TULIJADILI SWALA LA
USHOGA KWA MAWAZO MAPANA.
Tamasha la jinsia la
mwaka 2009, swala la ushoga na usagaji
lilijitokeza, tulilijadili na kuliandika kwa mapana na marefu yake. Baadhi ya
wachangiaji waliunga mkono hoja chanya zilizotolewa juu ya swala zima la ushoga
na usagaji, baadhi walipinga na wengine walilaani na kutukana. Tamasha la
jinsia la mwaka huu swala hili limejitokeza tena na zamu hii kelele, matusi,
kulaani vimekuwa vingi kiasi cha
kuvuruga amani na imani za watu wengi.
Kuna sababu mbili kuu
zilizovuruga hali ya hewa juu ya swala hili la Ushoga; si kwamba nia ni kuunga
mkono ushoga bali uelewa wa kulishughulikia jambo lililopo (Ushoga ni ukweli
ulio katika jamii yetu, tunataka tusitake) ulifungwa na sababu mbili
nitakazozitaja:
Moja, ni kwamba mashoga
wamedai haki zao za msingi ziingizwe kwenye katiba, kwa vile kuna baadhi ya
watu wanaofikiri Katiba ni mali yao, wao ndio watanzania na wao tu ndio wana
haki ya kuishi na kusikilizwa swala la mashoga liliwachefua na mbili ni kwamba
walijitokeza baadhi ya waandishi wa habari ambao kwa sababu zao binafsi
waliamua kupotosha agenda nzima ya Tamasha la jinsia kwa kuandika kwamba Ushoga
ni agenda ya TNGP kwenye Tamasha la jinsia.
Mada kuu ya Tamasha la
jinsia la 2011 ilikuwa ni Ardhi, Nguvu kazi na maisha endelevu katika muktadha
mzima wa Jinsia, Demokrasia na Maendeleo. Katika kujadili mada hii mambo mengi
yalijitokeza kama vile Katiba, ukatili
wa wafanyakazi wa majumbani, uporwaji wa ardhi, ukosefu wa ajira, uchumi kukua
wakati umasikini unaongezeka kwa kasi ya kutisha na mengine mengi likiwemo na
hili la ushoga.
Waandishi wa habari
wenye mtizamo finyu na wenye malengo yao binafsi, waliyaacha mengine yote na
kuliwekea mkazo hili la ushoga na kuendelea kupotosha kwamba hii ni kazi ya
TGNP. Tamasha la jinsia linaandaliwa na Mtandao wa Mashirika ya watetezi wa
Haki za Binadamu na Usawa wa Kijinsia (FemAct). Huu ni muungano wa mashirika
zaidi ya 40 mengi kati yao yakifanya kazi kama asasi za kiraia ndani ya
Tanzania. FemAct inajihusisha zaidi na ujenzi wa usawa katika mipango ya
maendeleo na usawa kati ya wanaume na wanawake. Uwepo wa FemAct ni kutokana na
imani ya ukombozi wa umma kutokana na aina yoyote ya unyonyaji, na ambamo haki
za wanawake ni haki za binadamu, na upatikanaji wake unakwenda sambamba na
upatikanaji haki kwa makundi mengine ya -kijamii.
Hivyo kutaja kwamba
Tamasha liliandaliwa na TGNP peke yao ni upotoshaji na kwamba agenda ya ushoga
ni ya TGNP ni upotoshaji pia. Tamasha la Jinsia linaandaliwa na FemAct na ni
jukwaa la wazi kwa watu wote na hasa watu wa pembezoni ambao sauti zao
hazisikiki kabisa. Hivyo mashoga nao kama watu ambao sauti zao hazisikiki,
walipata nafasi kwenye jukwaa la jinsia.
Hoja si kuunga mkono
ushoga au kuukubali na kuubariki. Hoja iliyo mbele yetu ni kwamba ushoga upo na
unashika kasi. Ushuhuda kutoka kwa mashoga wenyewe ni kwamba wateja wao ni
mawaziri na wabunge. Ukisikiliza maelezo yao ni kwamba kwa namna moja ama
nyingine kila mmoja wetu kwenye jamii yetu anashiriki. Hivyo dawa si kulaani au
kuwatukana mashoga na jukwaa lililowapatia nafasi ya sauti zao kusikika.
Tujiulize kama jamii ni kwa nini kuna mmomonyoko wa maadili na kwa wale
wanaozifuata dini za kigeni, tujiulize ni kwa nini hatuzingatii tena Amri za mwenyezi
Mungu?
Ukisoma kwenye kumbukumbu za wamisionari wa kwanza
walioeneza Ukristu barani Afrika, wanaungama wazi kwamba Waafrika waliziishi na
kuzishika Amri kumi za Mungu, hata
kabla ya kuletewa imani za kigeni: Walimpenda na kumwabudu Mungu, kiasi kila
familia ilikuwa na madhabahu ndani ya nyumba. Mungu, alikuwa karibu, waliongea
naye, walikula naye na kulala naye kwenye nyumba zao. Mungu wao aliyaongoza
maisha ya kila siku, alikuwa Mungu wa mvua, Mungu wa jua, Mungu wa ziwa na
bahari, Mungu wa uzima, Mungu wa mavuno, Mungu wa misitu na uwindaji nk. Kila
ukoo uliunganishwa na Mungu, chini ya madhabahu ya ukoo na kila kijiji
kiliunganishwa na Mungu, chini ya madhabahu ya kijiji. Watoto waliwaheshimu
wazazi wao, walipokea ushauri wao na kuchota hekima kutoka kwenye hazina ya
wazazi wao. Uhalifu haukuwepo, hata kama uhalifu ungetokea kwa bahati mbaya,
familia, ukoo au kijiji, ingemwajibisha mhalifu na kumrekebisha. Nyumba
hazikuwa na milango wala mlizi na wala wizi haukutokea. Ndoa zilizokuwa nyingi
zilikuwa za mme mmoja wanawake wengi, lakini wanaume walikuwa waaminifu kwa
wake zao, watoto wote walitunzwa sawa. Hakukuwepo kitu kama watoto wa mitaani
au nyumba za watoto yatima, kila mtoto alitunzwa kwenye familia: “Kitanda
hakizai haramu”! Tendo la ndoa kabla ya ndoa lilikuwa mwiko, hivyo haikuwa
kawaida msichana kubeba mimba kabla ya ndoa. Umalaya ,uchangudoa, ushoga na
usagaji ni misamiati ambayo haikujulikana kabisa.
Ingawa Ukristu unahimiza ndoa ya mme mmoja mke
mmoja. Uzinzi umeshamiri katika nyakati hizi tulizomo. Unafiki katika ndoa
umeongezeka, walio wengi katika ndoa za Kikristu wanamtunza mke mmoja kwenye
nyumba ya ndoa, lakini wanakuwa na nyumba ndogo kibao. Wengine wanashindwa
kabisa kuwatunza watoto wa nje ya ndoa kwa kuliogopa kanisa. Hivyo ndoa nyingi
za Kikristu zinachangia kuzalisha watoto wengi wa mitaani na yatima ambao baba zao wanaishi kwa furaha na
amani katika ndoa zao na kupokea sakramenti ya Ekaristi takatifu kila Jumapili
na kutoka sadaka kubwa kubwa makanisani!
Mbali na unafiki, uzinzi, kutowajibika na ukosefu
wa uaminifu katika ndoa za Kikristu, tumeshuhudia pia mambo kama ushoga na
usagaji ambayo hayakujulikana katika jamii za Kiafrika. Umalaya na uchangudoa
ni vitu vigeni katika jamii zetu. Imezuka na tabia ya wazazi kutembea na
mabinti zao, wengine kwa siri na kwa makubaliano, na walio wengi ni kwa
kuwabaka. Pia imezuka tabia ya ubakaji kwa jinsia zote mbili, mara nyingi
wanaotendewa vitendo hivi ni watoto wadogo walio chini ya umri wa miaka kumi!
Hili ni jambo ambalo lisingetokea kwenye jamii za Kiafrika kabla ya ujio wa
dini za kigeni.
Mtu anaweza kujiuliza ni kwa nini jamii za
Waafrika ziliishi na kuzishika Amri Kumi za Mungu kabla ya Ukristu na kushindwa
kuziishi na kuzishika baada ya kuhubiriwa “Neno” la Mungu?
Hapa kuna mambo matatu ya kuchambua:
-
Wamisionari walikazania kubatiza na kumwingiza kwenye imani mtu mmoja
mmoja. Walifikiri kila mtu alikuwa huru na kuishi kwa kujitegemea.
Hawakuugundua ushawishi wa jamii nzima kwa mtu mmoja mmoja na jinsi jamii za
Kiafrika zilivyokuwa zimesukwa kwa mshikamano. Walitakiwa kuibatiza jamii
nzima, badala ya kumbatiza mtu mmoja mmoja. Bahati mbaya hawakuwa na mfumo huu
na hadi leo hii kanisa halijafanikiwa kuubuni! Bado kanisa linakazania imani ya
mtu mmoja mmoja: “Okwo omuntu achuma omwoyogwe aba nikwo abintungwa” ( Jinsi
mtu anavyoishughulikia roho yake ndivyo anavyopata neema). Mfumo huu hauwezi
kusaidia watu kuzishika Amri za Mungu. Ni mfumo wa kuendekeza ubinafsi na
ubinafsi ni sumu ya Amri za Mungu!
-
Wamissionari waliamini kwamba masakramenti yangefanya miujiza ya
kuwabadilisha watu. Haikuingia akilini mwao kwamba, utamaduni, mila na desturi
na hali mbaya ya uchumi vingekwamisha nguvu za sakramenti. Badala ya kuubatiza utamaduni na kuuboresha, wenyewe
walikazana kuufuta! Mfano matendo mabaya(dhambi) katika jamii za Kiafrika
yalishughulikiwa na jamii nzima. Ilikuwa ni haki ya kila mwanajamii kufahamu ni
mtu gani ametenda mambo mabaya. Kila mtu aliruhusiwa kumsuta na kumsaidia
kujirekebisha yule aliyetenda dhambi. Hivyo watu waliogopa kutenda dhambi ili
wasiwekwe hadharani. Wamisionari walileta mfumo mpya, dhambi ikawa jukumu la
mtu binafsi, yeye na Mungu wake kupitia kwa padri. Mtu anatenda makosa katika
jamii, anakimbia kimya kimya kuungama kwa padri na kuondolewa bila ya jamii kushirikishwa.
Mfumo huu uliongeza kasi ya kuzivunja Amri Kumi za Mungu. Hakuna aliyekuwa
anaona aibu ya kutenda dhambi, maana akitenda dhambi hawekwi hadharani, hakuna wa kumsuta – bali ana
mchawi wake wa kumwondolea na kumwombea msamaha kwa Mwenyezi Mungu. Kwa vile
anatenda dhambi sirini na kutubu sirini, anaweza kuendelea kutenda dhambi na
kuleta madhara makubwa katika jamii. Ni wazi kabisa kwamba wale wanaotembea na
mashoga, wanaungama na kuondolewa: Hawatukanwi wala kulaaniwa! Dhambi inabaki
kwa mashoga, hawa ndio wanatukanwa na kulaaniwa!
-
Wamissionari walieneza neno la
Mungu, kwa kumfuasa Kristu. Kwa vile Kristu alifundisha na kuwatibu
watu, basi nao walijenga mashule na mahospitali. Matokeo ya shule hizi za
wamisionari hayakuwa mazuri kama walivyoyategemea. Karibu viongozi wote wa
Afrika Huru walipitia katika shule za wamisionari. Mfano Mobutu, aliyepora nchi
yake mali nyingi na kuwaacha watu wengi katika umasikini unaonuka, aliyechinja
ndugu zake bila huruma na kusababisha vita ya DRC isiyoisha, alisomea kwenye
shule za wamisionari. Nchi kama Burundi, ambayo imetawaliwa na ukabila na
mauaji ya kutisha, viongozi wake wote wamelelewa katika shule za wamisionari.
Kwa sababu ya uwezo mdogo wa kiuchumi, si watu wengi waliopata nafasi ya
kuingia kwenye shule zilizoanzishwa na wamisionari, hivyo shule badala ya
kujenga jamii moja, zilizalisha matabaka. Tabaka la wasomi walioishi maisha
kama ya wamisionari na wakoloni na tabaka la watu wa kawaida ambao hawakuenda
shule. Baada ya huru, tabaka hizi zilienda hadi leo hii. Tabaka hizi
zinachangia kuvuruga amani katika nchi nyingi za Kiafrika. Hivyo shule za
wamisionari hazikusaidia kumjenga mtu anayezishika na kuziishi Amri kumi za
Mungu! Kwanini basi shule hizi zilishindwa hivyo, ni makala nyingine
-
Kwa vile wamisionari hawakuubatiza uchumi, mahospitali waliyoyaanzisha, leo
hii yanawahudumia watu wenye kipato. Ni jambo muhimu kuwa na hospitali na ni
jambo jema kuzishughulikia afya za watu, lakini wamisionari waliwalenga watu wa
kipato cha chini na walilenga katika kutoa huduma. Hali halisi na uchumi wa
dunia ya leo ulivyo jambo hili haliwezekani. Tujuavyo Waafrika walio wengi wana
kipato cha chini, hivyo hawawezi kupata huduma katika hospitali hizi. Hivyo
hayana uwezo wa kuponya na kufanya miujiza kama ya Yesu.
Hoja ninayoijenga kwenye makala hii ni kwamba
badala ya kuwalaani na kuwatukana mashoga na majukwaa yanayowapatia nafasi ya
sauti zao kusikika, tujadili jinsi ya kuunda mifumo ya kuboresha maadili yetu
kama taifa na kutanzua matatizo mengine mengi katika taifa letu. Tuna tatizo la
katiba, tume huru ya uchaguzi, uchumi mbovu, uporaji wa ardhi, huduma mbovu za
-kijamii, uongozi mbovu, elimu duni, unyanyasaji wa kijinsia na sauti za walio
pembezoni kutosikika kwenye vyombo vya maamuzi. Hivyo tusilijadili swala la ushoga
peke yake, tulijadili ndani ya mawazo mapana maana lina mambo mengine mengi
yanalolizunguka.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
0 comments:
Post a Comment