UJASIRI WA SUMAYE NI PESA

MAKALA HII ILITOKA KWENYE GAZETI LA RAI 2005

UJASIRI WA SUMAYE NI PESA.

Ninaandika makala hii kwa wale wote wanaohoji ujasiri wa Sumaye, wa kutangaza kwamba anataka kugombea kiti cha Urais, ninawaandikia wale wanaofikiri Sumaye, amechanganyikiwa kuonyesha nia ya kutaka kuingia kwenye viatu vya Mkapa. Ninaandika makala hii nikicheka ingawa moyo wangu unanilazimisha kulia. Ninacheka kicheko cha huzuni na kujilaumu, kicheko ambacho ni dalili za kuonyesha ushujaa wa kijinga na ubwege! Ingawa ninacheka, wewe unacheka, nyinyi pia mnacheka, sote tunacheka, na wao kule wanacheka, ukweli ni kwamba, utalia wewe Tanzania! Utalia ukiwa umeshikilia kitanzi chako mikononi. Kamba uliyoitengeneza wewe mwenyewe kwa mikono yako mitukufu, ewe Tanzania, itayamaliza maisha yako, furaha yako, utulivu wako, amani yako na mshikamano wako. Dhambi uliyoilea wewe mwenyewe ewe Tanzania, mtukufu, ikutafune wewe na vizazi vyako. Mwalimu Nyerere, aliomba na Mungu, akamsikiliza, hayupo kushuhudia jinsi dhambi zetu zinavyotutafuna. Ningejua, huja baadaye. Ni heri ungesikiliza ewe Tanzania!

Jesse Kwayu na wenzako, nitumie maneno gani ili macho yenu yapate kufumbuka na masikio yenu kusikia? Maneno yangu niyapambe kwa vito gani ili myapokee na kuyakubali Tumrundishe nabii Isaya, aliyesema:
" Kusikia mtasikia, lakini hamtaelewa kutazama mtatazama, lakini hamtaona. Maana akili za watu hawa zimepumbaa, wameziba masikio yao, wamefunga macho yao. La sivyo, wangeona kwa macho yao, wangesikia kwa masikio yao, wangeelewa kwa akili zao, na kunigeukia, asema Bwana nami ningewaponya."
Haya ni maneno ya zamani, lakini leo yanatunyea kama mvua ya mawe. Mvua isiyokuwa na huruma, mvua isiyojali mafuriko, mvua ya kuleta maafa! Aisifuye mfua imemnyea! Ole wake mtu huyo atakayekulazimisha kuifuta historia yako kwa kamba uliyoitengeneza wewe mwenyewe, ewe Tanzania. Heri mtu huyo asingezaliwa!

Jesse na wenzako, ujasiri wa Sumaye ni pesa! Ana pesa! Pesa adui wa haki, pesa yenye uwezo wa kupindisha ukweli kuwa uwongo, pesa inayowanyamazisha mashujaa, wasomi na wacha Mungu! Pesa yenye nguvu za kuvunja undugu na kupandikiza chuki, kuvunja ndoa na kusambaratisha familia. Pesa chanzo cha rushwa, ujambazi, ufisadi na kuyapotosha maadili mema katika Taifa letu. Hicho ndicho kitanzi tulichokisuka kwa mikono yetu wenyewe. Na sasa kimegeuka kuwa hukumu ya maisha yetu. Tungemsikia Mwalimu, tungetambua kwamba pesa si msingi wa maendeleo, bali ni matokeo. Sisi tumetanguliza pesa! Wahaya wana msemo: " Ekilalema amaela onage". Tafsiri ya kubabaisha: Jambo litakaloshindwa nguvu ya pesa, achana nalo! Asilimia kubwa ya watanzania ni walalahoi, hawana pesa, hawana ajira! Hata wale wenye ajira, mishahara yao ndio hiyo chini ya dola mia kwa mwezi. Matumizi, juu ya dola miatano kwa mwezi. Wakimwagiwa pesa za uchaguzi wote wataimba CCM juu, Sumaye, apite!

Pesa zikimwagwa vizuri vyombo vyote vya habari na waandishi wa habari wataimba CCM juu, Sumaye, apite! Ni vigumu masikini mlalahoi kuhimili nguvu za pesa. Ni nani mwenye ubavu wa kukataa pesa na kutenda haki? Utakataa pesa wakati mtoto anataka kwenda shule, wakati mwenye nyumba anakufukuza kwa kushindwa kulipa pango, wakati huna pesa ya kulipia matibabu? Mtu hujawahi kushika 100,000 mikononi mwako, zikutembelee hizo kwa sharti la kumpitisha mbunge na rais, kwa nini usiimbe CCM juu, Sumaye, apite?

CCM, ina pesa na vyombo vyote vya dola. Ikitaka kumpitisha Sumaye, hata ukienda Bagamoyo, ukeshe makanisani na misikitini ni kazi bure! Kama "mwenye CCM" anamtaka Sumaye, wajumbe wa mkutano mkuu watanunuliwa kwa pesa, au hata sasa hivi ninapoandika makala hii wamekwisha nunuliwa. Wanajiandalia kitanzi chao wanyewe!

Mbali na Sumaye, kuwa na pesa zake binafsi, za chama na za serikali wale anaotaka kuwalinda wana pesa za kutosha. Na kwa vile bado wanataka kuchuma ni lazima wafanye chini juu ili mtu wao asimame. Sumaye, analionyesha hili wazi katika mahojiano aliyofanya hivi karibuni na gazeti moja la hapa nchini:
" Tumefanya kazi kubwa pamoja na rais, kwa miaka tisa sasa, najiuliza, hivi akija mwingine asiyetaka kuyaendeleza haya mafanikio, si wawekezaji watakata tamaa? Siku hizi kuna mashindano makubwa katika masuala ya uchumi kila nchi inavutia wawekezaji, sasa kukiwa na kiongozi asiyetaka kuendeleza haya mazuri, wawekezaji wataondoka. Lakini wawekezaji wakitambua kuwa nafasi imeshikwa na kiongozi aliyekuwa karibu na aliyeongoza mabadiliko hayo, watakuwa na uhakika wa kuwekeza zaidi".

Hiyo ndiyo sera yake, kuhakikisha usalama wa wawekezaji. Kuangalia usalama wa IPTL, ambayo inaliingizia taifa hasara kubwa. Si kulinda usalama wa raia, bali usalama wa wawekezaji! Cheka kama una cheka, na lia kama moyo wako unakusukuma kulia, ukweli ndio huo, wawekezaji kwanza!

Sumaye, ana wasiwasi kwamba kama si yeye kuingia Ikulu, watakuja wengine wasiopenda "maendeleo" na kuvunjilia mbali yale mazuri yaliyofanywa na serikali ya awamu ya tatu. Ni mtu gani anaweza kuharibu mambo mazuri? Kichaa anaweza kufanya hivyo. Lakini kama wananchi wana akili timamu, watamkatalia mwenda wazimu huyo. Akija mtu akakataa kuendelea na mikataba mibovu, akakataa hasara ya IPTL, akafichua madhambi ya wale walioliingiza taifa katika hasara kubwa kwa kukubali matapeli wa IPTL, mtu huyo atakuwa hayapendi maendeleo?

Sumaye, anaamini kwamba:
" Mimi ni sehemu ya mafanikio yote ya kiuchumi na kijamii ambayo nchi yetu imeyapata. Akija mwingine, asipoyaendeleza haya, nchi itarudi nyuma, nchi itaporomoka."

Wakati Jese na wenzake wanamlaumu Sumaye, kwa mikataba mibovu ya uwekezaji, mikataba ya TTCL, IPTL na NBC, yeye anaamini bila kuiongoza Tanzania, nchi itaporomoka! Huo ni ujasiri wa pesa. Bila kiburi cha pesa, asingeweza kusema hayo. Anajua kwa pesa atawanunua watu wote. Pesa, itafunika madhambi yake yote.

Bahati mbaya hatuna tena mtu mwenye busara kama mwalimu wa kuweka mambo sawa. Pesa itatuchagulia rais, wabunge na madiwani. Haya tuliyataka kwenyewe. Tulikuwa na nafasi ya kuwapigia kura za kutokuwa na imani viongozi wote waliokuwa na kashfa mbali mbali. Tulikuwa na wakati mzuri wa kumkataa Sumaye, alipoponda milioni 500 za taifa kwa ziara binafsi na pale alipojikanyaga na Kibaigwa, mara shamba si langu, mara nina hisa na mara ni shamba la mke wangu. Dalili zilijionyesha tukachagua kuwa vipofu! Tulikaa kimya kwa woga ili kuenzi amani na utulivu. Ya nini kulalamika? Tumeyavulia, tuyaoge!

Sasa si wakati wa kulalamika. Tumechelewa kwa hilo. Kama unasema hatujachelewa, sema usikike, tenda tukuone! Simama na kusema hapana, kataa kununuliwa, kataa kuchaguliwa rais, tumia haki yako ya kura kumchagua rais kufuatana na sifa zake za "Utanzania", sifa tulizoachiwa na waasisi wa taifa letu. Huu si wa kati wa kuhoji ujasiri wa wale wanaotaka kuingia Ikulu, wakati wamezungukwa na kashifa za rushwa na kutumia vibaya peza za umma. Tuliyataka wenyewe. Tulizembea, sasa matokeo yake ndio hayo. Kilichobaki ni kujililia sisi na vizazi vyetu.

Sasa hivi ni wakati wa kuwapamba marais wetu watarajiwa. Ni wakati kumpamba Sumaye. Yeye ni mnyenyekevu. Walio karibu naye wanaungama wazi kwamba mheshimiwa ana unyenyekevu wa hali ya juu. Hii ni sifa muhimu sana kwa nchi inayotaka kutunza amani na utulivu bila kuzingatia mambo mengine kama uchumi na utawala bora. Watu waendelee kuongelea kwenye umasikini huku wakiimba wimbo unaochefua wa amani na utulivu ni nguzo za taifa letu.

Sumaye, ni mvumilivu. Amejaliwa kipaji na mwenyezi Mungu, kuwa mvumilivu. Amevumilia maadui zake, hata na wale waliokuwa wakimpaka matope. Yeye mwenyewe anasema:
"Wapo wanaoamua kuwachafua wengine ili kutimiza malengo yao ya kisiasa, huu si ustaarabu. Unapotumia mbinu hiyo, maana yake mwenzako anakuzidi nguvu, kwani kama hakuzidi, ni kwa nini umchafulie?...Mimi siwezi kumhujumu mtu na wala sitamchafua mtu".
Hawezi kulipiza kisasi. Amekuwa kwenye nafasi ya juu serikalini. Alikuwa kiranja wa mawaziri, hatujasikia akijilipiza kisasi. Katika nchi kama Tanzania, inayotanguliza amani na utulivu na mshikamano, huyu ndiye anayefaa. Atashughulika na amani na mshikamano na kuwaachia wawekezaji wasombe kila kitu. Apite Sumaye! CCM, juu!

Sumaye, ana uzoefu wa muda mrefu katika siasa. Taifa kama Tanzania, linalotanguliza amani, utulivu na mshikamano, linahitaji rais mwenye uzoefu wa muda mrefu katika siasa. Elimu si jambo muhimu, hata Iddi Amin, aliitawala Uganda na kuiacha historia nyuma yake, yeye Sumaye anasisitiza jambo hili katika mahojiano aliyofanya na gazeti mojawapo siku za hivi karibuni:
" Sidhani kama suala la elimu ndicho kigezo kilichopo. Ni watu wanaonisema. Hata katika chama chetu tunasema mgombea awe na elimu ya chuo kikuu au inayolingana nayo. Sasa kama ni suala la elimu, mimi ninayo inayolingana na hiyo, kinachotakiwa zaidi ni uzoefu wa uongozi.. nimekuwa kwenye siasa kwa muda mrefu, nadhani hayo ndiyo muhimu".

Kama tungekuwa na mfumo mzuri wa demokrasia, tungemuuliza Mheshimiwa Sumaye, miaka yote katika siasa imezaa nini. Haitoshi kukaa miaka mingi katika siasa. Jambo la muhimu ni umefanya nini katika siasa. Kuna watu wanakaa muda mfupi katika siasa, lakini kwa vile walikuwa na vision na kusimamamia maoni yao katika jamii, wanakumbukwa kwa miaka mingi, wanaandika historia isiyofutika. Kennedy, hakuitawala Amerika kwa miaka mingi, lakini hadi leo hii anakumbukwa. Kwa vile sisi tunaongozwa na pesa, basi Sumaye, anaweza kusema lolote, na kupata kura! Si kwa sifa zake, bali kwa pesa zake! Cheka kama unataka na lia ukijisikia kulia, ukweli ndio huo!

Sumaye ni mtiifu. Tumeambiwa amemtii kwa kiwango kikubwa rais Mkapa. Huyu ndiye rais tunayemtaka. Alivyo mtiifu, ndivyo atakavyotaka wengine wamtii. Viongozi wakimtii, wakifuata kila anachokisema " Ndiyo mzee", nchi itakuwa na amani na utulivu.


Sumaye, ni rafiki wa karibu wa rais Mkapa. Huyu atamtunza vizuri rais wetu mstaafu. Hatupendi mpendwa wetu apate yale yaliyompata Kaunda na Chiluba. Tungependa mzee wetu akapumzike vizuri kule Lushoto kwenye hewa safi bila kusumbuliwa na malalamiko ya walalahoi.

Sumaye, ni mcha Mungu Tunakutana naye kanisani. Amekuwa mwaminifu kuhudhuria sherehe zote za kidini. Ziwe za Wakristu au Waislamu. Imani yake ni imara. Hatujamsikia kuhama kanisa lake la KKKT na kujiunga na makanisa mengine. Hatujamsikia akihama dini yake ya Ukristu na kuingia Uislamu au kutembelea Bagamoyo!

Sumaye ni kijana, ukimlinganisha na "Babu". Kuna msemo ya kihaya: "Abafu, bakilana okunuka", Tafsiri ya harakaraka: Maiti huzidiana kwa harufu mbaya.
Ingawa kampeni za Sumaye na "Babu" ni za kutumia nguvu ya pesa, pesa za "Babu" zinanuka zaidi, kuna mashaka kama zinaweza kuleta amani na utulivu.

Sumaye ana sifa nyingi! Labda Jesse na wenzake wanafikiri ninaandika haya nikilia na machozi yakidondoka. Si kweli! Ninaandika nikicheka. Ninafanana na mtu anayejinyonga kwa kamba aliyoitengeneza yeye mwenyewe. Ni lazima mtu huyu afe akicheka. Hata shujaa Mkwawa, alikufa akicheka. Kicheko cha huzuni na kujilaumu, dalili za kuonyesha ushujaa wa kijinga na ubwege! Maisha ni kitu muhimu, ukishayapoteza ni mwisho. Hekima ni kuyalinda maisha na wala si kuyapoteza!

Huu si wakati wa kulia. Hata tukilia haitasaidia kitu. Ni wakati wa kucheka kicheko cha huzuni na kujilaumu. Ni wakati wa kujinyonga kwa kamba tuliyoitengeneza sisi wenyewe.

Huu ni wakati wa kufikiria jinsi ya kubadilisha mfumo wa siasa katika Taifa letu. Ni wakati wa kukaa chini na kuandika katiba mpya ya taifa letu, ili tuachane na katiba iliyojaa viraka. Ni wakati wa kubuni mbinu za kuendesha uchaguzi wa haki. Uchaguzi utakaowaingiza watu madarakani kwa kufuata sifa na uwezo wao na wala si kwa kutumia pesa.

Nina imani akina Jesse Kwayu, wameupata ujumbe wangu. Ujasiri wa Sumaye, ni pesa. Kama kuna mtu au kikundi cha watu chenye uwezo wa kumpokonya Sumaye, ujasiri wa pesa, kuipokonya CCM, ujasiri wa pesa na kuwapokonya wawekezaji ujasiri wa pesa, na kama kuna mtu au kikundi cha watu chenye uwezo wa kuipokonya CCM, uwezo wa kutumia vyombo vya dola wakati wa uchaguzi mkuu,tunaweza kujadiliana juu ya ni nani ataingia kwenye viatu vya rais Mkapa. Kinyume na hapo hakuna mjadala. Mwenye nguvu mpishe! Mnyonge ni mnyonge daima hadi pale anapofumbua macho na kusema hapana!
Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment