WABUNGE WA CCM WANAISHI TANZANIA IPI?

Sina uhakika kama kwenye makala hii nitaandika kitu ambacho sijawahi kuandika siku za nyuma au ambacho wenzangu hawajakiandika; kwa vile bado tunajenga nyumba yetu na itachukua miaka mingi kuikamilisha haijalishi kama ninarudia yale yale! Ujenzi huu unahitaji kila aina ya mchango na kwa vile nyumba yenyewe ndio bado na msingi uliojengwa unabomoka; na watu wenyewe hawataki kusikia; tutaendelea na wimbo ule ule hadi masikio yao yatazibuka!

Sina tatizo tena na wabunge wa CCM kukisifia chama chao. Hata wakishinda wanakisifia na kukesha wakikisifia; ni chama chao; ni mkombozi wao; anayekulisha, akakutunza na kukuweka salama huyo ndio mfalme wako. Utaimba sifa zake na kumtukuza. Na wala hakuna jipya; wataimba, watasifia na mengine mengi, lakini ni lazima wataingia kwenye mnyororo wa historia wa kumpanda na kushuka na wakati mwingine kupotea kabisa. Hili tuliache maana lina wakati wake wa kulijadili au litajadiliwa na wale watakao kuwa wanajifunza historia ya nchi hii siku zijazo.

Sina lengo la kuwalaumu wabunge wa CCM kwa utamaduni wao wa kuunga mkono hoja asilimia miamoja huku wakiorodhesha matatizo chungu nzima ambayo yanasababishwa na Serikali inayoongozwa na chama chao; huu pia ni utamaduni wa chama chao ambao katika hali ya kawaida unazua wasi wasi juu ya namna yao ya kufikiri na kuyaona mambo. Labda wana matatizo la kuzitambua rangi, kwao nyeupe ni kijani, na nyeusi ni njano; inawezekana kabisa kwamba macho yao hayawezi kuona rangi nyingine zaidi ya kijani na njano.

Labda niwakumbushe wasomaji wangu kwamba hatuandiki na kufanya uchambuzi wa jinsi mambo yanavyokwenda katika taifa letu kwa lengo la chuki binafsi; kumchukia mtu, kukichukia chama ama kukipigia debe chama Fulani. Inaweza kuwa tafsiri ya msomaji, lakini si lengo! Tunalenga katika kujenga utamaduni wa kukubali kukosolewa, utamaduni wa kuambizana ukweli hata kama ukweli wakati mwingine unauma; tunajaribu kuona kama watanzania tunaweza kuwa na mwelekeo hata kama tunatumia njia tano tofauti, tufike tunakotaka kwenda.

Hoja yangu ya leo ni  AMANI. Kwenye Bunge la bajeti linaloendelea kule Dodoma, akisimama mbunge wa CCM, baada ya Litania ya kukipongeza chama chake kwa ushindi wa kishindo, kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete, Kumpongeza Mheshimiwa Spika mwanamke wa kwanza kukalia kiti hicho, kuwashukuru wapiga kura kwa kuchagua kati ya mbivu na mbichi, kuishukuru familia: mme, mke, watoto, wajukuu nk, wanageukia AMANI. Kwamba kuna watu wanataka kuivunja Amani ya taifa letu. Kwamba kuna watu wanashinda wanazunguka nchi nzima kwa lengo la kutaka kuvunja amani. Hata kama hawataji jina, lakini kila Mtanzania anafahamu wanachotaka kusema.

Wabunge wa CCM wanapoteza muda mwingi wakieleza jinsi watu wenye nia mbaya watakavyo vuruga amani ya Tanzania; wakati mwingine mtu anaweza kufikiri wako kwenye bunge la Afrika ya mashariki, wanatoa taarifa kwa Waganda, Wakenya, Wanyarwanda na Warundi wasioishi Tanzania. Wabunge wa CCM, pia wanakemea “vurugu” zinazojitokeza Bungeni, ambazo kwa kiasi kikubwa zinasababishwa na Spika na wenyeviti wake ambao wameamua wazi wazi kukibeba na kukipendelea chama chao cha CCM. Spika anaposhindwa kulisimamia bunge kwa kanuni zilizopo , na kwa mujibu wa katiba yetu; kwamba Bunge si mali ya chama, bali bunge la taifa zima anategemea nini kama si vurugu na uvunjifu wa Amani?

Swali langu ni je ni nani anataka kuivunja AMANI ya Tanzania? Hawa wabunge wa CCM wanaishi Tanzania ipi? Maana swala la amani si la ushabiki wa chama; swala la amani linatugusa sote. Kila Mtanzania ana wajibu wa kulinda usalama na amani katika taifa letu. Ndio maana uongo na uzushi wa wabunge wa CCM hauvumiliki. Wanataka kutulisha kasumba kwamba kuna mtu mwingine mbali na CCM anayetaka kuvuruga amani ya taifa letu? Nilishaandika miaka ya nyuma kwamba kama kuna kitu kitakachovuruga amani ya taifa letu ni Chama Cha Mapinduzi. Niwepo kulishuhudia hili nisiwepo, lakini historia itafanya kazi yake.

Tukiziangalia nchi zilizotuzunguka, nchi ambazo amani ilipotea na kupigana vita ya wenyewe kwa wenyewe, damu ikamwagika na maisha ya watu kupotea, chanzo chake ni nini? Ni kugombania madaraka, ni kugombania rasilimali, ni kugombania ardhi, ubaguzi na ushawishi wa kibeberu. Mfano wa Rwanda, Burundi, Uganda, DRC, Somalia; na vita nyingine mbaya iliyo mbele yetu ni kugombania maji na chakula; tunawahitaji viongozi wenye upeo na karama ya uongozi kuepusha janga hili kubwa. Maana hili likitokea hakuna nchi ya Afrika itakayobaki na amani.

Kama amani ya Tanzania itapotea; na dalili zinaanza kujitokeza; haitasababishwa na maandamano yanayoendelea ya kuzunguka nchi nzima na wala hayatasabahishwa na vyama vya upinzani. Tutapigana na kuuana tukigombania madaraka, tukigombania rasilimali, tukigombania ardhi, maji, chakula na kushinikizwa na ushawishi wa kibeberu.

Haya yakitokea ni nani wa kulaumiwa? Ni nani kinara wa kugombania madaraka katika taifa letu? Ni nani anashindwa kutunga sera nzuri za kuhakikisha kila Mtanzania ananufaika na rasilimali za nchi hii? Ni nani anashindwa kutengeneza sera nzuri za kulinda ardhi yetu? Ardhi inaporwa na kuuzwa kwa wageni! Ni nani anatengeneza mikataba mibovu ya uwekezaji kiasi kwamba rasilimali zetu zinasombwa na kupelekwa nje kwa bei ya kutupwa? Ni nani anazalisha umasikini mkubwa ndani ya taifa letu? Ni nani anaongoza ajenda ya ubaguzi katika taifa letu? Bila njano na kijani wewe si mwenzetu! Hata kama umesoma, hata kama una ujuzi wa hali ya juu; bila njano na kijani utabaguliwa! Nani anaongoza kuwasujudu na kuwaabudu mabeberu kiasi cha kulamba hata viatu vyao?

CCM ni chama kilicho madarakani miaka yote hii 50 ya uhuru wa taifa letu; pia ni chama kisichotaka kuondoka madarakani. Na ndani ya miaka hamsini kimejenga utamaduni wa kugombania madaraka. Tumeshuhudia na bado tunaendelea kushuhudia vita ya kugombania madaraka ndani ya chama hiki; tumeshuhudia mtandao na makovu yake; sasa kuna kuvuana gamba na nguvu za watu wachache wenye fedha na ushawishi mkubwa ndani ya chama cha CCM. Hoja yangu ni kwamba vita ya kugombania madaraka ikiibuka katika taifa letu, itakuwa na sura mbili: Kuna vita ya CCM wao kwa wao, na kuna vita ya vyama vingine kutaka kuiondoa CCM madarakani. Hili likitokea wa kulaumiwa ni nani?

Serikali iliyo madarakani ndiyo yenye wajibu wa kuhakikisha rasilimali za taifa zinawanufaisha wananchi wote. Hili halifanyiki! Rasilimali zinawanufaisha wachache na kuwaacha wale wanaoishi pembezoni wakitaabika kwenye umasikini usiopimika. Hawa wakiamuka na kuanza kudai usawa katika kugawana rasilimali, si patachimbika? Hili likitokea wa kulaumiwa ni nani?

Ardhi inauzwa, ardhi inaporwa na serikali imekaa kimya. Watu wakisimama na kuchukua silaha kuipigania ardhi yao, ni nani wa kulaumiwa? Tuliyoyashuhudia Nyamongo, Manyara na Loliondo; ni uchochezi wa vyama vya siasa  au ni wananchi wenyewe kugundua kwamba serikali yao inawasaliti?

Leo hii kilio cha watanzania wote ni kupata katiba mpya. Lakini mchakato unavyoendelea ni wa kuirekebisha na kuiwekea viraka katiba ya zamani. Na hili la katiba tutake tusitake kama likiendeshwa kinyume na matarajio ya wengi ni lazima patachimbika. Na hili likitokea utakuwa ni uchochezi wa vyama vya siasa au ni makosa ya chama kinachotawala ambacho kinaziba masikio na kutufanya tuamini kwamba nchi hii ni mali ya CCM?

Chama ambacho hakijaingia madarakani hakiwezi kuwa chanzo cha kuvunja amani. Vyanzo vyote vya uvunjifu wa amani vinatengenezwa na serikali; sina haja ya kutoa mifano maana sote tunaishi Tanzania; labda wabunge wetu wa CCM wanaoishi kwenye kivuli cha Tanzania. Ninasema wanaishi kwenye kivuli  kwa maana kwamba hawana uwezo wa kuviona vitu kwenye uhalisia wake. Mbali na kushindwa kuyaona hayo niliyoyataja hapo juu inashangaza kuwasikia baadhi ya wabunge wa CCM ambao sote tunajua hawakushinda uchaguzi, na wao wanajua kwamba waliupora ushindi; bado wanaendelea kutamba kwamba walishinda kwa kishindo na wananchi wanajua kuchagua mbivu na mbichi.

Kuna ushahidi wa kutosha kwamba kuna baadhi ya wa bunge wa CCM ambao hawawezi kwenda kwenye majimbo yao ya uchaguzi na kufanya mikutano ya hadhara. Na wao wenyewe wanajua fika  kwamba hawakubaliki; kuna wengine walitumia fedha kuwanunua watu ili wapitishwe bila kupingwa; lakini leo hii ukiitisha kura ya ndiyo na hapana yatakuwa kama yale ya Nyamagana. Inashangaza wabunge hawa wanasimama ndani ya Bunge na kujigamba kwamba walishinda kwa kishindo. Hizi ni dalili nzuri za kuilinda amani?

Kama wabunge wetu wa CCM wanaishi ndani ya Tanzania yetu hii, tunayoijua na kuifahamu vizuri; tunawaomba waache tabia yao ya kuwajengea hofu watanzania ili wavichukie vyama vya siasa; waache kusema uongo; wajifunze kusema ukweli na hasa wafanye jitihada za kusahihisha makosa ndani ya chama chao. Wajifunze mambo mapya na kuachana na mawazo mgando. Waone wenzao wa vyama vya upinzani wanavyotembea na wakati. Wakati wa Waziri wa Fedha anawasilisha hotuba yake kwa mtindo wa kizamani wa kulamba karatasi hadi mate yanakauka, mwenzake wa upinzani aliwasilisha hotuba yake kwa mtindo wa doti komu, teknolojia mpya ambayo haikulazimishi kubebana na makaratasi na mikoba. Vile vile  Waziri Mkuu aliwasilisha hotuba yake kwa mtindo ule ule wa kuyalamba makaratasi, lakini mwenzake wa upinzani alitumia teknolojia mpya.

Hili la serikali kuwa nyuma ya teknolojia wakati upinzani unakimbizana na teknolojia linaweza kuonekana ni dogo, lakini lina ujumbe mzito. Maana yake ni kwamba Serikali yetu imezeeka, haiwezi kutembea na wakati, haiwezi kutusaidia kupambana na dunia hii yenye kwenda kwa kasi ya kutisha; kuzilinda rasilimali zetu ni lazima tuwe tayari kupambana na dunia hii inayokwenda kasi; vinginevyo tutapotea na kumezwa! Mtu anayelamba karatasi huwezi kumlinganisha na yule anayebofya tu mambo yakajipa! Wabunge wa vyama vya upinzani wamekaa ki doti komu; Wakisimama kuchangia, si kulaumu tu wala kusifia, wanatoa hoja nzito, zilizofanyiwa utafiti, zenye uzalendo na zinazotoka kwa wananchi na hii ndiyo njia ya kujenga amani ndani ya taifa letu. Je wabunge wetu wa CCM hawaoni ukweli huu? Wanaishi nchi gani? Tanzania hii au Mwezini?

Na,
Padri Privatus Karugendo.

 

0 comments:

Post a Comment