UHAKIKI WA KITABU: WANAWAKE WA TANU, Jinsia na Utamaduni katika Kujenga Uzalendo Tanganyika: 1955-1965.1. REKODI ZA KIBIBLIOGRAFIA

Jina la Kitabu kinachohakikiwa hapa ni Wanawake wa TANU, Jinsia na Utamaduni katika kujenga Uzalendo Tanganyika: 1955-1965 na kimetafsiriwa na Kurahisishwa na Elieshi Lema.Mchapishaji wa kitabu hiki ni E&D kwa niaba ya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP). Kitabu hiki kimepatiwa namba ifuatayo katika sekwenzia ya vitabu duniani (ISBN): 9987 – 600 –11- 5. Kimechapishwa mwaka 2005 kikiwa na kurasa 116. Na anayekihakiki sasa hivi katika safu hii  ni mimi Padri Privatus Karugendo.

II. UTANGULIZI

Kitabu hiki ni tafsiri rahisi ya TANU WOMEN Gender and Culture in Making of Tanganyika Nationalism, 1955- 195, kilichoandikwa na Susan Geiger, na kuchapishwa na Heinemann, James Curry, E.A.E.P, Mkuki na Nyota, 1997.

Susan Geiger, alikiandika kitabu hiki katika lugha ya Kiingereza na katika mtindo wa kisomi ambao kwa kiwango fulani unawazuia watu wa kawaida wasiweze kupata maudhui yaliyomo. Mbali na ugumu wa lugha na mtindo wa kisomi wa kitabu hiki, ni kwamba hakipatikani na kujulikana kwa wengi hapa Tanzania. Hivyo tafsiri rahisi ya kitabu hiki inakifunua kwa watanzania wote. Jambo la kuomba kwa Mwenyezi Mungu, ni kuwajalia watanzania moyo wa kupenda kusoma vitabu.

“Historia ya maisha ya wanawake inachukua nafasi kubwa katika mpangilio wa kitabu. Tathmini ya mwandishi inakuwa kama uzi uliounganisha maudhui ndani ya kitabu, lakini chachu ya maelezo yaliyomo yanabaiki ni yale ya historia ya wanawake wanaharakaiti wenyewe” (Utangulizi wa kitabu, viii).

Kitabu hiki kimegawanywa kwenye sehemu tatu. Sehemu ya kwanza inayoongelea Kuvunja Ukimya, na ina sura tatu. Sura ya kwanza inachambua Wanawake na Siasa Wakati wa Ukoloni. Sura ya pili inaangalia Itikadi za Kikoloni na Uhalisi wa Maisha ya Mijini na Sura ya tatu inaongelea juu ya Wanawake Waafrika Walioishi Dar-es-salaam.

Sehemu ya pili ya kitabu hiki, inajikita juu ya Wanawake na Ujenzi wa Uzalendo. Sehemu ina sura tano. Kwa maana nyingine inabeba sura ya nne hadi ya nane ya kitabu hiki. Sura ya Nne inamjadili Bibi Titi Mohamed, na harakati zake za kisiasa ndani ya Dar-es-salaam. Sura ya tano inamwangalia Bibi Titi Mohamed, na harakati zake za kisiasa nje ya Dar-es-salaam. Sura ya sita inawaangalia wanawake wa TANU walivyoinuka kutoka Gizani, hawa ni wanawake walioshi Dar-es-salaam na walishirikiana na Bibi Titi Mohamed, katika harakati za kisiasa na ukombozi wa taifa letu. Sura ya Saba inaelezea juu ya wanaharakati wanawake wa TANU wa Kilimanjaro na Moshi Mjini na sura ya nane ni juu ya wanaharakati wanawake wa TANU kutoka Mwanza.

Sehemu ya tatu na ya mwisho ya kitabu hiki inajadili juu ya Uzalendo na Harakati za Wanawake Baada ya Uhuru.Hapa kuna sura tatu. Yaani sura ya tisa hadi ya kuminamoja za kitabu hiki. Sura ya tisa inayaangalia maisha ya Bibi Titi Mohamed, wakati wa Uhuru na Baada ya Uhuru.Sura ya kumi inaelezea jinsi kitengo cha Wanawake wa TANU, kilivyobadilishwa kuwa Umoja wa Wanawake na Sura ya mwisho, inaongelea juu ya Lucy Lameck.

Katika aya zifuatazo nitatoa muhtasari na tathmini ya kitabu hiki, lakini baada ya kudokeza mazingira yanayokizunguka kitabu chenyewe.

III. MAZINGIRA YANAYOKUZUNGUKA KITABU

Kuna ukweli usiopingika kwamba wanawake walishiriki kikamilifu katika harakati za ukombozi wa Taifa letu. Walipambana bega kwa bega na wanaume. Na katika mazingira mengine walikuwa mstari wa mbele kuliko wanaume:
 “ Nilipokuwa Mbunge, nilipigania haki sawa, nikijua kwamba wanawake walitoa mchango mkubwa kwa TANU.Kama haikuwa kwa juhudi za wanawake, uhuru ungekuwa mgumu kupatikana kwa sababu wanauwe walikuwa waoga” (Mahojiano ya Bibi Titi, Uk, 107).

Bibi Titi, anaelezea jinsi wanawake walivyokuwa mstari wa mbele kujiunga na TANU, ili kupigania UHURU wa taifa letu:
“ Tuliwapata wanawake 40 katika kilabu ya pombe, tukawachukua ofisi ya TANU, Wanaume walisikiliza hotuba za Nyerere lakini waliogopa, waliogopa kweli, lakini wanawake walijiunga. Waliunga mstari katika ofisi ya TANU
Wakinuua kadi. Wanaume walipeleka wake zao kuwanunulia kadi. Mimi nilificha kadi mia tatu na hamsini za watu walioogopa kuziweka ndani ya nyumba zao. Wanawake hawakuwa na woga hata kidogo….” (Mahojiano ya Bibi Titi Uk 37).

Baadhi ya wanawake hawa ndoa zao zilivunjika. Walichagua siasa, walichagua harakati za kulikomboa taifa lao, na kuzitelekeza familia zao. Walifanya biashara na kutumia pesa na mali zao katika harakati. Zaidi ya hapo, wanawake hawa wazalendo ndio waliojenga uelewa wa ni nini maana ya utaifa hapa Tanganyika, Utamaduni wa wanawake na hasa vikundi vya ngoma na matumizi ya lugha ya Kiswahili vilichochea moyo wa kizalendo na kuwaunganisha watu. Akina mama hawa hawakuwa wasomi, lakini walikuwa wapambanaji na wenye upeo mkubwa kuelekeka uhuru na kujitawala kwa nchi yetu. Mfano wa akina Mama hawa ni Bibi Titi Mohamed na akina mama wengine wa Moshi, Mwanza, Kagera na Dar-es-salaam.

Pia kuna ukweli usiopingika kwamba baada ya Uhuru, wanawake hawa, akiwemo na Bibi Titi Mohamed, waliwekwa pembeni. Kwa makusudi au kwa bahati mbaya walitupwa nje ya historia ya mapambano.

Ukweli mwingine usiopingika, ni kwamba nguvu za wanawake hawa zilitambuliwa na ziliogopwa. Tutaona jitihada zilizofanywa baada ya Uhuru, kuvunja nguvu za kitengo cha wanawake wa TANU, na kuunda Umoja wa Wanawake.Pia,kifo cha BAWATA, ni ushuhuda mwingine.

Pia kuna aina Fulani ya mgongano wa Wanawake wasomi na wale waliokuwa na elimu duni. Wasomi walikuwa wakristu, na kwa vyovyote walisimama upande wa wakoloni wakristu waliokuwa wakitawala. Inawezekana kwa kutotaka, lakini kwa woga wa kupoteza kazi zao.  Wanawake wa elimu duni walikuwa waislamu na hawa ndo walikuwa mstari wa mbele katika harakati. Baada ya uhuru, kisomo kilikuwa kigezo. Inawezekana wasomi walichukua nafasi na wale wa elimu duni wakatupwa nje, lakini hii si sababu tosha ya kufuta kabisa juhudi za akina mama hawa katika historia ya taifa letu.

Wanahistoria, wanasayansi wa siasa na wataalamu wengine wamepuuza kwa kiwango kikubwa mchango wa wanawake wanaharakati wa Tanganyika katika mapambano dhidi ya wakoloni. Hatuwasikii akina mama hawa. Baada ya Uhuru waliwekwa pembeni na kusahauliwa kabisa!

CCM, chama kilichotokana na TANU, hadi leo hii uongozi wake wa juu ni wa wanaume watupu! Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Katibu Mkuu. Kama sikosei na mtu anayeshikilia mfuko wa chama ni mwanaume! Marais wa awamu zote nne ambao wanatoka CCM ni wanaume. Hatujapata Waziri Mkuu Mwanamke! Watu wengi walitegemea kwamba Mwanamapinduzi kama Rais Jaka Kikwete, angeweza kumchagua Mwanamke kuwa Waziri mkuu, lakini na yeye ameendeleza mtindo ule ule wa kuwazika wanawake wa TANU!
Si kweli kwamba wanawake wa Tanzania, hawana uwezo wa kuongoza, na si kweli kwamba wanawake wa Tanzania, hawana kisomo. Profesa Anna Tibaijuka, anawika kwenye aga za kimataifa. Dr.Asha Rose Migiro, ameteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuwa Naibu wake. Wanawake wenye uwezo kama ule Bibi Titi Mohamed, na ambao wamesoma wapo na wamejaa tele! Tatizo ni nini? Wanawake wako wapi?

Inawezekana wanawake walizikwa kwa kauli ya Bwana Mgonja? :
 “ Akizungumza kwenye mkutano siku ya pili, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Bwana Mgonja, alizumgumza katika njia iliyofifisha ari ya siasa kwa wanawake na kuimarisha mamlaka ya serikali. Wakati Kitengo cha Wanawake kilikuwa kinahamasisha wanawake wajiunge katika harakati za kujenga taifa, Mgoja aliwaambia wanawake kwamba wakilea watoto watakuwa wamelea taifa zima. Aliwasifu wanawake Kwa juhudi zao katika kupigania uhuru, lakini Kwa sasa walichotakiwa kufanya ni kulima, kufuga kuku, kuchimba visima na kupanda miti pamoja na kushiriki katika kisomo cha watu wazima…” (Uk.110).

Je, kukivunja kitengo cha Wanawake wa TANU, na kuunda Umoja wa Wanawake, ndo chanzo cha kuwafunika wanaharakati hawa? ;  “Tarehe 2 Novemba, mwaka 1962, Mheshimiwa Nyerere  aliagiza kwamba vyama vyote vya wanwake Tanganyika vivunjwe; yaani YWCA, Baraza la Wanawake Tanganyika na UMCA, ili viungane kuunda Umoja wa Wanawake Tanganyika (UWT).Umoja wa Wanawake ulikuwa tofauti na Kitengo cha wanawake cha TANU….  Wakawakusanya wanawake pamoja na kuwafundisha usafi, upishi, malezi ya watoto… elimu yawatu wazima na ususi…Vitu vyote hivi havikuwepo katika Kitengo cha Wanawake cha TANU.Hatukuwa na muda wa kufanya vitu hivi…”(Mahojiano na Bibi Titi uk 106).

Inawezekana kwamba UWT, ndo kilikuwa kitanzi cha Wanawake wa TANU? Swali linabaki palepale!
Wako wapi Wanawake? Wako wapi wanawake wa TANU, waliopigana kuleta uhuru wa taifa letu. Utafiti wa Susan Geiger, ulilenga kulijibu swalihi hili. Mwana mama huyu ambaye ni marehemu alikuwa msomi mwanaharakati aliyefundisha masomo ya Kiafrika na yale ya Jinsia katika Chuo Kikuu cha Minnesota/Twin Cities, huko Marekani kwa muda wa miaka mingi. Alikuja Tanzania kwa mara ya kwanza akiwa mwalimu wa kujitolea katika miaka ya 1960. Baadaye aliendelea kurudi Tanzania, katika nyakati tofauti katika kipindi chote cha maisha yake.  Susan alifariki mwaka 2001.

Kazi yake kubwa ya utafiti ilikuwa juu ya historia ya uchifu wa Wachagga. Utafiti huo ndio uliokuwa chimbuko la kujipatia Shahada ya Udaktari wa Falsafa. Baadaye alianza utafiti wa wanawake wanaharakati wa Tanganyika.  Wanaharakati hawa walijulikana kama Wanawake wa TANU. Susan alikuwa mwanaharakati; Akiwa kiongozi wa wanaharakai wa jinsia, Susan alipigania suala la nafasi ya mafunzo ya jinsi ili mafunzo hayo yatolewe katika ngazi zote za jamii. Alishiriki kikamilifu katika harakati za mapambano hata nje ya vyuo vya masomo.Susan alikuwa chachu ya vikundi vya mshikamano ambavyo viliunga mkono harakati za ukombozi katika Bara la Afrika huko Marekani.

Baada ya maelezo haya sasa tuone kitabu chenyewe kwa muhtasari.

IV. MUHTASARI WA KITABU


Kitabu hiki ni ushuhuda wa kitaalamu (Utafiti) kwamba Wananchi wa Tanganyika walijipatia uhuru wao kutoka kwa Waingereza mwaka 1961 kupitia mapambano yaliyoongozwa na jumuiya yenye nguvu chini ya uratibu wa chama cha TANU.Na kwamba Wanawake wazalendo walikuwa ni viongozi mashuhuri katika medani zote kwenye ngazi mbalimbali.

Kitabu hiki kinauliza maswali kadhaa:

-         Ni kwa nini utaifa wa Mtanzania ulichukua sura mpya baada ya uhuru kuliko ilivyokuwa katika nchi nyingime?
-         Je, tunauelezeaje ukweli kwamba, licha ya tabia, utaifa wa Tanganyika umebaki kuwa alama tu ya utambulisho kwa wanawake?
-         Je, ukiangalia ukweli kuwa utaifa na utamaduni katika Tanganyika vilikuwa kazi zilizoendeshwa na wanawake wa TANU, matokeo ya kazi yao ni yapi?
-         Je, tuaneulezeaje ukweli kuwa utaifa hapa Tanzania haukujengwa na kikundi cha wanamapinduzi au haukuwa ni matokeo ya  kuibuka kwa matabaka kutaka kudhibiti dola?

Hata hivyo swali la msingi ni: Wako wapi wanawake? Hili ni swali muhimu kwa kila mtanzania. Susan Geiger, kwa utafiti wake anachangia jibu la swali hili katika kitabu chake.

Sehemu ya kwanza (uk.1-23), yenye sura ya kwanza hadi ya tatu ina ujumbe muhimu wa Kuvunja Ukimya. Sehemu hii ya kwanza inalenga kujibu maswali yafuatayo:
-         Kwanini wanawake waliitikia wito wa TANU kwa hamasa kiasi hicho? Walijipanga vipi?
-         Wanawake wapi walihamasika zaidi kisiasa? Shauku hiyo inaweza kuelezwa vipi?
-         Tukizingatia vipingamizi vya kijamii na kiutamadanuni ambavyo vilizuia wanawake kushiriki katika shughuli za umma, ni changamto zipi ziliandamana na kuibuka kwa uelewa wa kisiasa miongoni mwa vikundi fulani fulani vya wanawake wa Tanzania?

Maswali yote haya yanajibiwa kwa ufasaha katika sura hizi tatu. Historia ya Bibi Titi Mohamed, inaongoza majibu ya maswali haya.

Sura ya pili inachambua itikadi ya Kikoloni na Uhalisi wa maisha ya Mijini. Inaangalia jinsi wakoloni walivyowaelewa na kuelekeza maisha ya wanaume na wanawake Waafrika.Ni kwamba watawala wakoloni hawakuwaona wanawake Waafrika, isipokua tu pale matukio au hali Fulani ilipolazimisha waonekane. Wakoloni waliwachukulia wanume kama wazalishaji na wanawake kama tegemezi. Nyaraka za kikoloni zimejaa maelezo yamawasiliano kuhusu matatizo na masuala ya haki za wanaume kudhibiti au kupata huduma za ngono. Masuala haya yalijumuisha uzinifu- kwa kiasi gani wanawake wazinifu waadhibiwe au kufungwa; kiasi gani cha pesa au mali kitolewe kama mahari; faini gani itolewe kama adhabu ya kuwapa wasichana mimba. Masuala yaliyohusu wanawake kama kulipa kodi, kupangiwa sehemu za kazi na mishahara kwa walimu wanawake waafrika yalitazamwa kama vile yamo ndani ya mahitaji, haki na wajibu wa wanaume na wale waliowategemea…uk 17.

Sura ya tatu, inachambua wanawake waafrika walioishi Dar-es-salaam. Mwaka wa 1950, asilimia 90 ya wanawake walioishi Dar-es-salaam, walikuwa Waisilamu na wasiojua kusoma walikuwa wanafikia asilimia 88. Wanawake wachache sana walikuwa wasomi, ambao wengi wao walikuwa Wakristo. Kufikia miaka ya katia ya 1950, hili kundi la wanawake wachache wasomi, lilijumuisha wale wenye elimu ya kutosha kuajiriwa kama walimu, watoa huduma hospitalini na mjini.

Wanawake ambao hawakujua kusoma, walijipatia kipato kwa ukahaba, kupika pombe na kuuza samaki. Shughuli nyingine za kujipatia fedha zilikuwa ni pamoja na kupasua na kuuza kuni, kutengeneza na kuuza keki, kalimati, maharage, na nazi.

Makahaba walihitajika, kwani asilimia 39 ya idadi ya wanaume Dar-es-salaam hawakuwa na wake. Wanaume waliwaacha wake zao nyumbani ili waendelee kutunza mashamba na ardhi. Hivyo wanawake waliofanya ukahaba, walifanya hivyo kwa uamuzi wa kiuchumi na wengi wao walitumia pesa hizo kutunza familia. Mwaka 1956, asilimia 11.2 ya kaya zote Dar-es-salaam ziliongozwa na wanawake.

Kwa sababu kadhaa zilizoingiliana, ni wawawake wa Kiislamu wa Dar-es-salaam wenye umri wa makamu, na ambao hawakusoma, ndio waliokuwa wanaharakati. Harakati zao ndizo zilizoanzisha na kujaza ujasiri katika uzalendo nchini Tanganyika.

Sehemu ya pili ya kitabu hiki (Uk31-82) yenye ujumbe: Wanawake na Ujenzi wa Uzalendo, ina sura ya nne hadi ya nane na inalenga kujibu maswali yafuatayo:
-         Kwa nini wanawake hawa walipenda siasa za kizalendo?
-         Walitarajia kupata au kufanikisha nini?
-          Mchango wao kwa Utaifa, kukua na kuendelea kwa TANU ulikuwa nini?

Maswali yote haya yanajibiwa kwa ufasaha katika sura hizi tano. Katika sura hizi tunaelezewa juu ya harakati za Bibi Titi Mohamed, Dar-es-salaam na nje ya Dar-es-salaam, juu ya wanawake kuinuka kutoka gizani, juu ya wanawake wanaharakati wa Kilimanjaro na Moshi mjini na wanaharakati kutoka Mwanza.

“Kambona aliporudi nilianza kuwapanga wanawake katika idara. Tulianza kukutana katika ua wa ofisi ya TANU lakini haukutosha, kwa hiyo tukawa tunakutana Anartoughlo.Tukachagua viongozi wetu… Bi Kaundime kutoka Temeke, Asha binti Waziri, Temeke na Binti Kaundime, mwingine Saada binti Kipara.Hawa ndio wanawake waliokuwepo. Kulikuwa na wengine Kinondoni, Magomeni, Buguruni na Kigamboni… Tulitembea nyumba hadi nyumba, usiku  na mchana, tukingoja mlangoni na kuwasihi  wafike kwenye mkutano kesho yake.Tulitembea kila mahali…” (Mahojiano ya Bibi Titi, uk.37).

Na Bibi Titi, nje ya Dar-es-salaam tunasikia yafuatayo:
“ Safari yetu ya kwanza tulikwenda Tanga, Januari 1,1956. Tuiokwenda ni Bwana Mkubwa, mimi na Rajabu Diwani… Tulikwenda Tanga na Korogwe, tukazunguka mkoa mzima kwa muda wa siku  ishirini na moja, kisha tukarudi Dar-es-salaam.Kamati Kuu ilipokaa iliamua kwamba ninao uwezo wa kusafiri peke yangu… unajua, nchi hii ni kubwa, tusingeweza kusafiri pamoja kila wakati. Kwa hiyo, mimi nilikwenda upande wangu na Bwana Mkubwa wake. Siku hizo ilikukwa ni mimi na yeye tu tuliweza kufanya hivyo… Nilisafiri sana, na sio kwa niaba ya wanawake tu, hotuba zangu zote ziligusa wanawake na wanaume na nilifuatana na wanaume katika safari hizi. Niliweza kusafiri kwa miezi mitatu mfululizo. Ningeweza kuwa Mwanza, halafu nikaenda Musoma ambapo ningepata telegramu iliyonitaka niende Dodoma.Nikiwa Dodoma napata telegramu nyingine kwenda Mbeya…” (Mahojiano na Bibi Titi. Uk 39-41).

Sura ya sita inatufunulia wanawake mashujaa walioshirikiana na Bibi Titi Mohamed kwa upande wa Dar-es-salaam.Hawa ni akina: Tatu Mzee, Halima Hamisi, Salima Ferouz, Mashavu binti Kabonge, Binti Kipara, Mwasaburi Ali na Fatuma Abdallah.Wako na wengine wengi, lakini hawa ndo waliweza kufanya mahojiano na Susan Geiger.Mahojiano yao yanatoa mwanga wa kile kilichotendeka. Kwa vile waliongea wao na kuna ushuhuda wa kihistoria kubainisha ukweli wao, hakuna sababu yoyote kutilia mashaka maelezo yao. Wanawake wote hawa walijitoa muhanga, walitumia mali zao hadi wengine ndoa zao zikavunjika. Salima Ferouz, alieleza kwenye mahojiano yake na Susan Gieger:
“Niliuza vitumbua kupata fedha ya kununua kadi. Nilijiunga kwasababbu nilitaka uhuru na kuondokana na utumwa…. Ukoloni ulikuwa mgumu. Tuliwekwa ndani, au tuseme tuliolewa. Unakaa ndani na kuletewa kila kitu… kinachoendelea nje hukijui, hujui kinachoendelea duniani. Kwa hiyo tulifikiria, kama tusipopata uhuru sisi, watoto wetu wataupata, lakini tufanye kazi tuondokane na utumwa… Sisi wanawake tulikuwa na nguvu…. Tuliongoza njia kwa sababau ya uonevu wa watoto wetu na jinsi tulivyowekwa ndani…” (Uk. 55).
Wakati anahojiwa Bi Salima Ferous, alikuwa mwanamke mzee mwenye majonzi, ambaye afya yake ilikuwa dhaifu, na ni wazi alikuwa hakumbukwi tena na chama alichokitumikia kwa uaminifu kuleta Uhuru wa taifa letu. Wengi wa wanawake hawa hawakumbukwi wala kutajwa popote pale!

Sura ya Saba, inawaelezea wanaharakati wa Kilimanjaro na Moshi Mjini.Hawa walikuwa tofauti na wale wa Dar-es-salaam.Hawa walikuwa wasomi na wengi wao walikuwa wakristu. Wanawake hawa ni Halima Selengia Kinabo, Mwamvita Salim, Zainabu Hatibu, Morio Kibabo, Violet Njiro, Elizabeth Gupta, Kanasia Tade Mtenga, Natujwa Daniel Mashamba, na Lucy Lameck. Maelezo ya Elizabeth Gupta, yanaonyesha jinsi wanawake walivyokuwa mstari wa mbele katika harakati:

“ Kazi yetu ilikuwa kuimba. Tuliposhinda uchaguzi, nikaingia idara ya usalama na ulinzi. Ilikuwa kazi ngumu. Tulikuwa tunalinda nyumba moja huku Nyerere, amelala nyumba nyingine. Wakoloni walipotuona tunalinda nyumba, wao walijua kwamba Nyerere yuko ndani. Tulikuwa tukijificha kwenye magunia, askari wa kikoloni wakipita wanafikiri ni magunia ya mkaa…Nilisaidia kujenga ofisi ya chama ya Mabogini, ilikuwa nyumba ya Abdi Nuru aliyoitoa kwa chama. Nyumba yingine likuwa ya Bi Muhogo, alitoa chumba kimoja ambacho nilikikarabati mwenyewe… nilitoa mali na rasilimali zangu kwa TANU…” (UK,73).

Sura ya nane, inawaelezea wanaharakati wanawake wa TANU kutoka Mwanza. Hawa ni akina Agnes Sahani, Aziza Lucas, Tunu Nyembo, Halima Ntungi, Mwajuma Msafiri, Pili Juma, Mwamvua Kibonge, Zuhura Mussa na Chausiku Mzee. Mahojiano yanaonyesha jinsi wote hawa walivyoshiriki kikamilifu katika mapambano ya kuleta uhuru wa taifa letu. Bi Chausiku Mzee, anakumbuka maandamano ya Geita na Mwanza:

“…Tulipigwa mabomu ya machozi na wote tulifungwa. Baada ya hapo, tuliweza kufungua tawi la TANU Geita, halafu tukaenda Maswa, Ngudu, Shinyanga, Tabora mpaka Bukoba. DC alikuwa akituvuruga, mwishowe tukafanyia mikutano mbugani, akapeleka polisi kutufuata…”(Uk 93).

Sehemu ya tatu ya kitabu hiki (Uk 95- 113) inayoelezea juu ya Uzalendo na Harakati za Wanawake Baada ya huru inazo sura tatu, sura ya tisa hadi ya kumi na moja na zinalenga kujibu maswali yafuatayo:
-         Kwa nini Bibi Titi alisukumwa nje ya nuru ya harakati za kisiasa baadaya uhuru? Ukimya uliofuata unatoa changamoto gani kwa wanaharakati?
-          Ajenda ya waanawake wa TANU ya kuendeleza harakati za kisiasa baaada ya uhuru ilibadilishwa na kufanywa ya ustawi wa jamii. Ni kwa nini?
-         Wanaharakati wa jinsia katika Tanzania ya leo wanajifunza nini kutokana na harakati za kisiasa za wanawake wa TANU?

Maswali haya yanajibiwa vizuri. Katika sura hizi tunaelezwa maisha ya Bibi Titi Mohamed, wakati wa Uhuru na Baada ya uhuru, jinsi kitengo cha wanawake wa TANU, kilivyobadilishwa kuwa Umoja wa Wanawake na mwisho tunapata historia fupi ya Lucy Lameck, mwanamke aliyefanikiwa kuwa Mbunge na naibu waziri.

Wakati wa Uhuru Bibi Titi Mohamed, alikuwa upande wa kulia wa Mwalimu Nyerere. Kufuatana na wachambuzi wa mambo wakati wa Uhuru, Nyerere Na Bibi Titi Mohamed, ndio waliojulikana sana nchi nzima. Ingawa Bi Titi hakuwa msomi, alichaguliwa kuwa mbunge na kupata nyazifa serikalini. Baadaye alipoteza kiti chake cha Ubunge.Alifanya kosa la kudai ushikishwaji na kuhoji baadhi ya vipengele vya Azimio la Arusha.Alihoji wazi bila kificho. Matata yalianza. Alijitoa kwenye uongozi wa chama baadaye aliusishwa na mapinduzi. Aliwekwa kizuizini miaka michache na baadaye alisamehewa na Mwalimu Nyerere.Nyota yake ilizimika! Lakini hii haina maana ya kufuta kumbukumbu zote alizozifanya.

Mbali na pigo hili la Bibi Titi Mohamed, wanawake wa TANU, walipata pigo jingine la Kitengo chao ndani ya chama kugeuzwa kuwa Umoja wa wanawake.Kitabu kinaelezea vizuri pigo hili na kwamba malengo ya Umoja wa wanawake yalikuwa tofauti kabisa na kitengo cha wanawake wanaharakati.

Wanaume waliogopa nguvu za wanawake. Hawakutaka wanawake waendelee kujiingiza kwenye siasa. Na hadi leo hii, serikali inakuwa makini kwa vikundi vya wanawake. Ilipoanzishwa BAWATA ya Profesa Anna Tibaijuka, serikali iliifutilia mbali kwa kisingizio kwamba umoja huo ulikuwa unaelekea kujiiingiza katika siasa.

V. TATHMINI YA KITABU.

Baada ya kuona muhtasari huu sasa tufanye tathmini ya kazi hii aliyoifanya Susan Geiger.

Mwanzoni nilidokezea kwamba hii ni tafsiri iliyorahisishwa, lakini kwa kiasi kikubwa ujumbe na ukweli unaobebwa na kazi hii ya Susan Geiger, unabaki palepale. Elieshi Lema, aliyefanya tafsiri, hakuongeza wala kupunguza ukweli wa utafiti. Njia alizotumia Susan Geiger za kukusanya habari au takwimu za kitabu hiki ni za kipekee. Chanzo chake kikubwa cha kupata habari na tathmini kilikuwa wanawake wanaharakati wenyewe. Kwa kupitia utafiti uliofanyika, walipewa nafasi ya kuelezea maisha yao wenyewe kama walivyoishi ndani ya jamii. Hizi ni simulizi zao pamoja mkusanyiko wa matukio mengine ya historia. Wanawake wanaharakati walijieleza, jinsi walivyoshiriki mapambano.

Sambamba na hili la kuwahoji wanaharakati, inaonyesha Susan Geiger, alifanya utafiti wa kina kwenye nyumba za makumbusho ya mambo ya kale hapa Tanzania na huko Uingereza.Nyaraka muhimu za Serikali ya kikoloni hapa Tanganyika zilipatikana huko na katika vyanzo vingine vya habari. Alisoma na kazi yingine zilizoandikwa kuhusu harakati za ukombozi katika taifa letu. Kwa kuunganisha yote hayo aliweza kutoa kitu chenye uhakika, kinachoonyesha ushiriki wa wanawake katika mapambano ya uhuru wa taifa letu.

Hivyo nianze tathmini hii kwa kumpongeza Susan Geiger, kwa kazi yake nzuri ya kutufumbua macho na kutukumbusha historia yetu. Kitabu hiki ni muhimu sana. Pia pongezi ziwaendee Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kufikiria kufanya tafsiri ya kitabu hiki. Ni matumaini yangu kwamba, watu wakisoma, wataanza kujiuliza maswali mengi juu ya wanawake wa TANU.Wako wapi akina mama hawa? Je, wamekufa na ushupavu wao au ushupavu huu wameurithisha kwa wanawake wengine? Je maneno ya Bibi Titi, yanachukuliwa vipi na wanawake wa Tanzania, hasa wale walio mstari wa mbele kutetea haki za wanawake? :
“ Ingawa wanawake wanasema kwamba hawajaendelea, mimi ninayewafahamu tangu wakati ule, naona kwamba wameendelea sana, kwasababau serikali inataka kuwasaidia. Tatizo liko wa wanawake viongozi, siyo kwa wanawake kwa ujumla” (Mahojiano ya Bibi Titi Uk.104). Inawezekana Bibi Titi, aliyasema haya katika uzee wake? Kwamba alishaanza kupoteza kumbukumbu na moyo wake wa ushupavu? Au inawezekana kuna ukweli katika maneno yake?

Pili, nikubaliane na hoja iliyotolewa kwenye utangulizi wa kitabu hiki: “ Tunaamini kwamba vikaragosi vya wakoloni vimejitokeza tena hivi leo kutokana na kuwepo kwa sera za soko huria na kudhihirika kwa nguvu mpya za ubeberu. Tanzania inaweza kujikuta ina “uhuru wa bendera” hasa ukitilia maanani kwamba uchumi wake sasa unamilikiwa na mashirika ya watu wengi  wa kigeni….”.

Hii ni kweli. Ukiangalia wimbi la uwekezaji na hasa uwekezaji unaogusa ardhi, dalili za kuwa na wanahakarti kama wanawake TANU,siku zijazo halikwepeki kamwe!  Ni kama inavyosemwa kwenye utangulizi wa kitabu hiki:
“ Muda mfupi baada ya  Uhuru, Serikali ilipitisha sera ya ardhi ambayo ilitambua umiliki wa ardhi kuwa wa  jamii na kuwazuia wageni wasimiliki  ardhi. Sera hii ya ardhi imekuwa ikipigwa vita na wawekezaji tangu miaka ya 1980, na hatua kwa hatua, Serikali imekuwa ikiruhusu matumizi ya ardhi kwa wageni katika sekta za kilimo, utalii, uchimbaji wa madini na mabenki yanayowekeza hapa nchini. Hivyo basi, suala la ardhi limeanza kuibuka upya na wanaharakati pamoja na jamii katika sehemu mbalimbali wameanza kujipanga upya ili kulipinga.” (Utangulizi xi).

VI. HITIMISHO.
Kwa kuhitimisha, ninapenda kuwashauri watanzania kukisoma kitabu hiki cha Wanawake wa TANU. Pia ninapendekeza, Serikali itafute namna ya kuwaenzi wanawake hawa. Wale ambao bado wako hai, wapatiwe matunzo. Wale waliokufa, kifanyike kitu cha kumbukumbu. Si vibaya hata kama familia zao zitapatiwa kitu cha kumbukumbu.

Kuna haja ya dunia kuacha tabia ya kuwatumia wanawake katika harakati na baadaye kuwatelekeza na kuwaweka pembeni. Ukisoma kitabu cha Wanawake wa TANU, unapata picha ya Maria Magdalena wa kwenye Biblia, pamoja na wanawake wale wote waliomtumza Yesu.Luka, anaandika kwamba wanawake hawa, walitumia pesa zao na mali zao kumhudumia Yesu.Na walikwenda naye popote alipokwenda na kuhudumia umati wote uliomfuata Yesu.Lakini kwenye kumbukumbu ya Kanisa, wanatajwa Mitume wanaume peke yao na wanawake hawatajwi!

Maria Magdalena, alikuwa karibu na Yesu, alimhudumia na alikuwa mtu wa kwanza kushuhudia ufufuko wa Yesu, lakini katika kumbukumbu za kanisa, ametupwa pembeni!

Yote haya yanasababishwa na mfumo dume! Mfumo unaopenda madaraka kuliko kitu chochote kile! Mfumo ambao umeleta vita na maafa makubwa hapa duniani. Tunapofikiria amani ya dunia hii, na amani ya taifa letu la Tanzania tufikirie kuirudia mifumo inayowashirikisha na wanawake, kama ile mifumo ya wanawake wa TANU.

Na,
Padri Privatus Karugendo.


 

0 comments:

Post a Comment