MWALIMU NA WATOTO WAKE

MWALIMU NA WATOTO WAKE
 
Nilikuwa sikupanga kuandika makala hii. Nimekuwa nikijizuia kuandika juu ya Marehemu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Ninaogopa kuwekwa kwenye kundi la wanafiki, wanaoandika kumlilia na kumkumbuka Mwalimu, lakini matendo yao ni tofauti kabisa na ya Mwalimu. Wanamlilia Mwalimu wakati wanakataa Shirikisho la Afrika ya Mashariki. Wanamlilia Mwalimu wakati wanawafukuza wakimbizi na wahamiaji haramu. Wanamlilia Mwalimu  wakati wanawagawa watanzania katika makundi ya vyama, makabila na dini. Wanamlilia Mwalimu wakati wanayashibisha matumbo yao na kulitelekeza taifa. Wanamlilia mwalimu wakati wana ukumbatia ubepari na kuabudu fedha. Wanamlilia mwalimu wakati wanashindwa kuitetea na kuilinda Katiba ya Taifa letu. Wanamlilia Mwalimu wakati wanaitelekeza lugha yetu ya Kiswahili na kutupilia mbali utamaduni wa taifa letu. Mwalimu, alikuwa Mjamaa, alikuwa mtetezi wa haki za binadamu, alikuwa msomi na mchambuzi, alikuwa mwandishi, alikuwa na hekima na busara. Alikuwa na upendo na huruma, zaidi ya yote alikuwa na “vision”. Mwalimu hakutawaliwa na ushabiki wa kisiasa. Alikwenda kwa hoja, ukimshinda kwa hoja anakuunga mkono. Hakuna anayeyafuata ya Mwalimu. Wengi wanaojifanya kumkumbuka ni wanafiki wakubwa. Mifano mingi ya wanafiki. Sikupenda nichanganywe na wanafiki hao, hivyo niliamua kukaa kimya kuandika juu ya mwalimu.
 
Leo nimeamua kuandika kwa vile mhariri wa Raia mwema, amenitumia ujumbe na kuniomba kuandika kitu juu ya mwalimu, maana Jumatatu ni Nyerere Day. Na kwamba siku hiyo litakuwepo toleo maalumu la Mwalimu, hivyo nina uhuru kuandika maneno mengi kiasi nitakacho. Juu ya mwalimu ni vigumu kuandika maneno yaliyo chini ya elfu moja! Kwa wale wasiomfahamu Mwalimu, vizuri watashindwa kuandika hata maneno mawili. Lakini wale wanaomfahamu, wale wanaofahamu uwazi wake, wema wake, uzalendo wake, umaskini wake, ni lazima washawishike kama mimi kuandika mengi. Kwa vile Nyerere Day, ni mara mmoja kwa mwaka hakuna hatari ya watu kuzichoka makala ndefu.
 
Lakini la msingi lililonisukuma kuandika makala hii ni kitendo cha kukutana na Mtoto wa Mwalimu kwenye Daladala. Nilipanda daladala ya Posta-Mwenge. Tulipofika kituo cha Palm Beach, mtoto wa Mwalimu Nyerere, ambaye nilitokea kufahamiana naye siku za nyumba, alipanda kwenye Daladala. Sikushangaa, ila kusema kweli si jambo la kawaida na hasa kwenye nchi za Afrika; mtoto wa aliyekuwa Rais wa nchi, tena rais wa kwanza na Baba wa taifa kupanda daladala si jambo la kawaida. Huyu angekuwa na gari lake, na dreva wa kumwendesha. Huyu angekuwa na ulinzi mkali nk. Lakini Mtoto wa Mwalimu, aliingia kwenye  daladala kama msafiri yeyote yule. Nina imani ndani ya daladala ile ni wachache au labda hakuna mwingine zaidi yangu mimi aliyetambua kwamba huyo alikuwa mtoto wa Baba wa Taifa.
 
Siku nzima nilitafakari juu ya Mwalimu. Nilitafakari juu ya upekee wake. Nilitafakari juu ya uongozi wake, juu ya uzalendo wake, juu ya mapenzi yake kwa taifa la Tanzania na watu wake. Lakini zaidi nilitafakari juu malezi ya watoto wake: Mwalimu aliwapatia watoto wake malezi ambayo  watoto wote watanzania waliyapata. Watoto wake walisomea shule zile walikosomea watoto wote wa Tanzania. Mwalimu aliamua kutoa elimu ya bure si kwa watoto wake, bali kwa watoto wote wa Tanzania. Kama si mpango wa Mwalimu, wa kutoa Elimu ya bure watu wengi leo hii wasingekuwa na elimu waliyonayo.
 
Makongoro Nyerere, alipokuwa anasoma Tabora Boys, nilikuwa Seminari Kuu ya Kipalapala Tabora. Nilitokea kumfahamu kwa karibu. Alikuwa anakuja kutembea Kipalapala na kula mapera kama  watoto wengine. Alikuwa anapenda muziki na kuimba – pale Kipalapala tulikuwa na bendi ya muziki, hivyo alikuwa akijichanganya kwenye bendi hiyo na kupiga gita na kuimba. Alikuwa akitembea kutoka Tabora Boys hadi Kipalapala kwa miguu kama  watoto wengine. Bila kuambiwa kwamba ni mtoto wa Rais, ilikuwa vigumu kutambua. Alikuwa hana majivuno, kwa sababu alikuwa amelelewa katika mazingira ya kujitambua kwamba yeye hana tofauti na watoto wengine.
 
Mwalimu hakumpatia mtoto wake yeyote yule cheo cha upendeleo ndani ya serikali yake na wala hakuwashawishi watoto wake kuingia kwenye siasa. Sote tulishuhudia Makongoro, alivyojiingiza kwenye siasa – badala ya kuiingia kwenye chama cha Baba yake, akajiunga na upinzani.
 
Rose Nyerere, aliingia Bungeni, baada ya kifo cha Baba yake. Historia haituonyeshi mtoto wa Mwalimu, aliyependelewa kwa aina yoyote ile. Kila mmoja mahali alipo, amepambana kama watoto wengine wote wanavyopambana na maisha na kufanikiwa.
 
Mwalimu , hakuwapendelea watoto wake. Aliwapenda watoto wote wa Tanzania. Alijenga shule za watoto wote  wa Tanzania, alijenga vyuo vya watoto wote wa Tanzania. Lengo lake kubwa lilikuwa kuiandaa Tanzania  yenye neema kwa  vizazi vijavyo . Mwalimu, hakuwapeleka watoto wake kusoma nje ya Tanzania. Kama kuna mtoto wake aliyefanikiwa kusoma nje, atakuwa alisaidiwa na Wamisionari. Ninakumbuka Mwalimu mwenyewe akiwa hai, alisema kwamba mmoja wa watoto wake alipata msaada kusoma Canada, na kwamba msaada huo ulitolewa na wamisionari.
 
Nina imani kama Mwalimu angekuwa hai bado, wajukuu zake wangesoma kwenye sekondari za kata! Mwalimu, hakupenda kuwatenga watoto wake na jamii. Watoto wake  walijiunga na Jeshi la Kujenga taifa kama watoto wengine. Na kule waliishi na kufanya kila kitu kama watoto wengine wote walivyokuwa wakifanya.
 
Leo hii wale wote wanaojifanya wanamlilia Mwalimu, ni nani anafuata mifano yake? Ni mtoto gani wa kiongozi anapamba daladala? Ni mtoto gani wa kiongozi anasoma kwenye sekondari za kata? Ni mtoto gani wa kiongozi asiyesoma nje ya nchi? Tumesikia habari za  baadhi ya watoto wa viongozi kuwashikia watu bastola, lakini hawafikishwi mbele ya sheria. Tumeshuhudia watoto wa viongozi wakiingizwa kwenye siasa na kupata nafasi za juu. Tumeshuhudia watoto wa viongozi wakifanya biashara na kupata upendeleo.
 
Wapo baadhi ya watu wanaomlaumu sana mwalimu kwa siasa yake ya Ujamaa na Kujitegemea. Wengine wanamlaumu Mwalimu kwa kile wanachokiita “Kuitelekeza” familia yake, kwamba hakuwatafutia watoto wake nafasi nzuri katika mfumo wa serikali. Wanasema mwalimu alikosea, wanasema mwalimu alidumaza uchumi wetu. Ukweli ni kwamba Mwalimu, aliona mbali zaidi  yetu. Siasa ya Ujamaa na Kujigemea, ilikuwa silaha kubwa ya kupambana na Ukoloni mambo leo. Mwalimu, alijua wazi kabisa, kwamba utafika wakati tuzidiwe nguvu na Ukoloni Mambo leo, alijua wazi kwamba tutafikia mahali tuvamiwe na wawekezaji kwa mgongo wa Utandawazi. Hivyo alitaka kulijengea Taifa misingi ya kujilinda. Kama  tungefanikiwa kujenga Taifa la Ujamaa na Kujitegemea, kamwe tusingemezwa na Utandawazi, bali tungeshiriki kwenye utandawazi. Sasa, hakuna cha kushiriki ni kumezwa kabisa. Hakuna cha kushiriki bali ni utajiri wetu kuporwa na wageni. Badala ya kujenga uchumi wa taifa letu, tunajenga na kukuza uchumi wa mataifa mengine. Badala ya kuulinda Uhuru wetu, tunakubali kuwa “watumwa”!
 
Kwa mtazamo wangu, ni kwamba Mwalimu alifanya makosa mawili katika maisha yake: Kosa la kwanza, ambalo limemgharimu sana, ni kuwaamini sana watu. Mwalimu, aliwaamini watu. Watu hawa aliowaamini mwalimu, ndio wale wale walioangusha na kuzika Vision yake. Wale aliowaamini ndio waliolizika Azimio la Arusha kule Zanzibar. Ni  watu wachache wa aina ya Mzee Kawawa, walibaki waaminifu kwa Mwalimu. Wengine walikuwa wanafiki, walitaka vyeo na utajiri wa haraka. Walionyesha unyenyekevu kwa Mwalimu, walizungumza kama Mwalimu na kuvaa nguo kama za Mwalimu. Baada ya Mwalimu, kutoka madarakani, watu hawa walibadilika haraka, walianza kuongea lugha nyingine na kuvaa nguo za Kizungu. Kosa  la pili la Mwalimu, ni kwenda Haraka. Mfano, hakujipatia nafasi kufanya maandalizi ya kutosha kabla ya kufanya uamuzi wa Azimio la Arusha. Hakuwaandaa watu kupokea Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Alifanya haraka ya kutaifisha, viwanda, mashule na mahospitali. Uharaka huu, ambao haushangazi kwa Mwanamapinduzi, kama alivyokuwa Mwalimu, ndiyo sababu kubwa ya kuanguka kwa siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.
 
Mimi ni kati ya watu wanaomlaumu Mwalimu kwa uharaka wake. Mimi ni kati ya watu wanaoamini kwamba labda kama Mwalimu, angefanya maandalizi ya zaidi ya miaka 20 – watu wakajadili, wakatafakari na kutafuta uzoefu wa ujamaa katika nchi za ujamaa za wakati ule, labda Ujamaa wetu usingekufa. Lakini pia mimi ni miongoni mwa watu wanaotetea Uharaka wa Mwalimu. Ni kweli kwamba aliona mbali. Alifikiri kwamba bila kujenga Ujamaa kwa haraka, tungemezwa bila maandalizi.
 
Baada ya Uhuru, Mwalimu Nyerere alitangaza maadui wa Taifa letu kwamba ni Maradhi, Ujinga na Umaskini. Na kwamba silaha pekee ya kupamba na maadui hawa ni: Ardhi, Siasa safi, Uongozi bora na  watu. Aliamini pia kwamba ili haya yote yafanyike ni lazima tuwe na Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Siasa hii, ililinda utajiri wa Taifa letu. Hatukusikia malalamiko ya madini kusombwa na kupelekwa nje, hatukusikia wizi wa magogo, hatukuzikia vitalu vya wawindaji. Tulisikia Kisomo cha watu wazima, tulisikia Siasa ni Kilimo, tulisikia mvua za kwanza ni za kupandia n.k
 
Kama nilivyosema hapo juu, ni kwamba Mwalimu hakuwapendelea watoto wake, bali aliwapenda watoto wote wa Tanzania. Wimbo wetu wa Taifa, unaonyesha wazi jinsi Mwalimu alivyokuwa na upendo kwa watoto kama taifa la Kesho. Watoto wanatajwa na kuombewa baraka nyingi katika wimbo huu wa Taifa. Lakini upendo wake kwa watoto haukuishia hapo, ulivuka mipaka ya Tanzania, na kuenea kwenye bara lote la Afrika. Vituo kama kile cha Mazimbu, kule Morogoro, vilianzishwa ili kuwapatia Elimu ya ukombozi watoto wa wakimbizi kutoka Msumbiji. Lakini pia nchi nyingine nyingi za Afrika kama Angola, Botswana, Zimbabwe, Namibia n.k. zilipata Kivuli kizuri sana  kutoka kwa  Mwalimu.
 
Tunaposherehekea Nyerere Day, ni watanzania wangapi, ni viongozi wangapi wanawapenda watoto wa Tanzania, kama alivyowapenda Mwalimu Nyerere? Ni nani anahakikisha watoto wetu wanapata malezi bora, elimu bora na afya njema? Ni nani anawaandalia watoto wetu Tanzania ya kesho yenye neema? Hadi leo hii Taifa letu limeshindwa kusimamia usafiri salama wa watoto wetu kwenda shule. Watoto wanasukumwa na kunyimwa nafasi kwenye daladala. Wasomi wa vyuo vikuu wanasumbuka kupata mikopo. Maadili ya watoto wetu yanakwenda ovyo, watoto wameachwa bila mtu wa kuwaelekeza. Tunachimba madini na kuwaachia watoto wetu mashimo, tunakata miti kwa fujo na kuuza magogo nchi za nje na kutunza pesa hizo kwenye uchumi wa nchi za nje. Viongozi wanawapendelea watoto wao, wanawasomesha nchi za nje kwenye vyuo vizuri. Watoto wengi wanaobaki wanajengewa Sekondari za kata!
 
Tumkumbuke Mwalimu Nyerere, kwa kujiwekea mkakati wa kuongeza mapenzi kwa watoto wetu. Tuwapatie watoto wetu elimu bora, mazingira bora na yenye kuvutia, afya njema na kuwajengea Tanzania ya kesho yenye Neema. Mwenye Mungu, amlaze mahali pema peponi Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Baba yetu wa Taifa!
 
Na,
Padri Privatus Karugendo.
 
+255 754 633122

0 comments:

Post a Comment