tofauti zilizokuwepo baina ya baadhi ya viongozi wa mitaa na wananchi wao.
“ Nilibambikizwa shtaka polisi  la kuchoma nyumba ya waziri wakati hata nyumba yenyewe siifahamu ipo wapi na zaidi ya yote sehemu ya tukio   ni mwendo wa siku nzima sasa nilishirikije na wakati mimi  nilishinda kwenye kibanda changu sokoni hapa ambapo nilishuhudiwa kikiharibiwa na polisi”. Alituelezea mama mmoja ambaye ana kesi ya kuichoma moto nyumba ya waziri Fulani wa Mtwara.
Pia tume ya haki za binadamu ambayo ilifanya ziara wilayani humo kufuatilia ukiukwaji wa haki za binadamu inalaumiwa kwa kuchukua muda mrefu kutoa taarifa ya kasoro zilizojitokeza kwa upande wa serikali katika udhibiti wa vurugu hizo.
 “Vyombo kama tume ya haki za binadamu ndivyo vinavyojenga imani mbele ya jamii na kuisaidia serikali kujikosoa lakini kuchelewa kwa taarifa za tathmini yao kuhusiana na zoezi zima vinafanya tukose imani nacho na kuonekana ni mkono mwingine wa serikali kukusanya taarifa juu wananchi wanasema nini”. Alilalamika mama aliyebambikizwa kesi na polisi.
Dhamana zilizotakiwa kutolewa mahakamani ni kiashiria kingine cha kuwafanya wananchi waliokuwa kwenye tukio hilo wakose haki mbele ya chombo hicho ambapo kesi mojawapo kila mtu alipaswa kudhaminiwa kwa Tshs 107 Milioni taslimu! Hiki ni kiasi kikubwa kwa watu ambao kipato chao ni kidogo.
Viwango hivi ni dhahiri vililenga kuwakatisha tama wananchi katika mchakato mzima wa kupata haki kwa watuhumiwa wa tukio hilo.
Mwanaharakati mmoja anaeleza kuwa kwa ujumla kuna ukandamizaji mkubwa katika suala la tangu ukamataji hadi ufikishaji wa watuhumiwa mahakamani na hata uendeshaji wa mashauri yao na kuomba msaada wa kisheria kwa watuhumiwa.
Vyovyote vile  suala la Mtwara, linahitaji busara na hasa kutoa nafasi watu hawa wakasilizwa. Kuendelea kutumia nguvu za dola na kuwanyamazisha ni kuweka kiporo cha maswali yatakayoulizwa kesho na keshokutwa.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
+255 754 6331 22


0 comments:

Post a Comment