KOSA SI UTANDAWAZI NI UTEKELEZJI

MAKALA HII ILITOKA GAZETI LA RAI 2004.


KOSA SI UTANDAWAZI NI UTEKELEZAJI

Makala ya Patrick Sombe: Utandawazi Ni Ubepari na Ubepari ni Unyama, RAI 571,ni sawa na makala nyingine zote zinazoandikwa juu ya utandawazi. Zinaibuka na kuzama bila ya kuamsha majadiliano, mdahalo na “malumbano” ya kina. Ukimya unaojitokeza bada ya kujitokeza makala kama haya ya Partick Sombe, una sababu nyingi: Inawezekana Utandawazi ni msamiati usioelekewa vizuri kama ule wa “Sandauda”. Nikiwa mtoto mdogo wazazi wangu walikuwa wakiaga nyakati za jioni kwenda kwenye “Sandauna”. Nilikuja kufahamu baadaye nikiwa sekondari kwamba “Sandauna” ilikuwa “Sun down party”, yaani tafrija ya jioni. Leo hii kijijini kwetu bado kuna watu ambao wanaongelea “Sandauna” hata kama tafrija, sherehe au arusi ni ya asubuhi au mchana!

Inawezekana Utandawazi bado ni msamiati usioeleweka vizuri miongoni mwa watanzania walio wengi. Faida, hasara na athari za utandawazi hazifahamiki. Inawezekana watu wananufaika na faida za utandawazi bila kujua, au wanajiingiza kwenye matatizo na kuathirika bila kujua kwamba shinikizo ni utandawazi. Lakini pia inawezekana ni ule utamaduni wetu tuliouzoea wa kuchaguliwa kila kitu: Ukija ujamaa, sawa! Ubepari nao tukiletewa ni sawa! Soko huria, ni sawa! Utumwa nao ni sawa hata ukoloni ni sawa! Ngoma inayopigwa, tuko tayari kuicheza! Hatujajenga utamaduni wa kuchagua lile tunalolitaka na kulisimamia kwa gharama yoyote ile. Hii inaweza kwenda na tabia ya kila mtu kushughulikia mambo yake. Kila mtu anaangalia kile kitakachomletea yeye faida. Si kuangalia taifa ya jirani, faida ya kijiji, faida ya wilaya, faida ya mkoa au faida ya taifa.

Sababu nyingine ya kukaa kimya ni yale tuliyoyazoea: Kutokuwa na utamaduni wa kujisomea, ni watu wachache wenye hamu ya kusoma makala ndefu na hasa yenye mambo yasiyovutia kama ya utandawazi. Tabia ya kutofanya utafiti na kuhoji mambo mbali mbali na hasa watu wanakuwa na ule woga wa kuitwa mpinzani pale mtu anapotoa mawazo yanayokinzana na yale ya viongozi. Kwa vile kiongozi anataja utandawazi, basi kuhoji au kuuliza ni dhambi. Wakati mwingine viongozi wanatumia neno utandawazi pasipohusika na linakuwa halina maana yoyote ile – watu wanakaa kimya ili wasiitwe wapinzani!

Inashangaza, inauma na inakatisha tamaa kuona watu wanakaa kimya kwa jambo kama hili linalogusa uchumi wa taifa letu, linalogusa maisha na uhai wa kila Mtanzania. Bila majadiliano, bila uwazi, bila uzalendo, bila kulipenda taifa letu, utandawazi utatushinikiza hadi uchumi wa taifa letu utagonga mwamba. Uchumi ukigonga mwamba, kila kitu kitasambaratika. Amani itapotea, uhuru utapotea na utu utakimbia! Hili liko karibu kabisa!

Katika makala haya sipingani na Patrick Sombe, ila ninatofautiana naye kidogo pale anaposema, Utandawazi ni Ubepari na Ubepari ni Unyama. Hivyo basi Utandawazi ni unyama! Hapana! Utandawazi si unyama. Utandawazi unaonyesha sura ya unyama pale panapojitokeza utekelezaji mbaya. Utekelezaji ukiwa mzuri, utandawazi ni kitu kizuri.

Utandawazi umeifanya dunia kuwa kijiji. Sasa hivi jambo linalotendeka sehemu moja ya dunia linajulikana haraka sana sehemu nyingine ya dunia. Nchi za Asia ya Mashariki zimenufaika katika biashara, masoko na teknolojia kwa sababu ya utandawazi. Utandawazi umeboresha huduma ya afya duniani kwa kiasi cha kuleta matumaini. Utandawazi umeamsha moyo wa vikundi mbali mbali duniani kujipanga upya na kubuni mbinu za kupigania demokrasi na haki za binadamu. Hivyo shida si utandawazi bali ni jinsi unavyotekelezwa.

Kinachokosolewa na wala si kupinga kama wengine wanavyofikiri ni mfumo wa mashirika matatu makubwa duniani yanayouongoza utandawazi. Mashirika haya ni: IMF ( International Monetary Fund), World bank na WTO(World Trade Organisation). IMF na World Bank, ni mashirika yaliyoanzishwa July 1944, kwenye mkutano uliofanyika Bretton Woods,New Hampshire, baada ya vita vya pili vya dunia. Lengo kuu likiwa ni kuijenga ulaya mpya baada ya uharibifu wa vita. IMF, ilipewa jukumu kubwa la kuangalia na kuimarisha uimara wa uchumi wa dunia. Mashirika haya yalifanya kazi nzuri katika harakati za kuijenga Ulaya mpya. Wakati huo nchi nyingi za Afrika zilikuwa bado chini ya utawala wa nchi za Ulaya, hivyo mashirika haya hayakujihusisha moja kwa moja na mataifa ya Afrika. Baada ya uchumi wa Ulaya kutengamaa na baada ya nchi nyingi za Afrika kupata uhuru, mashirika haya yalielekeza nguvu zote katika maendeleo ya uchumi wa nchi zinazoendelea. Mwelekeo wa mashirika haya ulibadilika ghafla kwenye miaka ya 1980, wakati Rais Ronald Regan wa Marekani na Margaret Thatcher wa Uingereza walipoanza kuimba wimbo wa soko huria. Mashirika haya yaligeuka kuwa vinara wa wimbo huu wa soko huria.

Leo hii shughuli karibu zote za IMF na World Bank ziko kwenye nchi zinazoendelea, lakini kwa makubaliano yasiyokuwa na majadiliano au kwa maneno mengine mipango ya wenye “nguvu”, kiongozi wa shirika la IMF ni lazima atoke kwenye nchi za Ulaya na kiongozi wa World Bank ni lazima atoke Amerika. Izingatiwe pia kuwa viongozi hawa hawana masharti yoyote ya kuzifahamu kwa undani na wakati mwingine mahali zilipo kwenye ramani ya dunia nchi zinazoendelea! Hivyo viongozi hawa mara nyingi wanakuwa ni wahudumu wasiowajua watu na nchi wanazozihudumia!

Na mfumo mzima wa mashirika haya hauruhusu maoni na mapendekezo kutoka kwenye nchi zinazoendelea. Kinachofanyika ni kutoka mikopo na masharti.

Wafanyakazi wa ngazi za juu katika IMF na World Bank, huchaguliwa kutoka kwenye mashirika makubwa ya kibiashara ya Ulaya na Amerika. Uchaguzi huu hufanyika kwa siri kubwa. Mfano, aliyekuwa katibu wa hazina ya IMF kwenye kipindi cha 1997-2000,bwana Robert Rubin, alichaguliwa kutoka kwenye bank kubwa ya Goldman Sachs yenye uhusiano wa karibu na Citibank. Baada ya kipindi chake, IMF, aliendelea na kazi kwenye Bank ya Goldman Sachs. Na kiongozi namba mbili wa wakati huo bwana Stan Fischer, alipatiwa kazi kwenye Citigroup, baada ya kumaliza kipindi chake IMF.

Mifano hii michache ni ya kuonyesha jinsi watendaji wa siku kwa siku wa mashirika haya makubwa wanavyokuwa pale kulinda maslahi ya makampuni na mabenki yanayokuwa yamewatuma pale. Ni vigumu watu hawa kufanya kazi kwa kuangalia maslahi ya nchi zinazoendelea!

Mfumo mbaya wa mashirika yanayouongoza utandawazi ndio yanaufanya uonekane kuwa kitu kibaya. Watu ambao wamepata nafasi ya kufanya kazi kwenye mashirika haya, wanayalaumu kwa kuendesha mambo yake kwa usiri mkubwa. Joseph E.Stiglitz, katika kitabu chake cha “ Globalization And its Discontents”, anaelezea vizuri sana jambo hili.

Bahati mbaya inayoukumba utandawazi ni kwamba hakuna kitu kama serikali ya dunia. Mbaya zaidi ni kwamba mpaka sasa hakuna chombo chochote kile kinachoweza kufanya kazi kama serikali ya dunia. Tunakazania utadawazi wa utawala, kama ule unaongoza mashirika ya IMF,World Bank na WTO, bila kushughulikia utandawazi wa serikali ya dunia. Wengine wana mawazo ya ulazima wa kuwepo na utandawazi wa maoni, utandawazi wa elimu na utandawazi wa mashirika ya kijamii.

Mfano, ruzuku ambayo Amerika, inawapatia wakulima wake 25,000, wa zao la pamba ni kubwa kuliko kile wanachozalisha. Hali hii inawanyima wakulima wa pamba wa Afrika kuingia katika ushindani wa soko la pamba. Hii inawasababishia wakulima wa Afrika wa zao hili la pamba kupoteza dola milioni 350 kila mwaka. Hasara hii ni kubwa kuliko msaada wa Amerika inayoutoa kwenye nchi hizi kila mwaka. Kwa maneno mengine ni bora, Amerika kuacha kutoa msaada kwa nchi hizi, lakini ikasitisha kutoa ruzuku kwa wakulima wake wa pamba. Nchi zilizoendelea zinazibana nchi zinazoendelea kuacha kutoa ruzuku kwa viwanda vyao, lakini wenyewe wanaendelea kutoa ruzuku wa wakulima wao.

Nchi zilizoendelea zinashinikiza nchi zinazoendelea kufungua milango ya masoko yao, lakini zenyewe zinafunga milango ya masoko yao na hasa soko la mazao ambacho ndicho kitu cha msingi katika uchumi wa nchi nyingi za Afrika.

Kauli mbiu ya World Bank ni; “Our Dream is A World Without Poverty” tafsiri isiyokuwa rasmi, Ndoto yetu ni dunia isiyokuwa na umasikini”. Sasa hivi zaidi ya watu milioni 100 wanaishi kwenye umasikini unaonuka. Asilimia 46 ya watu wanaoishi Afrika kusini mwa jangwa la Sahara kipato chao ni chini ya dola moja kwa siku, wakati tunaambiwa kipato cha dunia kinaendelea kuongezeka kwa wastani wa asilimia 2.5 kila mwaka ( World Bank: Grobal Economic Prospects and the Developing Countries 2000).

Ili utandawazi ufanikiwe, ni lazima mifumo ya mashirika haya ibadilike. Mfumo wa sasa wa mashirika haya umeufanya utandawazi kushindwa vibaya katika nchi zinazoendelea. Hasa nchi zinazofuata masharti na mikopo ya IMF, zinashindwa vibaya sana. Ni lazima kuundwa chombo chenye madaraka ya kuangalia mambo niliyoyataja. Chombo cha kuweza kuzishinikiza nchi zinazoendelea kufungua milango ya masoko yao, chombo chakuweza kushinikiza mashirika haya kuongozwa na watu wa kutoka nchi zinazoendelea. Chombo cha kuweza kuyashinikiza mashirika haya kuingia kwenye meza ya majadiliano.

Botswana, ni kati ya nchi zilizofanikiwa na kuwa na uchumi mzuri bila kupata mikopo ya IMF. Ilifanikiwa vipi? Siri kubwa ya mafanikio haya ni kwamba viongozi wa Botswana, walikuwa waangalifu katika kuwachagua washauri katika mambo ya uchumi. Pili viongozi walikuwa na uzalendo. Walilitanguliza taifa lao, badala ya kuyatanguliza matumbo yao! Shirika la Ford Foundation, liliwashauri vizuri viongozi wa Botswana. Mipango yote ya maendeleo na uchumi ilijadiliwa na watu wote katika ngazi za vijiji hadi Bungeni. Semina mbali mbali ziliendeshwa vijijini hata na miongoni mwa mawaziri na wabunge. Mipango iliyopitishwa ilikuwa imekubaliwa nchi nzima. Hivyo ilitekelezwa na kila mmoja kwa moyo mkunjufu na uzalendo. Ingawa sasa hivi Botswana, inashambuliwa na UKIMWI kwa kasi kubwa na watu wengi wamekufa, lakini uchumi wake ni mzuri na wagonjwa wa Ukimwi, wanapata huduma nzuri kuliko popote Afrika. Pato kubwa la Botswana linategemea madini na mifugo! Karibu nchi zote za Afrika na Tanzania ikiwemo zina madini na mifugo, lakini kwa kukumbatia ushauri mbaya na kutokuwa na moyo wa uzalendo uchumi unakuwa mbaya kila kukicha.

Mashirika ya IMF na World Bank, hayana mfumo kama wa Ford Foundation, wa kuwashirikisha watu katika maamuzi. Mfumo wao ni wa kujadiliana na mawaziri wanaohusika na magavana wa mabenki. Miradi na mikopo wanayoitoa haijulikani kwa wananchi ambao ndio wanabeba mzigo wa kulipa madeni.

Hatuwezi kujilaumu sisi Tanzania, kuyakumbatia mashirika haya, maana ukishafanya kosa la kuyakubali ni vigumu kuyakataa. Ukiyakataa ni kujitenga na dunia nzima. Maana mashirika haya yakikutangaza vibaya, huwezi kumpata mwekezaji, hata na watalii wataikimbia nchi yako. Mashirika haya yanatawala karibu biashara yote ya dunia.

Kosa la Tanzania, ni uzalendo mdogo. Watu wanatanguliza matumbo yao badala ya kuitanguliza nchi. Ni kujiingiza kwa kasi katika mambo ambayo hatujafanyia utafiti. Tulijiingiza kwenye utandawazi kwa kasi, tumefanya ubinafsishaji kwa mwendo wa kutisha, tumeruhusu wawekezaji bila kutanguliza maslahi ya taifa. Watu hawakushirikishwa katika maamuzi mengi yanayogusa uchumi wa taifa letu. Tumejiingiza kwenye moto. Sasa hivi mtu yeyote anayonyesha kuusahihisha utandawazi, mwenye mawazo ya uzawa, mwenye kupinga soko huria, mwenye kupinga ubinafsishaji hawezi “kuteuliwa” kuliongoza taifa letu. Awe ni wa CCM au vyama vya upinzani. Mashirika ya kimataifa, makampuni yaliyowekeza katika taifa letu lazima yahakikishe (pesa) anachaguliwa mtu asiyefahamu lolote juu ya utandawazi au yule anayefahamu lakini anaweza kuingia mfukoni kiurahisi. Ni lazima mashirika na makampuni yahakikishe yanavuna vya kutosha kabla ya kututupia makapi. Hii imetokea kwenye nchi mbali mbali ambako utandawazi uliendewa kwa kasi. Ninachotaka kusema ni kwamba tunataka tusitake uchaguzi wa 2005 hauwezi kuwa mikononi mwetu, utakuwa mikononi mwa mashirika ya kimataifa na makampuni makubwa kutoka nje ya nchi yetu. Hapo ndipo mtu anaweza kusema kwamba utandawazi ni unyama. Kwa kifupi, tumetawaliwa tena! Zamu hii si ukoloni, bali utumwa!

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment