SHEREHE ZA MIAKA 50 YA UHURU WETU
 
Wakati tunajiandaa kusherehekea miaka 50 ya uhuru wa taifa letu, nimekuwa nikitafakari tangazo la Haki Elimu,  lililokuwa likirushwa kwenye luninga na kwenye redio. Tangazo hili ambalo  lilikuwa na  maneno tulia, tafakari na chukua hatua, lilisumbua sana akili yangu. Inawezekana tangazo hili lilisumbua pia akili ya watanzania wengine. Tangazo hili lilionyesha au lilieleza kwamba kufuatana na takwimu za kitaalam na kiuchumi, uchumi wetu unaendelea, na Tanzania imepiga hatua kubwa ya maendeleo, lakini hali hali halisi inaonyesha maisha duni ya wananchi. Kwenye luninga zilionyeshwa picha za nyumba mbovu, watu wenye afya na lishe mbaya, wamevaa nguo zilizochanika, wamekata tamaa na kuduwaa kwa kusikia habari za maendeleo ya taifa lao. Mzee Small, mwigizaji wa siku nyingi, alionekana akishangaa kwa kulinganisha yale yanayotangazwa na redio kwamba uchumi unaendelea na hali halisi. Tangazo hili ni muhimu sana wakati huu tunapoandaa sherehe za miaka 50 ya uhuru wetu. Ni vigumu kukataa ukweli kwamba baada ya miaka 50 ya uhuru watanzania wengi bado wanaishi maisha duni.
 
Mwaka huu mzima utakuwa ni mwaka wa kusherehekea. Na kusema kweli sherehe  zimeanza na shughuli nyingine nyingi zimeandaliwa ili kuanza mapema kuonyesha yale tuliyoyafanikisha ndani ya kipindi hiki kirefu cha miaka 50. Taasisi mbali mbali zimeanza kuonyesha mafanikio ya miaka hamsini.
 
Ukweli kwamba watanzania wengi wanaishi maisha duni, si kulenga kusema kwamba hakuna kilichofanyika baada ya uhuru. Wenye mawazo finyu wanafikiri kwamba kuonyesha dosari za serikali yetu ni upinzani na kwamba tunalenga kupotosha umma wa watanzania kwamba hakuna kilichofanyika miaka hamsini iliyopita.  Yamefanyika mengi na bado mengine yanafanyika. Hoja inayojengwa hapa ni kwamba ukilinganisha miaka hamsini na yale yaliyofanyika hadi leo, na hasa kwa kuangalia maendeleo ya mtu mmoja mmoja, ni sawa na hakuna! Lakini hata ukiangalia maendeleo ya taifa kwa ujumla,  bado kuna matatizo makubwa. Hatujafanikiwa kujijenga na kusimama imara kwa kiburi kama taifa lililo huru na lenye rasilimali nyingi. Bado tunaomba omba na kuamini kwamba kuna watu sehemu Fulani ya dunia hii watakuja na kutuleta maendeleo. Tunasahau kwamba ili tuendelee ni lazima sisi wenyewe tufanye kazi kwa bidii.
 
 Sote tunaisubiri siku hiyo  kwa hamu, siku ambayo taifa letu lilipata  uhuru miaka hamsini iliyopita. Wengi wa walioshuhudia tukio hili miaka hamsini iliyopita ni marehemu. Wazee wa leo ndo walikuwa vijana wakati tunapata uhuru. Tunasubiri kucheza, kuimba, kunywa na kula wakati wa kusherehekea miaka hamsini ya uhuru wetu.  Lakini, je ni kweli kwamba  uhuru wetu umekuwa uhuru wa kweli, uhuru wa neema kwa kila Mtanzania, uhuru wa kuleta maisha bora na ukombozi wa kila Mtanzania? Uhuru wa kujiamria mambo yetu sisi wenyewe? Je, si kweli kama tangazo la Haki Elimu, linavyoonyesha kwamba kwa nje yanaonekana maendeleo, lakini kwa ndani watu wanaishi maisha duni?
 
Kuna mafanikio makubwa yaliyopatikana baada ya  uhuru. Hata na kule kuwa huru ni mafanikio tosha. Lakini mafanikio ya kutuwezesha kufanya sherehe kubwa ya kula, kunywa na kucheza, yanatiliwa mashaka. Taifa letu limeweza kudumisha utulivu na amani, tumejenga mshikamano na aina Fulani ya uzalendo. Taifa letu limekuwa mstari wa mbele kuhakikisha na nchi nyingine za Afrika zinapata uhuru wake, haya ni mafanikio makubwa sana .Mashule yamejengwa, mahospitali na huduma nyingi za kijamii. Pamoja na mafanikio hayo yote, bado kuna ukweli unaosumbua, kwamba baadhi ya watanzania bado wanaishi maisha duni. Na namba ya wale wanaoishi maisha duni ni kubwa kuliko ile ya wenye neema!
 
Kwanini takwimu zinaonyesha uchumi kupiga hatua wakati hali halisi inaonyesha kinyume? Kwa nini  watanzania wanaishi maisha duni, wakati nchi yetu ina utajiri mkubwa? Tatizo ni nini? Je ni kweli tusherehekee sikukuu hii ya uhuru wetu, au tutulie, tutafakari na kuchukua hatua? Hatua gani? Elimu? Ukombozi wa fikira? Siasa safi na uongozi bora? Ni lazima kuna tatizo mahali Fulani, na tatizo hili haliwezi kutanzuliwa kwa kula kunywa na kucheza ngoma!
 
Baada ya miaka 50 ya uhuru wetu, huduma ya maji bado si nzuri. Watanzania wengi hawajui kwamba dunia ya leo maji yanamfuata mtu, na si mtu kuyafuata maji. Watu bado wanatembea kilomita zaidi ya kumi kuyafuata maji. Watu hawa hawajui maji ya bomba, hawajui maji ya ndani ya nyumba. Lakini mbaya zaidi hata na wale walio na maji ya bomba, bomba hizo hazileti maji! Tunajionea kila siku kwenye vyombo vya habari uhaba wa maji katika Jiji la Dar-es-Salaam na majiji mengine kama Mwanza, ambalo siku za hivi karibuni limekumbana na mgawo wa maji.
 
Miaka 50 ya uhuru imepita na bado kuna watanzania hawana mwanga nyakati za usiku. Hata bila kuongelea umeme, wako watu hawana uwezo wa kununua mafuta ya taa! Leo hii wakati bei ya mafuta inapanda kwa kisingizio cha thamani ya dola kushuka, serikali haina mpango wa kuwasaidia wananchi kupata huduma ya mafuta ya taa. Wananchi hawa wanatumia mwanga wa jua, hivyo inawalazimu kupata chakula cha usiku kabla ya jua kuzama, ili waweze kutumia mwanga wa jua!
 
Miaka 50 ya uhuru imepita na bado hakuna kitu hata kimoja ambacho tunakishughulikia vizuri na kwa kujitosheleza. Hatujaweza kushughulikia kilimo chetu na kujitosheleza kwa chakula. Tunaimba Kilimo kwanza wakati hakuna mpango wa wazi kueneleza kilimo cha umwagiliaji. Hatuwezi kuendesha kilimo kwanza kwa kutegemea mvua; tabia nchi inabadilika na ukame unaishambulia Tanzania. Ili kilimo chetu kifanikiwe ni lazima kuwa na mfumo wa umwagiliaji unaoaminika. Hatujaweza kuishughulikia elimu yetu na kuiendesha bila kutegemea misaada kutoka nje ya nchi. Hatujaweza kuendesha viwanda vyetu na kufanya uvumbuzi mbali mbali. Hatujaweza kuendesha hospitali zetu bila misaada kutoka nchi za nje. Hatujaweza hata kuendesha serikali yetu bila kutegemea misaada na ruzuku kutoka nchi za nje. Labda mimi ni kipofu, lakini ninatafuta ni kitu gani, hata kama ni kile ambacho hakina kisingizio cha pesa za kigeni, ambacho tunakishughulikia kikamilifu kwa kujitegemea, ni kipi? Kama hakipo, ni kwa nini tunataka kusherehekea? Kwanini tunataka kutumia pesa nyingi kula na kunywa, eti tunasherehekea sikukuu ya uhuru wetu?
 
Kuna haja ya kutulia, kutafakari na kuchukua hatua kama tunavyoelezwa na tangazo la Haki Elimu. Kuna mambo mengi ya kujiuliza juu ya uhuru wetu. Inatosha tu kuwa na uhuru wa bendera na kuendelea  na ukoloni mambo leo? Inatosha tu kuwa huru na watu kuendelea kuishi maisha duni? Inatosha tu kuwa huru na kuendeleza mifumo ya kikoloni? Inatosha kuwa huru na kuendelea kupokea misaada kutoka nchi za nje? Tunaimba utandawazi kwamba dunia imekuwa kijiji; wenzetu kutoka nchi za magharibi na Amerika wanaingia kwenye kijiji hiki kwa uhuru  bila ya kusumbuliwa, lakini sisi tukitaka kuingia kwenye kijiji hiki ni lazima kupitia kwenye mchujo wa hali ya juu. Wakati Afrika inaelekezwa kufungua milango yake yote kwa kisingizio cha utandawazi; wao wanaifunga milango yao yote kwa kuogopa kwamba sisi tukiruhusiwa kuogelea kwenye kijiji hiki cha utandawazi tutasambaza ugaidi.
 
Mwalimu Nyerere, alijitahidi sana wakati wa huru kubadilisha mifumo. Alileta falsafa ya Ujamaa na Kujitegemea na wakati anakaribia kutoka madarakani, alisukuma kwa nguvu zote demokrasia ya vyama vingi. Wakati Mwalimu, anakazana kuleta falsafa mpya, bado mifumo mingine ilibaki ni ya kikoloni. Katiba yetu ilifanyiwa marekebisho kutoka ile ya mkoloni. Bunge letu liliendeshwa na bado linaendeshwa kwa mifumo ya kikoloni. Rais wa nchi alipewa madaraka makubwa na jambo hili bado linaendelea. Mfano hadi leo hii Rais, ndiye anayemteua Jaji Mkuu, Rais ndiye anayeteua  Tume ya uchaguzi nk. Mfumo wa serikali ya kikoloni, ulikuwa umesukwa, kwa namna ya wakoloni kujilinda na changamoto ya wananchi, ulikuwa ni mfumo wa kuwasaidia kutawala kikoloni, kutawala bila demokrasia. Baada ya  uhuru, baada ya kumfukuza mkoloni, tulichukua mfumo ule ule wa kujihami, mfumo ule ule wa kuwaogopa wananchi, mfumo wa kuogopa changamoto za wananchi.
 
Wakati wa mkoloni, kufikiri kinyume na serikali ulikuwa ni usaliti. Wale wote waliofikiri kinyume na serikali ya mkoloni, walionekana kuwa magaidi. Leo hii tuko huru. Hakuna mkoloni, lakini kuna dalili zote za kutaka watu wote wawe na mawazo yale  yale, watu wote wawe wa chama kilele kile, kinyume na hapo ni usaliti. Tunawezaje kusherehekea kwa pamoja wakati uhuru wa baadhi ya watanzania unanyimwa pumzi?
 
Ni kweli tuko huru. Kwa maana ya kumfukuza mkoloni na kuendesha mambo yetu wenyewe. Lakini kwa maana yenyewe ya neno Uhuru, bado tuko chini ya mkoloni maana hata mbali na kuishi maisha duni fikira zetu bado zinatawaliwa. Hili linajionyesha kwenye mijadala inayoendelea kama ule wa kutumia lugha ya kingeni kufundishia. Watu walio huru hawawezi  kujadili kutumia lugha yao au kutoitumia! Ukikuta mtu ameweka mjadala wa kuitumia lugha yake au kutoitumia, utambue kwamba mtu huyo au watu hao wana matatizo mengi kichwani. Mtu huru hawezi kujivuna kuongea lugha ya kigeni; atajivuna kuongea lugha yake au hata kuongea lugha za kigeni.
 
Mbali na baadhi ya watanzania wanaoishi maisha duni, kuna kundi jingine la watanzania wasioipenda nchi yao. Watu hawa wanapora mali ya nchi na kuiwekeza nchi za nje, au wanajilimbikizia wao na familia zao hawa si sehemu ya mafanikio, bali ni sehemu ya ukoloni mambo leo. Ni dhambi kubwa watu hawa, waporaji wa mali za taifa kusherehekea pamoja na watanzania wanaoishi maisha duni. Uhuru wa waporaji ni tofauti na uhuru wa wazalendo walalahoi.
 
Hili tangazo la Haki Elimu, litusaidie kuona kwamba, pamoja na uhuru wetu, pamoja na mafanikio yetu, bado kuna mambo mengi ya msingi ambayo ni lazima kuyashughulikia kama taifa. Yapo mambo mengi ya kushughulikia ili kuleta uhuru kamili wa taifa letu. Tunahitaji kutulia, kutafakari na kuchukua hatua
 
 Badala ya kufanya sherehe kubwa na kutumia pesa nyingi kwa kula na kunywa, ni vyema  watu wakafanya mikutano ya majadiliano. Taifa liingie kwenye majadiliano. Ni lazima tuangalie sababu inayopelekea watu wengi kuendelea kuishi maisha duni. Ni wakati mzuri wa kuanza kufikiria kutengeneza katiba mpya na mifumo mipya inayoendana na Uhuru wetu. Tusherehekee kwa kuzama katika fikara!
 
Na,
Padri Privatus Karugendo.
 
 

0 comments:

Post a Comment