GESI HAITOKI

GESI HAITOKI! IKITOKA ITABADILIKA KUWA MAJI: KINJEKITILE NAMBA 2

Ikumbukwe awali lilishatolewa tamko kutoka Msimbati kwa bibi Samoe Mtiti (106) kuwa ikiwa serikali itaendelea kulazimisha mchakato wa gesi bila kusikiliza hoja za wananchi angegeuza gesi kuwa maji, hatua ambayo ililazimu mbinu mbalimbali za kumshawishi bi Samoe zifanyike ili hali hiyo isijitokeze. Wakazi wa Mtwara, wanaamini nguvu za  Bibi Mtiti, kwamba ana uwezo wa kubadili gesi kuwa maji, na akitaka gesi isitoke, haiwezi kutoka!
Ni yale yale ya Kinjekitile, ya kubadilisha risasi kuwa maji. Kwa haraka na kwa tabia ya kuangalia mambo juu juu unaweza kusema kwamba huu ni upuuzi. Lakini hapa kuna kitu cha kujifunza. Ule muujiza wa Kinjekitile, wa kugeuza risasi kuwa maji uliwapatia wapiganaji hamasa na nguvu za kupambana na wavamizi. Hata kama walishindwa, walikufa kwa heshima kubwa wa kipambana na silaha za kisasa kutetea nchi yao. Historia inawatambua na kuwaheshimu. Hivyo si lazima miujiza hii iwe upuuzi wakati wote.
Kuna habari za kuaminika kwamba Januari 24, 2013 gari lenye namba za usajili T609 BXG la mtu mmoja anayedhaniwa kuwa ni ofisa wa idara nyeti liliteketezwa kwa moto na wananchi wa Msimbati kwa kile kinachoelezwa kuwa lilifika kumteka bi Somoe ambaye kijijini hapo anajulikana kama mkuu wa kaya. Wako tayari kumlinda bibi huyu kwa gharama yoyote ile, kwa vile wanaamini ana nguvu za kutenda miujiza.
Imani hii kwa Bibi Samoe Mtiti, inaonyesha wazi jinsi suala zima la Gesi, halijaelezwa vizuri. Watu hawana elimu juu ya Gesi na matumizi yake. Kama bado wanaamini Gesi inaweza kubadilika kwa nguvu za miujiza ikawa maji, bado kuna kazi kubwa. Serikali ina wajibu mkubwa wa kuwaelimisha watu wa Mtwara. Kutumia jeshi kuwapiga na kuwanyamazisha si njia sahihi ya kuleta mabadiliko na maendeleo. Kinachohitajika ni kuwasikiliza, kujadiliana nao, kuwashirikisha na kuwaelimisha.
Vinginevyo watasimama kidete na miujiza ya Bibi Samoe Mtiti, itawatia hamasa kupigania haki yao na kukubali kufa, ili historia isiwacheke baadaye. Kama nilivyosema hapo juu si lazima miujiza iwe upuuzi wakati wote. Ni wazi hakuna muujiza wa kuibadilisha gesi kuwa maji na wala risasi kugeuka na kuwa maji. Lakini muujiza wa kubadilisha akili za mtu, akaacha kufikiri na kutenda kama wanyama wengine upo; tunashuhudia vitendo vya kujitoa muhanga kwa matumaini kwamba kule “Mbinguni” watakuta maisha mazuri na dhawabu kubwa.
Hivyo kiongozi yeyote mwenye busara, anaposhughulika na watu wenye Imani aina ya Bibi Samoe Mtiti, ni lazima awe makini kutotumia nguvu. Maana imani ikikolea, mtu anaacha kufikiri na kuyaweka maamuzi yake mikononi mwa watu wengine. Wanachosema anafuata kwa kuogopa kuambiwa hana imani! Au kuambiwa yeye ni msaliti! Ni vigumu kupambana na mtu wa namna hii, hata kama serikali ina nguvu za kutisha.
Mzee, aliyetuelezea habari hizi za Bibi Samoe Mtiti, wakati tukifanya utafiti juu ya vurugu za Mtwara, alikuwa  akijaribu kutufafanulia umuhimu wa ushirikishwaji. Kwamba serikali haikuzingatia hili, na watu wa Mtwara hawakushirikishwa juu ya uchimbaji wa gesi, kwani raslimali gesi sasa inazungumzwa kama bidhaa haramu kama ilivyo bangi kwenye vyombo vya dola! Ukitamka suala la gesi kwa wanamtwara wanakuona kama vile umetumwa kuwadodosa ili uwachomee utambi kwenye jeshi na hatimaye wapelekwe Gwantanamo kuteswa; hiki ni kituo cha Jeshi cha Nalyendele, ambacho kimebatizwa jina la Gwantanamo, kutokana na vitendo vya mateso vinavyoendelea kwenye kituo hicho.
Kwa maoni ya mzee huyo ni kwamba kwa namna yoyote ile ridhaa ya wananchi katika utekelezaji wa miradi inayolenga kutumia raslimali iliyolindwa kwa miongo kadhaa na vizazi vya jamii ya eneo ambapo mradi unakusudiwa kutekelezwa ni muhimu na vyema kuheshimiwa ili kuhakikisha kwamba laana za vizazi hivyo hazijengwi katika kizazi kinachofuata ndivyo imani za asili zinavyotambuliwa.
Wananchi wanaolizungumzia suala la gesi  kwa tahadhari wanatamka bayana kuwa vyombo vya  usalama  vinavyoshughulikia ukusanyaji wa taarifa havikujipa kazi ngumu kujua hasa kwa nini wananchi wanashinikiza  gesi haitoki bila kujali imani, vyama na hali zao. Hili lilichukuliwa kama ajenda ya kisiasa na watoa taarifa ngazi za juu na ndiyo sababu katika mazungumzo ya viongozi wa ngazi ya kitaifa wanaliona kama lilikuwa la kisiasa kumbe hii ni ajenda ya wana-Mtwara imezingatia zaidi maslahi na ustawi wa wana Mtwara na ni matokeo ya maumivu ya muda mrefu kucheleweshwa kwenye safari ya kufikia maendeleo ya kweli.
Hivyo maamuzi ya matumizi ya nguvu ndiyo yakachochea zaidi ufa wa mahusiano baina ya serikali na wananchi  hadi sasa ambapo kama mtu anafanya utafiti atabaini kuwa kati ya watu kumi unaokutana nao ni nadra kukutana na mtu anayesifia matunda tarajiwa ya miradi ya gesi kwa Mkoa wa Mtwara huku wengi zaidi wakilaumu mazingira ya utekelezaji mradi huo.
Matumizi ya nguvu kubwa za dola katika masuala yanayohitaji utashi wa watu ni kiashiria kuwa kuna pengo la mahusiano baina ya serikali na wananchi na hivyo kuhitaji chombo kingine kuunganisha makundi yanayotofautiana.
Wananchi wa Mtwara wanasema ukimya uliopo sasa si kwamba ni utulivu na amani bali ni utulivu pasipo amani, na wananchi wanafanya hivi kupisha udhalilishaji na manyanyaso ya matumizi makubwa ya nguvu za dola.
Kimsingi tangu kutolewa agizo la kutoitishwa mikutano ya wazi inayojumuisha watu kwenye maeneo ya wazi, Mtwara imekuwa kisiwa kwa muda sasa kutokana na wananchi kutopata fursa ya kukutanika kujadili maendeleo ya mkoa wao.
Hivi sasa  msimu wa korosho umeanza lakini hawawezi kukubaliwa kuitisha mikutano ya kujadiliana juu ya maslahi ya wakulima wa korosho kutokana na agizo hilo na kwamba ukifanya mkusanyiko wowote utakuwa umevunja amri halali ya serikali.
Utekelezaji wa kamata kamata ya watuhumiwa wa vurugu za Mei 23 ulioendeshwa kwa usiri mkubwa na nyakati za usiku kwa kutumia wanajeshi, umetajwa pia kufanywa kwa uonevu mkubwa  kwa sababu hata wale  ambao hawakuwepo mazingira ya tukio kubebwa kwa chuki na tofauti zilizokuwepo baina ya baadhi ya viongozi wa mitaa na wananchi wao.
Kwa ujumla kuna ukandamizaji mkubwa katika suala la tangu ukamataji hadi ufikishaji wa watuhumiwa mahakamani na hata uendeshaji wa mashauri yao na kuomba msaada wa kisheria kwa watuhumiwa. Dhamana zilizotakiwa kutolewa mahakamani ni kiashiria kingine cha kuwafanya wananchi waliokuwa kwenye tukio hilo wakose haki mbele ya chombo hicho ambapo kesi mojawapo kila mtu alipaswa kudhaminiwa kwa Tshs 107 Milioni taslimu! Hiki ni kiasi kikubwa kwa watu ambao kipato chao ni kidogo.
Viwango hivi ni dhahiri vililenga kuwakatisha tama wananchi katika mchakato mzima wa kupata haki kwa watuhumiwa wa tukio hilo.
Kulingana na maelezo ya wananchi, kwa sasa chombo kinachopewa nafasi katika kuunganisha mahusiano baina ya wananchi na mamlaka ya serikali ni mijadala ya pamoja ikihusisha asasi za kiraia ili kurejesha mawasiliano na kuaminiana ambako kumetoweka.
Na,                                                        
Padri Privatus Karugendo

0 comments:

Post a Comment