MGOGORO KKKT

MAKALA HII ILITOKA KWENYE GAZETI LA RAI 2004.
MGOGORO NDANI YA KKKT
Hivi karibuni tumesikia katika vyombo vya habari juu ya hatua ya Katibu Mkuu wa KKKT Bw. Amani Mwenegoha kuwafungulia kesi ya kashfa maaskofu saba. Hawa ni maaskofu ambao sisi wasikilizaji na waumini tunatambua kuwa wanamwajiri Bw. Mwenegoha kwa hiyo tunaamini kuwa sasa Bw. Mwenegoha si mtumishi tena wa kanisa hilo, maana angekuwa mtumishi angetafuta haki yake humo humo ndani. Nasema hivi kwa sababu naamini huko mahakamani anatafuta haki aliyonyimwa na mwajiri wake baada ya kufukuzwa, kujiuzuru, kuachishwa au kwa sababu yoyote iliyofanya ajira yake isitishwe. Kama bado ni mtumishi, kama ambavyo inasemekana, basi kuna mambo mawili yanaendelea hapa, nayo ni, kwanza Bw. Mwenegoha anatafuta kuwaanika na kuwadhalilisha maaskofu hao. Lengo lake si kutafuta haki hata kidogo. Pili, KKKT na siyo Mwenegoha, ina matatizo makubwa zaidi ya hili la kesi ya maaskofu na Mwenegoha. Watu wengi wanajiuliza hivi maaskofu wengine wako wapi wakati wenzao wanaburuzwa mahakamani? Hao nao wajihadhari maana alidhalilishwa Msuya, sasa maaskofu saba na baada ya hapo haijulikani nani atafuata.
Leo katika vyombo vya habari imetangazwa kwamba Mkuu wa Kanisa, amefanikiwa kumaliza mgogoro huu. Lakini habari za kuaminika ndani ya KKT, zinasema mgogoro huu bado uko palepale! Ni nani wa kuumaliza mgogoro huu? Ni mahakama, ni maaskofu saba, ni maaskofu wanaomuunga mkono Mwenegoha, ni maaskofu wanaokaa kimya bila ya kuwa na upande wowote au ni kanisa zima la KKKT? Hili ndilo swali la msingi la kujiuliza.
Wale tunaofuatilia mgogoro huu katika vyombo vya habari tunaweza kukosea sana katika kutoa hukumu zetu. Lakini kumbukumbu zangu zinaonyesha hivi: Bwana Msuya amemfungulia Bwana Mwenegoha kesi ya madai kwa ajili ya kumdhalilisha ama kumchafulia jina lake katika vyombo vya habari. Msuya katika kesi hiyo amesema wazi kabisa kwamba haamini kwamba kanisa lilimtuma kusema maneno hayo dhidi yake. Kwa hiyo alimshitaki Mwenegoha kama mtu binafsi.
Hatua ambayo ilichukua sura mpya ni lile ombi la Bwana Mwenegoha na kutaka KKKT ambayo yeye ni katibu wake Mkuu iunganishwe katika kesi hiyo.
Kwa mujibu wa habari ambazo nilizisoma katika gazeti moja tarehe 17.06.2004, ilionyesha kwamba kanisa liliwasilisha ombi la kutaka liunganishwe katika kesi hiyo na kwamba vikao vyake viliamua hivyo na hakimu alikubali.
Lakini kadri siku zilivyokwenda sisi ambao tunategemea zaidi vyombo vya habari kupata maendeleo ya kesi hiyo, tulisoma gazeti la Nipashe la Jumapili ya tarehe 22.08.2004 lenye kichwa “Maaskofu wa KKKT wamkana Mwenegoha”.
Katika makala hiyo wengine tulitegemea kusoma kwamba maaskofu 20 wa KKKT wamemkana katibu wao mkuu. Lakini tulichokutana nacho mle ni Maaskofu sita tu.
Nilipata picha kwamba katika kikao halali cha Halmashauri kuu kilichomalizika siku kadhaa kabla ya tamko hilo, ilishindikana kufikia muafaka wowote juu ya kuiunganisha KKKT ama kutoiunganisha katika kesi ya Msuya. Na sehemu ya taarifa hiyo ilisema wazi kwamba Katibu mkuu amewagawanya Maaskofu. Kwa bahati nzuri gazeti la Mwananchi ambalo lilichapa tamko lote la maaskofu sita na nilipolisoma niligundua kuwa maaskofu ambao ni sehemu kubwa ya maamuzi katika kanisa lolote, walikuwa hawana habari za kutosha kuhusu mwenendo wa kesi hiyo. Naomba msomaji univumilie najenga hoja. Si kazi nyepesi.
Kilichonishangaza zaidi mimi kama Mkristo (si wa KKKT) ni taarifa nyingine katika vyombo vya habari ya Mkuu wa Kanisa akijibu kuwapinga maaskofu sita (Maaskofu KKKT wapingwa, 26.08.2004).
1.Kwanza kabisa sikutegemea kwamba Mkuu wa Kanisa atajibu kupitia vyombo vya habari. Anawalaumu wale sita kwamba kanisa lina vikao halali vya kuzungumzia mambo hayo halafu yeye mwenyewe anakwenda kuzungumza na vyombo vya habari. Kama baba hapa nilimlinganisha na baba ambaye atatupiana maneno na mtoto wake hadharani. Kwa uzoefu wangu wa kufanya kazi kanisani, hili halikuwa tamko la Mkuu wa KKKT kwa maana liliongeza tatizo ndani na nje. Naamini alishauriwa vibaya na Mwenegoha au na watu walio karibu na Mwenegoha.
2. Nilitegemea kwamba yeye kama baba angeongea na Maaskofu sita faraghani na kupata msimamo wao kwa nini wamepeleka mambo hadharani wakati wao ni wajumbe wazito wa Halmashauri kuu. Hii inaonyesha kwamba Halmashauri kuu imeingiliwa ama imetekwa kiasi kwamba haiwezi tena kufanya maamuzi ya haki (katika tatizo hili). Kwani hao sita wanasema wazi kwamba “hawawezi kuacha ushuhuda wa kanisa ukiharibiwa.” Na ninaamini kabisa wamekaa na kufikiria kabla ya kwenda katika vyombo vya habari.
3. Taarifa ya Mkuu wa kanisa inasema kanisa hufanya kazi kwa njia ya vikao halali, maana yake ni kwamba hawa maaskofu si sehemu ya kanisa, kwa vile wamezungumza nje ya vikao?
4. Kwa mantiki ndogo kabisa niliyonayo, nilitegemea taarifa ya Mkuu wa kanisa itusaidie sisi Wakristu na wasomaji kuambiwa kwamba ni kweli kanisa lilimtuma Mwenegoha amtukane Msuya (kufuatana na madai ya Msuya). Hapo kazi kwetu ingebaki kujiuliza kama taarifa ya Maaskofu sita inavyosema kwamba si kazi ya kanisa kupeleleza siri za viongozi wa serikali. Mimi binafsi kama mkristo, nisingekuwa tayari kuunganishwa na kesi hiyo kwani hatutumi viongozi wetu ama wajumbe wetu kwenye halmashauri kuu ama mkutano mkuu kusema hayo.
5. Kauli ya Mkuu wa Kanisa inasema hakujawahi kutokea tuhuma zozote dhidi ya Katibu Mkuu. Kauli hiyo inaweza kuwa hatari mno kumshuhudia mwanadamu. Labda kama alizungumza lugha ngumu nami nikashindwa kumwelewa. Lakini nalinganisha na mzazi mmoja ambaye alishuhudia mbele ya umati akimtoa binti yake kuolewa kwamba binti yetu ameleleka, hana doa nk., wakati anasema hivyo baadaye vijana wananong’ona, “angetuuliza sisi ambao tumetembea naye.”
6. Taarifa ya Mkuu wa KKKT ilisema alitoa tamko lake baada ya kikao chake na kamati ya utendaji. Kwa mazingira ya tatizo lilivyo kamwe siamini kama kamati ya utendaji inaweza kusimama na kutenda haki. Kwani kamati ya utendaji kwa mazoea yetu na ya wengi ni sehemu ndogo sana ya Halmashauri kuu. Tena hatujui wajumbe wake wanapatikanaje? Wanachaguliwa ama wanateuliwa na katibu mkuu ama mkuu wa kanisa? Sasa kama jambo limeshindikana katika vikao vya Halmashauri Kuu, litaamriwa katika kamati ya utendaji? Hapo kuna uwezekano wa aina mbili tu: Kama wajumbe wengi wa kamati ya utendaji wapo kwa Mwenegoha basi watawaponda wale Maaskofu sita, kama wapo upande ule mwingine kama taarifa ya maaskofu sita inavyosema wamegawanywa, basi watamponda Mwenegoha. Lakini kwa jinsi taarifa ya Mkuu wa Kanisa ilivyokaa inaonekana kutoka katika maaskofu sita hakuna mjumbe wa kamati ya utendaji.(Naamua kwa mazingira tu, mimi siwajui wajumbe wa kamati ya utendaji)
7. Ninakuwa na mashaka makubwa juu ya washauri wa Mkuu wa kanisa. Ninaona kama anawashauri toka upande mmoja, ama inaweza kuwa mshauri mkuu ni mtuhumiwa mwenyewe. Ingekuwa heri kama angepata washauri nje kabisa ya wajumbe wa halmashauri kuu. Kwani vinginevyo ataendelea kujibu mambo kwa jazba na hivyo kuwapa watu faida juu ya mambo yanayoendelea ndani ya kanisa kubwa la KKKT.
8. Katibu Mkuu kama angekuwa mtu mnyenyekevu hakika angeamua kukaa pembeni, kwani kukanwa na maaskofu saba na ambao wanasema wanawakilisha tu wenzao, si jambo dogo hilo. Maana yake wamekosa imani juu yako. Na huna uhakika kama hajakukana na washarika wao. Lakini kuwa tayari kuligawanya kanisa kwa ajili ya mtu mmoja hii ni hatari sana kwa kanisa.
9. Wengine tunapata hisia kwamba hayo yanayotajwa labda ni ngazi tu ya kujaribu kutatua matatizo mengi yanayoikabili KKKT na ofisi yake kuu, ambayo nadhani haina ushuhuda mzuri na imepoteza heshima ya kanisa lenyewe.
Kama ambavyo Mwenegoha ameandikwa katika magazeti mengi kuwa kesi ya kashfa inayomkabili ni kesi ya kanisa kwa kuwa alisema hayo maneno akitekeleza wajibu wake kama Katibu Mkuu wa KKKT, maaskofu aliowashtaki wanaweza pia kusema walitekeleza wajibu kama viongozi wa KKKT kusema waliyosema. Na kama mgogoro kati ya Msuya na Mwenegoha ni sehemu ya mgogoro wa dayosisi ya Mwanga, basi hata maaskofu kushtakiwa ni mwendelezo wa mgogoro wa Mwanga. Suluhu ya jambo hili ni kwa KKKT kuruhusu dayosisi hiyo izaliwe ili Katibu wake Mkuu apone na kesi ya kashfa na pia maaskofu wake wapone kesi ya kashfa kutoka kwa Katibu mkuu wao.
Inatakiwa kuangalia mazingira ya Kijiografia ambapo maneno hayo Bwana Mwenegoha aliyatamka. Kama alitamka akiwa Ofisini na waandishi wa habari waliongea naye kama katibu mkuu, basi hakusema kama Mwenegoha, bali kama Katibu Mkuu wa KKKT.
Swali linalofuata sasa liwe je, anaruhusiwa kusema aliyosema? Maana yake hapo ni suala la kitaalamu kwa dhana ya uongozi: Je yeye ndiye msemaji wa KKKT? Kama sio basi hapo ameikosea ofisi yake. Na hapo zifuate taratibu zilizowekwa za kumshughulikia mtu aliyekiuka maadili ya ofisi yake. Wanasema mahali pengine huwa anawajibika kwa kujiuzulu, ama kupewa onyo. Nk.
Katiba za makanisa mengi msemaji Mkuu wa kanisa MKUU WA KANISA hilo ama MJUMBE WAKE. Juu ya mjumbe wake hakika hiyo ni tata. Ni kama cheki ambayo amesainiwa lakini haijajazwa tarakimu ( a signed blank check). Inaweza kujazwa tarakimu yoyote ile. Basi sasa labda tuangalie mazingira ya kuzungumza jambo hilo: Kwanini alitamka yeye na siyo mkuu wa kanisa?, Je, mkuu wa kanisa alimtuma kutamka hayo? Hapo ajibu mkuu wa kanisa. Ama ndio maana anamtetea? Kama hakumtuma, je, jambo hilo lilikuwa la dharura kwamba kama lingesubiri mkuu wa kanisa basi lingeharibika? Sidhani hivyo! Lakini pia, awe alitumwa na Mkuu au kikao, bado ni hatari kutumwa kufanya makosa na wewe ukakubali. Je angetumwa kuiba angeiba? Je akiiba wakati akitekeleza wajibu wake ni kosa la aliyemtuma? Hii kesi itapendeza kuisikiliza!
Hatua ya tatu ni kuangalia, huenda katiba ya KKKT inajipinga yenyewe. Anaweza asiwe msemaji wa jumuia ama taasisi hiyo, lakini alichofanya ni moja ya majukumu yake ya kikatiba. Maana yake hapo iangaliwe chini ya wajibu wa Katibu Mkuu wa KKKT. Sasa kwa vile mambo kama haya ni siri ya ndani ya KKKT ni vema yakatunzwa kwa sababu watu wengi hawakuzoea kusikia maaskofu wanaburuzwa mahakamani kwa kosa la kutekeleza wajibu wao. Kanisa kubwa kama KKKT ni mhimili mmojawapo wa ustawi katika nchi, kuliacha liyumbishwe ni hatari si kwa KKKT yenyewe bali hata kwa makanisa mengine na taasisi.
Jambo la nne la kuangalia ni yaliyomo katika tamko la Mwenegoha dhidi ya Msuya. Hapa niseme wazi kuwa, yawezekana kweli mtu kuwa msemaji wa jumuia ama taasisi lakini yale aliyosema yasiendane kabisa na VISION na MISSION za taasisi hiyo. Na hili likitokea kwa kawaida kamati husika ama management ama wale ambao mtu anafanya nao kazi katika uongozi taasisi hiyo wana uhuru wa kusema kwamba hata kama wewe ulizungumza kama Mkurugenzi wa Kampuni yetu, ama Mkuu wa Chuo, hayo uliyosema si mawazo yetu kwani hayatuwakilishi sisi. Ni maneno yako binafsi.
Na hii nadhani ni moja ya hoja za wale maaskofu saba. Wanasema si kazi ya kanisa: maana yake It does not represent the VISION and MISSION of the ELCT. Je nini kinafanyika kama tayari huyo kiongozi wenu ameshitakiwa mahakamani? Ni juu ya taasisi husika kuamua ifanye nini, si mahakama. Hata hawa maaskofu saba kama walisema bila kuwasiliana na dayosisi zao hawawezi kuziunganisha dayosisi zao katika kesi ya kashfa inayowakabili kutoka kwa Mwenegoha. Taasisi inaweza kusema pamoja na kuwa uliyasema hayo binafsi, sisi tutasimama nawe katika kesi kukusaidia. Haina maana lazima iwe kulipa, inaweza kuwa kumwombea radhi mahali alipoharibu. Nadhani hii ndio hoja ya Maaskofu saba kuwa iliwahi kutolewa ombi la kutaka kesi hiyo imalizwe nje ya mahakama lakini mhusika alikataa. Kulilazimisha kanisa kuwa lina kosa ni hatari. Na tena ni vema kutahadharisha kuwa yale yanayoamuliwa leo ndio yatakayotendewa kazi siku zote. Maana yake ni kuwa, KKKT ikisema kiongozi akitamka lolote basi kanisa limetamka, basi itakapotokea tena kwa mwingine mtalazimika kufanya hivyo hivyo.
Basi huu ni mchango wangu tu katika kulitafakari jambo hilo nyeti kwa ajili ya kanisa la Mungu. Kila mtu anaweza kutoa mchango wake maana vurugu katika kanisa ni vurugu katika jamii yetu. Ni lazima tushirikiane kuondoa vurugu za aina yoyote ile katika jamii yetu. Kimya akisaidii kitu chochote – ni bora kuongea na kujadiliana kuliko kukaa kimya na kuchochea vurugu kichinichini. Mungu libariki kanisa la KKT, Mungu ibariki Tanzania.
Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment