LINE ZA SIMU

KODI YA LINE ZA SIMU NI MAISHA BORA KWA KILA MTANZANIA?
 
Wakati bei ya muda wa maongezi iko  juu na yenye utata; na hili si kwa Vodacom peke yake bali ni kwa mitandao yote ya simu; wakati tunashangaa na kulalamika ni kwa nini wawakilishi wetu Bungeni, wasilione hili na kuhakikisha bei ya muda wa maongezi inakuwa na unafuu ili tuweze kufikia kile kinachoitwa maisha bora kwa kila Mtanzania tunaongezewa na hii kodi ya line za simu. Pamoja na faida kubwa itakayotokana na kodi hii (kama tulivyoelezwa, ambavyo si tofauti sana na yale tunayoelezwa kila mwaka bila kuona utekelezaji) bado huu ni mzigo mkubwa kwa mtu anayeitumia simu yake kwa matumizi ya lazima na muhimu.
 
 Binafsi nina mashaka na uwiano wa fedha na muda. Kwamba ninapolipa shilingi elfu moja ni mfumo gani unatumika kuhakikisha kwamba muda nilioutumia thamani yake ni shilingi elfu moja. Kuna mfumo gani wa wazi wa kuhakikisha fedha tunazolipa kwa kununua vocha za muda wa maongezi zinawiana na muda; mfano kama ni elfu moja kwa daika tatu ikajulikana, ikiwa kinyume mtu akalalamika  Pia na uwiano wa kodi na matumizi ya line ya simu; kwamba anayetumia simu kuzalisha milioni moja kwa mwezi, alipe kodi ya shilingi elfu moja na yule anayezalisha elfu kumi kwa mwezi alipe kodi ya line ya simu shilingi elfu moja na anayebeep akapigiwa alipe kodi ya elfu moja kwa mwezi! Tumelishwa kasumba na makampuni haya ya simu (Sawa na madawa ya kulevya) kwamba fedha zikiisha kwenye simu ni lazima utakwenda mwenyewe kununua. Hatulalamiki ili kutaka kujua uwiano wa fedha na muda. Kama mtandao una wateja milioni mmoja, hata ukigonga shilingi miambili kwa kila mteja, unakuwa una fedha nyingi. Inajionyesha wazi kwamba Vodacom, na mitandao mingine ya simu wanatengeneza faida kuliko kutoa huduma. Hii ni sawa kwa vile wao wanafanya biashara. Basi, biashara yao iwe nzuri kwa kutoa huduma iliyo juu ya kiwango na si chini  ya kiwango. Na biashara yao iwe na uwiano wa fedha na muda. Lakini pia kwa vile kodi ya line za simu imeanza, kuwepo uwiano kati ya matumizi ya simu  na ulipaji kodi.
 
Kwa mitambo ya kisasa, makampuni ya simu yanaweza kujua ni watu gani wanatumia huduma yao kutengeneza faida kubwa na ni watu gani wanatumia mitandao yao kwa huduma ya lazima kama kutoa taarifa za misiba, kutuma karo na matumizi mengine madogo madogo. Mfano, wale wanaotumia huduma ya Mpesa, wale wanaopitishia zaidi ya milioni kumi kwenye mtandao kwa mwezi, watalipa je kodi ya elfu moja sawa sawa na anayepitisha elfu hamsini kwa mwezi?
 
Wakati baadhi yetu tunajiuliza mantiki ya serikali inayoamini kwenye kauli mbiu ya Maisha bora kwa kila Mtanzania, kukubali viwango vya muda wa maongezi kuwa sawa kwa watanzania wote; maskini wa vijijini, wafanyakazi na wafanyabiashara  wakubwa, bado tunaletewa na  kodi hii ya line za simu iliyo sawa kwa watanzania wote. Katika hali ya kawaida na kwa nchi ambayo bado katiba yake inatambua na kufuata Ujamaa, mkulima wa kijijini anayetumia simu yake kuita gari la  wagonjwa kumbemba mama mjamzito, atalipa muda wa maongezi sawa na mfanyabiashara anayetumia simu yake kufanya “Dili” la bilioni tano? Au mkulima wa vijijini anayetumia simu kusambaza ujumbe wa msiba kwa ndugu na jamaa, atalipa muda wa maongezi sawa sawa na mfanyabiashara anayetumia simu yake kusambaza ujumbe wa kudai madeni yake kwa wateja wake zaidi ya bilioni kumi?
 
Kwa wengine mawasiliano ya simu ni anasa, wengine ni biashara na walio wengine ni huduma ya muhimu. Kuna wanaotumia simu kutongoza wanawake na kuzungumza mambo ya mapenzi siku nzima, hawa wakilipishwa kodi ya line za simu ni sawa, kuna wanaotumia simu kufanya biashara na kuwasiliana na wateja, hawa nao wakilipishwa kodi ya line za simu ni sawa, lakini  wale wanaotumia simu kama huduma muhimu kwenye jamii kuwatoza kodi ya line za simu si sawa sawa. Mfano mtu anayenunua simu ya kiganjani kwa bei ya shilingi milioni moja, na wakati mwingine anazo zaidi ya tano za bei hiyo hiyo, maana kila mtandao una simu yake, atalipaje kodi ya line za simu na muda wa maongezi sawa sawa na mtu anayenunua simu ya kiganjani kwa bei ya shilingi hamsini?
 
Kiasi kikubwa cha watu wa vijijini wenye watoto wao wanaoishi na kufanya kazi mijini, wanakuwa na simu ambazo mara nyingi hawana uwezo wa kununua muda wa maongezi, wanachofanya ni “Kubeep”, wasipotumiwa muda wa maongezi basi wanapigiwa simu na watoto wao. Leo hii hawa kuwatoza kodi ya line za simu ni kuwalazimisha kuachana na huduma hii muhimu.
 
Wakati tunategemea serikali iwe upande wa wananchi na kuwalinda dhidi ya makampuni makubwa ya uwekezaji, tunashuhudia kinyume chake. Makampuni ya simu kama yalivyo makampuni mengine yapo hapa kufanya biashara na kuendelea kuwapumbaza wananchi:
 
 
Tarehe 27 Januari Alhamisi mwaka 2005 vyombo vya habari vilitoa habari inayosema: " Vodacom yawaangukia wateja wake - KAMPUNI ya simu za  mkononi Vodacom imetoa maelezo yaliyosababisha hitilafu na kukatika kwa mawasiliano katika mtandao wake uliosambaa nchini kote Ijumaa iliyopita..... Tunawaomba radhi wateja wetu wapendwa kwa usumbufu uliotokea na hasa katika kipindi cha sikukuu na tunapenda kuwafahamisha wateja wetu kuwa tatizo limerekebishwa na huduma za Vodacom zitaendelea kama kawaida....Taarifa ilimkariri Jose dos Santos, Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom, akisema kama ishara ya kuonyesha masikitiko na nia njema, wateja wote wa Vodacom watapewa SMS 10 za bure kwa mkupuo kuanzia Januari 27,2005".
 
Wateja wa Vodacom, walifurahia meseji za bure. Kama kawaida yetu watanzania hatupendi kutafakari na kuyaangalia mambo kwa undani. Ofa hii inaweza kumfumba mtu macho akaacha kuona mambo mengine muhimu. Na kwa vile Vodacom, hawana mfumo wa kutoa maoni na kujadiliana na wateja wao, furaha hii ya meseji ilibaki kuwa furaha ya mtu mmoja mmoja au vikundi. Ukweli ni kwamba jambo hili linaigusa jamii nzima maana mtadao wa Vodacom umeenea nchi nzima. Na jambo la mawasiliano linamgusa kila mwananchi. Mtwara hadi Karagwe, Kigoma hadi Arusha, wanaguswa na mafanikio au matatizo ya Vodacom. Mawasiliano si anasa, ni kitu muhimu na cha lazima katika jamii yoyote ile.
 
Mbali na na sms za bure, makampuni haya ya simu yamekuwa yakitoa misaada ya madawati na vitu vingine vidogo vidogo vya kuwapumbaza watanzania na kuwafumba macho, lakini ukweli ni kwamba makampuni haya yanapata faidi kubwa. Kufuatana ukweli huo, serikali iliyo makini ingetengeneza mfumo wa viwango tofauti vya bei ya muda wa maongezi; watu wanaozitumia simu kwa anasa, wawe na viwango vyao, watu wanaozitumia simu zao kwa biashara wawe na viwango vyao na watu wanaotumia simu kwa matumizi ya lazima na muhimu wa wawe na viwango vyao. Na kwa mantiki hiyo hiyo basi hizi kodi za line za simu zitolewe na makampuni yenyewe, hata hivyo yanakuwa yamevuna vyakutosha. Kwa mfumo huu, tunaweza kuimba wimbo wetu wa maisha bora kwa kila Mtanzania, vinginevyo ni kuendelea kuwahadaa wananchi na kuwalazimisha kuendelea kuishi kwenye umaskini mkubwa.
 
Na,
Padri Privatus Karugendo.
+255 754 633122
www.karugendo.net
 
 

0 comments:

Post a Comment