MKIA WA SHETANI

MAKALA HII ILITOKA KWENYE GAZETI LA RAI 2004.

MKIA WA SHETANI.

Waingereza wana msemo usemao: “ Umeongelea shetani, ukauona mkia wake”(tafsiri ni yangu). Alhamisi iliyopita nilijadili kuhusu watanzania kujichukulia sheria mikononi; kuwachoma moto na kuwaua vibaka, majambazi, wezi na wahalifu wengine kama vile wavuvi haramu wanaovua kwa kutumia sumu. Kama usemavyo msemo wa Waingereza, siku hiyo ya Alhamisi ya tarehe 18.11.2004, niliuona mkia wa shetani. Vyombo vya habari vilitangaza habari za bwana mmoja(Dodoma?) na watoto wake wawili waliouawa na wanakijiji wenye hasira kwa kosa la uharibifu wa chanzo
cha maji. Kero zinaongezeka katika jamii yetu. Ilianzia kwa vibaka, na bado inaendelea, maana akikamatwa kibaka, kama hakuna muujiza wa kujitokeza polisi, hukumu ya kibaka ni kifo. Baada ya vibaka ilifuata kero ya majambazi, wezi na vikongwe – wote hawa hukumu yao ni kifo! Kero iliyoshika kasi baada ya hizi nilizozitaja ni uvuvi haramu wa kutumia sumu wanaokamatwa hukumu yao ni kifo! Leo tumeingia hatua nyingine ya uharibifu wa vyanzo vya maji. Ni nani ajuaye ni kero gani itafuata? Labda wala rushwa watakamatwa na kuchomwa moto na wananchi wenye hasira. Labda wale wanaohujumu uchumi wetu watakamatwa na kuchomwa moto na wananchi wenye hasira. Hii inaweza kuendelea hadi kufikia kwa wanasiasa waongo wanaotoa ahadi za uongo kila mwaka wa uchaguzi – watakamatwa na kuchomwa na wananchi wenye hasira. Wabakaji na wale wanaowanajisi watoto watoto wadogo watakamatwa na kuchomwa moto!

Kana kwamba haikutosha kwa siku hiyo ya tarehe 18.11.2004, nikiwa kwenye daladala Jijini Mwanza, nilikwapuliwa “wallet” yangu, iliyokuwa na pesa si zangu tu bali na za michango ya harusi ya jamaa yangu anayetarajia kufunga pingu za maisha hivi karibuni!

Si lengo la makala hii kuelezea nilivyokwapuliwa “wallet” yangu. Ni imani yangu kwamba tukio hili ni la kawaida na limewakumba watu wengine wengi. Wengine wanakwapuliwa simu za mikononi, saa, mikufu ya dhahabu, mikoba yenye pesa nk. Tukio la kukwapuliwa “wallet” ni tofauti kidogo na lile lililonipata 2002, la kutapikiwa na vijana wa Mererani, kwenye daladala ya Arusha- Moshi. Baada ya tukio hili, nilipofika mwisho wa safari yangu, nguo zilifuliwa na mimi mwenyewe nilioga na kurudi katika hali ya kawaida. Kukwapuliwa “wallet” yenye pesa za kukutunza mwezi mzima na ukizingatia jinsi pesa ya Mkapa, inavyoteleza kama nyoka, ni tukio zito kidogo.

Nimeandika makala hii kustaajabu, kusikitika na kuujadili huu msemo wa Waingereza. Alhamisi iliyopita niliongelea shetani, nikauona mkia wake! Jambo lililonisukuma kujadili tukio hili la kukwapuliwa “wallet” ni mambo mawili yanayohusiana kwa namna fulani. La kwanza ni kwamba nilimtambua kibaka aliyenikwapulia “wallet” yangu. Ni mtu niliyekaa naye kiti kimoja kwenye daladala. Niliogopa kumtaja, maana ningefanya hivyo, angepoteza maisha yake pale pale. Dadala dala ilikuwa imejaa, na watu hawataki kusikia kitu “mwizi”. Ninaungama wazi kwamba hata marafiki zangu wa Mwanza, sikuwaambia juu ya ukweli huu kwamba nilimtambua kibaka. Wangeniona mtu wa ajabu kumtambua kibaka na kuamua kukaa kimya. Ukweli huu sasa watausoma kwenye gazeti wakati joto la tukio limekwisha poa!

La kujadili hapa ni je, nilifanya kitendo cha upumbavu kumwachia kibaka kuondoka na pesa ambazo karibu zote hazikuwa za kwangu? Je, ulikuwa ujinga mimi baadaye kushinda ninahangaika huko na kule Jijini Mwanza, nikitafuta mkopo wa kulipa pesa zilizokwapuliwa na yule kibaka? Je, kibaka huyu ni aina ile ya vijana wa Mererani? Je, alizihitaji pesa saidi yangu mimi? Je, alizihitaji pesa hizo kwa ajili gani? Kunywa pombe na baadaye kuwatapikia watu kwenye daladala? Je, alizihitaji kuwatunza wadogo zake? Kununua chakula, dawa kutoa sadaka na zaka kanisani na msikitini. kulipia kodi ya nyumba? Je, kibaka huyu ni aina ya akina Neema Lukelo, mtoto yatima aliyetoa mada ya kugusa na kuchoma kwenye mkutano wa mwaka wa mfuko wa pensheni ya mashirika ya Umma (PPF). Neema Lukelo, alisema “ Mimi ni mtoto yatima, wazazi wangu wawili wamekufa kwa ugonjwa wa UKIMWI....... kuanzia hapo athari za UKIMWI ziliendelea kunipata bila kujua, mawazo ya mzigo wa kujilea na kulea wadogo zangu yalinijia nikaanza kupoteza mwanga wa matumaini.... nafikiria nitafanyaje juu ya mwaisha yangu na ya wadogo wangu, nimemaliza darasa la saba nasubiri matokeo na hata kama nikifaulu ni nani atanipa mahitaji muhimu ya shule mimi na wadodo zangu! Ni kweli ndugu wa mama au baba watanipa? Je, walipanga tangu awali? Ni ghafla mno kwao....”.

Je, mtu kama Neema Lukelo, akiamua kuwa kibaka kwa lengo la kupata pesa za kujilea yeye na wadogo zake, akikamatwa, anatahili hukumu ya kifo bila kupata nafasi ya kujieleza na kujitetea? Je, akiamua kuomba ni wangapi watamwamini na kumsaidia? Yule kibaka aliyekwapua “wallet” yangu, angenielezea juu ya maisha yake, kwamba yeye ni mtoto yatima na ana jukumu la kujilea yeye mwenyewe na kuwalea wadogo zake, na kwamba hajala mlo wowote kwa siku mbili, hajalipa kodi ya nyumba na mwenye nyumba anatishia kumtupa nje yeye na wadogo zake. Ningeweza kumsaidia? Je, kama ni wewe umekaa kwenye daladala ungeamini “story” ya huyo kibaka na kumsaidia? Neema Lukelo, aliwauliza swali gumu wajumbe wa mkutano wa mwaka mfuko wa pensheni ya mashirika ya Umma (PPF): “Je, ninyi wazazi wangu ambao mpo hapa ni wangapi kati yenu mnawatunza watoto yatima, Je matunzo hayo mnayowapa hasa kuhusu elimu ni sawa na mnayowapa watoto wenu? Najua ni vigumu bajeti zenu hairuhusu maana hamkuwa mmepanga hayo, najua hizo ndizo athari za UKIMWI.”

Watoto yatima wanaofanana na Neema Lukelo, ni wengi na wataendelea kuwa wengi. Ni vigumu kuwatambua kwa kuwaangalia machoni. Ni vigumu pia kuwahukumu kwa matendo yao. Mtoto yatima anaweza kuwa na tabia nzuri na mtoto mwenye wazazi akawa na tabia nzuri. Bila kujenga jamii inayosikiliza, kujali na kujadiliana kuna hatari ya kuyang’oa magugu na ngano nzuri ambayo kama ingeruhusiwa kukua sambamba na magugu ingeweza kuzaa matunda mengi. Si kila kibaka anakuwa na nia mbaya na si kila kibaka anastahili hukumu ya kifo. Hata hivyo uhai ni kitu cha thamani kubwa kuliko kitu kingine hapa duniani.

Idadi ya vibaka inaongezeka kadri idadi ya watoto yatima na watoto wa mitaani inavyoongezeka. Ni nani anajali maisha ya watoto yatima? Ni nani anashughulikia maisha bora ya watoto wa mitaani? Tunawaona wakilala na kuishi mitaani, sisi tunapita na kuendelea na shughuli zetu Watoto hawa wanatoka wapi? Inawezekana ni watoto wa ndugu zetu, rafiki zetu au watoto wetu. Mitaa, haina uwezo wa kuzaa watoto. Inawezekana kila Mtanzania anahusika kwa njia moja ama nyingine kwa ongezeko la watoto wa mitaani. Watoto hawa, hawana kipato, hawana elimu, hawana chakula, hawana mahali pa kulala. Na mbaya zaidi hakuna wa kuwasikiliza. Je, watoto hawa wakilazimishwa na hali na kuamua kuwa vibaka tuwakamate na kuwachoma moto?

Katika kulijadili hili tunaweza (tukipenda) kuongozwa na maneno haya: “ Mmesikia kwamba ilisemwa: ‘ Jicho kwa jicho, jino kwa jino’. Lakini mimi nawaambieni, usimlipize kisasi mtu mbaya. Mtu akikupiga kofi shavu la kulia, mgeuzie pia shavu la pili. Mtu akikupeleka mahakamani kutaka kukuchukulia shati lako, mwache achukue pia koti lako. Na mtu akikulazimisha kuubeba mzigo wake kilomita moja, ubebe kilomita mbili...” ( Matayo 5:38-41).

Haya ni maneno ambayo baadhi yetu wanayasoma kila siku ya Mungu, wengine wanayahubiri na kuwalazimisha watu kuishi kwa kuyashika na kuyafuata maneno haya, lakini hata wenyewe (wahubiri) hawako tayari kuwasamehe vibaka na majambazi. Kufuatana na maneno hayo hapo juu, mimi nilipokwapuliwa “wallet”, ilibidi nimfuate yule kibaka na kumpatia viatu vyangu, shati langu na mkoba wa nguo niliokuwa nimeushikilia mkononi. Ni ngumu kuamini – lakini tumeshauriwa hivyo kama kweli tunataka kujenga jamii yenye imani na amani. La msingi si vitu, bali kushirikishana furaha na utulivu wa rohoni.

Jambo la pili lililonisukuma kujadili tukio hili la kukwapuliwa “wallet” yangu ni kuwashirikisha wasomaji wa gazeti la RAI, maoni ya rafiki zangu wawili juu ya tukio hili. Rafiki yangu niliyemjulisha tukio hili akiwa mtu wa kwanza alinitumia ujumbe wa maandishi kupitia kwenye simu yake ya kutangatanga : “ Pari Karugendo, umepata fundisho. Tangia leo ukome kuwatetea vibaka na majambazi. Umeongelea shetani na kuuona mkia wake. Ujue kwamba dawa ya vibaka ni moja tu nayo ni kuwachoma moto hadi kufa”.

Rafiki yangu wa pili alikuwa na maoni tofauti kabisa. Huyu anafanya kazi kwenye chama cha Msalaba Mwekundu (RED CROSS): “ It is true ‘ there is nothing worthy Human life in your pocket’, huwa tunaambiwa sisi Red Cross, tunapoenda abroad kufanya kazi.”

Haya ni maoni tofauti ya watu wawili ambao wote ni marafiki zangu wa karibu. Yote nimeyapokea na kuyatafakari ingawa sikubaliani na kila kitu. Hivyo uwanja uko wazi- kila msomaji wa RAI, anaweza kutoa mchango wake. Hoja kuu ni je, tuendelee kuwachoma moto na kuwaua vibaka, majambazi, wezi na wahalifu wengine au watu hawa wapatiwe nafasi ya kutubu, kujirekebisha kujifunza na kuendelea kutoa mchango wao katika kulijenga taifa letu. Hoja nyingine ya nyongeza inaweza kuwa, je, maana ya utawala bora, utawala wa kisheria ni kuendelea kuwaachia wananchi kuzishughulikia kero zao zote kwa kujichulia sheria mikononi mwao? Wakati wa majadiliano ni lazima kuzingatia kwamba matendo ya vibaka, majambazi ,wezi na uhalifu mwingine wa aina yoyote ile hayakubaliki katika jamii yetu au jamii yoyote ile iliyostaarabika. Haya ni matendo yasiyofurahisha, yanavuruga amani na utulivu na kukwamisha maendeleo. Yote haya yakiwekwa kwenye mzani, tunabaki na swali moja la msingi: Tukio la kukwapua “wallet”, mkufu, saa, simu na mikoba linatosha kuutoa uhai wa mtu?

Si lengo langu kuushawishi mjadala huu. Ninalopenda kuweka wazi ni kwamba tuna changamoto mbele yetu. Changamoto ya kujenga jamii inayojali, inayojuliana hali, inayochukuliana na kujadiliana. Ni lazima tukwepe kwa nguvu zote kujenga jamii ambayo wachache wanakula na kushiba na kutupa wakati walio wengi wanalala njaa. Wachache wana nyumba za kifahari wakati walio wengi hawana mahali pa kulala. Wachache wanapata elimu na walio wengi wanabaki bila elimu. Wachache wanaendesha uchumi wa nchi na walio wengi wanabaki kuangalia na kusindikiza. Jamii kama hii ni lazima izalishe vibaka wengi, majambazi, wezi na wahalifu wa kila aina.

Kujenga jamii ni kazi ngumu. Inahitaji watu wa kujitolea, watu wenye upeo, wenye uzalendo watu wa aina ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Watu wasiokuwa na uchu wa madaraka, mali na anasa. Kujenga jamii ni kazi ya muda mrefu, si kazi ya mtu kufanya na kutegemea matunda. Ni kazi ya kila mtu kuchangia kwa kujenga msingi ambao kila jiwe linapangwa kwa vipimo sahihi. Si kazi ya kulipua kama tunavyofikiri na kutenda siku hizi. Nchi zote zilizofanikiwa kujenga jamii bora zilinufaika kutokana na jasho la vizazi vilivyopita. Ni lazima na watanzania wa leo tukubali kutoa jasho, kupata shida na kujitoa muhanga kwa maandalizi ya Tanzania bora ya siku zijazo.

Karibu tujadiliane, tuelimishane, turekebishane na tushirikiane kulijenga taifa letu.

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment