NCHI YETU TANZANIA

 
Tarehe 19.8.2011 Maa Media Centre ilizindua vipindi vya televisheni  vya Nchi yetu vitakavyoanza kuonyeshwa hivi karibuni kwenye TBC. Uzinduzi huu ulifanyika kwenye ukumbi wa New World Cinema (Nyerere Gallery –Mwenge). Mgeni rasmi katika uzinduzi huu alikuwa Waziri wa Habari, utamaduni na Michezo Mheshimiwa Nchimbi.
 
Ni jambo la kufurahisha na kusifia Waziri anapotambua wajibu wake kama alivyofanya Mheshimiwa Nchimbi kuzindua shughuli zilizo chini ya wizara yake. Kazi za Mawaziri si kukaa maofisini, bali ni kuzunguka nchi nzima kuhakikisha sera za chama chao na mipango ya serikali inatekelezwa. Kasoro iliyojitokeza (nilivyoona mimi) ni Mheshimiwa Nchimbi, kuwa Dar-es-Salaam, akizindua vipindi vya Maa Media Centre, wakati alitakiwa kuwa Bungeni Dodoma akiwawakilisha wapiga kura wake katika Bunge la Bajeti. Labda ufunguzi huu ungesogezwa mbele hadi mwisho wa Bunge la bajeti. Hata hivyo si Mheshimiwa Nchimbi peke yake, tumekuwa tukishuhudia baadhi ya Mawaziri wakiwa Mikoani, Dar-es-Salaam au nje ya nchi wakati Bunge likiendelea. Hata wabunge wengine ambao si mawaziri tunashuhudia wakiwa nje ya Dodoma wakati Bunge likiendelea. Ni vigumu kuwa na wabunge wote asilimia miamoja wakati Bunge linaendelea; kuna wagonjwa na wengine wenye sababu za msingi ambazo ziko juu ya uwezo wa mwanadamu; lakini Bunge linapofikia hatua ya kuwa hata chini ya nusu, inatisha na kutia mashaka. Je kanuni za Bunge zinalegea sana inapofikia kwenye mahudhurio?  Au ni makosa tunayoyafanya ya kuwapatia wabunge wetu uwaziri na kuwachagua wabunge wenye shughuli nyingi binafsi ambazo haziwezi kuwaruhusu kukaa Bungeni muda wote?
 
Watu wengi wakiwemo na baadhi ya mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa Tanzania, walifika pale Mwenge kushuhudia uzinduzi wa vipindi hivi vilivyoandaliwa na Maa Media Centre ambao pia ndio wanaoandaa na kurusha kipindi cha Dala Dala.
 
Vipindi hivi vya Nchi yetu vitajikita kwenye Haki za binadamu ndani ya nchi yetu ya Tanzania na vitarushwa na TBC  kwa miezi mitatu mfululizo. Ni vipindi vilivyofanyiwa utafiti wa kina na kuandaliwa si chini ya miezi sita kwa ufadhili wa Tanzania Media Fund, mfuko unaolenga kuboresha na kuinua kiwango cha kuandika habari za uchunguzi katika taifa letu la Tanzania.
 
Kwa kuzindua vipindi hivi Maa Media Centre walionyesha kipindi kimoja wapo cha ukatili majumbani kati ya vingi walivyoviandaa;  matukio ya ukatili yaliyotokea Zanzibar, Jijini Mwanza na Magu-Mwanza. Kule Zanzibar mama mmoja alipigwa na mme wake hadi akawa kipofu na kule Magu – Mwanza, mama mwingine mme wake walimkata pua na masikio na Jijini Mwanza, mama alipigwa na mme wake akiwa na mtoto mgongoni. Ni ukatili wa kutisha, hata hivyo ni ukweli ambao tunaishi nao katika nchi yetu ya Tanzania. Ukatili majumbani unasababisha vifo vya wanawake na watoto, kuvunjika kwa ndoa, ukosefu wa amani na utulivu katika familia, watoto wa mitaani na watoto wanaoishi kwenye mazingira hatarishi.
 
Kwenye hotuba yake ya uzinduzi Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Nchimbi, aliwapongeza Maa Media Centre kwa mafanikio yao ya kutengeneza vipindi vizuri vinavyoelimisha na kuwataadharisha wasiige mifano ya wale waliotengeneza utamaduni wa kuonyesha na kuandika juu ya mambo mabaya tu katika taifa letu. “ Kuna wale wanaotuonyesha wanafunzi wamekaa chini, hivi kweli hapa Tanzania hakuna wanafunzi wanaokalia madawati? Mbona hawaonyeshwi? Kwa nini itolewe mifano ya walimu wanaofundisha vibaya? Kwani hapa Tanzania hakuna walimu wanaofundisha vizuri? Kwa nini tunataka kujenga utamaduni wa kuonyesha mabaya tu katika Taifa letu?” Alihoji Mheshimiwa Nchimbi. Alisema kwamba kati ya vipindi ambavyo Maa Media Centre wameandaa kuna  kipindi kinachoelezea maisha ya Mwalimu mmoja aliyeanza kufundisha mwaka 1972 na kuendelea kuishi maisha duni hadi leo hii anamiliki kiti kimoja kwenye nyumba yake. “Msituletee mifano hii, mtu ambaye alianza kufundisha mwaka 1972, hadi sasa ameshindwa kuyaboresha maisha yake ni mlevi tu, hakuna maelezo mengine. Mimi, baba yangu alikuwa mwalimu, kama angekuwa aina ya huyo wa kiti kimoja basi na mimi nisingekuwa hapa leo hii….Tuonyesheni mifano ya walimu waliofanikiwa na wala si mifano ya wale walevi walioshindwa maisha….Tuonyesheni na mambo mazuri katika nchi yetu, msituonyeshe mabaya tu..” Alisisitiza Waziri Nchimbi.
 
Kwa Maoni ya Waziri Nchimbi, ni kwamba vitengenezwe vipindi vinavyoonyesha familia zinazoishi kwa amani. Waonyeshwe wanaume wanaopenda wake zao na kuishi bila kupigana ili watu wengine waige. Yeye anaamini kwamba familia hizo zipo. Vitengenezwe vipindi vinavyoonesha watoto wamekalia madawati na walimu wanafundisha vizuri. Anaamini Tanzania kuna mambo mazuri yanayotendwa na watu na serikali yao.
 
Maa Media Centre, waliijibu hotuba ya Waziri Nchimbi kwa unyenyekevu mkubwa. Walisema lengo lao si kuonyesha mabaya bali ni kuibua hali halisi; watu waone, wajadili na hatimaye kwa pamoja tutafute suluhu na kuyabadilisha maisha yetu: “ Ni vigumu kuwaridhisha watu. Tuliandaa kipindi cha Mwalimu Nyerere, kiliporushwa watu walilalamika kwamba  tulionyesha mazuri peke yake…sasa Mheshimiwa Waziri anatutaadharisha tusionyesha mabaya peke yake… tunajitahidi na kuamini kwamba kwenye mijadala uwiano utajitokeza. Tunaamini kwa kuonyesha hali halisi watu wanaweza kujifunza na kuyabadilisha maisha yao..” Alisema Furaha wa Maa Media Centre.
 
Vipindi vya Maa Media Centre, vitakuwa vinaonyesha ukiukwaji wa Haki za Binadamu. Inawezekana kabisa kuandaa vipindi vinavyoonyesha watu wanaozingatia haki za binadamu. Hapana shaka kwamba vipindi hivi vinaweza kusaidia kufundisha na kuyabadilisha maisha ya watu. Hili wala halina mjadala. Inawezekana kabisa kuandaa vipindi vinavyoonyesha kwamba Tanzania ni nchi ya neema, nchi yenye mafanikio, nchi yenye utulivu na amani; tunaweza kutengeneza vipindi kama vile vya Libya, vilivyoonyesha mazuri matupu kumbe chini ulifunikwa moto mkali ambao sasa umeripuka na kuleta maafa makubwa. Tunaweza kutengeneza vipindi vizuri vya kuelezea mafanikio yetu kama vile vya Idi Amin Dada wa Uganda hadi kufikia kutengeneza fedha nyingi zaidi kama shilingi yetu inashuka thamani; Iddi Amin, aliyafunika mabaya na kutangaza mazuri, wakati ulipowadia hakuweza kuyafunika tena! Hoja ya wanaharakati wa Haki za Binadamu ni kwamba kuna ukiukwaji mkubwa wa Haki za Binadamu hapa Tanzania. Mfano ukatili majumbani na udhalilishaji wa watoto wadogo ni mambo ambayo huwezi kupambana nayo bila kuyafichua na kuyaweka wazi. Ardhi inaporwa, mazingira yanaharibika, maisha ya watu yanaendelea kuwa magumu; ni mazuri yapi ya kutangaza? Kwamba shilingi yetu inaendelea kudidimia? Kwamba miaka hamsini baada ya uhuru hatuna hata kiwanda cha kutengeneza nyembe? Au kwamba  watawala wetu wanatembelea magari ya milioni mia mbili wakati wagonjwa wanabebwa kwenye machera kwenda hospitalini?
 
Baada ya onyesho la uzinduzi wa vipindi vya Nchi yetu kulikuwa na majadiliano. La kushangaza ni kwamba hoja ya Waziri Nchimbi ya kuonyesha mabaya tu haikuungwa mkono kwa maana kwamba hakuna mchangiaji yeyote aliyeirejea. Inawezekana Mheshimiwa Nchimbi, anaiona Tanzania kwa macho yake yaliyofunikwa na miwani yenye giza nene? Wakati anamshangaa mwalimu kufundisha miaka yote hiyo na kushindwa kuyaboresha maisha yake, walimu wanatishia kufanya migomo kudai malipo yao? Walimu hawana nyumba, walimu hawana usafiri, walimu wanafundisha kwenye mazingira magumu kiasi kwamba mshahara wao ni mdogo kuweza  kuyakabili maisha yao magumu? Mwalimu anayetegemea mshahara wake kuwasomesha watoto wake, kununua chakula, kulipia matibabu na matumizi mengine ya nyumbani atakuwa na fedha ya ziada? Walimu hawana posho, walimu hawana bahasha na walimu wenye maadili bora ya kazi yao hawapokei rushwa wala hongo. Au Mheshimiwa Nchimbi hajasikia ukweli kwamba mishahara ya Tanzania bila mtu kuwa na vyanzo vingine; miradi midogo, rushwa, ufisadi na fedha chafu haitoshi kiasi cha mtu kuweza kuyaboresha maisha yake? Umeme unapanda, mafuta yanapanda, karo inapanda na bidhaa nyingine zinapanda wakati mshahara unabaki pale pale au kupanda kwa nyongeza ya shilingi elfu mbili tu! Ni watanzania wangapi wenye mshahara wa kuweza kununua gari, kujenga nyumba na kuwasomesha watoto?
 
Miaka ya nyuma, mtafiti kutoka nchi ya Ujerumani, baada ya utafiti wake ndani ya Jiji la Mwanza, alibaini kwamba kulingana na gharama za maisha kuwa juu, watanzania wengi wenye kufanya kazi za kuajiriwa watakuwa ni wezi maana mishahara yao ilikuwa chini sana kulinganisha na matumizi yao ya mwezi. Hata leo hii ukilinganisha matumizi ya Mtanzania kwa mwezi na kipato chake, unashangaa fedha ya ziada inatoka wapi? Gharama za maisha ziko juu sana wakati kipato kiko chini. Hivyo haishangazi mtu kuwa mwalimu kwa miaka mingi akawa hana uwezo wa kujijengea nyumba. Hata waheshimiwa wabunge wetu tunaoamini wana mshahara mkubwa, bado tunasikia wanalalamika na kupiga kelele za kuongezewa mshahara wao na posho. Hizo  ni dalili kwamba mishahara ya watanzania bado iko chini. Kama wabunge wanalalamika, walimu je?
 
Badala ya kuunga mkono hoja ya Waziri Nchimbi, mjadala ulichukua mkondo mwingine; washiriki wengine walikubali kwamba “mabaya” yapo katika taifa letu. Mfano ukatili majumbani ni ukweli ambao hata mtu akijitahidi kuufunika utajitokeza tu. Hoja iliyojengwa na washiriki wengine ni ushauri kwa Maa Media Centre kuonyesha pande mbili za matukio wakati wa kuandaa vipindi vyao. “Tumeonyeshwa ukatili aliofanyiwa mama huyu wa Zanzibar, hatukuonyeshwa upande wa pili, kujua ni kwa nini mme wake alifikia hatua hiyo. Lazima kuna chanzo. Maa Media Centre, wangefanya jitihada kumtafuta mme wa mama huyu na kumhoji”. Alidokeza mshiriki. Na mshiriki mwingine alichangia hoja hiyo hiyo kwa upande wa ukatili aliofanyiwa mama wa Magu: “Ingekuwa vizuri kama mme wa huyu mama angepatikana na kuhojiwa. Kitendo alichokifanya ni kibaya, lakini tungependa kujua ni kwa nini alifikia hatua hiyo?”
 
Maa Media Centre, walipokea ushauri na kuahidi kuendelea kuviboresha vipindi vyao. Kwa wakati huo walichokuwa wamekiandaa ndicho hicho tulichokiona na ambacho watanzania wengine watakiona siku za hivi karibuni. Kwa mtu yeyote aliyeshiriki uandaaji wa vipindi hivi, atakubaliana na mimi kwamba Maa media Centre wamejitahidi sana ukilinganisha na changamoto nyingi walizokumbana nazo; kutokuwa na umeme wa uhakika, kutokuwa na wataalamu waliobobea wa kuchukua picha na uchanga wa kuandaa vipindi kama hivi; hata hivyo pole pole ndio mwendo kama wanavyoamini wao. Kazi yao ni nzuri na ya kupongezwa. Ubunifu wao ni wa kuigwa na vijana wengine wa nchi yetu ya Tanzania.
Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment