UTHIBITI WA HUDUMA ZA KIUCHUMI TANZANIA- MWANDOSYA

UHAKIKI WA KITABU:  UTHIBITI WA HUDUMA ZA KIUCHUMI TANZANIA
 
1.     Rekodi za Kibibliografia.
 
Jina la kitabu kinachohahikiwa hapa ni UTHIBITI WA HUDUMA ZA KIUCHUMI TANZANIA , Kimeandikwa na  Profesa Mark Mwandosya. Mchapishaji wa kitabu hiki ni E&D Vision Publishin Limited na amekipatia namba  ifuatayo katika sekwensia ya vitabu duniani (ISBN): - 978-9987-735-09-9 Kitabu kina kurasa 151  . Na anayekihakiki sasa hivi katika safu hii ni mimi Padri Privatus Karugendo.
 
II. Utangulizi
 
Udhibiti ni njia mojawapo inayotumika kusimamia uchumi wa nchi na kuendeleza ustawi wa jamii. Udhibiti wa huduma za kiuchumi (Public utilities) unahusu kuweka mizania kati ya kuwawezesha watoa huduma na kuwalinda watumiaji wa huduma kama vile maji, umeme, uchukuzi na mawasiliano. Suala Udhibiti wa huduma za uchumi lilijitokeza kwanza miaka zaidi ya 150 iliyopita, huko Marekani na Ulaya kwa madhumuni makubwa ya kumlinda mlaji katika mazingira ya uchumi wa soko huria.
 
Kitabu hiki kinaelezea chimbuko la udhibiti Tanzania katika muktadha wa mabadiliko ya uchumi duniani pamoja na udhibiti katika nchi nyingine. Ni kitabu chenye maarifa ya msingi kwa kila mtuamiaji wa huduma za kiuchumi, pamoja na wanafunzi, wasomi, wafanyakazi na viongozi. Lakini pia ni kitabu kinachomsaidia mwananchi kuelewa udhibiti na kufahamu jinsi mfumo huu unavyolenga kumtetea katika mfumo wa soko huria.
 
Kitabu hiki kina sura 15 ambazo zinaongelea: Sura ya kwanza ni Utangulizi, sura ya pili ni Dhana ya Udhibiti, ambayo inajadili malengo ya udhibiti, huduma za kiuchumi, mazingira sawa ya ushindani, uhuru wa Mdhibiti, Uteuzi wa Bodi na Ofisa Mtendaji Mkuu, Uhai wa bodi, nidhamu ya usimamizi wake. Sura ya  tatu ni juu ya Maeneo Muhimu ya Udhibiti, ambayo inajadili kwa undani juu ya Leseni, Kudhibiti Mwenendo wa Bei na  tozo Mbali mbali, mwongozo wa maadili. Sura ya nne ni juu ya Uwezo wa kifedha wa Mdhibiti. Sura ya tano ni juu ya kuwalinda watumiaji wa huduma na bidhaa. Sura ya sita ni juu ya Muundo wa vyombo vya Udhibiti. Sura ya saba inajadili Udhibiti wa sekta za Kiufundi na kufafanua zaidi juu ya Mifano ya dhibiti wa Masuala ya kiufundi, usimamizi wa Masafa ya Redio, Muunganisho wa mawasiliano na namba za simu kama rasilimali muhimu. Sura ya nane inajadili juu ya Uhusiano Kati ya serikali na mthibiti. Sura ya tisa inajadili juu ya Udhibiti na ushindani wa Biashara; Utaratibu wa kumlinda mlaji na mtoa huduma, Uhusiano wa udhibiti na huduma na wa biashara. Sura ya kumi inajadili juu ya Sheria za Kisekta. Sura ya kumi na moja inajadili juu ya Uhusiano kati ya Bunge na Mdhibiti. Sura ya kumi na mbili ni juu ya Udhibiti katika nchi nyingine. Sura ya kumi na tatu inaongelea Masuala Mtambuka. Sura ya kumi na nne inajadili Mafanikio na changamoto za udhibiti; Kusimamia utekelezaji wa sheria, utoaji wa Leseni, sekta ya mawasiliano, sekta ya maji, sekta ya umeme, sekta ya uchukuzi, sekta ya mafuta ya petroli na watumiaji wa hudumaza kiuchumi. Sura ya mwisho ya kumi na tano ni hitimisho na kitabu kinafunga na orodha ya marejeo.
 
Mwandishi wa kitabu hiki, Mark Mwandosya, amewahi kuwa Profesa wa Uhandisi wa Umeme Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Kamishana wa Nishati na Masuala ya Petroli, Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Nishati na Madini, Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, Waziri wa Nchi (Mazingira), Ofisi ya Makamu wa Rais, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, na waziri wa Maji. Kwa sasa yeye ni waziri wa Nchi(Kazi Maalum), Ofisi ya Rais.
 
Katika aya zifuatazo nitafanya uhakiki wa kitabu hiki, lakini kwanza kwa kudokeza mazingira yanayokizunguka kitabu hiki.
 
 
III. Mazingira yanayokizunguka kitabu
 
Kitabu hiki kimeandikwa na msomi tena profesa. Tumekuwa tukiwalalamikia wasomi wetu kukaa kimya na kushindwa kulielekeza taifa letu la Tanzania. Sasa mwandishi wa kitabu hiki amekata mzizi wa fitina. Ameandika, labda sisi tushindwe kusoma. Tumekuwa tukiwalalamika wasomi wanaojitahidi kuandika, lakini wanafanya hivyo kwa lugha za kigeni. Mwandishi wa kitabu hiki amekata mzizi wa fitini  kwa kuandika kitabu kwa lugha ya Kiswahili. Tumekuwa tukiwalalamika wanasiasa wetu kuhubiri majukwaani na kushindwa kutuandikia vitabu kama kumbukumbu za leo, kesho, keshokutwa na vizazi vijavyo, mwandishi wa kitabu hiki amekata mzizi wa fitini, atakuwa ni miongoni mwa wanasiasa wachache wa Tanzania wanaoandika vitabu. Tumekuwa tukiwalalamikia wanasiasa kuchanganya siasa na kila kitu hata kuiingilia taaluma nyingine za kisomi, mwandishi huyu amekata mzizi wa fitina, pamoja na kwamba anaongelea huduma za kijamii, huduma za kiuchumi, kitabu chake kutoka sentensi ya kwanza hadi ya mwisho hakuna neno CCM. Ingawa mwandishi ni kada, lakini amevuka ufinyo huo na kuwa juu katika uwanja wa wanazuoni. Anaandika kwa watanzania wote bila kujali siasa, dini wala kabila. Ni kitabu cha aina yake!
 
Udhibiti ni kitu kipya, na kusema kweli ni msamiati ambao ni mgumu kueleweka kwa watu  wengi ingawa tunashiriki mfumo huu siku kwa siku. Kitabu hiki, au niseme mwandishi wa kitabu amefanya kazi ya peke kuelezea maana ya udhibiti. Na sikuelezea tu, bali huyu ni mmoja wa watanzania walioshiriki kiazi kikubwa uanzishwaji wa udhibiti katika taifa letu.
 
Tumekuwa tukisikia EWURA – Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji, TCRA – Mamlaka ya Udhibiti wa  Mawasiliano, TCAA – Mamlaka ya udhibiti wa Usafiri wa Anga, SUMATRA – Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Maji. Lakini ni kiasi gani tumekuwa tukielewa misamiati hii? Ni kiasi gani wananchi wamefahamu vyombo hivi vya udhibiti na jinsi wao wanavyoweza kushiriki na kutoa maoni kwenye uendeshaji wa vyombo hivi? Mwandishi amejaribu kwa kiasi kikubwa na lugha nyepesi kuelezea maana ya udhibiti na chimbuko lake; kipindi cha mabadiliko makubwa ya mfumo wa uchumi wa Tanzania kutoka mfumo wa uchumi hodhi hadi mfumo wa uchumi wa soko. Katika uchumi hodhi, Serikali ilishikilia na kusimamia mihimili yote ya uchumi, kuanzia mitaji, njia za uzalishaji, upangaji wa bei na uendeshaji wa masoko kupitia mauzo ya jumla na maduka ya  rejareja. Katika mfumo huo, serikali kupitia idara zake, mashirika na kampuni zake, ilikuwa ndiye mwajiri mkubwa katika uwanja wa ajira rasmi. Kipindi hiki ni na zama hiyo ni ile ya kabla ya mwaka 1985.
 
“ Kipindi cha mwaka 1985 hadi 2005  ni kipindi cha miaka 20 ambacho kimehusisha Awamu ya Pili ya uongozi wa nchi kutoka mwaka 1985  hadi 1995; na Awamu ya Tatu, mwaka 1995 2005 iliyokuwa chini ya uongozi wa Rais Benjamin William Mkapa. Kipindi hiki cha miaka 20 ni kipindi ambacho kinaweza kikausishwa na zama ya mageuzi ya mfumo wa uchumi wa nchi kutoka mfumo hodhi na kuanzisha misingi na utekelezaji wa mfumo wa soko. Katika mifumo yote miwili, kumekuwa na udhibiti na usimamizi wa huduma za kiuchumi na miundombinu. Katika mfumo hodhi, udhibiti na usimamizi huo ulifanywa moja kwa moja na Serikali kupitia wizara na idara zake wakati mfumo wa soko umehitaji uanzishaji wa vyombo huru vilivyo nje ya mfumo rasmi wa wizara na idara  za serikali. Kwa urahisi wa uelewa, angalau kwa nadharia tu, fumo wa vyombo huru vya usimamizi wa huduma za kiuchumi na miundombinu unafana na uhuru, udhibiti na usimamizi unaofanywa na Benki Kuu katika sekta ya fedha nchini kupitia sera ya fedha” (Uk xv na xvi).
 
Mwandishi wa kitabu hiki hafanyi kazi ya kubahatisha, maana mwaka 1985 aliteuliwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kuwa kamishna wa kwanza wa Nishati na Petroli na hivyo kuanzisha kwa mara ya kwanza idara kamili ya huduma ya kiuchumi, Idara ya Nishati. Pia aliwahi kuwa mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya lililokuwa Shirika la Posta na Simu Tanzania na mjumbe wa Bodi ya TANESCO, kwa nafasi hizo aliweza kuwa na uzoefu na uelewa wa huduma tatu za kiuchumi, mawasiliano ya posta, simu na nishati.
 
Mwaka 1992, mwandishi wa kitabu hiki alihamishiwa Wizara ya  Viwanda na Biashara kama katibu mkuu, akapata nafasi ya kuhusiana moja kwa moja na mageuzi ya kiuchumi kwa kuanzisha mfumo wa na taratibu za awali za ubinafsishaji wa viwanda. Pia alikuwa mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi ya shirika la Petroli Tanzania (TPDC) na kupata nafasi ya kusimamia huduma muhimu ya kiuchumi.
 
Mwandishi wa kitabu hiki kati ya mwaka 2000 na 2005, alikuwa Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi na kupata fursa ya kipekee ya kusimamia maandalizi ya kupitisha Bungeni sheria zilizoanzisha mamlaka  tatu za udhibiti; Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano(TCRA), Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Anga (TCAA), Mamlaka ya udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA). Na mwaka 2008, Rais Jakaya Mrisho Kikwete, alimteua mwandishi wa kitabu hiki kuwa waziri wa Maji na Umwagiliaji. Waziri mwenye dhamana ya sekta ya maji kwa sasa ndiye Waziri anayesimamia Mamlaka ya Udhibiti wa huduma za Nishati ya Maji (EWURA). Hivyo mwandishi anajua vizuri mada hii hivyo atatufumbua macho.
 
 
 
 
IV. Muhtasari wa Kitabu
 
Kitabu hiki kinajadili na kufafanua kwa kina juu ya suala la udhibiti wa huduma za uchumi; kwamba suala hili la udhibiti  lilijitokeza kwanza miaka zaidi ya 150 iliyopita, huko Marekani na Ulaya kwa madhumuni makubwa ya kumlinda mlaji katika mazingira ya uchumi wa soko huria. Pia kwamba mfumo wa sasa wa udhibiti nchini Tanzania ulianza kipindi cha muongo mmoja uliopita ikiwa ni matokeo ya mabadiliko ya mfumo wa uchumi, kutoka uchumi hodhi kwenda uchumi wa mseto, mfumo ulioutambua umuhimu wa soko huru na sekta binafsi katika kuchochea kukua kwa uchumi. Taratibu za kuanzisha mfumo wa sasa wa udhibiti zilienda sambamba na zoezi la ubinafsishaji. Na kwamba mfumo wa sasa wa udhibiti unafanana na mifumo katika nchi nyingi, na kwa kiwango kikubwa, umefuata misingi mizuri ya kimataifa. Misingi hiyo imefafanuliwa katika kitabu hiki. Mwandishi wa kitabu hiki anaweka wazi kwamba: “ Ni jambo la kujivunia kwamba nchi nyingi hasa za Afrika kusini mwa Sahara zimekuja Tanzania kujifunza jinsi ya kudhibiti huduma za nishati, maji na mawasiliano”  (Uk 132).
 
Sura ya kwanza ya kitabu hiki ni Utangulizi. Hapa mwandishi anafafanua kwamba udhibiti kwa maudhui ya kitabu chake unahusu huduma za kiuchumi, na kwamba mfumo wa sasa wa udhibiti wa sekta za uchumi Tanzania unatokana na mabadiliko ya mfumo wa uchumi kutoka uchumi hodhi kwenda kwenye uchumi wa kati au uchumi mchanganyiko.
 
Hapa ndipo mwandishi anatuelezea na kufafanua juu ya Uchumi wa soko (Market economy): Kwamba “ huu ni mfumo wa uchumi ambao maamuzi kuhusu uwekezaji, uzalishaji na ugawaji wa bidhaa na huduma hutegemea upatikanaji wake na mahitaji... katika mfumo huu wa uchumi, bei za bidhaa na huduma hupangwa na soko lililo huru..” (uk 1);
 
Pia juu ya Uchumi hodhi au uchumi wa mipango (planned economy), kwamba “Mfumo huu wa uchumi unatoa maamuzi yanayohusu uwekezaji, uzalishaji na ugawaji wa rasilimali, huduma na bidhaa yanatokana na mpango wa Serikali. Kwenye mfumo wa aina hii, mipango ya uzalishaji na utekelezaji wake inatakiwa kuzingatia mahitaji ya jamii na watumiaji wa huduma...”( Uk 1-2);
 
Na juu ya Uchumi mseto ( mixed economy), kwamba huu ni mfumo ambao “ Serikali na sekta binafsi hushirikiana katika kuendesha uchumi. Katika uchumi wa aina hii, uwekezaji unaachiwa sekta binafsi wakati Serikali inauwa na wajibu wa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji...” (Uk 2). Katika mfumo huu wa uchumi Serikali hutumia vyombo vya udhibiti katika kusimamia uchumi. Mwandishi anatufahamisha kwamba nchi nyingi duniani zina uchumi wa mfumo huu. Na Tanzania ni miongoni mwa nchi hizo zinazofuata mfumo wa aina hii. Na kudokeza kwamba..  “... inabidi soko huria lisimamiwe na lidhibitiwe ili kumlinda mlaji au mtumiaji wa huduma na kumhamasisha mto huduma aongeze  tija na kuleta faid katika uchumi kwa ujumla...” (uk 3).
 
Baada ya ufafanuzi huo, mwandishi anajadili juu ya Udhibiti kabla ya Sera ya ushindani na kipindi cha mpito. Linalo elezwa hapa na mwandishi ni kwamba hata kabla ya mabadiliko au mageuzi ya kiuchumi yaliyoletwa na kuanzishwa kwa soko huru na serikali kujitoa katika kufanya biashara,  kwa kiwango kikubwa, usimamizi na udhibiti ulifanywa na wizara husika na idara za Serikali. Waziri muhusika na sekta ndye aliyekuwa na mamlaka ya mwisho katika usimamizi wa sekta husika , akisaidiwa na  Mkurugenzi wa Idara, Kamishna mhusika na Katibu mkuu wa wizara.
“ Hata hivyo, katika sekta za kiufundi na miundombinu, kama vile uchukuzi na mawasiliano, vilikuwepo vyombo ambavyo vilianzishwa kisheria kusimamia baadhi ya maeneo yaliyohitaji udhibiti wa kiufundi. Kwa mfano, kabla ya mageuzi ya uchumi, sehemu kubwa ya sekta ya mawasiliano ya simu na posta ilidhibitiwa na Shirika la Posta na Simu la Tanzania (TPTC)...”
 
“ Kwa upande wa uchukuzi, udhibiti, pamoja na  kusimamiwa na wizara yenye dhamana ya uchukuzi, kiutendaji ulikuwa chini ya vyombo vilivyoanzishwa chini ya wizara mbali mbali...” (Uk 7).
 
“ Jeshi la Polisi nalo lilikuwa ni Mdhibiti kwa minajili ya Sheria ya Usalama wa Barabarani, kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani. Wizara yenye dhamana na uchukuzi nayo ilikuwa na Kitengo cha Usalama Barabarani (Road Safety Unit). Wakala wa Barabara, kupitia sehemu ya mizani, nao ni sehemu ya udhibiti pamoja na kwamba lengo lao kuu ni kutunza barabara na kurefusha uhai wa barabara...” (Uk 8).
 
Mwandishi anaendelea kutuelimisha juu ya kipindi hiki cha udhibiti kabla ya sera ya ushindani kwamba “... nyenzo muhimu ya udhibiti kabla ya mfumo wa sasa ilikuwa ni marekebisho ya bei... Kwa eneo la bidhaa, kiliundwa chombo kilichofahamika sana, Tume ya Bei. Tume ya bei ilianzishwa kwa mujibu wa Sheria ya udhibiti wa Bei ya mwaka 1973” (Uk8).
 
Tukiwa bado kwenye sura ya kwanza ambayo kwa kiasi kikubwa ni utangulizi, mwandishi anaelezea juu ya udhibiti wa Huduma za Maji Dar es salaam, Kipindi cha mpito. Kwamba “ Wazo la kuwa na mdhibiti kwa ajili ya kusimamia sekta ya maji lilijitokeza wakati wa zoezi la kubinafsisha shughuli za Mamlaka ya Maji safi na Maji taka Dar-es-Salaam - DAWASA au kuwe na udhibiti kupitia mkataba wa ubinafsishaji. Hatimaye, ilikubalika kwamba awepo mdhibiti maalum” (Uk 11).
 
Pia katika sura hii mwandishi anafafanua juu ya udhibiti wa Kimataifa. Kwamba kwa vile Tanzania ni sehemu ndogo ya ulimwengu, katika masuala ya kimataifa, inaongozwa na makubaliano ambayo kwa kiwango kikubwa yanasimamiwa na Umoja wa Mataifa na mashirika yake. Anaelezea chanzo cha kuanzishwa Umoja wa mataifa na sheria zinazoongoza mashirika ya umoja wa mataifa na kwamba mikataba yote ambayo Tanzania inaingia na umoja wa mataifa ni lazima ipate nguvu za kisheria.
 
“ Katika maeneo ya matumizi ya rasilimali za pamoja, makubaliano ya kimataifa yamewezesha kuanzishwa kwa vyombo au mashirika ya usimamizi na udhibiti wa kimataifa. Mashirika haya yamewezesha pia kuwekwa kwa sheria za kimataifa, taratibu na kanuni za usimamizi na udhibiti wa kijumla” (Uk 15). Taasisi au vyombo hivyo vinavyojadiliwa hapa ni pamoja na Shirika la Simu Duniani, Shirika la posta duniani, Shirika la Kimataifa la Usalama wa usafiri wa Anga na Shirika la Kimataifa la Usafiri Majini. Aidha, kuna mashirika ya kimataifa yasiyo chini ya Umoja wa Mataifa moja kwa moja lakini yanadhibiti maeneo muhimu kama viwango vya kimataifa vinavyoshughulikiwa na Shirika la Viwango Duniani.
 
Sura ya pili ya kitabu hiki, mwandishi anafafanua juu ya dhana ya udhibiti. Hapa ndipo anapotuelezea malengo ya udhibiti, huduma za kiuchumi, mazingira sawa  ya ushindani, uhuru wa mdhibiti, uteuzi wa bodi na ofisa mtendaji mkuu, uhai wa bodi, nidhamu na usimamizi wake.
 
“ Kwa maoni ya mwandishi, madhumuni muhimu ya udhibiti ni kukuza uchumi wa nchi, ingawa madhumuni haya hayajitokezi waziwazi katika kazi za udhibiti za kila siku. Bila udhibiti wenye ufanisi, uwekezaji utalegalega na uchumi hautaweza kukua haraka...” (Uk 17)
 
“Maneno ‘Huduma za Kiuchumi’(Public Utilities) yanatumika katika kitabu hiki kumaanisha huduma ambazo hutolewa kupitia miundombinu ambayo inakuwepo wakati wote na ambayo inamwezesha mtumiaji wa huduma kuipata huduma hivyo wakati inapohitajika. Huduma hizi ni kama vile umeme, mafuta ya petroli, gesi asilia, maji, uondoaji maji taka , mawasiliano ya posta na mawasiliano ya kielektroniki kama vile simu, intaneti, radio na  televisheni. Kwa maana hiyo pana ya huduma za kiuchumi, huduma hizo ni pamoja huduma za uchukuzi, kama vile uchukuzi wa anga, ardhini (reli, mabasi, malori) na uchukuzi wa majini” (Uk 18).
 
La kujifunza hapa ni kwamba huduma za kiuchumi huangaliwa kwa karibu na Serikali zote duniani.
 
Kazi kubwa ya mthibiti ni kuweka mazingira sawa ya ushindani ( Uwanja sawa wa ushindani) “...Kwani inatarajiwa kwamba soko litajirekebisha lenyewe na huduma na bidhaa kuendelea kutolewa ipasavyo. Lakini soko la namna hiyo ni ndoto tu ambayo kama ilivyo njozi nzuri, tungependa itimie. Kwa kawaida haiwezekani. Ndipo unapokuja umuhimu wa mdhibiti. Na moja ya majukumu yake muhimu sana ni kuweka mazingira sawa ya ushindani, kwa lugha nyingine kuweka uwanja wa ushindani ulio sawa (level playing field)” ( Uk 19).
 
Ili mdhibiti aweze kutekeleza majukumu yake kikamilifu na kusimamia ushindani kwa ufanisi na kutenda haki ni lazima awe huru. Uhuru unamwezesha kupima katika mizania haki za mtumiaji wa huduma au bidhaa, haki za mtoa huruma au mzalishaji na muuzaji wa bidhaa, gharama za kutoa huduma, gharama za kuzalisha bidhaa na kuzisambaza, kudhibiti mwenendo wa bei ya huduma hizo au bidhaa hizo kwa mtumiaji na kuhakikisha sera za nchi zinafuatwa na sheria na taratibu zinatekelezwa. Mwandishi anafafanua vizuri zaidi juu ya uhuru huu wa mdhibiti katika kitabu chake. Kwa kukisoma, mtu ataelewa vizuri juu ya uhuru wa mdhibiti na kwamba: “ Katika kurekebisha hali hii ya kumpa Mdhibiti uhuru wa kutosha wa kutenda kazi kwa misingi ya haki bila woga, sheria zote zinazoanzisha mamlaka za udhibiti zinampa Waziri uwezo wa kusimamia mamlaka hizi kisera na kiutawala tu na sio katika masuala yaliomo ndani ya himaya ya Mdhibiti...” ( Uk 21).
 
Dhana muhimu ya uhuru wa Mdhibiti inadhihirika pale ambapo muhula wa kazi wa bodi unalindwa kisheria na taratibu za uteuzi wa bodi na ofisa mtendaji mkuu zinatambuliwa kisheria.  “Sheria zote zinazoanzisha vyombo vya udhibiti Tanzania zinaunda Kamati ya Uteuzi (Nominations Committee). Kamati hii si kamati ya kudumu. Inakutana pale tu inapohitajika kupendekeza majina ya uteuzi wa mjumbe au wajumbe wa bodi pamoja na ofisa mtendaji mkuu wa mamlaka ya udhibiti... Kamati huwa chini ya uenyekiti wa katibu mkuu wa wizara ya kisekta inayomsimamia Mdhibiti. Sheria pia zinafafanua sifa na aina ya wajumbe wa kamati ya uteuzi, ikisisitizwa kuwepo kwa mwakilishi wa sekta binafsi..” (Uk 23).
 
Katika sehemu hii, mwandishi ameelezea vizuri uhuru wa mdhibiti na sheria zinazompatia uhuru huo na kuulinda. Pia, hapa anatuelezea Uhai wa Bodi, mfano kwamba “ ... kwa mujibu wa sheria ya TCRA, sheria Na.12 ya 2003, Mwenyekiti wa bodi anateuliwa kwa muhula wa miaka (4),Makamu wa Mwenyekiti muhula wake ni miaka mitatu na wajumbe wengine wawili kipindi chao ni miaka mitano” (Uk 26).
 
“Kwa mamlaka zote, mjumbe wa bodi akimaliza muhula wake anaweza kuchaguliwa tena kwa kipindi kingine kimoja. Hawezi akazidisha mihula miwili. Vilevile, katika mamlaka zote, mkurugenzi mkuu ambaye ndiye ofisa mtendaji mkuu, ni mjumbe wa bodi kwa wadhifa wake...” (26). Katika sehemu hii mwandishi anaelezea  vizuri uzoefu uliopo, mfumo ulivyo juu ya uhai wa bodi. Hivyo mtu akijisomea mwenyewe kitabu hiki atapata ujuzi na uelewa mpana juu ya suala zima la udhibiti, uteuzi wa bodi na uhai wa bodi hizi.
 
Sura ya tatu ya kitabu hiki inajadili juu ya  Maeneo  Muhimu ya udhibiti, Leseni, Kudhibiti Mwenendo wa Bei na Tozo Mbalimbali na mwongozo wa maadili. “ Sheria zilizoanzisha mamlaka za udhibiti Tanzania zimeainisha maeneo muhimu matatu ambayo mamlaka zinatakiwa kisheria, kufanya uchunguzi wa kina, wa wazi, na unaohusisha wadau na wananchi kwa ujumla (taftishi) . Maeneo hayo yanahusu: Kutoa leseni, kuongeza muda wa leseni au kufuta leseni ambazo mdhibiti ana uwezo wa kufanya hivyo; Kudhibiti mwenendo wa bei ya bidhaa na /au huduma zinazotolewa katika sekta inayodhibitiwa; na kupitishwa kwa kanuni za maadili (code of conduct)” (Uk 33). Hayo yote yaliyotajwa hapo juu yanajadiliwa kwa ufasaha mkubwa katika kitabu hiki.
 
Sura ya nne ya kitabu hiki inajadili Uwezo wa kifedha wa Mdhibiti: “Kutokana na yaliyoelezwa mpaka sasa, ni dhahiri mdhibiti ana madaraka na mamlaka makubwa, na hali kadhalika ana dhamana kubwa aliyopewa na Taifa kupitia sheria za kisekta na sheria zinazoanzisha vyombo vya udhibiti. Ana uhuru mkubwa katika masuala na maamuzi yanayohusu udhibiti. Mamlaka, madaraka, dhamana na uhuru huo unaweza kudhihirika pale tu ambapo mdhibiti ana uwezo wa kujiendesha; na pale upatikanaji wa rasilimali fedha na rasilimali watu unatabirika ili aweze kuendesha shughuli zake. Vinginevyo atakwazwa katika utekelezaji shughuli zake...” (Uk 39).
 
Katika sehemu hii mwandishi anaelezea jinsi mdhibiti anavyopata fedha za kujiendesha na ni kutokana na:
- Ada zinazolipwa kwa mdhibiti ikiwa ni pamoja na ada za kudurusu au kutoa leseni;
- Tozo mbalimbali kutoka kwa wazalishaji na/au watoa huduma; na
- Misaada ya aina mbalimbali au michango inayoweza kutolewa kwa Mdhibiti.
 
Mfano: “ Mapato ya EWURA kwa kiwango kikubwa yanatokana na tozo ya udhibiti (regulatory levy) ambayo wadhibitiwa (regulated entities) wanatozwa kiwango kisichozidi asilimia moja (1%) ya mapato ghafi, katika sekta za umeme, petroli, gesi asilia, maji na uondoaji majitaka.” (45).
 
Mwandishi, anaelezea mapato ya mdhibiti, matumizi na sheria zinazoongoza kukusanya na kutumia mapato haya. Mtu akijisomea kitabu hiki ataelimishwa kwa kina juu ya jambo hili la  uwezo wa kifedha wa mdhibiti.
 
Sura ya  tano inajadili juu ya  kuwalinda watumiaji wa huduma bidhaa zinazodhibitiwa... “Pamoja na haki za mlaji au mtumiaji wa bidhaa kuwekwa bayana kisheria, baina ya wadau wote wa udhibiti, mlaji au mtumiaji ndiye asiye na nguvu na anaweza akaonewa. Hii inatokana na ukweli kuwa mlaji kwa kawaida hajajipanga kutetea maslahi yake kama ilivyo kwa watoa huduma na wazalishaji. Jamii imelitambua hilo na kuanzisha mifumo mbalimbali ya kisheria kutambua makundi au vikundi vya watumiaji. Katika nchi zilizoendelea, vikundi vya hiari vya watumiaji wa huduma vina nguvu na ushawishi mkubwa. Hata katika nchi hizo bado imewekwa mifumo rasmi ya kupokea na kushughulikia kwa haraka kero na migogoro inayoweza kuadhiri utoaji wa huduma au inayotokana na haki kutotendeka (Ombudsman)” (uk 49)
 
“Katika nchi zinazoendelea, Tanzania ikiwa ni mfano, hakuna vyama vya hiari vinavyounganisha  watumiaji wa huduma au bidhaa ambavyo vingeweza kutetea kundi hilo la jamii katika sekta inayodhibitiwa. Baada ya mjadala mrefu uliohusu uanzishaji wa mamlaka za udhibiti, ilionekana vema yakaanzishwa mabaraza ya ushauri ya watumiaji wa huduma zinazodhibitiwa (Consumer Consultative Councils- CCC). Mabaraza haya ni EWURA-CCC, SUMATRA-CCC, TCAA-CCC, na TCRA-CCC, Pia, chini ya Sheria ya Fair Competition Act limeanzishwa Baraza la watumiaji linaloitwa National Advocacy Council (NCAC)” (Uk 49)
 
Mwandishi anaendelea kufafanua zaidi kuhusu kuwalinda watumiaji wa huduma na bidhaa zinazodhibitiwa. Msomaji wa kitabu hiki atapa hayo yote na kupata majibu ya maswali mengi ambayo watu wamekuwa wakijiuliza kuhusu dhana nzima ya udhibiti wa huduma za kiuchumi.
 
Sura ya sita, inajadili muundo wa vyombo vya udhibiti. Hapa tunafahamishwa kwamba: “...mifumo ya vyombo vya udhibiti ina mambo mengi yanayofanana. Hata hivyo, mfumo wa uchumi, historia, ushirikiano wa kikanda, na ushirikiano wa kimataifa ni baadhi ya vigezo vinavyotofautisha mfumo mmoja na mwingine” (Uk 54).
 
Hapa mwandishi anaelezea mfumo unaotumika Tanzania. Faida na hasara zake. Na kulinganisha mfumo wetu wa udhibiti na mifumo ya nchi nyingine. La kuzingatia hapa ni kwamba misingi ya udhibiti inafanana na inakubalika kote duniani. Kwa mfano ukilinganisha mfumo wa udhibiti wa Tanzania na Uingereza, tofauti  zake ni matokeo ya tofauti za mazingira ikiwa ni pamoja na historia ya utawala, utamaduni, biashara, mazingira ya masoko, ushindani, na hali ya uchumi.
 
Sura ya saba inahusu Uthibiti wa Sekta za Kiufundi. Hapa ndipo tunafafanuliwa juu ya mifano ya udhibiti wa Masuala ya Kiufundi, Usimamizi wa Masafa ya Redio, Muunganisho wa Mawasiliano na Namba za simu kama Rasilimali Muhimu.
 
“Sekta ya mawasiliano ina mifano mzuri inayohusu udhibiti wa masuala ya kiufundi. Ni sekta yeye changamoto kubwa kwa wadhibiti. Kwani teknolojia katika sekta hii inabadilika kwa kasi kubwa sana na kufanya  teknolojia ya miaka miwili au mitatu iliyopita kuwa ya kizamani”  (Uk 62-63)
“Usimamizi wa masafa ya redio unahusu kuhakikisha matumizi bora ya masafa, kupunguza mwingiliano wa masafa kwa watumiaji mbalimbali, kuhakikisha kwamba hakuna anayetumia masafa ya redio bila kuruhusiwa kisheria, na kwamba aliye na leseni ya kutumia masafa ya redio anayatumia vizuri na kwa mujibu wa masharti yaliyo katika leseni...” (uk 63)
 
Mwandishi anaelekea kwa kirefu juu ya muunganisho wa mawasiliano. Anaelezea jinsi muunganisho wa mawasiliano unavyorahisisha mawasiliano ya kampuni mbali mbali za simu. Anatoa mfano muunganisho wa mawasiliano baina ya TTCL, Vodacom, Tigo, Airtel, Zantel, Sasatel na kampuni nyingine.
 
“Suala la muunganisho linapohusu mawasiliano ya kimataifa linasimamiwa na Umoja wa Simu Duniani (ITU) kama mdhibiti wa kimataifa wa mawasiliano. Usimamizi huo unahusu makubaliano yavifaa, viwango vya huduma na miongozo kuhusu malipo” (65).
 
Pia katika sura hii ya saba, mwandishi anaelezea juu ya namba ya simu kuwa rasilimali muhimu: “ Namba ya simu huwezesha mteja kutambulika mahali ilipo
Kijiografia; kampuni ambayo yeye ni mteja kujulikana; mteja kuunganishwa na mtumiaji mwingine wa simu katika eneo lake na eneo la mbali na hata nje ya nchi. Namba ya simu kwa mpangilio wake humwezesha mitambo kutambua chanzo cha simu na kuiwezesha mitambo hiyo kuielekeza kwenye kituo au vituo vya mpito mpaka kumtambua na kumfikia mlengwa” (Uk 67)
 
Kuhusu namba ya simu na udhibiti, mwandishi anafafanua hivi: “ Namba za simu ni rasilimali ambayo iwepo itahodhiwa na kampuni moja, itakuwa sirahisi kampuni hiyo kugawa rasilimali hiyo kwa kampuni nyingine, na hivyo kuzuia ushindani na kuongeza gharama kwa m teja wa simu. Kabla ya kufungua sekta ya mawasiliano ya simu na kuruhusu ushindani, TTCL ilikuwa ndiyo pekee iliyopanga na kutoa namba za simu. Baada ya soko la mawasiliano kuwa huru, jukumu la kupanga na kusimamia namba za simu limekuwa ni jukumu halali la Mdhibiti wa mawasiliano ya simu” (Uk 68).
 
Mwandishi, kwenye sura hii anaendelea kuelezea umuhimu wa namba ya simu, jinsi zinavyopangwa, namba za kila nchi na namba ya kila mteja. Kusema kweli hapa anatupatia elimu ambayo wengi wetu hatukuwa nayo.
 
Sura ya nane, mwandishi anatuelezea uhusiano uliopo kati ya serikali na mdhibiti. “Changamoto kubwa inayomkabili Mdhibiti yeyote hasa katika nchi zinazoendelea ni uhusiano wake na Serikali. Katika mazingira ya kawaida, changamoto hii haipaswi kumpa shida Mdhibiti au kuisumbua serikali. Kwanza, ili Mdhibiti awepo kisheria, ni Serikali ambayo inamwanzisha. La, pili na la muhimu ni madhumuni ya kuanzishwa kwa Mdhibiti na majukumu ambayo anapewa kisheria. Madhumuni makubwa ni kuhakikisha kwamba maisha ya wananchi yanaboreshwa. Madhumuni haya ndiyo yanayoifanya Serikali iwepo. Madhumuni haya hayawezi kuwa chanzo cha mgogoro kati ya serikali na Mdhibiti...” (70)
 
Kwa maoni ya mwandishi ni kwamba sheria zikifuatwa na kila mtu akajua mipaka yake, haiwezekani hata kidogo pakatokea changamoto kati ya Mdhibiti na Serikali. Lakini: “ Katika nchi kama Tanzania, mara nyingi hutokea kutokuelewana kati ya Serikali na mdhibiti hususan pale ambapo mwekezaji, au mtoa huduma anapoona kwamba kwa kupitia maamuzi yake mdhibiti, hataweza kuyapata yale anayoyataka na hasa katika kipindi alichojiwekea. Anakuwa hapendi ushindani huru, na kwa hakika huyu si mwekezaji mwenye tija...”
 
Mwandishi anatoa mifano kuonyesha changamoto zinazojitokeza kati ya mdhibiti na serikali ya Tanzania: “ Mawasiliano na makubaliano kati ya  Wizara ya Nishati na Madini na Songas yalikuwa ni njia ya kujaribu kukwepa udhibiti wa EWURA. Kama hii haitoshi, na kwa kuwa EWURA ilishikilia msimamo wake wa kuhakikisha Songas haikiuki maagizo ya kiudhibiti, Kampuni ya Songas ilifungua kesi kwenye Baraza la Ushindani (FCT). Katika tukio ambalo halitarajiwi kwenye utawala bora, Wizara ya Nishati na Madini na TANESCO waliamua kuisaidia Songas katika kesi yake dhidi ya EWURA ingawaje EWURA kwa wakati ule ilikuwa inatetea maslahi ya Taifa. Ikumbukwe pia kwamba waziri wa Nishati na Madini ni waziri msimamizi wa sekta ya nishati kwa mujibu wa Sheria ya EWURA, Sura ya 414 ya Sheria za Tanzania. TANESCO ilikwenda mbali zaidi na kuomba kuunganisha katika kesi hiyo kama mlalamikaji, yaani ikiungana na Songa dhidi ya EWURA katika shauri lililofunguliwa kwenye Baraza la Ushindani, ombi hilo lilikataliwa. Hata hivyo, mwezi Desemba 2009, Songas iliondoa mashitaka yake kabla hayajasikilizwa” (Uk 74)
 
Pamoja na mfumo mzuri unaoeleweka kama huu wa udhibiti, bado kuna changamoto na mgongano. Labda ni kwa vile mambo haya yalikuwa hayajafafanuliwa vizuri kama alivyofanya mwandishi wa kitabu hiki. Kwa mfano, mwandishi anaelezea vizuri nafasi ya waziri na katibu mkuu katika mfumo huu wa udhibiti na kuonyesha wazi kwamba kila mtu akifuata wajibu wake vizuri katika mfumo huu ni vigumu kabisa kutokea mgongano.
 
Sura ya tisa mwandishi anafafanua kwa kina juu ya udhibiti na ushindani wa biashara. Na hapa ndipo tunatambua utaratibu wa kumlinda mlaji na mtoa huduma na uhusiano wa udhibiti wa huduma na wa biashara.
 
Mwandishi anatoa historia ya chanzo cha kumlinda mlaji na mwongozo wa ushindani. Mfano hapa Tanzania “ Ili kusimamia, kukuza, na kulinda ushindani wa haki katika biashara, na kuwalinda walaji dhidi ya mwenendo wa soko usio na haki, ilitungwa sheria ya Ushindani wa Haki ya mwaka  2003 (Fair Competition Act, 2003). Sheria hii imeanzisha vyombo viwili vya kutekeleza azma ya Serikali ya kusimamia biashara ya haki vyombo hivi ni Tume ya ushindani (FCC), na Baraza la Ushindani (FCT). FCC inashughulikia udhibiti wa mwenendo unaokwaza au unaozuia ushindani wa kibiashara (anti-competitive conduct).” (Uk 84).
 
Sura ya kumi, mwandishi anafafanua na kuelezea kwa kina juu ya sheria za kisekta, taratibu, maagizo na miongozo ya kisheria.
 
Sura ya kumi na moja inaelezea vizuri uhusiano kati ya Bunge na Mdhibiti: “ Kwa upande wa Bunge, Mdhibiti anawajibika kwa njia moja iliyo dhahiri ambayo pamoja na uhuru alionao hawezi kukwepa. Fedha anazokusanya na kuzitumia Mdhibiti ni fedha za umma. Kwa mantiki hiyo, hesabu zake za mapato na matumizi hukaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG). CAG anatakiwa kuwasilisha ripoti ya ukaguzi wa hesabu hizo kwa Rais na baada ya hapo kupitia waziri mwenye dhamana ya fedha, ripoti hiyo huwasilishwa Bungeni...”
 
Mwandishi anaendelea kufafanua zaidi juu ya uhusiano uliopo kati ya mdhibiti na Bunge, hivyo kwa kukisoma kitabu hiki, msomaji atajipatia elimu zaidi juu ya suala zima la udhibiti wa huduma za kiuchumi Tanzania.
 
Sura ya kumi na mbili, mwandishi anaelezea na kufafanua udhibiti katika nchi nyingine. Hapa tunaelimishwa jinsi nchi nyingine zinavyofanya katika suala zima la udhibiti. Changamoto na mafanikio katika nchi nyingine. Hii inatufumbua macho na kutambua kwamba si Tanzania peke yake inatumia mfumo huu wa udhibiti wa huduma za kiuchumi.
 
Sura ya kumi na tatu, mwandishi anajadili masuala mtambuka, kama vile kupima ubora wa udhibiti, udhibiti wa utawala bora, kupima ufanisi wa udhibiti na uthibiti wa sera za kitaifa.
 
Sura ya kumi na nne, mwandishi anaelezea juu ya mafanikio na changamoto za udhibiti katika kusimamia utekelezaji wa sheria, utoaji wa Leseni, sekta ya mawasiliano, sekta ya maji, sekta ya umeme, sekta ya uchukuzi, sekta ya mafuta ya petroli na watumiaji wa huduma za kiuchumi.
 
Sura ya kumi na tano ni hitimisho: “ Kwa kuhitimisha, inatarajiwa kwamba huko utendako udhibiti hautahusika tu na fikra finyu ya udhibiti wa kiufundi. Tasnia ya udhibiti itapimwa, pamoja na mambo mengine, kwa jinsi uwepo kwake kutakavyokuwa kumechochea kasi ya kukua kwa uchumi wa nchi. Ili iweze kufanikisha jukumu hilo, lazima tasnia ya udhibiti iwe wakala wa mabadiliko ya mtazamo katika jamii, mabadiliko  yanayozingatia uaminifu, uwajibikaji, utawala bora, utawala wa sheria, amani, usalama, haki za binadamu, demokrasia, na wajibu wa kulinda kushirikisha jamii zisizojiweza katika maendeleo” ( Uk 140)
 
Sehemu ya mwisho ni marejeo.
 
 
V. TATHIMINI YA KITABU.
 
Nianze kwa kumpongeza Profesa Mark Mwandosya  kwa kazi hii nzuri sana aliyoiandika. Kusema kweli kazi hii inafundisha na kufumbua macho. Tulikuwa tukisikia EWURA, lakini hatukufahamu kwa undani hiki ni kitu gani. Wengine walifahamu kidogo, lakini hawakuwa na uelewa mpana na elimu ya kutosha juu ya chombo hiki. Sasa kwa kusoma kitabu hiki watafahamu zaidi. Tumekuwa tukisikia SUMATRA, lakini hakuna aliyetambua maana yake, zaidi ya kuchukiwa na wenye daladala na wasafiri. Kwa wengine SUMARA, ilikuwa ni kero na kuchukuliwa kwa kusema kwamba hii ni miradi ya wakubwa. Kwa ufafanuzi uliotolewa kwenye kitabu hiki, wale watakao soma kitabu hiki, wataelewa vizuri na hawezi hata siku moja kuibeza na kuichukia tena SUMATRA.
 
Pili, nimpongeze mwandishi wa kitabu hiki kutumia lugha ya Kiswahili kuandika kitabu hiki. Imekuwa ni tabia ya wasomi wetu kuandika kwa lugha za kigeni na kuifanya elimu kuwa ni faida wanayoipata  wachache. Kwa kuandika kitabu hiki kwa lugha ya Kiswahili, watu wengi watakisoma na kuipata elimu hii.
 
Tatu, ni kumshukuru kwa kuandika. Wanasiasa wetu wanapenda kuhubiri na kupiga siasa za maneno bila kuandika. Viongozi ambao wanapata uzoefu mkubwa kwa kutunga sera na sheria, na baadaye kusimamia utekelezaji wa sera hizo na sheria hizo, hawafanyi kazi kuandika ili uzoefu wao uwe na faida leo, kesho, keshokutwa na siku zijazo. Profesa Mwadosya amefanya kazi hii kubwa kama anavyosema yeye mwenyewe: “ ...wazo la kuandika kitabu hiki ni na chimbuko lake ni mazungumzo niliyoyafanya na wenzangu wawili: Ndugu Haruna Masebu, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji; na Profesa John Nkoma, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano. Mazungumzo haya yalifanyika ofisini kwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Ubungo, Dar-es-Salaam, tarehe 7 Septemba 2009. Sote, kwa nafasi zetu tofauti, tulikuwa tumehusika katika mijadala ya kisera, kuandaa miswada ya sheria na kuanzisha mamlaka za udhibiti. Baada ya mjadala mrefu, tukakubaliana kwamba njia pekee ya kuwa na mchango wa kudumu kwa Taifa, ni kwa kila mmoja wetu katika nafasi yake kuweka katika maandishi, uelewa na uzoefu tulioupata, tukiamini kwamba uelewa na uzoefu huo utakuwa wenye manufaa katika usimamizi wa uchumi ,kwa zama hizi, na rejea muhimu kwa zama zinazokuja” ( xviii – xix)
 
Nne, ni kumshukuru mwandishi jinsi alivyofafanua Udhibiti, historia yake, sera yake na  sheria zake. Kusema ukweli, baada ya kukisoma kitabu hiki mtu anakuwa na ufahamu mpana juu ya suala hili la udhibiti. Ni vigumu kabisa baada ya kukisoma kitabu hiki mtu akapinga suala hili.
 
Tano, ni kumshukuru mwandishi, ambaye ni mwanasiasa na kada wa chama tawala kukumbuka usomi wake, na kuandika kitabu hiki “Kisomi” bila kutawaliwa na “upepo” wa siku hizi wa kushabikia vyama vya siasa hata pale ambapo si nafasi yake. Mwandishi ameandika kitabu hiki kwa watanzania wote bila kuangalia itikadi za siasa, maana ustawi wa jamii na maendeleo ya watanzania ni ya wote na wala hakuna itikadi. Ameandika kitabu chake, neno la kwanza hadi la mwisho bila kutaja CCM. Hii si kawaida kwa kada wa  chama kwa utamaduni uliojengeka. Angeweza kusema kwamba udhibiti ni sera iliyoanzishwa na chama cha mapinduzi. Angeweza kukitukaza chama chake kwa mafanikio hayo, kama tulivyozoea, lakini Profesa Mwandosya, ameonyesha kuvuka mipaka ya “Uchama”; wakati huu ambapo taifa letu linaelekea kuchanganyikiwa na kuingia kwenye mapambano ya vyama vya siasa; tunawahitaji watu kama Profesa Mwandosya, ili waweze kuturudisha kwenye njia sahihi.
 
 
VI. HITIMISHO.
 
Kama kawaida yangu, ningependa kuwashauri watanzania kukitafuta kitabu hiki na kukisoma. Wasiishie kusoma uchambuzi huu kwenye gazeti. Huu ni uchambuzi mfupi na kitabu ni kikubwa zaidi na kimesheheni mambo mengi ambayo nimeyagusia kidogo tu. Ni imani yangu kwamba kwa kukisoma kitabu hiki watajifunza mengi kutoka kwenye kitabu hiki na hasa juu ya ufafanuzi wa udhibiti na mambo mengine kama EWURA,SUMATRA  na mengine kama hayo ambayo kwa kiasi kikubwa yalikuwa ni msamiati kwa wananchi wengi.
 
Mwandishi ameonyesha wazi kwamba Tanzania bado haina sera ya kumlinda mtumiaji wa huduma za kiuchumi. Na kuonyesha wazi kwamba hakuna popote mtumiaji anaposhirikishwa katika uanzishwaji wa vyombo hivi vya udhibiti kama vile EWURA na SUMATRA. Hivyo ni muhimu hili kuzingatiwa ili itungwe sera ya kumlinda mtumiaji na ushirikishwaji wa watumiaji katika mfumo mzima wa  udhibiti.
 
Dokezo la mwandishi kwamba  “ Katika hali ya kawaida vyombo vya udhibiti vingeanzishwa kwanza kabla ya zoezi la ubinafsishaji. Ingekuwa vema pia iwapo zoezi la ubinafsishaji lingekwenda sambamba na uanzishwaji wa vyombo vya udhibiti...” (Uk 4) ni la kuzingatiwa, ingawa lilifanyika kinyume, lakini jitihada zinaweza kufanyika, hasa kwa kuwaelimisha watu juu ya mfumo huu wa udhibiti, kama mwandishi alivyofanya kwenye kitabu chake. Udhibiti usibaki ni “fumbo” au chombo cha kunyanyasa pande zote mbili, watoa huduma na watumiaji.
 
Pia, ni muhimu kuzingatia maneno yanayotolewa na mwandishi kwenye kitabu chake kama vile : “ Mamlaka za Udhibiti huwajibika kwa maamuzi yake, lakini pasipo na changamoto chanya baina ya serikali, Mamlaka za Udhibiti na watoa huduma, maendeleo hayawezi kupaikana”(Uk 100). Na “ Pamoja na uhuru wa Mdhibiti, ili aweze kufanikiwa ni muhimu Mdhibiti akayaelewa mazingira ya kisiasa” (Uk 100).
 
Kwa upande wake Profesa Mwandosya, amefanya kazi yake. Ametuelezea umuhimu wa kuwa na mfumo wa udhibiti na jinsi mfumo huu unavyopaswa kufanya kazi. Amedokeza changamoto na baadhi ya mafanikio. Mtu mwingine anaweza kuanzia hapa na kuandika juu ya mafanikio ya mfumo huu, je unafanya kazi, je ni kitu gani kinakwamisha mfumo huu? Je ni kuingiza siasa katika utendaji au ni watu kutotambua nafasi zao au ni watu kutofahamu mfumo wenyewe. Bado kuna kazi kubwa kwa upande wa wachambuzi, watoa huduma na watumiaji.
 
Na,
Padri Privatus Karugendo.
+255 754 633122
 

0 comments:

Post a Comment