GRACE AIKAELI MBOWE

MWANA MAMA MAREHEMU GRACE AIKAELI MBOWE

Mungu ailaze mahali pema peponi roho ya Marehemu Grace Aikaeli Mbowe! Pia Mungu awafute machozi watoto wake, mme wake na ndugu na jamaa wote! Siandiki tanzia hii kwa vile Grace, alikuwa dada wa rafiki yangu Mheshimiwa Freeman, wala siandiki tanzia hii kwa vile marehemu alikuwa ni dada wa Mwenyekiti wa Chadema, na wala siadiki tanzia hii kwa vile Grace, alizikwa na Askofu na viongozi wa Serikali na vyama siasa.
Na wala siandiki tanzia kumsifia dada Grace, kuwa ni mtu mwema, mwenye huruma, mwenye upendo, mvumilivu na mnyenyekevu, maana kila mtu akifikia hatua hiyo ya kulala milele, hizo ndizo sifa zinazomsindikiza. Labda mchawi! Lakini katika hali ya kawaida; unyenyekevu, upendo, uvumilivu na huruma, ni sifa za kila binadamu anapoiacha dunia yetu na kujiunga na muumba wake.
Na wala sina lengo la kumpamba Grace kwa sifa nyingi, maana mimi ni nani? Mwenye uwezo wa kumsifu ni Muumba wake aliye Mbinguni. Hata hivyo ni imani yangu kwamba sifa zake zimeimbwa na wanasiasa ambao wameteka nyara wasifu wa marehemu na kuugeuza kuwa mtaji wa siasa zao.
Hata hivyo siwezi kuukataa ukweli kwamba ninalia na wanaolia na kusikitika na wanaosikitika. Msiba wa ndugu yako ni msiba wako pia, msiba wa rafiki yako ni msiba wako pia. Pamoja na kwamba natafuta maneno ya kuwatuliza wafiwa na kuonyesha kushiriki msiba huu, halikuwa lengo langu kubwa:
Naandika tanzia hii kuendeleza kusudio la kuanzisha safu hii ya Mwana Mama. Hii ni nafasi ya kuandika Mwana mama ambaye ametoa mchango mkubwa katika taifa letu, lakini hasikiki na wala hakuna kilichoandikwa juu yake. Na  marehemu Grace, ni miongoni mwa akina mama hao.
Ni bahati mbaya kwamba dada yetu Grace, amesindikizwa na malumbano ya kisiasa! Vyombo vyote vya habari, mitandao ya kijamii, imeamua kuweka pembeni mchango wake katika taifa letu na kuelekekeza nguvu zote kwenye siasa. Ni jambo la kusikitisha sana kwamba Tanzania tunapoteza mwelekeo na uandishi wetu umekuwa ni  wa kuongozwa na kuelekezwa na wanasiasa.
Chadema na CCM, ni vyama vya siasa ambavyo vimetekea nyara wasifu wa dada yetu Grace. Badala ya kutuelezea mchango wake katika maisha yake ya miaka hamsini kasoro, tunaletewa siasa na mambo mengi ya kuzusha kwa faida ya siasa na wanasiasa.
Grace alifariki katika ajali ya gari  katika eneo la Kabuku, Wilaya ya Handeni, mkoani Tanga wakati akielekea jijini Dar es Salaam. Watu wengine walipoteza uhai katika ajali hiyo. Hivyo  ni kifo kama vifo vingine.
Bahati mbaya hadi sasa hivi hakuna anayetwambia kwamba dada yetu Grace alikuwa mwanamke wa pili kusajiliwa na bodi ya wahandisi nchini akiwa kama Ofisa mpimaji (Quantity Surveyer) baada ya kuhitimu elimu ya juu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kitengo ardhi (ARU).
Hii ni sifa kubwa kwa marehemu. Ni wazi kwa ujuzi huo na kisomo chake ametoa mchango mkubwa katika taifa letu. Hapana shaka kwamba kwa kifo chake, pengo kubwa limetokea katika fani yake ya uhandisi. Haya ndiyo tunataka tuyasikie, na haya ndiyo yanatusukuma kuandika tanzia hii, ili kumlilia huyu dada yetu ambaye kifo kimemchukua mapema.
Kuiacha sifa hii kubwa na kuendeleza nyimbo za siasa, ni kumkosea haki marehemu. Kila binadamu ana uhuru wa kufanya mambo yake binafsi. Suala la mapenzi ya siasa ni suala la mtu binafsi, lakini huduma kwa jamii, kama hii ya(Quantity Surveyer) ambayo dada yetu alikuwa amesomea, si suala binafsi. Hili ni suala la kijamii na ni suala la kitaifa. Kwa kujenga sifa ya mtu ndani ya jamii, masuala ya kijamii yanashika nafasi ya kwanza mbele ya masuala ya binafsi. Hata kama Grace, alihama chama cha Chadema, chama ambacho kaka yake ni Mwenyekiti, hili ni suala binafsi ambalo si muhimu sana ukilinganisha na mchango wa dada Grace katika jamii kubwa ya watanzania.
Kama Grace, alifika chuo kikuu na kusoma masomo hayo ya sayansi, ni wazi huko nyuma alifanya vizuri. Tunataka tusikie wasifu wake katika shule za sekondari. Tungependa kusikia na kufahamu alikuwa ni mtoto wa namna gani wakati akisoma. Huo ndio wasifu wa Grace na wala si huu wa Chadema na CCM.
Nina imani kuna mambo mengine mengi aliyoyatenda dada Grace, zaidi ya haya ya Chadema na CCM. Hivyo ninategemea, baada ya wasifu huu wa uchokozi, wengine watajitokeza na kutuimbia wasifu chanya wa dada yetu.
Mpaka mazishi yake yakaongozwa na Askofu, ina maana huyu alikuwa mtu wa sala, alikuwa mtu wa kanisa. Tusikie wasifu wake wa kumpenda Mungu wake na watu wake. Huu ndiyo wasifu  wa dada yetu Grace na wala si huu wasifu wa CCM na Chadema.
Dada Grace alikuwa na watoto. Huyu alikuwa mama wa namna gani? Tunataka kusikia watoto wake wakiimba wasifu wake. Lakini vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, imewanyamazisha watoto wa marehemu na kuteka nyara wasifu wa mama yao mpenzi.
Grace, ni mtu aliyesimama kama mtu, kama mama wa familia. Kuunganisha wasifu wake na wa ndugu zake, ni kumkosea haki kama binadamu. Hata hivyo kama nilivyodokeza hapo juu, huyu ni mama mhandisi, kuna mengi ya kuandika juu yake na kumbukuka zaidi ya kumeza wasifu wake makusudi mazima.
Pia, watanzania tujifunze kuandika na kuheshimu wasifu wa watu. Tusichanganye wasifu na vitu vingine ambavyo vinakuja na kupita. Daima wasifu wa mtu ni vitu vile visivyopita! Ni  mchango wa marehemu katika jamii husika; na mara nyingi tunafikiria mchango chanya!
Mungu amlaze mahali pema dada yetu mpendwa Grace Aikaeli Mbowe.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
+255 754 633122

0 comments:

Post a Comment