MAMA ELIESHI LEMAElieshi Lema, ameandika hadithi za watoto. Mwandishi huyu amejizolea sifa nyingi katika uwanja huu wa hadithi za watoto. Safari ya Prosper, Freshi na Maisha, Mkate Mtamu, Mwendo na vinginevyo vimedhihirisha “umama” wa mwandishi na hasa ujuzi wake wa kueleza mambo makubwa kwa lugha ya kawaida; ujuzi wa kufundisha mambo makubwa kwa watoto wadogo. Mama huyu ni mwanafalsafa wa enzi hizi tulizomo, ni mtetezi wa haki za binadamu na mwanaharakati asiyechoka kuitumia kalamu yake na kipaji chake kuwaelimisha watanzania na ulimwengu mzima

Enzi tulizomo ni za kutetea Haki. Kuna harakati za kutetea haki za watoto, haki za wanawake, haki za wanaume, haki za walemavu, haki za wazee, haki za yatima, haki za wajane nk. Semina nyingi zinafanyika na fedha nyingi zinatumika katika harakati hizi. Wakati mwingine utetezi huu unakuwa kama upepo uvumao na kupita, maana walengwa wanabaki katika giza, wakati wale wanaojiita watetezi wakinufaika kiasi kikubwa kutokana na mchakato mzima wa kutetea haki za watoto, wanawake, wanaume, wajane, wagane, wazee, yatima na wagonjwa wa UKIMWI.

Mara nyingi wale wanaotetewa hatusikii sauti zao, hatusikii kilio chao, hatupati hali halisi ya mazingira yao; tunasikia tu sauti za wanaharakati. Tunajifunza matatizo yao kupitia sauti za wanaharakati.

Katika uandishi wa Mama Elieshi, tunapata picha nyingine tofauti. Yeye anaibua sauti za wahusika na kuwaacha wajisemee wenyewe. Ni uandishi wa aina yake, ndiyo maana kwa macho ya waliowengi, huyu ni mama wa mfano; ni mama mwenye sifa mbele ya watanzania. Ingawa si mwanasiasa au mfanyabiashara mashuhuri kiasi cha jina lake kuandikwa kwenye kila gazeti, mchango wake ni mkubwa na ni lazima kuutambua.

Tunaweza kufumba macho na kukataa kuutambua mchango wa mama huyu mwandishi, lakini kilichoandikwa kimeandikwa. Kesho na keshokutwa vitabu vyake vitasomwa na wengi. Tutashitakiwa na historia, kwa kushindwa kuona mchango wake wakati wa uai wetu.


Yeye mwenyewe anasema:
“Tumekuwa tukifanya makosa makubwa, kufikiri kwamba tunafahamu yote wanayoyataka watoto wetu, hatuwapatii nafasi ya kuwasikiliza.

Tunafikri wao hawana uwezo wa kutamani mambo fulani fulani na kuyachukia baadhi ya yale tunayotaka kuwafundisha. Watoto nao wana utashi, wana maonjo na wana namna yao ya kuyaangalia matukio mbalimbali katika jamii. Tukiwapatia nafasi ya kujielezea, tukiwasikiliza, tunaweza kugundua mengi..”

Hivyo katika maandishi yake yote, anaawacha wahusika wanazungumza. Vitabu vyake vya watoto, tunasikia sauti za watoto.Mfano kitabu chake kipya cha Mashitaka. Kinachosikika ni sauti ya watoto. Watoto wanauliza maswali magumu juu ya hadithi ya Katope mtoto wa ajabu.

Bi Elieshi Lema ni mama wa watoto watatu na mwanamama aliyeweza kufanikisha mengi katika ulimwengu wa vitabu. Ametunukiwa shahada ya Fasihi katika Chuo kikuu cha Dar es Salaam na Shahada ya Uzamili katika hiyo hiyo Fasihi, nchini Marekani katika miaka ya themanini . (BA in Literature and MA in Literature) Bi Elieshi Lema alianza uandishi wake rasmi akiwa mtu mzima. Uandishi wake kwa ujumla huakisi jamii na yeye hupendelea kuandika yale anayoyaona au kusikia au yanayomgusa kwa namna moja au nyingine.

Msukumo alioupata katika kuandika Parched Earth ni kutokana kuona mengi yanayo mzunguka mwanamke kama kitovu cha jamii. Kwake yeye kama mwandishi ameshuhudia mengi yanayomkumba mwanamke, hasa mwanamke wa kitanzania na hivyo kusukumwa kuyaandikia jamii.

Kitabu hiki kimeandikwa kwa lugha ya kiingereza, kitu kinachoongeza mvuto wa kitabu na hadidhi yenyewe. Ukweli ni kwamba mpaka sasa hapaTanzania tuna vitabu vichache vya hadidhi za kiingeleza vilioandikwa na watanzania wenyewe. Inavutia kuona Mtanzania, anavyoweza kuandika hadihi inayohusu maisha ya kitanzania kwa kiingereza. Huu ni mchango mkubwa katika kukuza na kendeleza lugha hii ya kingeni ambayo ni lugha ya kimataifa na inaongoza katika kijiji cha Utandawazi. Na wala huku si kupiga vita kiswahili, bali nikuiendeleza lugha hii katika jamii ya kitanzania.Mwandishi wa riwaya hii ya kiingereza, ameandika riwaya nyingi kwa lugha ya kiswahili.Jambo la msingi ni kuzipatia nafasi lugha zote na hasa lugha kuu,mfano lugha ya taifa na lugha za kimataifa kama kiingereza.

Ujumbe wa Mama Elieshi Lema, katika riwaya hii, kama nilivyoelewa mimi ni kwamba uhusiano wa mtu na mtu, na hasa uhusiano wa mwanamke na mwanamme, si jambo la kuachiwa hivi hivi kila mtu akafanya apendavyo. Ni swala la kiroho linalohitaji mfumo wa kijamii. Si mfumo dume, unaowafanya wanawake kuwa vyombo vya kuzaa watoto wa kiume au kufanya kazi za kumfurahisha mwanaume, bali mfumo unaohimiza uhusiano unaolenga kuunganisha nyoyo za watu zaidi ya kuunganisha miili ya watu!


Mfumo ambao unaweza kusaidia kuwafundisha vijana wetu juu ya uhusiano, juu ya kupenda na kupendwa, juu ya kuoa na kuolewa na juu ya kujenga familia zilizo bora. Vijana wakisoma “Parched Earth”, wakapata nafasi ya kujadiliana na kubadilishana mawazo na kusikiliza uzoefu wa wazee waliowatangulia, inaweza kusaidia kutoa mwanga katika maisha yao. Changamoto anayoitoa Mama Elieshi Lema, katika riwaya hii ni swali la kawaida: je, Mwanamme anahitaji nini kutoka kwa mwanamke na mwanamke anahitaji nini kutoka mwanamme. Na je ni mazingira gani yanaweza kumfanya mwanamke atambue anachohitaji mwanamme, na ni mazingira gani yanaweza kumfanya mwanamme atambue anachohitaji mwanamke.


Inawezekana hili ni swali la kawaida. Lakini tukiingia kwa undani hili linaweza kuwa swali kubwa ambalo halina jibu katika maisha yetu ya kawaida. Tuna mifano mingi ambapo wa kinamama wanaachwa na mabwana zao kwa vile hawakuzaa watoto wa kiume. Je, hicho ndicho wanaume wakitakacho kwa wanawake? Wapo pia akina mama wanaoachwa kwa vile hawakuzaa. Je wakitakacho wanaume ni watoto tu? Upendo wa mahusiano ni watoto?


Hadi sasa mama huyu ameshaandika vitabu zaidi ya ishirini vingi vikiwa vitabu vya watoto. Vitabu vingine alivyokwisha andika ni kama Safari ya Prosper, Pendo’s Dream (Ndoto ya Upendo) Fresh na Maisha Mkate Mtamu, Mwendo, na vingine vingi. Amekwisha tunukiwa na Tuzo ya Fasihi Tanzania (Tanzania Literary Award) mwaka 2001 ya kitabu hiki cha Parched Earth kama Kitabu bora nadharia cha watu wazima(best adult fiction) na mwaka 2002, kitabu chake cha Ndoto ya Upendo kilitunukiwa tuzo ya Kitabu bora cha watoto. Kwa sasa anafanyia kazi kitabu chake kipya cha Mashtaka kitakacho toka hivi karibuni.


Ukiacha uandishi pia Bi. Elieshi Lema amejikita kwenye shughuli za maendeleo ya kijamii. Ameshakuwa mwenyekiti wa Tanzania Cultural Trust Fund, pia ameshakuwa Mwenyekiti wa Hakielimu. Vivyo hivyo yeye ni mmmoja wa wamiliki wa E&D Publishers Ltd iliyochapa kitabu hiki cha Parched Earth: A Love Story pamoja na kazi za waandishi maarufu kama za Hayati Prof. Chachage.

Ni mama mwenye mchango mkubwa katika taifa letu, ni mama wa mfano, ni mama wa kuigwa!

Na,
Padri Privatus Karugendo.

1 comments:

mchambuzi said...
This comment has been removed by the author.

Post a Comment