TAMASHA LA KUMI LA JINSIA: MAFANIKIO NA CHANGAMOTO.


Tamasha la kumi la Jinsia, lililofunguliwa tarehe 13.9.2011 na kufungwa tarehe 16.9.2011 kwenye viwanja vya TGNP- Mabibo Dar-es-Salaam, limefanikiwa kwa kiasi kikubwa likiwa limeibua changamoto nyingi pia. Tofauti na matamasha mengine yaliyotangulia; tamasha hili lilikuwa ni la kumi na limefanyika wakati tunasherehekea miaka hamsini ya uhuru wetu. Hivyo lilikuwa tamasha la kipekee.

Upekee wa tamasha hili haukujikita tu katika kusherehekea miaka kumi ya tamasha na miaka hamsini ya uhuru wa taifa letu, bali hata muundo wake ulikuwa wa kipekee: Tumezoea kuwa na wageni rasmi kwenye sherehe zetu, na mara zote wageni hawa ni viongozi wa serikali, viongozi wa kidini na viongozi wa mashirika. Tamasha la mwaka huu, wageni rasmi walikuwa ni wananchi kutoka pembezoni. Wanawake na wanaume kutoka pembezoni, kutoka vijijini ndio walikuwa wageni rasmi. Hawa ndio walioikalia meza kuu, hawa ndio walionekana na kusikika kwenye vyombo vya habari. Sauti zao zilisikika na kutoa ushuhuda kwamba Tamasha la jinsia ni Jukwaa huru la kila mtu hata na wale  walio pembezoni ambao sauti zao hazisikiki katika mfumo wetu uliozoeleka. Sauti za wanawake wanaoteswa na kunyanyaswa na kunyima fursa ya kumiliki rasilimali za taifa lao, sauti za wafanyakazi wa majumbani, sauti za wananchi wanaoporwa ardhi yao, kilio cha watanzania cha kutaka katiba mpya, sauti ya mashoga wanaotaka haki zao za msingi ziingizwe kwenye katiba. Kuzipatia nafasi sauti za wale walio pembezoni ni mafanikio makubwa ya Tamasha la kumi la jinsia.

Mada kuu ya mwaka huu ilikuwa ni “ Ardhi, nguvu kazi na Maisha endelevu”, na mchokoza mada hii alikuwa ni Profesa Dzodzi Tsikata kutoka Chuo Kikuu cha Ghana, huyu ni mwanaharakati na mtetezi wa haki ardhi wa siku nyingi. Akichokoza mada hii iliyogusa hisia ya washiriki wote na kuibua tatizo sugu la watanzania, alisema
 “ Haijalishi unaongelea ukiwa ncha ipi ya kidunia, iwe ni kaskazini au kusini mwa dunia, wale ambao mtaji wao ni guvu kazi ndio wanaoathirika zaidi kwa kuiishi katika hali duni ambayo imekuwa sehemu ya maisha yao. Wakati ambapo wamiliki wa mitaji mikubwa wamepata ulinzi wa dhamana za mikopo ya kibenki na vyombo vingine vya kifedha, wafanyakazi wamekosa uhakika wa ajira endelevu, kukosa ajira zenye hadhi, na kupoteza makazi hifadhi ya jamii ya kudumu. Kiwango cha tatizo hili kwa ujumla wake kinahatarisha maendeleo na demokrasia iliyopo”

Tatizo sugu la watanzania lililojitokeza kwa nguvu kubwa kwenye tamasha hili na kuonyesha wazi dalili za vurugu na machafuko siku za mbeleni kama hekima, busara na uzalendo vitaendelea kuwa mbali na watanzania ni Ardhi na uwekezaji wa kigeni unaokuja kwa kasi ya kutisha. Kilio cha uporaji wa ardhi kililitawala jukwaa la jinsia. Mchokoza mada, Profesa Dzodzi Tsikata, alisema
“ Changamoto kubwa inayowakabili wanawake katika ngazi ya jamii kote, mijini na vijijini, ni kutokuwa na uhakika wa kufikia rasilimali muhimu kama vile ardhi, kunyonywa na kunyanyaswa katika mahusiano ya ajira, mitaji na teknolojia ili kufanikisha ndoto yao ya kuishi maisha bora. Changamoto nyingine zinahusiana na sera za kiuchumi ambazo haziwasaidii, sera dhaifu za –kijamii, na kukosekana kwa jitihada madhubuti katika kushughulikia athari za maisha duni. Changamoto hizi zinafanya harakati za mapambano haya kuwa ngumu na hivyo kuendelea kufukarisha wananchi kizazi hata kizazi”.

Ujumbe mzito ulitolewa na wanawake kutoka Loliondo:
 “ Ardhi ni uhai. Wanatufukuza kwenye ardhi yetu,  tutawazalia wapi watoto wetu? Hatuondoki kwenye ardhi yetu liwalo na liwe” walisema akinamama hawa kutoka Loliondo. Ushuhuda wa Loliondo unatia simanzi na kuzua maswali juu ya nia ya serikali yetu; ukitilia maanani kwamba pamoja na unyama uliofanyika kule Loliondo, ardhi iliyoporwa na wawekezaji ina bango linaoonyesha kwamba ardhi hiyo ni mali ya watu wengine na ni kama nchi ndani ya nchi

“Hadi leo hii zimeundwa zaidi ya tume 13 kushughulikia swala la Loliondo, la kushangaza ni kwamba tume zote hizi haziweki ripoti zake wazi. Anayepewa ripoti ni mwekezaji, lakini wananchi wanaachwa gizani. Serikali inawalinda na kuwatetea wawekezaji na kuwatelekeza wananchi wake” Alisema mama kutoka Loliondo

Inasikitisha tunapoelekea kusherehekea miaka hamsini ya uhuru wetu, watu bado wananyanyaswa kwenye ardhi yao. Mapendekezo ya wanawake wa Loliondo  ni kwamba wakati umefika wa kuhakikishiwa usalama wao na kulindwa na serikali yao, washirikishwe katika kuandika katiba mpya, wapewe fursa ya kuitumia ardhi kwa maisha yao ya kila siku, maana bila ardhi hakuna maisha; na kwamba anapokuja mwekezaji aje kwa unyenyekevu mkubwa, maana ardhi ni yao, akija kwa mabavu wako tayari kupambana naye, maana sasa wamechoka. Hawataki kuwa wakimbizi kwenye ardhi yao.

Martha Sumaye kutoka mkoani Manyara alieleza kwamba:  “Hivi sasa kuna wanawake wanaoishi porini baada ya kuamua kuandamana kushinikiza wakulima kutoka   katika eneo la ziwa Basutu. wakulima wamevamia eneo la wafugaji na  viongozi wa serikali wamekaa kimya juu ya mgogoro huo ambao unawaathiri zaidi kina mama na watoto kwani hivi sasa hawana sehemu ya kuchota maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani”

Emmiliana Kimaro, alielezea jinsi wanakijiji wanaoishi katika Msitu wa West Kilimanjaro  eneo la   Ngaranairobi Kata ya Nduma, walivyotolewa kwenye maeneo yao na ardhi hiyo akapewa mwekezaji  “Kitendo kilichofanywa na serikali kuchukua eneo la msitu huo wakati ndani yake kulikuwa na wakazi wa kudumu bila kuwatafutia njia mbadala ya kuwahamishia wanakijiji hao, ni ukatili uliovuka mipaka”. Alisema bi Kimaro na kuongeza
“Serikali ilitangaza kuwa wanakijiji wa Ngaranairobi tumepatiwa ardhi ni uongo,  waliomilikishwa ardhi na serikali ni wanakijiji wa Ngurushani, na wengi wao ni wazee na ardhi waliyokabidhiwa ni vipande vidogo. Naongea kwa masikitiko pia naomba mtandao huu unilinde kwani kufichua siri iliyofichwa na serikali kwa muda lolote laweza kutokea hata hivyo ukweli utabaki pale pale lazima kilio chetu jamii ikifahamu” alisisitiza Bi Kimaro.

Ushuhuda kutoka Morogoro ni kwamba Serikali inapora ardhi na kuwagawia wakoloni! Na kwamba sasa hivi ardhi imegeuka kuwa biashara kama ilivyo biashara ya nguo au biashara nyingineyo. Sehemu za Mikese- Morogoro, ardhi imemegwa na wananchi wamefukuzwa kwenye makao yao ili ardhi hiyo agawiwe Mwekezaji.

Aidha Anna Louchiro kutoka Kilosa alieleza kuwa ni dhahiri watendaji wa serikali walio wengi wamekuwa mstari wa mbele katika kutumia vibaya madaraka waliyopewa na hivyo kusababisha migogoro mingi ya ardhi nchini.

Ushuhuda kutoka Ruvuma, ni kwamba watu wanarubuniwa kutoa ardhi yao bure, kumbe baadaye serikali inaiuza ardhi hiyo kwa bei kubwa.

Alex Japhet kutoka Ruvuma alieleza kwamba sheria za ardhi ni dhaifu na hazina meno na hivyo kuitaka serikali kuziboresha na kuzisimamia ipasavyo kwa maslahi ya Watanzania wote.

Ushuhuda kutoka Mwanza, ni kwamba ili kupata kiwanja mjini ni lazima kulipia fomu kwa shilingi 50 elfu, na viwanja vyenyewe bei yake ni milioni tatu, tano hadi kumi. Swali ni je mtu wa kawaida anaweza kupata  kiwanja? Au viwanja ni kwa ajili ya watu wenye fedha?

Margerth Ogongo, mwanaharakati kutoka Zimbabwe, alielezea mapambano ya ardhi yanayoendelea Zimbabwe na kuelezea jinsi walowezi walivyonunua ardhi kwa pesa kidogo, walinunua eka moja kwa shilingi moja. Kwa njia hii waliweza kujilimbikizia ardhi. Baada ya makubaliano ya kugawana ardhi kwa njia ya amani kushindikana, walowezi walikataa kupunguza ardhi yao kuwapatia wananchi, matokeo yake ni kwamba wananchi walikasirika na kuamua kuyavamia mashamba ya walowezi. Alitoa ushauri wa wanawake wa Tanzania kusimama kidete kutetea ardhi, maana ni haki ya kila mtu kuwa na ardhi, ili alime na kupata chakula na ili ardhi hiyo iyalinde na kuyatunza maisha yake.

Ujumbe uliojitokeza kwenye mada hii ni kwamba wananchi wamechoshwa na uporwaji wa ardhi unaoendelea na sasa hivi wako tayari kwa lolote. Kama serikali haisikilizi na wabunge wanakwenda kulala Bungeni, basi wananchi watahakikisha wanailinda ardhi yao kwa gharama yoyote ile.

Ajira majumbani ilijitokeza kuwa ni changamoto kwa washiriki wa tamasha la kumi; hoja iliyojitokeza ni kwamba kazi za nyumbani si mbaya, tatizo linalojitokeza ni kuwanyanyasa mabinti wanaoajiriwa kufanya kazi za nyumbani, kuwalipa fedha kidogo na kuwaajiri watoto wadogo ambao hawana uzoefu wa kazi za nyumbani, kama kutunza nyumba, kuwalea watoto na shughuli nyingine za siku kwa siku ndani ya familia.

Michango ya mawazo kutoka kwa washiriki ni kwamba wasichana wanaofanya kazi za ndani wanatendewa mambo mabaya na wakati mwingine wanabakwa na kuambukizwa virusi vya UKIMWI. Bwana Masege Mandoma, kutoka shirika la KIVULINI la Mwanza, alitoa ushuhuda kwamba watoto wa kike wanaletwa Mwanza kufanya kazi za ndani na mawakala. Ni kwamba mawakala hawa wanapanga na wazazi wao kwamba mshahara wote utakuwa unatumwa nyumbani. Matokeo yake watoto hawa wanafanya kazi bila malipo. Pamoja na mateso yote wanayokubana nayo kwenye kazi za majumbani, hawapati chochote zaidi ya kupigwa, kulala njaa, kufanya kazi masaa mengi bila kupumzika na wakati mwingine kufanyiwa vitendo vya kudhalilishwa. Kuna ushahidi wa binti wa miaka kumi na miwili aliyepachikwa mimba wakati akifanya kazi majumbani.

Prisca Haule kutoka Ruvuma, alitoa ushuhuda wa zaidi ya watoto wa kike 50 kuuzwa Msumbiji, ambako pamoja na kazi za majumbani wanafanya kazi ya kupigwa picha za uchi. Serikali inafahamu mtandao huu wa watu wanaowanunua watoto hawa kwa shilingi elfu hamsini kila kichwa, lakini hakuna linalofanyika kukomesha biashara hii haramu.

Pia kuna ushuhuda uliotolewa kwamba wanawake wanaofanya biashara ya kuwakusanya watoto wa kike kutoka mikoani na kuwaleta kuwauza Dar-es-Salaam, ili wafanye kazi za ndani, kuuza kwenye baa na kufanya bishara ya ngono wanafahamika, lakini serikali haichukui hatua ya kukomesha biashara hiyo.

Changamoto iliyojitokeza ni kwamba hata baadhi ya washiriki wa  tamasha wanawatumikisha watoto wa kike kwenye familia zao. Na mbaya zaidi ni kwamba wazazi wanashirikiana na mawakala kuwauza watoto wao. Hii ni changamoto kubwa kwa wanaharakati ambao wanajiweka mstari wa mbele kutetea haki za binadamu na kupinga ajira kwa watoto, lakini bado wao wanafanya hivyo.

Nini kifanyike kuzuia unyanyasaji huu: Msemaji kutoka Msumbiji, alitoa mfano wa nchi yake, kwamba wao wameamua kuanzisha harakati za kumkomboa mtoto wa kike kwa kumpatia elimu. Wana msemo: “Kumwelimisha mtoto wa kike ni kulielimisha taifa zima” Hata wale ambao hawafanikiwi kusoma hadi vyuoni, wanawekwa kwenye makundi na kupatiwa mafunzo ya kutetea haki zao. Anasema mfumo huu umeanza kupunguza wimbi la wasichana wanaofanya kazi majumbani na unyanyasaji umepungua, maana hata kama  msichana akifanya kazi za ndani anakuwa anafahamu kazi zake vizuri na kutambua haki zake.

Imependekezwa kwamba Tanzania, ni nchi tajiri, hivyo itoe elimu bure kwa wasichana. Lakini pia na wazazi wabadilike, waache tabia ya kuwauza watoto wao. Wavumilie maisha magumu na wasiwatumie watoto wao kama mitaji. Na wanaharakati wabadilike, wasiwatumikishe watoto wadogo. Wale wenye watumishi wa ndani wasiwanyanyase: Ushauri ni kwamba “Mabadiliko yanaanza na mimi ndio yanaenda kwa wengine”

Changamoto nyingine iliyojitokeza kwenye Jukwaa la jinsia, ni kitendawili cha uchumi wetu kukua kwa kasi wakati na umasikini ukiongezeka kwa kasi ya kutisha. Kigoda Cha Mwalimu, waliandaa takwimu na kuelezea kitendawili hiki: Wakati dhahabu inachangia asilimia 36 kwa mauzo ya nje, inachangia asilimia 3 tu kwa pato la taifa. Mauzo ya dhahabu, fedha hazirudi ndani ya nchi ili kuendeleza mzunguko wa fedha, bali zinawekwa kwenye mabenki ya nje na sheria inaruhusu! Na hili ndilo litakalotokea kwenye uwekezaji wa kilimo unaokuja kwa kasi. Watalima si kwa kuwalisha watanzania au kukuza uchumi wa Tanzania, bali watalima kuzalisha chakula cha kuuza nje na fedha hizo zitawekwa kwenye mabenki ya nje.

Swala jingine lililojitokeza kwa nguvu zote kwenye tamasha ni Katiba. Mchangiaji Magdalena Rwebangila alisisitiza kwama maswala ya ardhi na mengine yote yanayoleta duku duku kwa wananchi yaingizwe kwenye katiba. Naye Bwana Deus Kibamba alitaadharisha “ Sasa hivi tuko kwenye wakati mgumu: Maana dola inawalinda na kuwakingia kifua wale wenye fedha na wawekezaji badala ya kuwalinda kuwakingia kifua wananchi wa pembenzoni. Na hii ni hatari kubwa tunapotaka kuandika katiba mpya. Hivyo kuna haja ya kudai kwa nguvu zote kuingia kwenye mchakato wa katiba”

Mecy, kutoa Kenya, alitoa ushuhuda wake kwamba Kenya iliwachukua zaidi ya miaka 25 kutengeneza katiba mpya.
“ Pamoja na juhudi zote hizo, machafuko ya 2007, yalichangia kuharakisha upatikanaji wa katiba mpya. Siwaombei watanzania kufika huko” Alisema bi Mercy na kuongeza “ Jambo la kujivunia ni kwamba katiba ya sasa ya Kenya, imezingatia haki za wanawake. Mafanikio hayo yalitokana na wanawake kushinikiza kwa nguvu zote kushiriki mchakato mzima wa kuandika katiba mpya”.
Ushauri wake ni kwamba mtandao ndio unasaidia harakati za kuunda katiba mpya, maana mtu mmoja mmoja, au taasisi moja, au vyama vya siasa na  madhehebu ya dini haviwezi kujitosheleza kutengeneza katiba mpya, ni lazima kuwepo na mtandao na watanzania wasichoke kuendelea kudai katiba mpya, na kwamba elimu ya urai itasaidia sana kuchochea madai ya katiba.

Vicensia Shule, mhadhiri kijana kutoka Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam alichangia mada ya katiba kwa hisia kali:
 “ Tunasherehekea miaka hamsini ya uongo, miaka hamsini ya kudanganywa, miaka hamsini ya kudharauliwa. Kwa vile tumepumbazwa kwa miaka mingi wanaotusikia tunaongea juu katiba, wanatukejeli kwamba tunataka kuingiza kila kitu kwenye katiba”.
Kwa maoni yake ni kwamba kwa vile mfumo uliotufikisha hapa ulikuwa unatufundisha uongo na kutudanganya, ulikuwa ni mfumo wa kutugawanya kiasi cha kunyosheana kidole na kubaguana kwa rangi zetu, dini zetu, uwezo wetu na makundi yetu, ni lazima sasa tukae chini, tujadiliane,  na kukubaliana ni kitu gani tunataka.

Mashoga nao walitoa maoni yao na kutaka haki zao ziingizwe kwenye katiba mpya. Hapana shaka kwamba Jukwaa la mwaka huu limefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuibua sauti za wananchi walio pembezoni.

Na,
Padri Privatus Karugendo.
 

0 comments:

Post a Comment