UKATILI MAJUMBANI, KIVULINI NI MFANO WA KUIGWA

MAKALA HII ILITOKA KATIKA GAZETI LA RAI 2004

UKATILI MAJUMBANI, KIVULINI NI MFANO WA KUIGWA

Mwezi jana katika kijiji cha Ruhita- Karagwe, mtoto wa kiume alipoteza maisha yake wakati akiamua ugomvi kati ya baba yake na mama yake. Mtoto huyu aliyaokoa maisha ya mama yake aliyekuwa anapigwa mithili ya nyoka, na kupoteza maisha yake yeye mwenyewe. Fimbo iliyokuwa imelengwa kwenye kichwa cha mama wa mtoto huyu, ilielekezwa vizuri kwenye kichwa cha kijana huyu na kuyamaliza maisha yake hapo hapo! Sikufanikiwa kufahamu chanzo cha ugomvi huo uliosababisha kifo cha kijana mdogo ambaye alikuwa bado ni tegemeo la taifa letu, lakini jinsi ninavyokifahamu kijiji cha Ruhita, wenyeji wake, hali ya uchumi mila na hasa unyanyasaji wa wanawake, inawezekana kabisa kwamba ulikuwa ni ugomvi wa shilingi 200!! Mama, alizitumia bila idhini ya baba! Litaonekana jambo la kushangaza katika dunia ya leo mtu kupigwa kwa kutumia shilingi 200 bila idhini na mtu kupoteza maisha yake akiamua ugomvi wa shilingi 200.

Ya kushangaa ni mengi katika kijiji cha Ruhita, kijiji ambacho sitegemei kinatofautiana na vijiji vingine katika Taifa letu la Tanzania. Utashangaa ukijua inamchukua mtu siku ngapi kuzipata hizo shilingi 200. Utashangaa zaidi ukijua idadi ya watu katika kijiji cha Ruhita, wanaoishi zaidi ya miezi sita bila hata ya kuzishika hizo shilingi 200 mikononi mwao. Utashangaa kugundua kwamba wanaofanya kazi mashambani ni akinamama na watoto lakini wanaouza mazao na kupokea pesa ni wanaume, hata kama mwanamke amepata pesa kwa njia zake anazozijua, hana ruhusa ya kuzitumia bila idhini ya mwanaume! Yakushangaza ni mengi katika kijiji cha Ruhita, yakushangaza ni mengi katika dunia ya leo na yakushangaza ni mengi katika Taifa letu Tanzania. Yanayoshangaza kwa upande wa familia yanasababishwa na ukweli kwamba familia zimeachwa bila ushauri bila mfumo wa kuzisaidia kujikwamua kimaadili, kielimu, kiutandawazi na kiuchumi. Kila familia inabaki peke yake bila kuwa na jukwaa la kuiunganisha na familia nyingine katika mtaa, kijiji, kata, wilaya na taifa. Je, ni jambo la kushangaza au kusikitisha ukisikia mtoto wa kike amebakwa na baba yake mzazi? Matukio kama haya yanaongezeka kila kukicha. Utafiti usiokuwa rasmi unaonyesha kwamba watoto wa kike wanafanyiwa ukatili wa kingono/kimapenzi na wazazi wao, ndugu zao, jamaa na marafiki wa karibu. Kwa vile hekima ya kipuuzi inamtukuza mwanamke anayejua kutunza siri, mwanamke anayefunga mdomo, mwanamke mvumilivu na mwenye heshima, mabinti wanafundishwa kufunga midomo yao. Kwa njia hii ya hekima ya kipuuzi ukatili wa kingono/kimapenzi, unaendelea na kushamiri. Aina zote za ukatili wa majumbani: Ukatili wa kimwili, ukatili wa kimawazo na ukatili wa kiuchumi, zimegubikwa na kufunikwa na hekima ya kipuuzi ya kutunza “siri” za majumbani.

Baadhi ya “siri”(udhalilishaji na ukatili) hizi za majumbani ni: Kupigwa (kwa makofi, ngumi chuma fimbo), kuchomwa(kwa moto, kisu, chuma nk),kutukanwa, kufanyiwa dhihaka/dharau, kuaibishwa au kulaumiwa bila sababu, kutishiwa, wanawake au watoto katika familia kulazimishwa kufanya ngono/mapenzi bila ridhaa yao, wanaume kuwazuia wanawake kutembelea jamaa, ndugu na marafiki, wanaume kuwazuia wanawake kufanya kazi mbali na nyumbani hata kama kazi hiyo ni ya manufaa makubwa katika familia kwa kuongeza kipato, wanaume kutumia pesa kwenye ulevi au pombe wakati familia inahitaji chakula na matumizi mengine, kumlazimisha mtu kufanya kazi na kumnyang’anya au kumdhulumu mshahara wake, kutoa upendeleo kwa watoto, mfano kuwapa watoto wa kike nafasi ndogo ya elimu, matibabu au chakula kidogo kuliko watoto wa kiume

“Siri” za majumbani hutengeneza kitu kinachoitwa mzunguko wa ukatili katika familia. Mzunguko huu huanza na vitendo vya ukatili/unyanyasaji (kipigo, vitisho, matusi makali, kulazimishwa mapenzi/kubakwa). Hali hii husababisha utulivu na amani kupotea katika familia. Mzunguko huu hukamilika kwa kufikia mtafaruku katika familia. Mara nyingi inakuwa vigumu kuufunika mtafaruku katika familia. Watu wachache wanaweza kufanikiwa lakini matokeo yake si mazuri!

Matukio kama kifo cha mtoto wa kijiji cha Ruhita- Karagwe, matukio kama ya watoto wa kike wanaobakwa na wazazi wao, matukio kama ya watoto wa mitaani wanaozikimbia familia zenye mitafaruku, matukio kama ya wanawake kupigwa hadi kupoteza maisha yao, matukio kama ya wanaume kuzitelekeza familia zao, matukio kama ya machangudoa wanaozikimbia ndoa za kulazimishwa na ndoa zilizoshindikana yanazifichua “siri” za majumbani.

Sasa hivi ukatili majumbani si “siri” tena. Hili ni tatizo la kijamii na linahitaji mfumo wa kulirekebisha. “siri” hizi za majumbani haziwezi kuongozwa tena na hekima ya kipuuzi bali hekima yenye busara!
Ukatili wa majumbani huumiza watu wengine wengi mbali na wasichana na wanawake ambao mara nyingi ndio waathirika wakuu. Ukatili wa majumbani pia unawaathiri watoto na jamii nzima.

Wanawake ambao mara nyingi ndiyo hufanyiwa ukatili majumbani wana hatari ya kupata madhara yafuatayo katika maisha yao ya kila siku:
- Maumivu makali; majeraha na ulemavu wa kudumu kama kuvunjika mifupa, kuungua, magonjwa kama asthma, maumivu ya kichwa ,kifua, tumbo n.k.
- Wanaweza pia kupata matatizo ya kiakili; kama woga, hofu ya mara kwa mara, mgandamizo wa mawazo, kutengwa, aibu na kujilaumu, matatizo ya kula na kulala. Ili kukabiliana na ukatili, wanawake huanza tabia mbaya na ya hatari kama vile ulevi wa pombe, madawa na kuwa na wapenzi wengi.
- Wanaweza kuwa na matatizo katika afya ya uzazi. Wanawake wengi hushindwa kumudu ujauzito kutokana na kupigwa kipindi cha ujauzito. Pia wanaweza kupata mimba zisizotarajiwa, magonjwa ya zinaa au UKIMWI kama matokeo ya unyanyasaji kingono/kimapenzi.
- Unyanyasaji kingono/kimapenzi unaweza kusababisha hofu ya kufanya mapenzi, maumivu wakati wa tendo la ndoa, na kukosa hamu ya kufanya mapenzi. Unyanyasaji kingono/mapenzi kwa watoto (wadogo) unaweza kusababisha kuchanganyikiwa na hofu ya kuwa na mahusiano salama ya kimapenzi maishani.
- Na katika matukio mabaya ya ukatili wa majumbani husababisha kifo.

Ukatili majumbani unaathiri jamii nzima maana unaweza kusababisha kila mtu kuamini kuwa, ukatili ni njia sahihi ya kusuluhisha matatizo na kuendelea kuwa na imani potovu kwamba wanaume ni bora kuliko wanawake na wanawake wanapaswa kupigwa. Watoto katika familia zenye ukatili mara nyingi hawali vizuri, ukuaji na uelewa wao ni dhaifu ukilinganisha na watoto wengine, huwa ni wajeuri shuleni, pia huwa na magonjwa mengi. Watoto wanaoshuhudia ukatili uliokithiri majumbani wanaweza kujenga fikra kwamba ndivyo wasichana na wanawake wanapaswa kutendewa katika familia na jamii. Huwa na uwezo mdogo sana wa kujifunza njia mbadala za kutatua migogoro.

Kama nilivyosema hapo juu hatuna mfumo wa kuzuia ukatili majumbani. Serikali yetu haina mfumo huu kama isivyokuwa na mfumo wa kuwalea vijana wa kutengeneza familia za kesho! Labda mfumo wa nyumba kumi kumi na vijiji vya ujamaa ungesaidia? Hii ni historia iliyofunikwa! Maana ili kuzuia ukatili wa majumbani ni lazima kujenga jukwaa la majadiliano kuanzia kwenye familia, kaya, mitaa, vijiji, kata, wilaya hadi Taifa. Ni lazima kuwa na jukwaa la kujadili, kutafakari, kuelimishana juu ya vyanzo vya ukatili majumbani na kwa pamoja kutafuta la kufanya.

Baadhi ya vyanzo vya ukatili majumbani ni:
- Kukosekana kwa usawa katika mgawanyiko wa madaraka ndani ya familia na jamii.
- Ukosefu wa mbinu za mawasiliano na utatuzi wa matatizozo bila kutumia ukatili.
- Imani kwamba wanawake wanapaswa kuwa tegemezi kiuchumi kwa wanaume ingawa wanawake wengi wanachangia angalau kipato Fulani katika familia.
- Imani kwamba wanawake na watoto ni milki ambayo mwanaume anaweza kuitawala.
- Jamii, mashahidi, marafiki na majirani kutochukua hatua za kuzuia ukatili na unyanyasaji.

Bahati mbaya hakuna chombo cha kuandaa jukwaa la kujadili haya niliyoyataja. Mashirika mengi yanajaribu lakini yanaishia kwenye semina, makongamano na kuendesha magari ya kifahari kwa kisingizio cha kutetea haki za wanawake na watoto. Dini zetu tulizonazo na hasa hizi dini za kigeni, zimeshindwa kabisa na nyingine zinabariki ukatili kama njia mojawapo ya kuomba toba! Kanisa katoliki lilijaribu, lakini baada kusambaratishwa juhudi za kujenga jumuia ndogo ndogo na jumuiya za mkamilishano nimekuwa nikitafuta bila ya mafanikio njia ya kujenga jukwaa la majadiliano ya mambo mbali mbali katika taifa letu. Tunataka tusitake, ni majadiliano, ushirikishwaji na demokrasia vinavyoweza kusaidia kuijenga jamii yenye haki au kwa maneno mengine, jamii yenye kuziheshimu haki za binadamu.

Mwezi wa sita mwanzoni nilisafiri na kijana kutoka Dar-es-Salaam hadi Mwanza. Mimi sikuwa na mizigo mingi. Kijana huyu alikuwa na mizigo mingi, hivyo wakati wa kupima mizigo kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Dar-es-Salaam, aliniomba nimsaidie. Kawaida ya watanzania kusaidiana. Mizigo ilitufanya tuwe karibu na kwenye ndege tulikaa sehemu moja. Maongezi yetu yaliegemea kazi anazozifanya kijana huyu. Alinieleza, anafanya kazi “Kivulini”. Kwa mkazi wa jiji la Mwanza, asingeuliza maana ya “Kivulini”. Mimi si mkazi wa jiji la Mwanza, hivyo nilihitaji maelezo. Alinielezea: Kivulini, ni shirika lisilo la kiserikali la kutetea haki za wanawake lenye makao yake makuu jijini Mwanza, linalokutanisha watu wa jinsia zote kujadili, kutafakari na kutafuta suluhisho la ukatili majumbani. Neno kivuli linalotambulisha shirika hili lisilo la kiserikali limetokana na neno kivuli, kwa maana ya chini ya mti au paa ambako watu hukutana na kujadiliana kwa amani juu ya matatizo yao katika jamii.

Nilivutiwa na maelezo ya Kivulini. Kijana huyu, alinikaribisha kuitembelea kivulini. Nilisita! Nilifikiri ni shirika kama mengine ninayoyajua. Baada ya kupata habari za kifo cha mtoto wa kijiji cha Ruhita-Karagwe, aliyepoteza maisha yake wakati akiamua magomvi ya wazazi wake, RFA, nayo ikaendelea na kipindi chake cha matukio ya kila siku chenye kusheheni habari nyingi juu ya ukatili majumbani, niliamua kuitembelea Kivulini, miezi mitatu baada ya mwaliko!

Shirika la kivulini, linatofautiana na mashirika mengine ninayoyajua kwa kitu kimoja muhimu: Jinsi shirika hili lilivyofanikiwa kuunda na kutengeneza jukwaa (Kivulini, chini ya mti au chini ya paa) la majadiliano na ushirikishwaji katika makundi mbalimbali ya kijamii kama familia, viongozi wa mitaa, vijiji, dini na vikundi vya kijamii. Jukwaa hili limejengwa katika wilaya mbili za jiji la Mwanza: Nyamagana na Ilemela, katika kata za Mirongo, Mbugani, Pamba,Nyakatio, Buswelu,Mahima,Isamilo na Ilemela.

Jukwaa hili la majadiliano halimilikiwi na shirika la Kivulini, hii ndiyo tofauti kubwa inayojitokeza, jukwaa hili linamilikiwa na wananchi wenyewe! Shirika linatoa mwanga na kuwajengea wananchi uwezo wa kuelewa madhara ya ukatili unaotendeka majumbani na kuwaachia wenyewe kuamua wanawezaje kuchukua hatua dhidi ya ukatili majumbani katika maeneo yao. Katika jukwaa hili la majadiliano wahusika kukubaliana ni kitu gani wangependa kujifunza na kujadiliana zaidi juu ya mirathi, ndoa, jinsia, uchumi, ushauri nasaha, biashara nk. Shirika halipangi cha kuwafundisha, bali wenyewe hutoa maombi nini wafanyiwe, katika lengo zima la demokrasia shirikishi. Wahusika ndio wanaleta maombi juu ya aina ya mdahalo wanaoutaka na njia yake. Kama ni kwa filamu, midahalo, ziara za kimafunzo, uchoraji, muziki, msaada wa kisheria, usuluhishi wa kifamilia au warsha.

Jambo linalovutia zaidi juu ya shirika hili la Kivulini, lilioanzishwa mwaka 2000 na akinamama sita wanaharakati wa haki za Binadamu/wanawake, ni jinsi lilivyoanzisha shughuli zake kwenye eneo dogo la kata nne. Ninasema eneo dogo, maana mashirika mengi yamekuwa na tabia ya kuanza kazi katika maeneo makubwa kama wilaya nzima, mkoa, mikoa kanda au taifa, na matokeo yake inakuwa ni kazi ya kulipua tu. Kwa njia hii ya eneo dogo shirika la Kivulini, limeweza kujikita vizuri, bila kulipua, kwenye familia, mitaa na vijiji na kujenga misingi imara. Usuluhishi wa kifamilia ni eneo muhimu katika kazi za Kiuvulini, likilenga kuhakikisha wanafamilia wanajenga mahusiano mazuri. Baadhi ya wanaume huchukia wanaposhitakiwa mahakamani au kwa viongozi wao wa dini na wanawake, lakini kwa kutumia njia ya jukwaa la majadiliano na usuluhishi la Kivulini inakuwa ni furaha wanafamilia hurudi nyumbani na kuendelea na maisha na hata kurudi kwa mwenyekiti wa mtaa au kiongozi wa dini kuelezea jinsi wanavyoendelea. Hadi sasa hivi shirika hili limefanikiwa kuwa na jukwaa la zaidi ya watu 600, viongozi wa serikali 120 na viongozi wa dini 60. Watu wote hawa sasa ni chachu ya utetezi na ushawishi juu ya ukatili majumbani. Wamejifunza na kugundua njia za kushawishi mabadiliko ya miundo, sheria na kanuni zinazopingana na mikataba ya kimataifa ya Haki za binadamu/wanawake, hasa haki ya kulindwa kisheria kuanzia katika ngazi ya kaya hadi taifa.

Shirika la Kivulini, lina programu mbali mbali, mfano programu ya ushauri nasaha na msaada wa kisheria ambayo hulenga kuwashauri wanawake kuhusu haki na wajibu wao. Hutoa pia msaada katika kusuluhisha maswala ya ndoa, mirathi, wosia na ardhi. Programu nyingine ni ya mafunzo ambayo hulenga kujenga uelewa na maarifa kwa makundi maalum ya watu kama viongozi wa serikali za mitaa na viongozi wa dini wasimamizi wa sheria, walimu, wauguzi na vijana.

Mbali na programu zote hizo la kujifunza na kuiga kutoka Kivulini ni muundo wa jukwaa la majadiliano na ushirikishwaji, ni kuiga kutengeneza kivuli lilichojikita kwenye familia, mitaa vijiji, kata na wilaya. Ni kuiga kutengeneza kivuli cha kuikinga jamii na mvua na jua la Ukatili majumbani.

Na,
Padri Privatus Karugendo.

2 comments:

Fadhy Mtanga said...

Padri Karugendo, karibu sana katika ulimwengu wa kublog. Nimeanza kukusoma katika Rai ya enzi zake nikiwa mwanafunzi. Leo naona fahari kuwa nawe katika ulimwengu wa kublog.
Pamoja daima.

Yasinta Ngonyani said...

Napenda kuchukua nafasi hii na kukukaribisha sana Padre Karugendo, Karibu sana katika katika ulimeingu wa kublog.
Upendo Daima.

Post a Comment