Uhakiki wa Kitabu - ChamaniUHAKIKI WA KITABU: HAKI ZA MADEREVA, ABIRIA NA POLISI BARABARANI.

1.     Rekodi za Kibibliografia.

Jina la kitabu kinachohahikiwa hapa ni Haki za Madereva, Abiria na Polisi Barabarani. , Kimeandikwa na Al-Muswadiku K.Chamani . Mchapishaji wa kitabu hiki ni Tanzania Educational Publishera LTD(TEPU) na amekipatia namba ifuatayo katika sekwensia ya vitabu duniani (ISBN): 978 9987 07 048 0 Kitabu kina kurasa 85 . Na anayekihakiki sasa hivi katika safu hii ni mimi Padri Privatus Karugendo.

II. Utangulizi
 Jina refu la kitabu hiki linastahili liwe “ Haki na Wajibu wa Madereva, Abiria na Polisi Barabarani kwa mujibu wa sheria na kanuni”. Kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu iliyochapishwa na Oxford University Press, maana ya neno dereva ni mwendeshaji wa vyombo vinavyosafiri nchi kavu, kama vile trekta, treni, motokaa, pikipiki na baiskeli; neno abiria lina maana ya mtu anayesafiri kwa chombo chochote cha usafiri na neno polisi lina maana ya askari mwenye dhamana ya kuona kuwa sheria na usalama wa nchi hauvunjwi. Kwa upande mwingine, hakuna mtu mzima ambaye hajawahi kuwa abiria au anayeweza kusema kuwa hatakuwa abiria maishani mwake.

Ili shughuli za usafiri na usafirishaji ziendeshwe kwa usalama, sheria kadhaa zimetungwa kuongoza wadau, na makundi matatu, yaani Madereva, Abiria na Polisi hayaepukiki kukutana. Wajibu wa polisi ni kuhakikisha kuwa sheria hizo zinazingatiwa kwa usalama wa abiria na wadau wengine na wajibu wa madereva ni kuzizingatia.

Katika kufanya kazi hii, baadhi ya polisi wa barabarani na wakubwa wao, hawana sifa nzuri. Wanatuhumiwa na madereva kuwa hudai na kupokea rusha. Lakini, si polisi wote wanabebeshwa tuhuma hii. Hata hivyo, mara nyingi madereva au/na vyombo vyao kweli huwa na makosa. Lakini ni si wote huyakubali. Wao wanadai wameonewa, hata makosa yanapokuwa dhahiri.

Lakini, sheria za usalama barabarani zinasema nini katika kulinda usalama wa madereva, abiria na watumiaji wengine wa barabara? Je, kwa mujibu wa sheria hizo, haki na wajibu wa Madereva, Abiria na Polisi ni upi? Katika kitabu hiki, mwandishi, anayajibu maswali hayo kwa utaalamu na umakini. Katika kurasa zinazofuata nitafanya uhakiki wa kitabu hiki baada ya kukaangalia mazingira yanayokizunguka.III. Mazingira yanayokizunguka kitabu

Tanzania, tuna tatizo kubwa kutofuata sheria. Kwa maneno mengine hatupendi kufuata utaratibu. Unaweza kutaja mambo mengi ambayo mara nyingi watanzania wanapenda njia za mkato. Na kufuata njia za mkato ni chanzo cha rushwa katika taifa.

Lakini kwa hoja iliyo mbele yetu, njia za mkato zinasababisha vifo. Ajali nyingi za vyombo vya usafiri na hasa vyombo vya abiria ni matokeo ya utamaduni wa kutofuata sheria. Vifo vinavyobabishwa na vyombo vya usafiri vinaongezeka siku hadi siku. Wakati polisi wanalaumiwa kuwanyanyasa madereva, kwa upande wao wanajitetea kuzingatia sheria. Bila kuwapendelea polisi, ambao nao kwa upande wao kuna ambao wanatanguliza rushwa na maslahi binafsi kabla ya sheria, kwa kiasi kikubwa madereva wanachochea utamaduni wa rushwa kwa kutaka kukwepa usumbufu wa kusimamishwa muda mrefu na maswali mengi.

Pamoja na ukweli kwamba Tanzania, ina baadhi ya sheria ambazo ni nzuri, lakini watu hawazifuati na kuzitekeleza. Ni wazi kuna baadhi ya sheria ambazo ni kandamizi na zilitungwa wakati wa ukoloni na zinaendelea kuwepo kwa vile zinawalinda viongozi wanaokuwa madarakani, kwa vyovyote vile ili maisha yaende vizuri ni vyema kufuata sheria.

Serikali, mashirika yasiyokuwa ya kiserikali na watu wengine wenye mapenzi mema wamekuwa wakijitahidi kuhimiza utawala wa sheria na watu kufuata sheria. Mwandishi wa kitabu hiki Bwana Al-Muswadiku K Chamani, ni mmoja wao. Ameandika vitabu vingi juu ya sheria mbali mbali katika taifa letu, baadhi ya vitabu hivyo ni: Ufafanuzi wa Sheria ya Kumiliki ardhi vijijini Tanzania, Mwalimu katika Sheria Tanzania, Fahamu kisheria afisa mtendaji wa kata nchini Tanzania, Sheria ya ardhi: Umilikaji na matumizi ya ardhi mkoani Kagera, Haki zangu mbele ya polisi, Haki za mwalimu Tanzania, Ufafanuzi wa sheria ya kumiliki ardhi vijijini Tanzania. Na sasa kitabu hiki cha Haki za Madereva, Abiria na Polisi Barabarani kinaongezeka kwenye orodha ya mwandishi huyu.

Wakati sote tunalalamika kwamba watu hawafuati sheria, na wakati mwingine hata wale wanaofanya kazi serikalini hawafuati sheria, mwandishi amevunja utamaduni huu wa kulalamika, na kuhakikisha anatumia elimu yake ya sheria, kuwafahamisha watu sheria mbali mbali na kuzieleza katika lugha nyepesi, ili kila mtu azifahamu.

Mfano, alipoandika kitabu juu ya Watendaji wa vijiji, watu wengi walifurahi kufahamu wajibu wa watendaji wa vijiji na mipaka yao. Tabia ya watendaji wa vijiji kujifanya Miungu watu, kuwapiga watu na kuwaweka ndani ilipungua sehemu ambazo vitabu hivi vilisambazwa. Ni wazi watendaji ambao walitumia nafasi yao kujipatia fedha na mali kwa kuwanyanyasa na kuwatesa wananchi, hawakukipenda kitabu cha Chamani, hata hivyo ukweli unabaki pale pale kwamba tunahitaji utawala wa sheria.

Huyu ni miongoni mwa watu wachache wanaotumia elimu yao kuwaelimisha watu wengine na hasa kwa kuandika vitabu. Mzee Pius Ngeze, amefanya hivyo kwenye kilimo na kuandika vitabu vingi vya kilimo katika lugha nyepesi. Sasa na Chamani, anafanya hivyo upande wa sheria. Watanzania wakijijengea utamaduni wa kusoma, na kuvisoma vitabu hivi, ni lazima maendeleo ya taifa letu yatakwenda kwa kasi kubwa.

Mwandishi wa kitabu hiki ni wakili wa kujitegemea, aliyezaliwa wilayani Karagwe, mkoani Kagera, mwaka wa 1952. Al-Muswadiku K Chamani, maarufu kwa jina la “Kaka Alli”, alimaliza elimu ya msingi katika shule ya Msingi Katembe iliyoko wilayani Karagwe, mwaka wa 1967 na kujinga na Shule ya Sekondari ya Nyakato, wilayani Bukoba, kuanzia mwaka wa 1968 hadi 1971.

Baada ya hapo, alijiunga na kozi ya ualimu katika Chuo cha Ualimu cha Tabora,mwaka 1972 hadi 1973. Kaka Alli alianza kufundisha mkoani Mara katika shule ya Msingi Kanyega, wilayani Musoma, mwaka 1974 hadi 1977. Alifanya mtihani wa kidato cha sita mwaka 1975 na akafaulu kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam, kuanzia 1977 hadi 1980 alipotunukiwa shahada ya B.A. (Hons).

Aliteuliwa kuwa Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi wilayani Ngara mwaka 1981 na baadaye kuhamishiwa wilayani Biharamulo mwaka 1982. Alijiunga tena na masomo ya Stashahada ya Juu ya Sheria kuanzia mwaka 1983 hadi 1984, katika Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam. Baadaye alijiunga na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, akafaulu kupata shahada ya Sheria (LLB- Hons) mwaka 2004.

Sasa hivi ni wakili wa kujitegemea kwenye mikoa ya Kanda ya Ziwa akiwa katika kampuni ya Mawakili ya Chamani And Company Advocates, makao makuu yakiwa ndani ya Manispaa ya Bukoba, Kagera.

IV. Muhtasari wa Kitabu

Kitabu kimegawanywa kwenye vipengele 50. Vipengele 1 – 8 vinaongelea;
Wajibu wa raia katika kulinda sheria za nchi, wajibu wa Mwanasheria wa Serikali na Kamanda wa Takukuru katika kuhakikisha sheria zinalindwa,
Sheria zinazohusiana na usalama wa magari barabarani, Adhabu bila kushatakiwa,, Kumkamata mtu aliyetenda kosa, Makosa ya taarifa na kuwekwa chini ya ulinzi kwa makosa yasiyoorodheshwa katika kanuni ya taarifa ya makosa.
Ibara ya 26 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,(Sura ya 2 R.E.2002) inampa raia wajibu wa kuhakikisha hifadhi ya Katiba na Sheria za nchi” (Uk 1).

“Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye ni mteule wa Rais, madaraka yake yanaonyeshwa katika Ibara ya 59 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwa ni mshauri wa serikali juu ya mambo ya sheria na kutekeleza shughuli zozote zenye asili au zinazohusiana na sheria zitakazopelekwa ofisini kwake au atakapoagizwa na Rais kuzitekeleza na kutekeleza shughuli nyingine zilizokabidhiwa kwake na Katiba hii au sheria yoyote” (Uk2)

“Sheria zinazohusu usalama barabarani ambazo ni muhimu zaidi ni ni: Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya jinai,  Sheria ya Usalama Barabarani (sura ya 168 R.E. 2002), Sheria ya Leseni za Usafirishaji (Sura ya 317 R.E. 2002), Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Sheria ya Moto na Jeshi la Uokoaji ( Sheria namba 14 ya mwaka 2007) na Sheria ya Mamlaka ya usafirishaji wa Nchi kavu na majini (Sura ya 413 R.E. 2002)” (Uk 4).

“Fungu la 110 la Sheria ya Usalama Barabarani (Sura ya 168 R.E. 2002) limeonyesha kosa ambalo likitendeka, basi, Ofisa wa Polisi atakuwa na madaraka ya kumkamata mtuhumiwa” (Uk 11).

Vipengele kuanzia cha 9 hadi 25, vinajadili juu ya; Madaraka ya  polisi kusimamisha gari, kupekua na kuzuia gari, Umuhimu wa Ofisa wa Polisi kufuata sheria, Tafsiri ya “Sababu za maana”, Watoza ushuru wa maegesho kukamata gari na kuyafunga minyororo, Utaratibu wa kupinga Sheria ndogo inayokinzana na Sheria andishi, Kuwa na leseni wakati wa kuendesha gari, Mtuhumiwa kutoroka, Bima ya gari, Stika ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani, Leseni ya barabara na Stika ya Zimamoto, Kutoa kibao cha usajili wa gari na kunyang’anywa leseni, Muda wa kulipa faini baada ya ilani ya kosa kutolewa, Matumizi ya pikipiki kibiashara, Utaratibu wa kufuta leseni, Makosa ya pikipiki ya biashara, Nani hulipisha faini za pikipiki za biashara, Muda na kiwango cha kulipa faini ya pikipiki ya biashara, Nauli ya abiria na Kuweka petroli wakati gari lina abiria.

“ Madaraka ya Polisi kusimamisha, kupekua na kuzuia gari lisiendelee na shughuli zake yapo katika fungu la 25 la sheria  ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (Sura ya 20 R.E. 2002)” (Uk 14).

“Mtu yeyote kwa makusudi anayetumia vibaya nafasi yake katika kufanya au kushindwa kufanya tendo kwa kukiuka sheria, wakati akitekeleza wajibu, atakuwa ametenda kosa..” (Uk 23).

“Iwapo itaonekana ( kuwa mtu huyo) hakuamini kuwa  (Mtu aliyetuhumiwa) alikuwa katenda kosa, basi, hakuna “sababu ya maana” kwa upande wake na hawezi kusikilizwa kwa kusema hali halisi ambayo ilikuwa haifahamiki kwake ingeweza kumfanya mtuhumiwa kuwa na kosa” (Uk 24).

Juu ya matumizi ya Pikipiki kibiashara tunaambiwa na mwandishi kwamba:
“ Kanuni za Lezeni za Usafirishaji (Pikipiki na Pikipiki yenye magurudumu matatu) za mwaka 2010, zilizotolewa katika Gazeti la Serikali 144 ya mwaka 2010, imeruhusu pikipiki kutumiwa katika shughuli ya biashara ya kusafirisha abiria kwa mashati yafuatayo:
- Kuwa na leseni halali ya huduma ya barabara inayotolewa na mamlaka ya serikali za Mitaa inayohusika, vinginevyo ukiendesha pikipiki bila leseni hii utakuwa umetenda kosa na ukitiwa hatiani utatozwa faini isiyopungua shilingi elfu hamsini au kifungo kisichopungua miezi sita wala kuzidi mwaka mmoja au vyote kwa pamoja.
- Leseni hii, itatolewa kwa mwombaji mwenye pikipiki inayofaa kufanyiwa biashara hii.
- Mwombaji awe na umri zaidi ya miaka kumi na nane
- Mwombaji atapaswa kulipa ada, faini na gharama nyinginezo kwa SUMATRA kupitia mamlaka ya Serikali za Mitaa ili kuweza kupata leseni hiyo” ( UK39)

Juu ya  utaratibu wa kufuta leseni, tunaambiwa kwamba: “Kanuni ya 19 ya Kanuni za Leseni za Usafirishaji (Pikipiki na Pikipiki za Magurudumu matatu) za mwaka 2010 inaonyesha utaratibu utakaotumiwa katika kufuta leseni hiyo iwapo atakiuka masharti yaliyotolewa” ( Uk 41).

Vipengele vya 26 mpaka 40, vinajadili juu ya: Taarifa ya kito cha kushukia, Gari likiharibika, abiria hurudishiwa nauli?, Ukaguzi wa gari kwa kuwekwa chini ya ulinzi, Madaraka ya Ofisa wa Polisi Mkaguzi kukagua gari la abiria, Wafanyakazi wa gari la abiria, Wajibu wa abiria, Uzito wa mizigo ya abiria, Kulipia tiketi mapema na kusitisha safari, Nauli ya mtoto na mwanafunzi, Kiwango cha nauli, Kutotoa huduma ya usafiri kwa muda uliopangwa, Kosa la kutotoa tiketi ya nauli, Abiria kushindwa kulipa nauli nakuteremshwa.

Juu ya taarifa ya kituo cha kushukia, tunasikia kwamba: “ Anayefanya huduma ya gari ya kusafirisha abiria atapaswa ahakikishe anawatangazia kituo kinachofuata” (Uk 48) na hii ni kwa mujibu wa “ Kanuni ya 103 ya Kanuni za SUMATRA (Usalama wa Kiufundi na kiwango cha huduma (Magari ya abiria) za mwaka 2008. Hivyo ni lazima kituo cha kushukia kitangazwe, ingawa mara nyingi hawafanyi hivyo, ni vizuri kupitia kitabu hiki abiria wakatambua haki zao ambazo mara nyingi zinakiukwa.

Je Gari likiharibika, abiria hurudishiwa na nauli? Kanu ya 11 ya Kanuni za SUMATRA(Usalama wa Kiufundi na Kiwango cha huduma) (Magari ya abiria) za mwaka 2008, inaonyesha kuwa; “ Iwapo gari lililoharibika linafanya shughuli zake katika maneno ya mji, basi, mwenye gari atapaswa atoe usafiri mwingine ndani ya dakika kuma na tano au arudishe kiasi cha nauli ambacho kitamalizia sehemu ya safari iliyobakia kwa kila abiria. Kama gari hilo linafanya safari za nje ya mji, basi mwenye gari atapaswa alitengeneze  na kuendelea na safari ndani ya muda wa saa mbili au atoe usafiri mwingine ndani ya saa mbili...... Kutokana na msimamo wa kisheria ni kuwa, iwapo gari la abiria limeharibika, basi, unazo haki zako na utapaswa utendewe kwa mujibu wa sheria” ( Uk 49)

Ni abiria wangapi wanatendewa hivyo? Au ni abiria wangapi wanafahamu kwamba sheria inawalinda na gari likiharibika ni lazima sheria ifuate mkondo wake?

Vipengele vya 41 mpaka 50, vinajadili juu ya: Vizuizi barabarani, Vizuizi kwa ajili ya kutoza ushuru, Kuzuia polisi kufanya wajibu wake, Polisi kufunguliwa madai akiwa kazini, Kutovaa helmeti ni kosa? Kukamatwa, kushtakiwa na udhamini wa mahakamani, Pikipiki za polisi barabarani, Majedwali, marejeo na mwisho kabisa ni wasifu wa mwandishi wa kitabu hiki.

Kwa kifupi kitabu hiki kinalenga kusaidia kupunguza ufa wa ushirikiano uliopo kati ya madereva na wa vyombo vya usafiri vinavyotumia barabara, abiria na Jeshi la polisi. Wananchi wakifahamu madaraka na wajibu wa polisi inakuwa rahisi kushirikiana nao badala ya kuwaona kama maadui wake.

Mada zilizogusiwa humu zinahusu zaidi Haki na Wajibu wa madereva wa polisi wakiwa barabarani; utaratibu wa kumaliza makosa yaliyotendwa na dereva wa chombo  cha usafiri; ukamataji wa dereva na chombo chake; amri ya kulipeleka Kituo cha Polisi na magari ya abiria, pikipiki za biashara, baiskeli na masharti yake.V. Tathmini ya Kitabu

Baada ya kuona muhtasari huu sasa tufanye tathimini ya kazi hii aliyoifanya Bwana Al-Muswadiku K Chamani.

Awali ya yote lazima niseme kwamba, kwa kuangalia hadhira anayoikusudia mwandishi, kitabu kinasisimua, kinafundisha na kinafikirisha kutokana na mtindo alioutumia mwandishi.  Ametumia mtindo wa Maswali na Majibu kuwasilisha ujumbe kwa msomaji, huku akinukuu vifungu vya sheria kwa makusudi ya kuweka msisitizo na kufanya wepesi wa marejeo kwani sheria zilizo nyingi hazipatikani kwa wadau.

Pili,  mwandishi kwa kutumia vitabu vyake hivi vya sheria mbali mbali katika jamii yetu anatufumbua macho na kutuaminisha kwamba utawala wa sheria unapofuatwa, basi, haki na amani vitakuwapo kwa manufaa ya maendeleo.

Tatu, kama nilivyodokeza kwenye utangulizi, mwandishi huyu anajiunga na waandishi wengine ambao baada ya kusoma kuihitimu wanaitumia elimu yao kuwaelimisha wengine ambao hawakupata bahati ya kufikia hatua hiyo ya elimu. Si kila Mtanzania anapata nafasi kusomea Sheria, hivyo kwa kutumia kitabu hiki, hata yule ambaye hakusomea sheria anaweza kutetea haki zake.

Nne, kitabu hiki kinakuja wakati wake, ambapo magari yakiharibika abiria wanajijua. Ni wachache wanaofahamu haki zao. Sasa wakisoma kitabu hiki, na kufahamu haki zao, kufahamu kwamba Gari, likiharibika ni lazima mwenye Gari kuhakikisha abiria hao wanaendelea na safari wenye vyombo vya usafiri wa abiria wataacha kiburi chao na vitendo vya kuwanyanyasa abiria. Tunaweza kuanza kushuhudia mabadiliko makubwa katika usafirishaji wa abiria. Uzuri wa kitabu hiki kinaelezea vizuri haki na wajibu wa kila mdau. Ni kwamba kinasisitiza kufuata sheria ili mahusiano ya polisi, madereva na abiria yawe mazuri.

Tano, kitabu hiki ni msaada kwa wadau wote, madereva, abiria na polisi. Kuna wakati polisi anawakamata madereva, kwa uonevu tu au kwa utamaduni wa kutaka rushwa na hasa sikukuu kubwa za kidini na kufunga na kufungua mwaka zinapokaribia, lakini kwa vile madereva hawafahamu haki zao, wanakubali kunyanyaswa na kutoa fedha. Hivyo madereva wakisoma kitabu hiki watafumbuka macho na kuanza kuzitetea haki zao.

Sita, kwa upande wa mijini  na hasa mikubwa kama vile Dar-es-Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya na mingine, ambako karibia kila siku ya Mungu, kila mtu anapanda magari ya abiria, kitabu hiki kitakuwa msaada mkubwa.

Saba, kwa vile sasa hivi tuko kwenye siasa za vyama vingi, ufahamu wa sheria ni muhimu sana. Ule upendeleo wa wazi, kwa watu wanaokiunga mkono chama tawala, kiasi hata cha kuvunja sheria zote hata na zile za barabarani utakwisha! Sheria haina vyama, sheria haina dini na sheria haina kabila. Hivyo kitabu hiki kitawasaidia wengi na uonevu wa ovyo utapungua.

VI. Hitimisho

Kwa kuhitimisha, nawaomba watanzania kukitafuta kitabu hiki na kukisoma.  Kusema kweli ni kitabu cha msaada kwa wale wanaosafiri mara nyingi na vyombo vya abiria. Pia ni muhimu kwa polisi nao kukisoma kitabu hiki ili kupunguza mapambano yasiyokuwa ya lazima katika ya polisi na madereva.

Lakini pia ni muhimu kuvitafuta vitabu vingine vya Al- Muswadiku Chamani na kuvisoma, maana vyote vinaelezea utawala wa sheria.

Mwisho kabisa, nampongeza Bwana Al-Muswadiku Chamani kwa kujitoa kuandika vitabu vya sheria ili kuwasaidia watu wengi ambao wananyanyaswa na kupokwa haki zao kwa vile hawana utaalamu wa sheria. Vitabu vyake vimekuwa msaada mkubwa kwa watu wa vijijini na hasa vitabu vyake vinavyohusu sheria za Ardhi na watendaji wa vijiji.

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment