USHINDI WA KISHINDO MAANA YAKE NI NINI?

MAKALA HII ILITOKA KWENYE GAZETI LA RAI 2004.

USHINDI WA KISHINDO MAANA YAKE NI NINI?

Bada ya uchaguzi wa serikali za mitaa, uchaguzi uliojaa vurugu, ghasia na mauaji, Chama tawala cha CCM, kimejigamba kwa kuushinda uchaguzi huu kwa kishindo. Na kwamba hizi ni mvua za rasharasha, maana mvua za masika ni mwakani wakati wa uchaguzi mkuu! Ukitaka kuiona furaha ya Mheshimiwa Rais William Benjamin Mkapa, mwangalie wakati akijigamba juu ya ushindi wa kishindo wa uchaguzi wa serikali za mitaa na ushindi wa kishindo unaotarajiwa na chama chake cha CCM kwenye uchaguzi mkuu mwakani, ni furaha kubwa inayoamsha tafakuri nzito. Nimekuwa nikitafakari jambo hili kwa makini. Ni imani yangu kwamba kila Mtanzania mwenye kulitakia mema taifa letu atakuwa anatafakari jambo hili pia: Ushindi wa kishindo maana yake nini? Ni kweli kwamba CCM imeshinda kwa kishindo katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliomalizika hivi majuzi?

Tuangalie mfano huu: kitongoji chenye wakazi 800. Waliojitokeza kupiga kura ni 400 tu! Kati ya hao 380 walipiga kura za hapana kwa mwenyekiti wa kitongoji na 20 ambao ni wanachama wa CCM walimpigia kura za ndiyo mgombea wa CCM, maana alisimamishwa peke yake kugombea baada ya wagombea wengine wa vyama vya upinzani kuwekewa mizengwe na kuenguliwa katika kinyanganyiro cha kugombea. Mgombea mwenye kura 20 za wakazi 800, anatangazwa kuwa mwenyekiti wa kitongoji cha Lubamba! Je, mwenyekiti huyu anakuwa amechaguliwa kweli na wakazi wa Lubamba, kuwa mwenyekiti wao? Au anakuwa ni mwenyekiti wa wanaCCM peke yao? Je, huu ndio ushindi wa kishindo tunaousikia? Kitongoji cha Lubamba ni jina la kubuni, lakini huu ni ukweli uliotokea katika baadhi ya vitongoji kwenye uchaguzi uliopita Niko tayari kukosolewa!

Mfano mwingine: Kitongoji cha Bambalu, jina la kubuni pia, kina wakazi 500. Waliojitokeza kupiga kura ni 200 tu! Na matokeo yalikuwa hivi; mgombea wa CHADEMA, alipata kura 50, mgombea wa CUF alipata kura 55, mgombea wa TLP alipata kura 20, mgombea wa NCCR-Mageuzi alipata kura 25 na mgombea wa CCM alipata kura 100! Ingawa kura ni nyingi kuzidi idadi ya watu waliopiga kura mgombea wa CCM anatangazwa kuwa mwenyekiti wa kitongoji cha Bambalu! Je huu ndio ushindi wa kishindo tunaousikia? Hii ni mifano tu ya kubuni. Niko tayari kukosolewa! Lakini maeneo ambayo yamepata matukio kama haya watakubaliana na mimi kwamba ushindi wa kishindo wa CCM katika uchaguzi wa serikali za mitaa hauwezi kupita hivi hivi bila ya kuhojiwa!

Ni chombo gani kiliusimamia uchaguzi huu? Chombo huru, kisichokuwa na upendeleo na kuegemea upande wowote – uwe upande wa CCM au upande wa vyama vya upinzani? Nilishuhudia walimu wa shule za msingi wakisimamia uchaguzi huu wa serikali za mitaa. Ingawa si lazima mwalimu awe mwanachama wa CCM, lakini kila mwalimu katika shule za serikali ni mwajiriwa wa serikali inayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi na katika wilaya anakuwa moja kwa moja chini ya mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ambaye ndiye mwajibikaji mkuu wa uchaguzi wa serikali za mitaa katika wilaya. Hivyo ni vigumu kwa walimu wa shule za msingi kuendesha uchaguzi kwa haki bila ya kuwa na tahadhari kubwa ya kutomsaliti mwajiri wao!

Hoja inayojitokeza hapa ni kwamba kwa vile CCM ni chama tawala, na tukizingatia mfumo mbovu tulionao, mfano wa kutokuwa na tume huru ya uchaguzi; CCM inakuwa imezungukwa na vyombo vya kuisaidia si kushinda bali kulazimisha ushindi katika baadhi ya maeneo ambayo yana upinzani mkali.

Siwezi kujifanya kipofu na au kujidanganya kwamba CCM haikushinda kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa uliopita. CCM, imeshinda lakini si kwa kishindo! Imeshinda kwa mizengwe, ujanja, kulazimisha na kwa kutumia nguvu za dola!

Kukubali kwamba CCM imeshinda kwa kishindo ni sawa sawa na kumshangilia mtu mzima wa miaka 45 mwenye kilo 100 anapopigana na mtoto mdogo wa miaka 12 na kumchakaza vibaya sana na mtu huyu kujigamba kwamba amemshinda nguvu mtoto huyo wa miaka 12 kwa kishindo! Kama si wendawazimu basi huo unakuwa mchezo wa kuigiza au ndoto za mchana!

Ushindani wa kweli unakubalika katika mazingira yaliyo sawa. Huwezi kumshindanisha mpiga ngumi mwenye uzito wa kilo 150 na yule wa kilo 80. Unakuwa unamtakia mnyonge kifo. Kwa mfumo wa siasa tulionao sasa hivi kuvipambanisha vyama vya upinzani na CCM ni sawa na kumpambanisha bondia wa kilo 150 na yule wa kilo 80. Ni kuvitakia vyama vya upinzani kifo! Vyama vingi vinaonyesha afya mbovu na vingine viko njiani kufa. Tumekuwa tukisema kwamba vyama vya upinzani havina nguvu inawezekana kuna ukweli fulani wa hoja hii, lakini la msingi si kwamba vyama havina nguvu ila ni kwamba vinapambana na Jitu! CCM, ina nguvu za dola, ina pesa za serikali, ina watu waliosinzia usingizi wa pono – piga garagaza wao ni CCM damu damu; wengine hawana hata viatu miguuni, hawana nyumba, hawana uwezo wa kulipa matibabu, hawana uwezo wa kuwapeleka watoto shuleni, hawana nguo, t-shirt za Chagua Mkapa, Chagua CCM, zimechanika – Mungu, bariki watapata nyingine mwaka kesho wakati wa kampeni. Inatosha watu hawa kuwapatia pilau na pombe wakati wa kampeni. Sehemu nyingine zoezi hili limekwisha anza. Ng’ombe wanachinjwa, pilau inapikwa na pombe juu. Hii inawatosha wakereketwa wa chama kuwa na nguvu za kutisha kuimba CCM baba CMM mama na CCM ina wenyewe. Ni kazi kubwa kupambana na chama chenye nguvu kama CCM!

Vyama vingine vya upinzani vinabweka tu! Ni bora mbwa anayebweka kuliko anayeng’ata kimyakimya! CCM, haibweki, lakini inang’ata! Mbwa, anayebweka akikung’ata unakuwa ni uzembe wako! Kubweka ni ishara ya tahadhari. Mbwa akibweka ni lazima mtu kukaa chonjo. Ndio maana mimi na watu wengine wanaoyachambua matuko ya siasa katika taifa letu tunakataa kuamini kwamba vyama vya upinzani vinaweza kusababisha umwagaji wa damu katika taifa letu. Vyama vya upinzani vinabweka tu na wala havina meno ya kung’ata! Ingawa ni kweli kwamba mbwa hata asipong’ata, akibweka anakuwa amehisi hatari. Mbwa akibweka, anasaidia pande zote mbili: Mwenye mali anatambua kwamba kuna hatari inakuja, hivyo anajiandaa kupambana na adui ili kuilinda mali yake. Kwa upande wa pili mbwa anayebweka anamsaidia mwizi kuhisi upinzani unaokuwa mbele yake na kuamua ama kukimbia au kusimama kidete na kupambana na mwenye mali.

Mbwa, asiyebweka ni hatari kwa pande zote mbili. Anamshambulia mwizi ghafla na kung’ata! Mwizi anaweza kukimbia kimyakimya, au kama wezi ni wengi mbwa anaweza kuzidiwa nguvu na mwenye mali akashambuliwa ghafla bila ya tahadhari yoyote!

CCM, haibweki! Inang’ata bila ya tahadhari yoyote ile. Mauaji yaliyotokea Zanzibar, baada ya uchaguzi mkuu wa 2000, yalikuwa ni kung’ata na wala si kubweka! Maandamano ni kubweka! Lakini kutumia risasi za moto kama zilizotumika kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa uliopita si kubweka! Wananchi wanapofikia hatua ya uamuzi wa kufanya maandamano wanakuwa wamelazimishwa kubweka. Tahadhari isipochukuliwa na wahusika, mtu hawezi kuwalaumu wananchi kwa matokeo mabaya Vyama vya upinzani vinapobweka, serikali isipochuchukwa tahadhari, lawama si vya vyama vya upinzani!

Kuna mifano mingi inayoonyesha kwamba CCM, haibweki. Ni heri ingebweka! Zoezi la kuwanyang’anya watu uraia lililojitokeza mara baada ya uchaguzi wa 2000, si kubweka. Zoezi hili lilikuwa likiwalenga wale waliokuwa wakibweka! Limetokea bara na visiwani!

Maamuzi mengi ya kibabe yaliyofanywa na serikali ya awamu ya tatu licha ya watu wengi kubweka na kupinga, yalikuwa ni ya kung’ata tu. Mfano ununuzi wa ndege ya rais, ununuzi wa rada uuzaji wa mashirika ya umma nk.

Uamuzi wa kufanya uchaguzi wa serikali za mitaa licha ya ushauri wa vyama vya upinzani na uamuzi wa mahakama – si kitendo cha kubweka. Ni kitendo cha kung’ata na matokeo yake tumeyaona.

Serikali ya awamu ya tatu kushindwa kuwakamata wala rushwa na kuipunguza makali rushwa ni kitendo cha kung’ata, Maana anayeshindwa kumkamata mlarushwa anakuwa naye ni mlarushwa! Waswahili wa Pemba hujuana kwa vilemba! Sasa hivi ni vigumu kupata huduma katika ofisi za serikali bila ya kutoa rushwa na hongo. Iwe rushwa ndogo au kubwa, rushwa ni rushwa na ni kero kubwa. Ni kweli kwamba serikali ya rais Mkapa, imefanya mambo mengi mazuri. Imejenga barabara, imejenga mashule, imejenga madaraja, imeboresha mahospitali, imekusanya kodi, imejitahidi kwa nguvu zote kupambana na ugonjwa wa UKIMWI, kwa kushirikiana na Uganda na Kenya imeimarisha ushirikiano wa nchi za Afrika ya Mashariki nk. – lakini bila kuitoa rushwa, kazi yote hiyo nzuri itakufa haraka. Barabara zitakufa, majengo yatabomoka hivi karibuni na hospitali zitakosa madawa. Rushwa ni adui wa kila kitu katika kusukuma maendeleo ya taifa.

Serikali ya awamu ya tatu imeshindwa kwa kiasi kikubwa kufundisha na kuhimiza uwajibikaji kazini. “Ametoka kidogo” ni msamiati usiojulikana popote duniani, isipokuwa Tanzania. Hivi tunapoingia kwenye ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, watanzania tutamezwa. Ajira watapata watu wa Kenya na Uganda, wasioufahamu msamiati wa “Ametoka kidogo”. Utaambiwa mtu “Ametoka kidogo” wakati wa kazi. Na mtu huyo harudi kazini mpaka baada ya masaa matu hadi matano! Mwisho wa mwezi mtu huyu anataka alipwe mshahara wa masaa yote ya mwezi. Pamoja na mambo yote mazuri yaliyofanywa na serikali ya awamu ya tatu, bila uwajibikaji na nidhamu ya kazi yote ni kazi bure! Mrema, alijaribu kujenga utamaduni huu wa uwajibikaji na nidhamu ya kazi, lakini ilikuwa nguvu za soda na zoezi halikuenda mbali. Kuna watu wachache sana wanaofanya kazi kwa kujituma na kwa nidhamu. Walio wengi ni akina “Ametoka kidogo”!

Vyama vya upinzani vinabweka: Nchi yetu ni lazima iwe na daftari la kudumu la wapiga kura! Matatizo yanayolizunguka daftari hili zote tumeyasikia. Tatizo ni lilelile, jinsi tusivyokuwa na tume huru ya uchaguzi ndivyo tusivyokuwa na tume huru ya kusimamia daftari hili la kudumu la wapiga kura. Hadi sasa daftari hili kwa kiasi kikubwa linasimamiwa na serikali inayoongozwa na CCM. Iweje CCM isijiandalie mazingira ya kushinda kwa kishindo kwenye uchaguzi mkuu wa mwakani?

Vyama vya upinzani vinabweka: Taifa letu linahitaji katiba mpya! Badala yake katiba inawekwa viraka kila kukicha. Sote tunajua madhara ya kuweka kiraka kipya kwenye nguo iliyochoka.

Hivyo si kweli kwamba vyama vya upinzani vinatishia kumwaga damu endapo havitashinda uchaguzi mwakani. Mungu, apishe mbali! Lakini endapo ikatokea damu ikamwagika, kama ilivyomwagika 2001, CCM ijiandae kubeba lawama zote na iwe tayari kuwajibika mbele ya Mungu na mbele ya watanzania wote.

CCM, inaonyesha dalili zote za kutaka kung’ang’ania madarakani, inaonyesha dalili za kutotaka kushindwa na hamu ya kushinda kwa gharama zozote zile. Hizi ndizo dalili za hatari na hizi ndizo dalili zilizosababisha nchi nyingine katika bara la Afrika kumwaga damu.

Na si kweli kwamba CCM, imeshinda kwa kishindo. Kujigamba kwamba imeshinda kwa kishindo kwenye kura za serikali za mitaa ni dalili mbaya pia. Ushindi wa kishindo unasubiriwa pale taifa letu litakapokuwa na katiba mpya, tume huru ya uchaguzi, vyama vyote vya siasa kuwa na hadhi sawa ya kujitangaza nchi nzima na nguvu za dola kutumika kuvilinda vyama vyote kwa usawa. Mazingira sawa katika uchaguzi ndio yanaweza kuleta ushindani wa kweli na kuwa chanzo cha ushindi wa kishindo. Tukumbuke kwamba taifa letu lina idadi ya watu zaidi ya milioni 35. Wanachama cha wa CCM si zaidi ya milioni 4?Niko tayari kukosolewa! Hivyo si kwamba CCM ina mvuto wa kishindo bali ni kwa vile imeshikilia UTAMU wa dola!

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment