“VURUGU” BUNGENI NI KOSA LENYE HERI?

Kwenye miaka ya themanini nchini Ujerumani, niliishi na jumuiya ya watu waliokuwa na  theolojia ya kushangilia makosa. Mwanzoni theolojia hii ilinichanganya na kunipunguzia kiwango fulani cha imani yangu. Baada ya kuishi miaka mitatu ndani ya jumuiya hii na kuielewa theolojia yao, niliipenda na kuikumbatia na imenijenga kiimani hadi leo hii. Nilikuwa nimelelewa kwenye utamaduni na theolojia ya kulaumu makosa na kunyosheana vidole.  Mtu akikosea, analaumiwa, anazomewa ananyoshewa kidole, anaadhibiwa na wakati mwingine anatengwa na jumuiya husika. Hawa ndugu zangu Wajerumani, mtu akikosea; anashangiliwa na kupongezwa kwa kuisaidia jumuiya kugundua kasoro zake. Waliamini kwamba mtu mmoja kwenye jumuiya hawezi kufanya makosa bila kusababishwa na mazingira yanayomzunguka. Maana yake ni kwamba kosa la mtu mmoja linaweza kuwa lina mnyororo wa matukio yanayowagusa watu wengi ndani ya Jumuiya.

Wajerumani hawa, au niseme wanajumuiya hawa, maana ni jumuiya ambayo pamoja na kuwa nchini Ujerumani ilikuwa na watu wa mataifa mbali mbali, waliamini kwamba kila tukio lilikuwa na fundisho. Liwe tukio baya au zuri kwao ni fundisho. Walijitahidi kutafakari kila tukio na makosa ya wanajumuiya kwao yalikuwa ni makosa yenye heri. Waliamini kwamba uhai wa jumuiya yao ulikuwa unasimama juu ya matukio, yawe ya watu binafsi, ya jumuia nzima, ya taifa au ya dunia nzima. Na kwao kila tukio; baya au zuri ni sherehe!

Mtu akikosa uaminifu kwenye ndoa yake,  badala ya kumhukumu na kumlaani, wanampongeza kwa kuwasaidia kuonyesha mapungu yaliyo kwenye Jumuiya yao. Hawakai wakatulia mpaka watafute chanzo cha mtu huyo kuisaliti ndoa yake. Hatimaye, wanagundua kwamba wote wanashiriki kosa hilo; hivyo kwa pamoja wanatafuta njia za kuisaidia ndoa hiyo. Wakifanikiwa; wanasherehekea na kufanya ibada ya kumtukuza Muumba wao. Mfumo huu wa kuyashangilia makosa na kuyatumia kujisahihisha, kuchukuliana, kuvumiliana, kukamilishana na kupiga hatua kwa pamoja ndani ya jumuiya ya watu wenye mapungu yanayokamilishana kujenga kitu imara zaidi ulitumika kwa makosa yote yaliyokuwa yakijitokeza kwenye jumuiya yao; kutowajibika, udanganyifu, ubinafsi, uchoyo, ubaguzi, upendeleo nk.

Si lengo langu kuelezea kwa kirefu juu ya theolojia hii ya kuchukuliana, kusameheana, kuvumiliana na kukamilishana, bali ni kutaka kuona kama sisi watanzania tunaweza kujifunza kitu kutokana na theolojia hii ya Kosa lenye heri? Je tunaweza kuyatumia makosa yanayojitokeza kwenye taifa letu, kugundua kasoro tulizonazo kama taifa? Je makosa haya hayatokani na mazingira ambayo kila Mtanzania anayachangia?

Ingawa binafsi siamini kama Bunge letu lina “Vurugu”, au hata kama vurugu hizi zipo ni makosa, ninalazimika kulijadili hili maana watu wanataka kulipotosha. Wasomi, wanaharakati na viongozi wastaafu kama vile Waziri Mkuu Mstaafu Jaji Warioba, wamesikika wakilalamika kwamba Bunge letu la sasa lina vurugu na wanataka hatua za haraka zichukuliwe kurudisha heshima za  Bunge letu. Vurugu hizi ni ile hali iliyojitokeza ya Wabunge wa Upinzani kuhoji mambo mbali mbali na Spika kuonyesha wazi upendeleo wa chama chake na kupelekea malumbano na mivutano hadi baadhi ya wabunge wa upinzani kufukuzwa kwenye vikao vya Bunge.

Tumesikia wengine wakilalamika kwamba walifukuzwa bungeni kwa kosa la kuwasha taa za vipaza sauti bila kuruhusiwa na kubishana na kiti. Wabunge kusinzia Bungeni, viti vya Bunge kuwa wazi na hoja nyingi kupitishwa kwa “Ndiyo” mamoja na kasoro nyingi zinazojitokeza kwenye hoja hizo, si makosa na wala hakuna mtu anapiga kelele juu ya kasoro hizi.

Sina uhakika Kanuni za Bunge zinasema nini juu ya idadi ya wabunge inayohitajika ili kikao kiendelee. Tunashuhudia viti vingi bungeni vikiwa wazi; au Mbunge akisha orodhesha jina lake asubuhi, hata asipoendelea na vikao vyote, akaingia mitaani kula nyama choma, kufanya shughuli nyingine za kutumwa na Spika au kujituma yeye mwenyewe anahesabika yuko Bungeni? Posho inaingia mfukoni na wananchi wanajisikia kuwakilishwa? Maamuzi muhimu yanapopitishwa bila Mbunge huyo kuwepo au kura ndiyo na siyo zinapopigwa  na kupitisha maamuzi muhimu, wananchi wa jimbo lake wanakuwa wamewakilishwa kiasi  gani? Kama kuna “Vurugu” ndani ya Bunge letu, ni wabunge kutohudhuria vikao vya Bunge. Kama kuna “Vurugu” ndani ya Bunge letu ni wabunge kupitisha hoja kwa ushabiki wa vyama vyao vya siasa bila kuzingatia maslahi ya taifa  zima la Tanzania. Na hayo ndiyo ya kulalamikiwa!

Lakini kwa vile msemo wetu wa Kiswahili unasema kwamba wengi wape, basi tulijadili hili la Wabunge wa upinzani kubishana na Kiti, na Kiti kuonyesha upendeleo wa wazi wazi kwa chama kinachotawala kama Kosa lenye heri.

Sote tuna vibanzi. Kila mtu kwa nafasi yake. Tusiwanyoshee wabunge kidole wala kuwalaumu. Tunapenda sana kulaumu. Ni watanzania wangapi wangefanya kinyume kama wangepata nafasi ya kutuwakilisha Bungeni? Ni wangapi wangeongea bila woga wa kupoteza viti vyao? Bila woga wa kupokonywa nafasi zao za kugombea kupitia vyama vyao vya siasa? Ni watanzania wangapi wanayatanguliza maslahi ya taifa mbele? Kama ni kila mtu kujihoji, kama ni kila Mtanzania kujipima, kasoro ni nyingi. Kasoro ni nyingi na makosa ni mengi. Labda  tungeliangalia kosa la wabunge kwa namna tofauti. Mtizamo ambao ni tofauti kabisa na kulaumiana na kunyosheana kidole. Kuna kitu kinaitwa kosa lenye heri. Hili ni kosa ambalo kutokana nalo watu wanajifunza, watu wanajisahihisha na kupiga hatua kubwa katika shughuli zao kinyume na kabla ya kosa kutendeka. Ukweli ni kwamba, kosa linapotendeka, ni kwamba kunakuwa na kasoro fulani katika jamii husika. Hivyo kosa hilo linasaidia kufichua mengi. Yaliyofichika yakifichuliwa, na kama hayo yaliyofichika ni mabaya, basi hekima inaongoza na njia pya zinatafutwa, na jamii inasonga mbele kwa kujiamini zaidi. Ndio hapo, kosa linageuka kuwa lenye heri. Kwa maana kwamba bila kosa hilo, labda hatua nzuri zaidi isingefikiwa.

Hii haina maana kwamba walichokifanya wabunge ni kizuri au haina maana kwamba mimi ninawatetea. Kama ni kuwatetea mimi ningekuwa mtu wa mwisho! Maana yake ni kwamba wametufumbua macho. Wametusaidia kuziona kasoro zilizokuwa zimefichika. Watu walihisi tu, lakini sasa wameona kwa uwazi zaidi kwamba Spika wa Bunge kutoka kwenye chama tawala au chama cha siasa si vizuri.

Hili la wabunge ni tatizo kama yalivyo matatizo mengine makubwa katika jamii yetu. Mfano wale wanaowapora maiti wakati wa ajali katika barabara zetu, wengine wanaiba nyaya za umeme na transfoma, wengine wanahujumu TTCL, wengine wanachimbua mabomba ya maji na kuharibu mtandao wa maji, wengine wanaiba alama za barabarani kwa kutumia vyuma kutengeneza nondo za madirisha na majiko ya mkaa, wengine wanakata misitu kiasi tabia nchi inabadilika, wengine wanapora raslimali bila kuangalia mahitaji ya kizazi kijacho, wengine ni majambazi wanaiba na wakati mwingine kutoa roho za watu. Ni matatizo mengi!

Sote tuna vibanzi! Unyonge wa wabunge  hauna tofauti na unyonge wa watanzania walio wengi. La msingi ni je, tunajifunza nini kutokana na unyonge wetu? Ukiona mtu anakata tawi la mti alilolikalia, ujue mtu huyo ana matatizo makubwa na anahitaji msaada. Ukiona mtu anabomoa nyumba yake ya kuishi, anatoa milango anauza, anatoa madirisha anauza, ujue mtu huyo ana matatizo makubwa na anahitaji msaada.

Kama kweli sote tuna vibanzi, ni lazima tujenge jamii inayojifunza na kupiga hatua kutokana na matukio mbali mbali. Na kawaida jamii iliyo hai ni ile inayokua na kuendelea kusonga mbele kutokana na matukio mbali mbali. Ni ukomavu wa tukio baada ya tukio. Ni lazima tujenge jamii inayotafakari na si jamii ya kulalamika kila wakati.

Je, ni kweli wabunge wetu wanafahamu kazi yao? Na je, wananchi wanafahamu kazi za mbunge? Je, wanawahitaji wabunge? Kwamba tuwe na wabunge, ulikuwa ni uamuzi wa wananchi? Kama kuna waliowafanyia uamuzi kwa vile ndio kwanza tulikuwa tunajitawala, sasa inawezekana wananchi wakapata nafasi ya kutoa maoni yao juu ya Bunge? Au juu ya kuwa na wabunge na wabunge wa aina gani? Wa kujitegemea au wakutoka kwenye vyama? Mbunge ni wa kupika pilau na kugawa kanga au ni mwakilishi wa wananchi katika Bunge? Dhana nzima ya uwakilishi inaeleweka vizuri? Je, watanzania walipewa nafasi ya kuamua ni jinsi gani wangependa kuwakilishwa? Mifumo yote tuliyonayo imejadiliwa na nani? Maana kama watu wangepewa nafasi ya kutoa maoni juu ya mifumo mbali mbali, isingewezekana wakakubali kupokea pombe, kanga na pesa kutoka kwa mbunge. Wao ndio wana shida, wanataka kumtuma mwakilishi Bungeni, badala yao kupokea kanga, sukari na pesa kutoka kwa Mbunge, wao wangekuwa wanatoa sukari, kanga na pesa kwa mbunge, ili akubali kuwawakilisha.

Hivyo hili la wabunge ni lazima kuliangalia kwa upana wake. Si jambo la kufanyia mzaa na si jambo la kupuuzwa. Bunge ndicho chombo cha kutunga sheria. Bunge, Serikali na Mahakama, nchi inasimama. Kama Bunge halina   uwezo wa kuyaangalia matatizo ya nchi hii na kuyatafutia ufumbuzi , basi kuna tatizo kubwa katika jamii yetu, kuna tatizo kubwa ambalo kama tukibweteka, litatutafuna sisi na vizazi vijavyo.

Kosa lenye heri limeweka mbele yetu ukweli kwamba hapa Tanzania, chama ni kikubwa kuliko Bunge, chama ni kikubwa kuliko serikali. Tumejifunza kwamba wabunge wa chama tawala wanatanguliza chama chao kabla ya kuangalia na kuwakilisha matatizo na hoja za wananchi waliowapigia kura. Je, hii ndio misingi ya demokrasia na utawala bora? Ni lazima kuendelea na mfumo huu ambao unakitukuza chama kuliko hata Katiba ya nchi? Tujifunze na  kuchukua hatua.

Tukianza mchakato wa kutengeneza katiba mpya ni lazima Kosa lenye heri litatuongoza: Tutahakikisha Katiba yetu inatamka wazi wazi bila utata wowote nafasi ya Bunge, nafasi ya vyama vya siasa na nafasi ya serikali. Tutahakikisha Katiba inatamka wazi bila utatata wowote juu ya nani awe Spika wa Bunge letu; Kwamba asitoke kwenye vyama vya siasa: awe Mtanzania msomi, mwadilifu, mzalendo, mwenye hekima, mwenye msimamo, anayeongozwa  na kanuni za Bunge, sheria na kuiheshimu Katiba ya nchi.

Ndio maana hoja ninayoijenga leo hii ni kwamba yale tunayoyaona kama “Vurugu” Bungeni,  tuyachukulie kama “Kosa” lenye heri. Yatusaidie kugundua kasoro tulizonazo kwenye taifa letu, kujisahihishe, tuchukuliane, tuvumiliane na kukamilishana. Tanzania ni yetu sote!

Na,
Padri Privatus Karugendo.


0 comments:

Post a Comment