ULEMAVU WA FIKRA

MAKALA HII ILITOKA KWENYE GAZETI LA TANZANIA DAIMA JUMAPILI 2005


ULEMAVU WA FIKRA

Nimemsikia Mzee Mengi, akiongelea ulemavu wa fikra kwenye matukio mawili tofauti. Kama si taifa letu kushambuliwa na ulemavu wa fikra. Maoni ya Mzee Mengi, yangezua mjadala mkali. Watu wangejiuliza ana maana gani anaposema ulemavu wa fikra. Mara ya kwanza nilimsikia Mzee Mengi, akiongelea ulemavu wa Fikra, wakati akiongea na walemavu. Aliwaambia wasifikirie kwamba kwa vile wana ulemavu wa viungo vya mwili, basi wao ndio walemavu; au kufikiri kwamba wao si watu muhimu katika taifa; au kujisikia unyonge na kukata tamaa, hata watu wenye viungo kamili vya mwili wanaweza kuwa walemavu na hasa ulemavu wa fikra Kwa maoni ya Mzee Mengi, mtu mwenye viungo kamili vya mwili, lakini ana ulemavu wa fikra, anaweza kuwa mnyonge na mtu asiyefaa katika jamii kuliko mtu mwenye ulemavu wa viungo!

Jana nimemsikia tena Mzee Mengi, akiongelea ulemavu wa fikra wakati akitoa hoja za kususia mkutano wa Mawasiliano. Yeye pamoja na wamiliki wa vyombo vya mawasiliano Tanzania, walisusia mkutano wa kupendekeza masharti mapya ya kutoa leseni za vyombo vya mawasiliano.

Mzee Mengi, alilalamika, kwamba watu wenye ulemavu wa fikra, waliwaacha wataalam wa mawasiliano hapa nchini na kutafuta wataalam kutoka nchi za nje Zimetumika pesa nyingi, ambavyo wataalam wangepatikana hapa kwa malipo nafuu. Kosa kama hili linafanyika kila wakati kwenye wizara nyingine. Madaktari Muhimbili, kwenye kitengo cha mifupa (MOI), walimfukuza mzungu aliyekuwa akifanya kazi ambazo watanzania wengi wangeweza kuzifanya kwa malipo nafuu. Makampuni yetu yanatupwa nje, na kazi yanapewa makampuni kutoka nje ya nchi yetu.

Inawezekana wengine wakasema kwamba watanzania hajui kufanya kazi, wanashindwa kuwajibika, wanashindwa kufanya kazi kwa uaminifu, wanafanya kazi kwa upendeleo wa kuwaajiri ndugu zao. Huo ndio ulemavu wa fikra, anaouzungumzia Mzee Mengi. Mtu mwenye fikra pevu, angejitahidi kuunda mifumo ya kutoa dosari, kabla ya kukimbilia kuwatafuta wataalam nje ya nchi. Kufunika tatizo, zi kulimaliza tatizo! Ulemavu wa fikra ndio unasababisha tuendelee kufunika matatizo!

Maoni ya Mzee Mengi, yamenifanya nitafakari mambo mawili: Kwanza nilitafakari juu ya kitabu “ Why God Won’t Go Away”. Kitabu hiki ni matokeo ya utafiti uliofanywa na Andrew Newberg,Eugene D’aquili na Vince Rause, juu ya Sayansi ya Ubongo na Biolojia ya Kuamini. Wazo kuu katika utafiti wao ni: Je, Mungu anautengeneza Ubongo au Ubongo unamtengeneza Mungu? Kitu wanachokigundua ni kwamba Ubongo ndicho chombo cha pekee katika mwili wa mwanadamu kinachotengeneza kumbukumbu na kuzitunza. Ubongo unamsukuma mwanadamu kuwa na woga na kujiuliza maswali mengi ambayo majibu yake yanamfanya mwanadamu kuishi tofauti na wanyama wengine. Mwanadamu hujiuliza: Kwanini tulizaliwa kama mwisho wetu ni kufa? Kunatokea nini tukifa? Nafasi yetu ni ipi katika ulimwengu mzima? Kwanini kuna mateso? Ni nani anayatuma mateso? Ni nani anautunza na kuulinda ulimwengu? Ulimwengu utaendelea kuwepo hadi lini? Tunawezaje kuendelea kuishi kwenye ulimwengu usioaminika bila kuwa na woga? Majibu ya maswali haya ni lazima yamwelekeze mwanadamu kwa Mungu. Majibu ya maswali haya ndio chimbuko la dini zote za dunia hii. Mtu asiyejiuliza maswali kama haya, hapana shaka ataishi kama mnyama mwingine wa porini! Huu ni mjadala mrefu na ni utafiti wa kisayansi, ni vigumu kuujadili kwenye makala hii. Unahitaji makala inayojitegemea, Mungu, akiniwezesha, nitauendeleza siku za usoni! La msingi katika mfano huu ni kutaka kuonyesha jinsi maneno ya Mzee Mengi, yalivyonifanya kutafakari mambo mazito.

Baada ya kutafakari kitabu cha “Why God Won’t Go Away”, nilitafakari maneno ya Bwana Yesu: “ Ndiyo maana ninasema nao kwa mifano, kwa sababu wanatazama lakini hawaoni, wanasikiliza lakini hawasikii, wala hawaelewi..” (Matayo13:13).

Kama anavyosema Mzee Mengi, kwamba walemavu si wale tu walio na upungufu katika viungo vya mwili, bali pia na wale wenye ulemavu wa fikra. Maana kama mtu ana macho lakini hawezi kuona, ana masikio lakini hawezi kusikia, ana pua, laikini hawezi kunusa, huyu anakuwa ni kilema. Ni wangapi wanauona umasikini wa taifa letu? Ni wangapi wanayaona magonjwa yanayotishia uhai wetu? Ni wangapi wanaosikia kelele za “Mvua za kwanza ni za kupandia”, “Tumia chandarua kujikinga na malaria”, “UKIMWI unaua”, “Usitumie pesa kuuza uhuru wako wa kuchagua, chagua kiongozi bora”, “Rushwa ni adui wa Haki, usitoe wala kupokea rushwa”. Maana yake ni kwamba kilema wa hivi ambaye ana macho lakini hawezi kuona, ana masikio lakini hawezi kusikia na ana pua lakini hawezi kunusa, Ubongo wake unakuwa umedumazwa na kupunguziwa nguvu za kutengeneza kumbukumbu na kuzitunza. Anakuwa anaelekea kwenye hali sawa na mnyama wa porini. Mara nyingi matendo yake yanakuwa ya kinyama. Ubongo ukishindwa kutengeneza kumbukumbu na kuzitunza, wema, haki na huruma, hutoweka. Mauaji ya Wayahudi milioni 6, mauaji ya Watutsi ya mwaka 1994,magomvi kati ya Waisraeli na Wapalestina, chuki kati ya Wahutu na Watutsi ni vielelezo vizuri. Ulemavu huu ni mbaya zaidi. Mtu, ambaye ana mguu mmoja, lakini ubongo wake unafanya kazi vizuri, anakuwa na manufaa makubwa katika jamii kuliko mtu ambaye ana viungo vyote vya mwili lakini ubongo wake umedumazwa.

Yesu alielezea vizuri hali kama hii:
“ Kwao yanatimia yale aliyosema nabii Isaya: ‘Kusikia mtasikia, lakini hamtaelewa; Maana akili za watu hawa zimepumbaa, wameziba masikio yao, wamefunga macho yao. La sivyo, wangeona kwa macho yao, wangesikia kwa masikio yao, wangeelewa kwa akili zao, na kunigeukia, asema Bwana nami ningewaponya”( Matayo 13:14-15).

Ulemavu wa fikra unaweza kusababishwa na mambo mengi. Mtu anaweza kuzaliwa akiwa na ulemavu wa fikra. Inawezekana ubongo ukawa na kilema cha kutoweza kutengeneza kumbukumbu na kuzitunza vizuri. Wapo watu wanazaliwa wakiwa pungwani, vichaa na wendawazimu Lakini pia kuna ulemavu wa fikra wa kujitakia au kulazimishwa. Wale wanaotumia madawa ya kulevya na ulevi wa kupindukia, wanaulazimisha ubongo kushindwa kutengeneza kumbukumbu na kuzitunza. Lakini pia kumtawala mtu kimawazo kunaweza kusababisha ulemavu wa fikra. Utumwa na ukoloni ni kati ya vitu vilivyosababisha ulemavu wa fikra. Athari hii inajitokeza katika nchi karibu zote zilizotawaliwa na kuonja adha ya utumwa. Mfano Utumwa na Ukoloni, ulisababisha baadhi ya watu kukataa mila zao, rangi ya ngozi zao, lugha zao nk.

Mtu anayeichubua ngozi yake, anakuwa na ulemavu wa fikra. Mtu anayebadilisha nywele zake na wakati mwingine kulazimika kuvaa nywele za bandia ili afanane na mzungu, anakuwa na ulemavu wa fikra. Mtu anayebadilisha jina lake la kienyeji na kujipachika jina la Wazungu au Waarabu, anakuwa na ulemavu wa fikra. Mtu anayeshabikia bidhaa kutoka nje ya nchi na kuzorotesha uchumi wa nchi yake, anakuwa na ulemavu wa fikra n.k.

Kama anavyosema Yesu: “Maana akili za watu hawa zimepumbaa….”. Ni ukweli, Wazungu walipumbaza akili zetu hadi Ubongo ukatengeneza kumbukumbu na kuzitunza kwamba Mwafrika hawezi kitu. Wazungu walituzabishia ulemavu wa fikra. Ndo maana hadi leo hii bado tunatafuta wataalam kutoka nje, kama anavyolalamika Mzee Mengi, juu ya swala zima la mawasiliano.

Tuchukulie mfano wa jamii za kwanza kuishi hapa Tanzania. Jamii zilizoanza kushuhudia kifo. Mwanaukoo anakufa. Mwili wake unawekwa mbele ya ukoo mzima, na kila mtu anashangaa ni kitu gani kimetokea. Kila mtu anajitahidi kuugusa mwili wa marehemu na kuhisi hauna uhai tena. Mtu aliyekuwa akitembea, akicheka na kufanya kazi sasa, amelala mbele yao bila kujitingisha, mwili wake hauna joto tena, hawezi kuzungumza wala kucheka. Kiongozi wa ukoo anaagiza ukokwe moto mkubwa, wanaukoo wanauzunguka moto huo wakiwa na mwili wa mwanaukoo mwenzao asiyeweza kusimama. Kila mtu anatafakari juu ya tukio hilo. Ni kitu gani kimetoweka kwenye mwili wa ndugu yao, je kitu hicho kitakuwa kimekwenda wapi. Jinsi muda unavyopita kasi ya moto mkubwa inaanza kupunguka. Kuni zilizokuwa rundo zinaanza kuungua na kuwa majivu. Kadri moto unavyopungua ndivyo moshi unavyokazana kupaa juu mawinguni. Moto unatoweka na moshi unaishia mawingu. Kiongozi wa ukoo anaanza kutafakari juu ya kuni, moto, moshi na majivu. Ubongo wake unaanza kutengeneza kumbukumbu na kuleta fikra pevu, jinsi kuni, moto na moshi vinavyopotea na kubakiza majivu, ndivyo mwili wa rafiki na mwanaukoo aliye lala mbele yao ulivyopoteza kicheko, sauti, kusimama na kubaki mwili usiokuwa na uhai. Jinsi moshi unavyoishia mawinguni, ndivyo uhai wa rafiki yao unavyoishi mawinguni pia! Fikra hii ya kiongozi inasambazwa kwa wanaukoo wote. Kwa njia hii ukoo wote unamgeukia Mungu na…. Yasemavyo maandiko: “La sivyo, wangeona kwa macho yao, wangesikia kwa masikio yao, wangeelewa kwa akili zao, na kunigeukia, asema Bwana nami ningewaponya”

Mtu ambaye hana ulemavu wa fikra. Mtu ambaye ubongo wake unafanya kazi sawa awa ni lazima ajifunze kutokana na matukio. Kama mfano nilioutoa wa watu wa jamii za mwanzo walivyokumbana na kifo bila kujua kifo ni nini, lakini kwa kuagalia kuni zikiteketea kwa moto na moshi ukipaa juu mawinguni walianza kutafakari na kutengeneza fikra pevu ambayo iliendelea vizazi na vizazi.

Mtu ambaye ana ulemavu wa fikra, hawezi kutafakari. Atakazana kulimbikiza pesa ambazo hazitamnufaisha yeye wala familia yake. Ni nani ananufaika na pesa za Mobutu au Sani Abacha? Pamoja na mifano hii ya wazi, bado kuna watu hapa Tanzania, wanaendelea kulimbikiza pesa. Watu wanakufa kwa njaa, watoto hawawezi kwenda shule, Watu wanakufa kwa magonjwa yanayotibika, Wafungwa wananyimwa haki ya kukutana na wake/waume zao kwa kisingizio kwamba serikali haina pesa, wakati kuna watu wachache wamelimbikiza pesa ambayo ingeweza kumaliza matatizo yote hayo!
Mtu mwenye fikra pevu, anaangalia uhai wake na uhai wa taifa zima. Mzee Mengi, anasema kuna mbinu za makusudi au za bahati mbaya za kuua uwezo wa wamiliki wa vyombo wa mawasiliano hapa nchini. Kipaumbele wanapewa watu kutoka nje ya nchi. Kama hii ni kweli, wale wanaotengeneza mbinu hizi wanaupenda uhai wao na uhai wa watanzania wote? Watu hawa wana fikra pevu au ni walemavu wa fikra?

Leo imetokea kwa vyombo vya mawasiliano. Kesho ni Shelaton, Royal Palm….(jina jipya ni lipi?), hivyo hivyo wanakuja wanachuma na kuondoka. Sisi tunabaki na marehemu wetu tukiwa na maswali kibao: Mbona hapumui, mbona acheki, mbona hawezi kutembea, ni kitu gani hiki kinatokea. Tukiishia hapo ndio mwisho wetu!

Ningependa kuunga mkono mawazo ya Mzee Mengi, kwamba walemavu, wasikate tamaa wala kujiona ni watu wasiokuwa na muhimu. Ulemavu wa kuchukia ni ule wa fikra.

Hivyo tunapojiandaa kuwachagua viongozi wetu, tusiwapime kwa ubora wa viungo vyao, ubora wa pua, miguu urefu, ufupi, uzuri wa sura, ubora wa kuongea lugha za kigeni, ubora wa kuvaa suti za kigeni! Tuwapime kwa ubora wa fikra zao. Kiongozi ambaye ubongo wake hauwezi kutengeneza kumbukumbu na kuzitunza, kiongozi ambaye anaitizama maiti bila kutafakari, kiongozi anayeziangalia kuni zikiteketea na moshi ukiishia mawinguni bila kutafakari, kiongozi anayeona yanayotokea kwa majira zetu akaendelea kuishi bila kutafakari, kiongozi anayeishi kwa kunywa, kula na kulala hawezi kuitawala Bongoland! Mlemavu wa viungo vya mwili anaweza kuwa kiongozi mzuri, lakini mlemavu wa fikra ni moto wa kuotea mbali!

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment