UCHAGUZI WA IGUNGA, MKAPA ANATUKUMBUSHA YA NYUMA.
Waswahili wanasema
yaliyopita si ndwele, lakini kwa vile Rais Mstaafu William Benjamin Mkapa,
ameamua kupanda tena jukwaani na kuendeleza siasa “Uchwara” alizoziacha nyuma
yake hatuna budi kuyafufua ya nyuma. Tulishauriwa kutomgusa ili apumzike kwa
amani; yeye hataki kupumzika! Yuko Igunga akipigana kufa na kupona ili kiti
hicho cha ubunge kisiende upinzani. Pamoja na idadi kubwa ya wabunge wa CCM ,
bado Mkapa ameona ni muhimu sana kupigana kufa na kupona kutetea kiti hicho. Je
huo ni U- Tanzania?
Tumkumbushe hotuba yake
ya kufunga mwaka 2004: Hotuba hiyo
ilikuwa nzuri na ya kumgusa kila “Mtanzania”.
Ambaye hakuguswa na hotuba hiyo basi huyo si “Mtanzania”. Nimeweka neno
Mtanzania kwenye mabano, maana si kila Mtanzania ni Mtanzania! Hili linahitaji
mjadala unaojitegemea! Kama mtu
hakuguswa na maelezo ya Mkapa juu ya hali ya kisiasa, basi atakuwa aliguswa na
maelezo yake juu ya hali ya uchumi, hali ya kijamii, mambo ya nje au basi
atakuwa aliguswa na hitimisho. Kila mtu atakuwa aliguswa kwa namna yake. Kama
alivyosema yeye mwenyewe kwenye hotuba hiyo.
“ Penye
wengi, pana mengi. Nasi tuko wengi, zaidi ya milioni 35. Hivyo haishangazi
wakitokea wachache wenye sababu zao za kuziba macho na masikio wasiyaone wala
kuyasikia yale ambayo Serikali yenu ikishirikiana nami tumeweza kufanya au
kuyaanzisha. Watu hao ni wa kuonewa huruma, wanapigana na ukuta”.
Ni kweli watanzania ni
wengi na namna ya kuangalia na kuamua vitu inatofautiana. Ndiyo maana ninasema
hotuba yake itakuwa ilimgusa kila mtu
kwa namna yake. Bahati mbaya hotuba hiyo haikutoa takwimu ili kuonyesha
wachache kati ya milioni 35 ni ngapi?
Hivyo ni vigumu kujua watu wa kuhurumiwa ni wangapi – inawezekana pia
kwamba wale anaodhani ni wengi ndio wanaopigana na ukuta. Wakati ukuta,
Waswahili wanasema.
Kwenye hotuba hiyo Rais
Mstaafu William Benjamin Mkapa alisema:
“ Utaona pia watu
wanabishana juu ya mambo mengine madogo, au hata ya kipuuzi kabisa. Lakini
ubishi huo ndiyo unaitwa ushindani wa kisiasa, unachangamkiwa pia na vyombo vya
habari”,
Bahati mbaya katika hotuba hiyo hakuweka bayana maana ya mambo madogo na mambo ya kipuuzi. Hakutoa mifano!
Malalamiko ya walio wengi ni rushwa, kuiba kura, kujilimbikizia mali, kupora
nchi, kujiingiza kwenye utandawazi bila mbinu na maandalizi, kuuza mashirika ya
umma kwa wawekezaji wa nje bila ya uangalifu wa kutosha. Siku chache kabla ya
hotuba hii tulisikia kwenye vyombo vya habari wawekezaji waliokamatwa kwenye
uwanja wa ndege wa Mwanza, wakitoroka bila kulipa ushuru. Hao walikamatwa, ni
wangapi wametoroka bila kukamatwa?
Inawezekana haya ni mambo madogo na ya kipuuzi? Kwa vile Mheshimiwa
Mkapa, hakutoa mifano – labda wasaidizi wake walipitiwa. Kila Mtanzania ana
uhuru wa kutoa mifano yake. Na kujiuliza ni yapi mambo madogo na yapi ni ya
kipuuzi! Kwa Mtanzania wa kawaida, wale tunaozoea kuwaita walalahoi ununuzi
ndege ya Rais ya bilioni 40, ya aina yake Afrika kusini mwa jangwa la Sahara na
yenye uwezo wa kuruka kwa masaa mengi bila ya kutua kujaza mafuta na yenye
uwezo wa kutua kwenye viwanja vichache nchini Tanzania, ni upuuzi wa hali ya
juu. Watu wanakufa kwa njaa, malaria inawaua watoto, barabara mbovu, watu
hawana maji, hawana umeme, hawana kipato cha kutosha nk – inawezekana
kuyajadili haya ni upuuzi? Lakini kwa yule aliyeshiriki kuiagiza ndege ya Rais
na kupokea michuzi ya asilimia kumi, atauita mjadala wa kununua au kutonunua
ndege ya Rais kuwa ni kujadili mambo madogo!
Hoja nyingine kwenye hotuba hiyo ilikuwa:
“ Na sera haiwezi KUINGIA IKULU. Sera ya
kuingia IKULU ni sera ya ubinafsi; tena ubinafsi wa hali ya juu. Maana hoja si
kwenda IKULU: hata tausi wanaishi IKULU. Hoja ni unakwenda IKULU kuwafanyia nini Watanzania”,
Ni mtu gani asiyejua kwamba IKULU, kuna
Neema? Bila Neema, hata tausi wataikimbia Ikulu!
Hotuba hiyo iligusia
mambo mengi;
“ Kwanza, kuhakikisha kuwa asilimia 93 ya
Watanzania ambao hawajaambukizwa virusi vya UKIMWI hawaambukizwi. Kila mbinu na
kila silaha itumike. Wakati wa kuchagua silaha kwenye vita hivi umepita. Wakati
wa unafiki nao umepita. Tukifanya ajizi taifa litaangamia.”,
Kwa kipindi chote cha utawala wake Rais
Mkapa, hakuonyesha mzimamo wake waziwazi juu ya kudhibiti ugonjwa huu. Kwenye
hotuba yake alishindwa kutuelezea ni mbinu gani zitatumika kuhakikisha asilimia
93 haiambukizwi. Ni mbinu gani? Miujiza? Hakuunga mkono matumizi ya kondomu,
waziwazi bila ya kuzunguka na bila ya mafumbo. Yeye kama Rais wa nchi alikuwa
na nafasi ya pekee ya kuhakikisha kila mbinu inayofaa inatumika bila kuangalia
au kulenga kuyafurahisha baadhi ya makundi fulani katika jamii yetu. Vita ni
vita na vita haina macho! Aliendelea na mbinu potovu ya kutotaka kupoteza
uhusiano mzuri na viongozi wa kidini. Kwa mshangao wa wengi amehitimisha hotuba
yake kwa kupiga marufuku tangazo la “Usione Soo”. Tunajua sote jinsi wanawake
walivyo kwenye hatari kubwa ya kushambuliwa na UKIMWI, utamaduni wetu umekuwa
ukimkandamiza mwanamke na kumfanya “Aone Soo”, akubaliane na kila kitu asemacho
mwanaume. Utamaduni huu umewaingiza wanawake wengi kwenye matatizo yasiyokuwa
yao. Utafiti unatuonyesha kwamba sehemu ambazo wanaume wanawaacha wanawake
vijijini na kwenda kufanya kazi na kuishi mijini, imeshambuliwa sana na UKIMWI.
Wanaume wanapokuja likizo nyakati za Christmas na mwaka mpya wanabeba virusi.
Wanawake vijijini wanaona Soo, kuwauliza waume zao juu ya hali zao. Pamoja na
zawadi za Christmas wanazozipata kutoka mijini ni UKIMWI. Utamaduni huu wa
mfumo dume umekuwa hatari kubwa katika dunia ya leo. Mtu yeyote anayetaka
kuuendeleza, hatufai kabisa. Huyu ni adui wa UMMA! Adui wa UMMA, ni lazima
kumkataa na kusema, hapana huo si U-Tanzania!
Katika hotuba hiyo mimi
binafsi niliguswa na nukuu ya Mwalimu:
“ Hoja lazima ijengwe kwamba hatimaye kinga
madhubuti ya haki za raia, uhuru wa raia, na mambo yote wanayoyathamini,
hatimaye yatahifadhiwa na maadili ya kitaifa. Taifa linapokuwa halina maadili
yanayowezesha Serikali kusema: ‘ Hatuwezi kufanya hivi, huu si U-Tanganyika.’
Iwapo watu hawana maadili ya aina hiyo, haisaidii sana hata kama wangekuwa
na Katiba iliyoandikwa vizuri sana.
Bado raia wanaweza kukandamizwa…. Tunachopaswa kukifanya ni kujenga maadili ya
taifa hili, kila mara kuimarisha maadili ya taifa hili, maadili yatakayomfanya
Rais yeyote yule kusema, ‘Ninayo madaraka ya kufanya jambo hili chini ya Katiba, lakini sitalifanya, maana huu si
U-Tanganyika. Au kwa watu wa Tanganyika, iwapo wamekosea na kumchagua mwenda
wazimu kuwa Rais, mwenye madaraka ndani ya katiba ya kufanya XYZ, akijaribu
kufanya hivyo, watu wa Tanganyika waseme, ‘Hatukubali hili lifanyike, hata
alitake Rais au Rais maradufu, hatulikubali, maana huu si U-Tanganyika’."
Haya maneno ya Mwalimu, yaliyotamkwa tarehe
28 Juni 1962, wakati mwalimu akiwasilisha Bungeni mswada wa kuifanya iliyokuwa
Tanganyika kuwa jamhuri, ni kipimo cha
Vyama, Viongozi na watanzania wanaojigamba kwamba wao ni “Watanzania”.
Bahati nzuri au mbaya
viongozi wetu wote wa kitaifa tulionao hadi leo hii ni wa CCM. Chama
kinachotawala ni cha CCM. Je, Chama hiki na viongozi wake wametufikisha mahali
pa kusema kwamba huu ni U-Tanzania? Ni kiongozi gani mnyenyekevu, tumtaje kwa
jina, nani? Unyenyekevu unaonekana wakati wa uchaguzi, baada ya hapo viongozi
wetu wanakuwa miungu watu! Ni kiongozi gani asiyetafuta kutumikiwa bali
kutumikia? Tumtaje kwa jina!
Waasisi wa taifa letu
walituachia utamaduni wa kutolimbikiza mali. Ni kiongozi gani leo hii
halimbikizi mali? Tumtaje kwa jina!
Waasisi wa taifa letu
walituachia utamaduni wa kung’atuka. Ni kiongozi gani wa Tanzania, ameonyesha
dalili za kung’atuka kwa hiari? Je CCM,
yenyewe imezingatia utamaduni huu wa kung’atuka. Ikafika mahali ikaviachia
vyama vingine. Maana huu ndio utamaduni wetu na huu ndio U-Tanzania?
Je ni U-Tanzania,
kiongozi wa nchi kutamka:
“ Maana wanaojaribu
kupanda mbegu za chuki, mbegu za udini, mbegu za ukabila, ni wachache. Kwa
pamoja tutang’oa mbegu zao, na ikibidi tutawang’oa wao”.
“ikibidi utawang’oa wao”
ina maana gani? Hapa kuna utetezi wa
uhai? Tujuavyo sisi uking’oa kitu kinakufa. Je, ni U-Tanzania,
kuwatishia wananchi? Huku si kutangaza vita au kutaka kuwanyamazisha wenye
maoni tofauti?
“ Ninarudia. Tutanya
kila liliko ndani ya uwezo wa Serikali, kwa mujibu wa sheria, kuhakikisha
wanaotaka kuleta fujo, vurugu na uvunjifu wa amani hawafanikiwi kamwe, na hasa
mwaka ujao wa Uchaguzi Mkuu.”
Kama hakuna maelezo ya
fujo na vurugu ni nini ni lazima wananchi wawe na mawazo tofauti, wanaofikiri
CCM, haikufanya vizuri wawe na wasiwasi wa maisha yao. Ni lazima watafute mbinu
za kuyalinda maisha yao. Historia imetufundisha kwamba wapambanaji wote daima
wanawekwa kwenye kundi la watu wa fujo, vurugu na ugaidi. Makaburu, walikuwa
wakitumia nguvu za serikali na mujibu wa sheria kumdhibiti Mandela na juhudi za
ANC, za kutaka kuleta mabadiliko Afrika ya kusini. Wapigania huru wote
waliwekwa kwenye orodha ya watu wenye fujo, vurugu na wanavunja amani.
CCM, imeshindwa
kupambana na rushwa. Nchi nzima inanuka rushwa ndogo na rushwa kubwa kubwa.
Tumeshuhudia miradi hewa. IPTL, inaleta hasara kwa Taifa. Viongozi wenye mishahara
ya kawaida wanajenga mahekalu, wana magari ya bei mbaya, watoto wao wanasoma
nchi ze nje nk. Haya yote yanatendeka chini ya uongozi wa CCM. Hakuna hatua
inayochukuliwa. Hakuna anayewajibishwa. Inaendelea kuwa kero kwa wananchi wa
kawaida na wale wote wanaojali maendeleo ya taifa zima la Tanzania. Je, ni
vurugu au ni fujo, watu wakianza kuhoji uwezo wa CCM, kuendelea kuliongoza
taifa letu? Je, hawa ndio watakaong’olewa na Serikali ya CCM? Hawa ndio watakao
poteza maisha yao? Ni nchi gani duniani iliyoendelea kwa kuongozwa na viongozi
wala rushwa?
Tujiulize, U-Tanzania,
unanyesha kama mvua? Inatosha kuzaliwa Tanzania, mtu akatenda na kuishi ya
U-Tanzania? Mtanzania, hawezi kuisaliti nchi yake, hawezi kuipora nchi yake.
Mtanzania wa kweli ni mzalendo. Mtanzania wa kweli analitanguliza taifa bila
kuangalia kwanza maslahi yake binafsi, analitanguliza taifa bila kutanguliza
tumbo lake. Huyu yuko tayari kuyapoteza maisha yake kwa kutetea uhai wa taifa
lake. Ili kuujenga U-Tanzania, mwalimu
Nyerere na waasisi wengine, walibuni mbinu na mifumo mbali: Lugha moja,
siasa ya ujamaa na kujitegemea, vijiji vya ujamaa, kuwasambaza watoto kwenye
shule za mikoa mbalimbali, jeshi la kujenga taifa, mwenge wa uhuru nk.
Leo hii Lugha
yetu tunaipiga vita. Tunataka kutumia lugha za kigeni! Ujamaa tumeuweka
kaburini. Vijiji vya ujamaa havisikiki tena. Jeshi la kujenga taifa liliokuwa
linawakutanisha vijana waliomaliza kidato cha sita, limekufa kifo kitakatifu!
Mwenge wa huru umetaifishwa na CCM, badala ya kujenga umoja wa kitaifa
unatumika kukipigia debe chama cha
Mapinduzi. Tuna mbinu gani za kujenga U-Tanzania?Ni nani mwenye sera ya wazi ya
kuujenga U-Tanzania? Tusijidanganye na
kuamini kwamba jambo hili linaweza kunyesha kama mvua. Ni jambo la kufanyia
kazi. Na mwenye nafasi ya kufanya jambo hili, hawezi kupata nafasi ya
kujilimbikizia mali, nafasi ya kuwa na viwanja na kujenga nyumba kila mkoa,
Mwalimu Nyerere, alikuwa na nyumba ngapi? Je, nyuma yake ameacha vitabu vingapi
vyenye sera, vision, falsafa na mambo mengine mengi ya kuujenga U-Tanzania na
Ubinadamu? Alitumia muda wake, kufikiri, kusoma, kupanga na kuandika. Kujenga
U-Tanzania, kunahitaji umakini. Huwezi kushinda na kulala kwenye pombe,
kufukuzia dogodogo, kujenga nyumba ndogo, kugombania viwanja, kufukuzia asilimia
kumi kwa kila mradi upitao, ukapata muda na uwezo wa kujenga vision.
Majumba yamejengwa,
viongozi wetu wanavaa suti za Ulaya, wanaendesha magari ya bei mbaya, ofisi
zinapendeza – lakini uko wapi urithi wa vitabu? Ni nani anaandika, ni kiongozi
gani anakaa chini kusoma, kufikiri na kutunga sera. Viko wapi vitabu hivi
tuvisome. Viongozi wetu wa sasa wanaongozwa na falsafa ipi? Ni nani mwenye
kuitetea falsafa hii na kuifundisha?
Tulitegemea baada ya
kustaafu Mheshimiwa Mkapa, angekaa chini na kuangalia ya nyuma. Kuona alikosea
wapi na alifanikiwa wapi. Angetumia muda wake uliobaki kuandika vitabu vya
kuwashauri na kuwaongoza watanzania na si kujiingiza kwenye upuuzi huu wa
“Siasa Uchwara” kutumia fedha nyingi kuhakikisha jimbo la Igunga linabaki CCM. Wapinzani
nao ni Watanzania, kama Mkapa halioni hili, basi kumbe naye hakufaa kuiongoza
Tanzania!
Na,
Padri Privatus
Karugendo.
0 comments:
Post a Comment