MWANA MAMA BEATRICE SHIMENDE KANTIMBOSafu ya Mwana Mama, imeanzishwa kwa lengo la kuandika na kutangaza mchango wa akina Mama katika taifa letu la Tanzania. Wanawake wana mchango mkubwa, lakini mara nyingi mchango wao unafunikwa kiasi kwamba vyombo vingi vya habari vinatawaliwa na sifa za wanaume. Akiandikwa mwanamke inakuwa ni kashifa za ngono na mambo mengine kama hayo. Wakati wanawake wana mchango mkubwa: Uvumilivu, kuishi kwa matumaini, kutokukata tama na kubwa zaidi hawa ni mama zetu. Hakuna mtu anayekuja hapa duniani bila kuzaliwa na Mwanamke. Hivyo tunataka tusitake ni lazima tutambue kwamba mwanamke ana mchango mkubwa katika jamii yetu.

Leo katika safu yetu ya Mwana Mama tunawaletea Beatrice Shimende Kantimbo, mkazi wa Kwembe, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam wilayani Kinondoni ,mama ambaye amepambana na ugonjwa wa mguu kwa miaka 15. Jana amerudi kutoka nchini India, akiwa amepona!

Mapokezi makubwa aliyoyapata mama huyu Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Dar-es-Salaam ni ishara kwamba ugonjwa wa mama huyu uliwagusa watu wengi. Na labda sasa wakati umefika wa kuacha kuchangia tu sherehe za ndoa na kuanza kuchangia matibabu na elimu ya watoto wetu. Watanzania tunasifika sana kwa vikao vya harusi na kuchanga fedha nyingi za harusi kuliko tunavyochangia wagonjwa na elimu.

Tuna mengi ya kujifunza kutoka kwa mama huyu mwenye umri wa miaka 48, ambaye kabla ya kupata ugonjwa huu alikuwa mchapakazi akijishughulisha na shughuli mbalimbali za biashara na nyingine kama msherekeshaji aliyejulikana kama Kimbaumbau.

Mama huyu ameonyesha uvumilivu mkubwa. Hakukata tama wala kukubaliana na wale waliomshauri mguu wake ukatwe. Pamoja na maumivu makubwa aliyokuwa nayo mama huyu, daima alionyesha matumaini na tabasamu lilitawala uso wake. Aliishi kwa imani na matumaini. Mme wake naye amekuwa mfano wa kuigwa; alisimama kidete kumhudumia mke wake kwa miaka yote hiyo 15 hadi kumsindikiza India. Huyu ni mwanaume wa mfano!

Habari za Mama huyu zilipoanza kuandikwa kwenye vyombo vya habari, mama huyu alihojiwa akisema:

“NIMEKUWA nikiteseka kwa kuuguza mguu wangu kwa miaka 15 sasa, hakika napata maumivu makali sana, naomba Mungu anisaidie na awajaze moyo wa huruma Watanzania wenzangu ili niweze kwenda kutibiwa.”

Alisimulia jinsi alivyoanza kuugua mguu wake: “Nakumbuka mwaka 1998 nikiwa kwenye biashara zangu pale Ubungo, kuna kitu kilinichoma hapa (anaonyesha pajani) maumivu yake yalikuwa mithili ya sindano, hata hivyo hayakudumu sana wala hapakuwa na alama yoyote.

“Baada ya dakika chache nikajihisi homa kali. nikaanza kutetemeka mwili mzima, nikaamua kwenda hospitali inayojulikana kwa jina la Neema, Daktari akanipima, akagundua nilikuwa na malaria.

“Wakati huo mguu haukuonyesha dalili zozote za maumivu wala jeraha. Malaria ilikuwa kali, nikalazwa kwa muda wa wiki mbili pale hospitali. Nikaruhusiwa, nikarudi nyumbani na hapo ndipo nilipoanza kuona mguu unavimba. Kadri siku zilivyozidi kwenda ndivyo mguu nao ukazidi kuvimba”

“Baadhi ya madaktari wa Muhimbili walinishauri nikubali kukatwa mguu. Wanasema nyama imeoza na mfupa wa mguu umeharibika. Mimi sikukukubaliana na ushauri wao kwa sababu baada ya kupigwa X-ray 2007 iligundulika tatizo kubwa lilikuwa kwenye mishipa ya kupitisha maji kutokana na nyama kuharibika. Sio mfupa.

“Nilikataa kwa imani kuwa nitapona tu. Nikijiangalia nina uwezo wa kusimama na kutembea isipokuwa tu kinachonipa taabu kwa sasa ni nyama za mguu zimekua sana kiasi kwamba nikitembea zinagusa mguu wa kushoto, hivyo naomba Wasamaria wema wanipe msaada ili niende India kwa matibabu zaidi.” alisema.

Kilio cha mama huyu kilisikika, lakini si kwa kasi iliyotegemewa. Mwanzoni ilitia mashaka kama watanzania wameishiwa na moyo wa huruma. Mama huyu alikuwa akionekana akilia kwa maumivu kwenye vyombo vya habari na hasa ITV, lakini uchangiaji ulienda polepole. Sam Mahera, mtangazaji wa ITV, alikuwa akihamasisha uchangiaji kwa mbinu zote na kwa nguvu zote, lakini uchangiaji haukushika kasi haraka, hata hivyo baadaye watanzania walifunguka na kuweza kumchangia mama huyu. Na sasa amerudi akiwa ametibiwa.

Pamoja na furaha kubwa ambayo watu wameonyesha Mama huyu kurudia hali yake ya kawaida, wana maswali mengi ya kujiuliza: Hivi huko India kuna nini? Ina maana Madaktari wa India wamesoma zaidi ya wetu wa hapa Tanzania? Mbona ugonjwa wa mama huyu haukutibiwa hapa kwetu mpaka mama huyu alipolazimika kusafiri hadi India. Au tatizo ni vifaa? Kama tatizo ni vifaa, kwa nini serikali yetu isinunue vifaa ili kuweza kuokoa maisha ya watanzania wengi? Si wa Tanzania wote watapa bahati ya kuchangiwa fedha kama alivyochangiwa Beatrice. Kuna watanzania wengi ambao maisha yao yanapotea kwa kushindwa kupata matibabu kwa wakati.

Ugonjwa wa Mama Beatrice, utufumbue macho. Walio wengi waliamini hakuna la kufanya zaidi kwenye mguu wa Mama huyu. Pendekezo lilikuwa ni kuukata. Sasa Wahindi wameutibu? Wana nini hawa? Kama wana utaalamu zaidi, kwa nini serikali isiwapeleke vijana wakajifunza utaalamu huo?

Tumesikia kwamba pamoja na michango ya wananchi, serikali pia imechangia kiasi kikubwa kwa matibabu ya Mama Beatrice. Ni jambo zuri kwamba serikali imesaidia. Hata hivyo kwa nini serikali inaamua kusaidia imechelewa? Mama huyu amekuwa kwenye maumivu makali kwa muda wa miaka 15. Miaka hii ni mingi kwa mtu kuishi na maumivu kiasi hicho.

Tunampongeza Beatrice Kantimbo, kupona mguu wake: Ametufundisha uvumilivu, kuishi kwa matumaini na kujiweka mikononi mwa Mwenyezi Mungu na kutufunulia ukweli kwamba magonjwa mengi yanatibika watu wakiwa na mshikamano wa kuchangiana fedha za matibabu nje ya nchi. Kwa kuujua ukweli huu ni lazima sasa sote kuwa macho ili watu wasipoteze maisha yao kwa kushindwa kupata fedha za kwenda nje ya nchi kutibiwa. Magonjwa yanayotibika, yasitoe uhai wa watanzania: Tuishinikize serikali, kama inashindwa kuziboresha huduma za afya, basi itenge fedha za kutosha za kuwasafirisha watu nje ya nchi kutibiwa. Uhai, ukitoka haurudi, hivyo ni jukumu letu sote watanzania kuulinda uhai wa kila Mtanzania kwa gharama yoyote ile.

Na,

Padri Privatus Karugendo

+255 754 633122

.0 comments:

Post a Comment