Utandawazi

MAKALA HII ILITOKEA KWENYE GAZETI LA RAI 2004.

UTANDAWAZI WENYE SURA YA UBINADAMU

Kwenye makala yaliyopita nilisisitiza kwamba ili utandawazi ufanye kazi vizuri, hasa kwenye nchi zinazoendelea, ni lazima mifumo ya mashirika ya kimataifa yanayouongoza utandawazi(IMF,World Bank na WTO) ibadilike. Pia niligusia kwamba mashirika haya ya kimataifa yanaielekeza Tanzania, kwenye utumwa. Utumwa ni kitu kibaya. Tulipokuwa watoto tulikuwa tukiimba wimbo wa: Utumwa ni kitu kibaya, tuliuzwa kama samaki, samaki wa kwetu wanono si kama wale wa Amerika........ Wimbo wenye hasa ulikuwa: Afrika nakutamani nikikumbuka sifa zako, ingawa niko nchi za mbali furaha haishi moyoni. Ni wazi hizi zilikuwa nyimbo za watumwa! Utumwa ni hali ya mtumishi asiyelipwa chochote na ambaye amefungwa, hana sauti, hana huru na huweza kutendwa lolote na bwana wake! Utumwa hauna sura ya ubinadamu!

Siwezi kupendekeza Tanzania, tuachane na utandawazi pamoja na hali hii mbaya inayojitokeza ya kutuelekeza kwenye utumwa. Hatuwezi kuutupilia mbali utandawazi na tukaendelea kuishi kwenye “kijiji kimoja” na mtaifa mengine ya dunia hii. Hali ya sasa hivi inaonyesha kwamba tunauhitaji utandawazi na utandawizi unatuhitaji. Jambo la kuzingatia ni kwamba tunauhitaji utandawazi wenye sura ya ubinadamu. Tunauhitaji utandawazi wenye uwezo wa kusukuma mbele gurudumu la uwajibikaji, uwazi, ukweli, kujitegemea, demokrasia na maendeleo. Utandawazi unaoweza kuisaidia Tanzania, kubadilika: Maisha ya watu masikini yakawa bora, kila raia akapata elimu bora, huduma bora ya afya na mambo mengine muhimu kama maji, umeme, chakula, mawasiliano nk.

Mfumo wa sasa hivi wa utandawazi unawaruhusu watu wachache, nchi chache na makampuni machache kutajirika na kupindukia wakati mamilioni ya watu duniani wanaogelea kwenye dimbwi la umasikini.

Itakuwa ni ndoto kutupilia mbalii ukweli wa ugumu uliopo wa kuibadilisha hali ya sasa. Mabadiliko ni kitu kigumu na kina gharama zake. Kila mtu anaweza kujipima mwenyewe binafsi inavyokuwa vigumu kubadilisha tabia moja na kukumbatia nyingine, kuacha ubinafsi na kuwahudumia watu wengine, kuacha ukabila na kuyakumbatia makabila na mtaifa mengine, kukubali maoni ya watu wengine, kuwakubali watu wengine jinsi walivyo nk., ni vigumu na inaumiza sana kubadilika. Mashirika ya kimataifa yanalazimika kuchukua uamuzi ambao ni mgumu na wa kuumiza wa kubadilisha mifumo yake ili mchango wake uweze kujenga utandawazi wenye sura ya ubinadamu. Kinyume chake ni kushindwa kujenga dunia yenye sura ya ubinadamu. Ugaidi ni matokeo ya utandawazi usiokuwa na sura ya ubinadamu. Hili linahitaji makala yanayojitegemea!

Mfano IMF, isikazanie tu uimara wa uchumi katika nchi zinazoendelea, bila kuangalia upatikanaji wa ajira katika nchi hizo. Watu wengi wanapoteza kazi kutokana na mashinikizo na masharti ya IMF na World Bank. Hawa watu watashughulikiwa vipi? Ni tatizo na mzigo mkubwa wa nchi zinazoendelea. Watashindwa kuendesha maisha yao, watakuwa majambazi na kujiingiza kwenye biashara ya madawa kulevya, biashara ya kuwatorosha watu na kuwapeleka kwenye nchi zilizoendelea ili kuwatumikisha na kuuza miili yao, watajiingiza kwenye matendo ya ugaidi na kuivuruga dunia nzima. IMF, isikazanie ushuru, kwamba nchi zinazoendelea zikusanye kwa nguvu zote ushuru katika nchi zao, bila kuangalia uboreshwaji wa sera ya umilikaji wa ardhi katika nchi zinazoendelea. Katika nchi hizi watu wachache wanamiliki ardhi au wana uwezo wa kuiendeleza ardhi na walio wengi wanabaki kuwa vibarua. Shinikizo na ubanfsishaji na uwekezaji linalowekwa na IMF katika nchi zinazoendelea, linachangia watu masikini kuendelea kunyong’onyea na kupoteza uwezo wa kutumia na kumiliki ardhi. IMF, inakazana kutoa mikopo kufuatana na ushauri wa wataalamu wake wa nchi zilizoendelea bila kufuata matakwa ya nchi husika kama kuboresha elimu na afya.

IMF, inajua fika kwamba nchi yenye serikali fisadi na viongozi wala rushwa haiwezi kuendesha vizuri zoezi zima la ubinafsishaji. Viongozi walewale walioshindwa kusimamia vizuri uendeshaji wa mashirika ya umma ndio hao hao wanaosimamia kuyauza mashirika hayo. Matokeo yake mashirika yanauzwa kwa bei ndogo, kwa upendeleo, na mara nyingi kwa wawekezaji wa kutoka nje ya nchi ambao wako tayari kutoa chochote (rushwa) kwa viongozi. Matokeo ya zoezi hili ni kuweka uhai wa uchumi mikononi mwa wawekezaji kutoka nchi za nje, ambao kazi yao kubwa ni kulinda maslahi yao. Nchi isipotawala uchumi wake, inakuwa si huru tena!

Utandawazi usiokuwa na sura ya ubinadamu unayaruhusu makampuni makubwa kama Coca-cola, Pepsi na Unilever kutawala soko la dunia nzima la vinywaji baridi. Hii inaua kabisa jitihada za viwanda vidogo katika nchi zinazoendelea. Mfano kiwanda cha Mali Juice, cha Bukoba, kinachotengeneza juice kutokana na matunda: Nanasi, machungwa nk, kinauza chupa nyenye ujazo sawa na wa chupa ya pepsi kwa shilingi 300-400. Pepsi wanauza 150-200. Hivyo pepsi inanyweka zaidi ya Mali Juice. Ushindani ni mkubwa. Pepsi au Coca-cola, wana uwezo wa kusambaza vinywaji vyao hadi vijijini kwa wateja na bei ya vinywaji ikabaki vile vile. Kitu ambacho kiwanda kidogo kama cha Mali Jice, hakiwezi kumudu. Kikifanya hivyo basi chupa ya mali juice itafikia 500, kitu ambacho kitaifanya isiwe na wateja!

Utandawazi usiokuwa na sura ya ubinadamu unazalisha masikini wengi. Si ukweli kwamba masikini ni wavivu na hawafanyi kazi. Masikini wanafanya kazi kubwa kwa faida kidogo, kwa mfano kama nilioutoa wa kiwanda cha Mali Juice. Na masikini wengine wanafanya kazi sana na wakati mwingine katika mazingira magumu, wengi wao wanajikuta katika mzunguko wa maisha magumu yasiyokuwa na mwisho: Bila chakula cha kutosha na chenye kiwango kinachokubalika kimataifa, mtu hawezi kuwa na afya bora ya kumwezekesha kufanya kazi kwa masaa yanayokubalika kimataifa, bila kufanya kazi kwa masaa yanayokubalika kimataifa ni vigumu kupata kipato cha kukidhi mahitaji muhimu kama kulipa karo ya watoto, bila kulipa karo, watoto hawawezi kupata elimu. Ni watanzania wangapi sasa hivi wataweza kumudu kusomesha watoto wao hadi chuo Kikuu? Mfumo mpya wa kulipia gharama za Chuo Kikuu, ni watanzania wangapi wanaweza kuukabili? Matokeo watoto watabaki bila elimu na watalazimika kuishi kwenye umasikini. Hivyo umasikini unakuwa ni kitu cha kurithi kizazi hadi kingine!

Umasikini unazaa unyonge na kutojiamini. Utafiti uliofanywa na Benki ya dunia 2000, katika zoezi lililoitwa “the voice of the poor” (sauti ya masikini tafsiri ni yangu) ulibainisha kwamba masikini wanajihisi kutokuwa na sauti, wananyanyaswa na hawana uwezo wa kuendesha mambo yao wenyewe. Wanafunikwa kwa nguvu za uchumi zilizo juu ya uwezo wao kuzidhibiti. Kwa maneno mengine wanaishi katika utumwa.

Utandawazi usiokuwa na sura ya ubinadamu unavunja mila na desturi za nchi zinazoendelea bila ya kuwa na mpango madhubuti wa kuingiza na kufundisha mila desturi mpya. Watu na hasa vijana wanapokea mila na desturi mpya kwa kuiga bila ya maandalizi yoyote yale. Matokeo yake ni vurugu, kuchanganyikiwa na kuwepo kwa utupu wenye hatari kubwa. Sasa hivi watu wengi na hasa vijana katika nchi zinazoendelea wanavikimbia vijiji vyao na kuelekea mijini. Matokeo yake ni mlipuko mkubwa wa idadi ya watu kwenye miji wasiokuwa na makazi bora. Viunga vya miji kama Dar-es-Salaam, Nairobi na Kampala, vina wakazi wanaoishi maisha ya kutisha bila huduma muhimu kama nyumba, choo, maji, chakula, hospitali, chule nk. Magonjwa ya hatari kama Kipindupindu, malaria na UKIMWI yanawashambulia bila ya huruma yoyote. Vijana wenye nguvu na uwezo wa kufanya kazi wanayapoteza maisha yao katika umri mdogo kutokana na kuishi kwenye makazi yasiyomfaa mwanadamu.

Utandawazi wenye sura ya ubinadamu ungesambaza mazuri ya utandawazi. Nchi zilizoendelea zimefika zilipo kwa kusaidiwa na kuwepo kwa serikali bora na viongozi imara na wenye mwelekeo. Mafanikio haya yalisukumwa na demokrasia, elimu, uwazi, ukweli na kuheshimu uhuru wa vyombo vya habari. Mfano nchini Marekani, demokrasia, elimu, uwazi, ukweli na uhuru wa vyombo vya habari si zawadi ya serikali kwa wananchi, bali ni HAKI ya kila raia wa Amerika.

Je, Amerika, imezisaidiaje nchi zinazoendelea kama Tanzania, kiasi kwamba kila Mtanzania akatambua kwamba demokrasia, uwazi, ukweli, elimu na uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa kutoa maoni ni haki yake? Je, mashirika ya kimataifa yanayouongoza utandawazi yanaisaidiaje Tanzania, kujichagulia viongozi wake wenyewe? Kama nilivyodokeza kwenye makala yaliyopita uchaguzi wa 2005, utatawaliwa na wawekezaji ambao wengi wao wanatoka nje ya nchi. Sina haja ya kulielezea hili zaidi hadi pale kila Mtanzania atakapolishuhudia kwa macho yake mwenyewe. 2005, haiko mbali. Tusubiri!

La kusema hapa ni kwamba hata demokrasia Tanzania, bado ni kitendawili. Mtu kuwa kwenye chama cha upinzani ni kama kufanya dhambi ya mauti. Nimesikia kwamba kuna baadhi ya viongozi wa dini wanaofundisha kwamba upinzani wa kisiasa ni dhambi. Wanawalinganisha wapinzani wa kisiasa na wapinzani waliokuwa wakijitokeza kwenye dini zao katika historia. Tumeshuhudia vituko vingi wanavyofanyiwa watu waliojitenga na CCM na kujiunga na vyama vya upinzani, hadi wanapiga magoti kuomba msamaha wa kurudishwa ndani ya kundi. Mheshimiwa Cheyo, mwenyekiti wa UDP, angekuwa mwanaCCM, macho yangefumbwa. Deni la nyumba yake wangelipa wajukuu. Baada ya kiboko cha Bariadi, sasa ni lala salama. Akipiga magoti anaweza kubaki kwenye nyumba na kupata zaidi na kuongezewa. Utandawazi haujatufundisha kuheshimu maoni tofauti na uhuru wa kutoa maoni. Hatujafahamu demokrasia ya vyama vingi ni kitu gani!

Serikali tuliyonayo sasa hivi ni ya Uwazi na Ukweli. Katika hali ya kawaida ingekuwa miongoni mwa serikali zinazozingatia utandawazi wenye sura ya ubinadamu. Yale tunayoyashuhudia yanaleta mashaka. Mifano ni mingi na kila mtu ana mifano yake na wengine wanauona huu kama uzushi. Waswahili wanasema: Lisemwalo lipo, vinginevyo litakuwa njiani. Nitoe mfano mmoja “unaowatonesha” wakazi wa kanda ya ziwa. Sakata la meli ziendazo kwa kasi. Leo hii zingekuwa Mwanza, zikitoa huduma kati ya Bukoba na Mwanza. Hili lingekuwa Jambo la maendeleo na jambo la kukuza uchumi wa Taifa. Meli hizi kushindwa kufika Mwanza, kunazua maswali mengi: Je, huu ndio uwazi na ukweli? Je, huu ndio utandawazi? Je ni siasa au kampeni? Sina haja ya kurudia yaliyotokea ya Waziri mmoja kuzibariki meli kusafirishwa hadi Mwanza, na waziri mwingine kuweka vikwazo. Mawaziri wa chama kimoja na serikali moja! Watanzania wanayajua haya labda yule asiyesoma magazeti na kusikiliza radio na luninga. Tunajua pia kwamba hata taarifa za wataalamu wa nchi yetu kuhusu upana na uzito wa meli hizo inatofautiana! Labda walisoma vyuo tofauti na maprofesa wanaozidiana ujuzi! La kushangaza zaidi katika sakata hii zima ni hoja inayotolewa kwamba meli hizo zitaharibu barabara na madaraja ,Ni nani atawajibika kufanya ukarabati? Wizara ya ujenzi inauliza!

Mtu unaweza kulazimika kuuuliza swali la kipumbavu: Barabara na madaraja yakiharibiwa na El-nino, tunaambiwa iko njiani. Ni nani atawajibika kufanya ukarabati? Au madaraja yakihujumiwa – kama nguzo za umeme zinahujumiwa, inawezekana na madaraja pia – ni nani atawajibika kufanya ukarabati? Ndege ya mtukufu Rais, inaingia hivi karibuni, ni bilioni 40, ni nani atawajibika kuzilipa? Hizi meli zingekuwa silaha za kwenda kuyamaliza maisha ya watu, kuharibu barabara na madaraja kule Rwanda, Burundi, Uganda na DRC, zingezuiliwa? Mbona tulishuhudia vifaru vikipita kwenye barabara zetu kukoka kwenye bandari ya Kemondo kuelekea Mutukula Uganda? Barabara na madaraja viliharibika, tuliviona. Ni nani alifanya ukarabati?

Swali jingine la kipumbavu: Sasa hivi tunashuhudia ziara za viongozi wa ngazi za juu serikalini katika mikoa na wilaya hadi vijijini. Kasi ya ziara hizi haikuonekana miaka mitatu nyumba. Wachambuzi wa mambo wanasema hizi ni kampeni za chini chini. Je, ni nani anawajibika kuzilipia safari hizi? Akisafiri Waziri mkuu anatumia pesa ngapi? Akisafiri makamu wa rais anatumia pesa ngapi? Bila kuwataja waheshimiwa mawaziri wanaopitapita kila sehemu sasa hivi. Umuhimu wa ziara hizi ni upi? Kama si kampeni? Mbona hatuuulizi gharama hizi? Huduma kwa wananchi yanakuja maswali, huduma kwa viongozi kigugumizi?!

Na hawa ni wajinga gani waliofanya ununuzi wa meli kwa bei zote hizo bila kwanza kufanya utafiti wa namna ya kuzisafirisha? Mbona tumeishaupita ulimwengu huu wa giza? Kwa mtandao mtu anajua hali ya barabara ya Dar- Mwanza, akiwa amekaa kwenye ofisi yake ya Amerika Huo ndio utadawazi! Kinyume chake ni kujifanya vichokoo na kujifunga kamba shingoni. Tutachekwa kama siyo kusutwa!

Swali jingine la kipumbavu: Mikoa ya Kagera na Mwanza, au mikoa ya kanda ya ziwa ukitaka, inachangia kiasi gani katika pato la Taifa? Kahawa, pamba, tumbaku, samaki, nyama, maziwa, ngozi, madini, utalii nk. Hii haitoshi kuisukuma serikali kuziruhusu meli hizi kusafirishwa hadi Mwanza, kwa gharama yoyote ile. Hata mkoloni aliamua kujenga reli ya Dar-Mwanza, baada ya kuzingatia umuhimu wa pato la mikoa hii kwa taifa zima la Tanganyika!

Meli hizi zingeharakisha kasi ya maendeleo katika mikoa hii. Hata hivyo ni nani asiyejua matatizo ya usafiri katika mikoa hii, hasa mkoa wa Kagera? Historia itufundishe nini? Mradi wa bonde la Ngono, ulihujumiwa hivi hivi ukafa! Mradi wa bonde la Kagera hivyo hivyo. Sasa meli ziendazo kwa kasi zinarudishwa zilikotoka? Haya ndio maendeleo? Huu ndio uwazi na ukweli? Huu ndio utandawazi?

Wakati tunayashinikiza mashirika ya kimataifa kubadilisha mifumo yake na kuyataka kutuletea utandawazi wenye sura ya ubinadamu, ni lazima na sisi tuanze kubadilika. Tujifunze kuwajibika, tujifunze kuwa wazi, tujifunze kusema ukweli, tujifunze kulitanguliza taifa letu kuliko kutanguliza sifa, tamaa na maslahi binafsi. Ni lazima sisi pia tuonyeshe utayari wa kupokea utandawazi wenye sura ya ubinadamu. Vinginevyo tunajiingiza kwenye Utumwa, na utumwa daima hauna sura ya ubinadamu.

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment