VIWANDA VYA SAMAKI, WAVUVI, UVUVI HARAMU, MAWAKALA, UHARAMIA NA UJAMBAZI

MAKALA HII ILITOKA KWENYE GAZETI LA RAI 2004

VIWANDA VYA SAMAKI,WAVUVI,UVUVI HARAMU,MAWAKALA,UHARAMIA NA UJAMBAZI.

Majuma mawili yaliyopita niliandika makala juu ya Sangara. Nilionyesha jinsi Sangara, alivyo adui wa wavuvi wadogo wanaolizinguka ziwa Victoria. Adui mwingine mkubwa wa wavuvi hawa ambaye sikumtaja kwenye makala iliyopita ni viwanda vya kusindika minofu ya samaki. Viwanda hivi pia ni kichocheo kikubwa cha uvuvi haramu, ujambazi na uharamia katika ziwa Victoria. Kwa maneno mengine, viwanda vya samaki, wavuvi, uvuvi haramu, mawakala, uharamia na ujambazi katika ziwa Victoria ni mnyororo unaojisuka wenyewe! Huu ni mnyororo wa neema kwa walioneemeka na ni kitanzi cha wanyonge!

Mwaka huu mwezi wa tisa mwishoni nilihudhuria msiba wa mvuvi. Kijana mvuvi alifiwa na mke wake. Kufuatana na maelezo ya mzee wa hekima niliyekutana naye kwenye msiba huo wa mvuvi, siku hizi hali ya maisha inatulazimisha kuishi kitabaka au kimakundi, Kama msiba ni wa daktari, utakutana na madaktari, waganga na manesi kwenye msiba huo. Kama msiba ni wa mwalimu, utakutana na walimu na wanafunzi kwa wingi kwenye msiba huo na kama msiba ni wa mvuvi utakutana na wavuvi wengi. Watu wengine wanashiriki msiba, lakini mipango na michango mikubwa inakuwa mikononi mwa kundi husika. Maisha yanatulazimisha kuishi kitabaka, kufikiri kitabaka, kutenda kitabaka na kuongea lugha ya kitabaka au lugha ya vikundi. Maongezi ya madaktari ni tofauti na ya walimu, na maongezi ya walimu ni tofauti kabisa na ya wavuvi!

Katika msiba huu wa mvuvi nilikutana na wavuvi wengi. Lugha na maongezi yaliyoutawala msiba yalikuwa ya uvuvi. Siku nne za msiba mimi pamoja na waombolezaji wengine ambao hawakuwa wavuvi, tulikaa na kuwasikiliza wavuvi. Ilipobidi tulijadiliana na kupanuana mawazo. Makala hii ni matokeo ya maongezi na majadiliano katika msiba wa mvuvi. Na ni katika maongezi haya nilipojifunza kwamba viwanda vya kusindika samaki ni adui mwingine wa wavuvi wadogo.

Wavuvi wenyewe wanajigawa katika makundi matatu: Kundi la kwanza ni la wavuvi wa jadi. Hawa ni wavuvi ambao miaka nendarudi wamekuwa wakiishi kwa kutegemea uvuvi katika ziwa Victoria. Wanavua kwa kutumia mitumbwi midogo, nyavu kidogo na wakati mwingine wanavua kwa kutumia ndoana. Hili ni kundi la wavuvi wadogo. Kundi la pili ni la wavuvi waajiliwa. Hawa ni wavuvi wanaoajiliwa na matajiri wenye mitumbwi, nyavu na injini. Kwa kawaida kila mtumbwi unakuwa na wavuvi wanne. Kundi la tatu ni la wavuvi mawakala au wavuvi wafanyabiashara. Hawa ni wavuvi matajiri ambao wanamiliki mitumbwi, nyavu na injini na wananunua samaki kutoka kwa wavuvi wengine na kuwauzia wenye viwanda. Hawa ndo wenye siri ya bei ya kiwandani na bei ya mwaloni.

Ukiyaunganisha makundi yote matatu, inavyokadiriwa sasa hivi, utapata idadi ya wavuvi 80,000, katika mikoa ya Mwanza, Mara na Kagera. Idadi hii ya wavuvi inaongezeka kwa kasi ya kutisha. Kati ya mwaka 2000 na 2003 kulikuwa na ongezeko la silimia 42.9. Mwaka 2000,idadi ya wavuvi ilikuwa 55,985. Viwanda vya samaki vinaajili zaidi ya watu 200,000! Pia vinaingiza kipato cha bilioni 72 kwenye mikoa husika. Hivyo uvuvi si jambo dogo na wala si la kupuuzia. Kaa kitako!

Kuna aina nyingine ya mawakala, ambao si wavuvi. Hawa ni matajiri wenye pesa na wanafanya biashara ya samaki. Wananunua samaki kwa wavuvi na kupeleka viwandani. Hawa wanafanya karibu sana na wamiliki wa viwanda na wengine wanakuwa na hisa viwandani. Kundi hili lina ushindani mkubwa na wavuvi mawakala. Matokeo ya ushindani huu nitayataja baadaye kwenye makala hii.

Msiba niliohudhuria ulikuwa wa mvuvi mfanyabiashara au mvuvi wakala. Hivyo wavuvi tuliokuwa nao walikuwa ni wavuvi wa kundi hilo la wavuvi mawakala. Kuwaangalia kwa nje, walionyesha kuwa na maisha ya juu kidogo. Karibu wote walikuwa na magari, wamejenga nyumba nzuri na za kisasa, walikuwa na simu za bei mbaya – michango yao kwenye msiba ilionyesha kwamba ni watu wazito. Nimesema ukiwaangalia kwa nje, lakini wakianza kuongea yaliyo moyoni unagundua kwamba ya nje ni mapambo tu! Magari, majumba na mbwembwe zote ni mikopo inayowatoa jasho kuilipa!

Wavuvi hawa wanailalamikia serikali. Viwanda vya kusindika minofu ya samaki vinamilikiwa na “wageni”. Kama serikali ingewawezesha, wangeweza kuvimiliki na kuviendesha viwanda hivi kizalendo zaidi ya “wageni”. Wangeweza kuzuia uharibifu wa mazingira unaofanywa na viwanda hivi maana wenyewe wana uchungu na nchi yao. Wanaishi hapa, wataendelea kuishi hapa na kuendelea kulitegemea ziwa Victoria maisha yao yote, hivyo wanawajibika kulilinda. Wasingeruhusu uchafu wa viwanda kulichafua ziwa lao! Wangeweza kufanya biashara ya haki kiasi cha kumnufaisha hata mvuvi anayepata adha kubwa kule ziwani. Viwanda vilivyopo sasa hivi vinaendesha biashara isiyokuwa ya haki! Wananufaika wenye viwanda na mawakala, lakini wavuvi wanaambulia mnyororo wa mikopo isiyolipika!

Mfano: Wamiliki wa viwanda wanatoa mikopo kwa mawakala(wavuvi). Mikopo hii ni kama vile mitumbwi mikubwa, nyavu, injini, magari, nyumba nk. Malipo ya mikopo hii ni samaki! Hivyo kila mvuvi anafanya jitihada kubwa kupata samaki wengi ili amalize kulipa mkopo. Wamiliki wa viwanda ni wajanja wanacheza na bei ya samaki, mizani na visingizio vya samaki wasioruhusiwa. Tuseme mvuvi analeta kiwandani tani 5 za samaki, yeye anaaminini ni tani 5, lakini mizani ya kiwandani inaonyesha ni tani 4, na kwa bahati mbaya anakuta bei ya samaki kwenye soko la dunia “imeporomoka”! Hivyo tani 4, zinapata thamani ya tani moja! Huo ni mfano mmoja.

Lakini pia mvuvi anaweza kuleta tani 5 kiwandani. Akaambiwa kati ya hizo tani 4 ni samaki wasioruhusiwa. Uamuzi unakuwa ni wake, kukubali bei ya chini au kuzirudisha samaki mwaloni! Mvuvi akibisha zaidi, vinaitwa vyombo husika. Matokeo yake mvuvi anapoteza tani zote 5! Nimesikia, bado ninafanya utafiti, kwamba samaki hao wasioruhusiwa wakikamatwa, kinakuwa kitoweo cha wafungwa wa Butimba! Wengine wanasema samaki hao wanaishia viwandani na wavuvi wanapata hasara! Matukio kama haya humfanya mvuvi kuchelewa kumaliza kulipa mkopo wa kiwanda. Anapokaribia kumaliza mkopo, nyavu zinakuwa zimechakaa, mitumbwi na injini vimechoka. Anapokea mkopo mpya kutoka kiwandani. Hivyo huo unakuwa mzunguko usiokuwa na mwisho. Wavuvi hawa wanajikuta si wafanyabiashara bali watumishi wa viwanda vya kusindika samaki! Walio wengi wanapumbazwa na mikopo ya magari na majumba, lakini kama wanavyokiri baadhi yao, vitu hivyo yanakuwa ni mapambo yasiyokuwa na faida yoyote ile.

Wamiliki wa viwanda vya samaki wana mbinu nyingine ya kuwaangusha wavuvi mawakala. Mbinu hii ni ya kuwatumia mawakala ambao si wavuvi. Kwa mapatano na wamiliki wa viwanda, mawakala hawa wanapandisha bei ya samaki mwaloni. Hivyo na wavuvi mawakala wananunua samaki kwa bei ya juu mwaloni, wakifika kiwandani wanakuta bei ya chini na kulazimika kuuza samaki kwa hasara na kushindwa kupunguza makali ya mkopo wa kiwanda. Kwa maneno mengine wamiliki wa viwanda wanawachonganisha mawakala na wavuvi mawakala. Matukio kama haya yanajenga chuki kubwa na kuchochea ujambazi!

Jinsi wavuvi mawakala wanavyozungushwa na kudhulumiwa na wamiliki wa viwanda vya kusindika minofu ya samaki ndivyo hivyo nao wanavyowazungusha na kuwadhulumu wavuvi wadogo na wavuvi wa kuajiliwa. Bei ya samaki kwenye soko la dunia wanaijua wamiliki wa viwanda vya kusindika minofu ya samaki. Bei ya samaki kwenye soko la kiwandani wanaijua wavuvi mawakala. Bei ya samaki ikidondoka kwenye soko la dunia, inadondoka kwenye soko la kiwanda na kudondoka kabisa kwenye soko la mwaloni. Wakati mwingine bei ya samaki kwenye soko la dunia inakuwa haikudondoka, ila wavuvi mawakala wadondosha bei ya samaki mwaloni ili kufidia dhuluma ya viwandani. Anayepunjwa kati ya wote ni mvuvi anayeingia ziwani na kupambana na hali ngumu ya ziwani.

Tatizo linalojitokeza; ili wavuvi mawakala kukabiliana na dhuluma ya viwandani wanalazimika kupata samaki wengi kutoka kwa wavuvi wadogo na wavuvi wa kuajiriwa kwa bei nafuu. Ili kupata samaki wengi kwa bei nafuu, mbinu mbali mbali zinabuniwa. Mbinu hizi ni kutumia nyavu zisizoruhusiwa, kuiba nyavu, kuiba mitumbwi kutumia sumu, kuteka wavuvi na kuwanyang’anya samaki, nyavu, pesa, injini na mitumbwi. Kwa maneno mengine ni kwamba viwanda, vinachochea uvuvi haramu, uharamia na ujambazi.

Nilichojifunza kutokana na maongezi ya wavuvi ni kwamba:

Serikali yetu haijawa makini kutunga sheria za kuwalinda wavuvi na uvuvi. Serikali imeshindwa kuwawezesha wavuvi kuweza kuendesha viwanda vya kusindika minofu ya samaki. Biashara hii imeachwa mikononi mwa wawekezaji ambao hawana uchungu na maendeleo ya taifa hili. Serikali imeshindwa kuunda chombo cha kusimamia mikataba kati ya Viwanda, mawakala na wavuvi. Mikataba hii inaendeshwa kienyeji kiasi cha kusababisha hatari kubwa. Mfano uvuvi wa sumu ni hatari kwa kila mtu! Sasa hivi wenyeji wanajichukulia sheria mkononi, anayekamatwa anavua kwa kutumia sumu anahukumiwa kifo hapo hapo! Mtu anahukumiwa kifo bila kufikishwa mahakamani, na hii inatokea kwenye nchi inayojigamba kuheshimu utawala wa kisheria. Wavuvi wadogo, wanaoendesha biashara ya wakubwa wanapoteza maisha yao. Matukio kama haya yanajenga chuki miongoni mwa wananchi masikini na kuwaacha wakubwa wakineemeka. Wavuvi wadogo hawawezi kuvua kwa kutumia sumu! Mradi wa kuvua kwa kutumia sumu unahitaji mtaji mkubwa, sumu yenyewe inanunuliwa – na si kilo moja au mbili! Ukitumia sumu unapata samaki kwenye tani 5, hivyo ni lazima kuwa na mitego mingi, mitumbwi mikubwa na magari au vituo vyenye majokofu. Huu hauwezi kuwa mradi wa wavuvi wadogo!

Wamiliki wa viwanda vinavyosindika minofu ya samaki wana umoja wao. Umoja wa viwanda kumi na viwili. Viwili vya Kagera, nane vya Mwanza na viwili vingine vya Musoma. Umoja huu unaitwa “The Lake Victoria Fish Processors Association of Tanzania”. Umoja huu unavisaidia viwanda hivi kufanya biashara. Kupitia katia umoja huu viwanda hivi vinaweza kufanya majadiliano na serikali kwa sauti yenye nguvu, vinaweza kuwa na sauti moja katika kupanga bei ya samaki kwenye soko la viwandani, vinaweza kujadiliana bei ya samaki katika soko la dunia . Sasa hivi bei ya kiwandani imepanda kutoka sh. 600 kwa kilo hadi sh. 1200. Na ni kwa sababu sasa hivi viwanda hivi vinasafirisha tani 700 kwenda nje tofauti na tani 200 za mwezi wa Juni hadi Septemba mwishoni. Kama nilivyosema awali, bei ya soko la dunia wanaijua wenye viwanda. Sasa hivi wameweka hizo 1,200 lakini je kwenye soko la dunia bei ni ipi?

Kama wavuvi wangekuwa na umoja wao, wangeweza kufahamu bei ya samaki kwenye soko la dunia. Jambo hili si gumu. Siku hizi kila kitu kinapatikana kwenye mtandao. Wizara ya Maliasili na Utalii ikishirikiana na Wizara ya Ushirika na Masoko, hazijafanya kazi ya kuwasaidia wavuvi. Ili wavuvi wakaunda ushirika wao na kuendesha biashara yao katika ushirikiano na kuweza kuwa na nguvu za kupambana na wenye viwanda.

Niliumia kugundua kwamba sasa hivi tunajenga jamii ya watu waoga na wasiojisimamia. Ukizingatia malalamiko yote hayo ya wavuvi, hakuna aliyekuwa tayari kutoa ushuhuda wa haya ninayoyaandika. Walitaka yabaki kama maongezi. Hawakutaka yanaswe na mwandishi wa habari. Wanaogopa majina yao kutajwa kwenye gazeti. Wanaiogopa serikali, wanawaogopa wamiliki wa viwanda vya samaki. Wanamshukuru Mungu, kidogo hicho wanachokipata! Uovu wanauona, lakini ni nani amfunge paka kengele? Hivyo si kwamba ninaandika kitu kipya au ninaandika kitu kisichojulikana, ninaandika kuwasaidia wale wenye midomo lakini hawataki kusema, wenye mikono lakini hawataki kuandika, wenye mali waliogeuzwa kuwa watumishi!

Jambo la mwisho nililojifunza kwenye maongezi ya wavuvi ni kwamba badala ya serikali kulaani uvuvi haramu, uharamia na ujambazi, kufanyike juhudi za makusudi za kuchunguza chanzo za matatizo haya ambayo ni mageni katika uvuvi wa ziwa Victoria. Ni lazima zitungwe sheria na vyombo vya kusimamia biashara ya samaki inayoendeshwa kwa haki. Ni lazima wavuvi waelimishwe, wawezeshwe na wasaidiwe kuunda umoja wao. Miradi ya kimataifa ya kuhifadhi Ziwa Victoria, ielekeze nguvu zote kwa wavuvi wadogo na wenyeji wanaolizunguka Ziwa Victoria, maana hawa wanaweza kulitunza vizuri ziwa lao. Ushirikishwaji unaweza kupunguza matatizo yanayojitokeza kwenye Ziwa Victoria. Kinyume na hayo huu mnyororo wa Viwanda, mawakala, wavuvi, uvuvi haramu, uharamia na ujambazi utaendelea kujisuka na kuwanyonga walio wengi. Kaa chonjo!

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment