KILIO CHA TAIFA LETU; NANI WA KUTUVUSHA?

Kuna uvumi kwamba mapacha watatu; Lowassa, Rostam na Chenge, wamejipanga vizuri kutumia kila njia kujisafisha; kosa la mwenyekiti wa CCM kushindwa kuwafukuza na kuwaachia uhuru wa kupima wenyewe na kuondoka; umekuwa ni wakati mzuri kwao kufanya mbinu za kujisafisha; wana fedha za kufanya hivyo na wana watu wengi nyuma yao ( Watu ni fedha, maana watanzania tunanunuliwa kama bidhaa mnadani – mwenye fedha nyingi ni lazima awe na watu wengi nyuma yake) wanaamini ni haki yako kujisafisha maana ndani ya CCM kuna wachafu zaidi yao. Inawezekana kabisa kwamba hoja hii ya Kikwete kuandaa watu wake ambao wametajwa tajwa kama vile Asha-Rose na Hussein Mwinyi; ambao wote ni waisalimu, ni ya kutungwa kwa lengo la kumchafua Kikwete; hoja ihame kutoka kwa mapacha watatu na kuanzisha mjadala mpya wa Waislamu kupokezana vijiti. Na kete hii imsaidie Lowasa ( ambaye ni Mkrisut-Mlutheri) kusafishwa na hatimaye kutimiza ndoto zake za muda mrefu za kuingia Ikulu. Lakini pia yawezekana ni kweli kwamba Mheshimiwa Rais wetu ana mpango huo wa kuhakikisha kiti chake kinakaliwa na mtu atakayemhakikishia usalama wakati wa kustaafu kwake. Yote yanawezekana maana “uchu” wa madaraka katika taifa letu ni mkubwa kuliko “uchu” wa maendeleo ya wananchi.

Hata hivyo Kikwete, amwandae nani ndani ya chama chake cha CCM? Waliomsaidia yeye kuingia madarakani, walitegemea angewaachia nao wakale “Utamu”, lakini dalili zinaonyesha wazi kwamba amewazidi kete; walifikiri wako njia moja kumbe walikuwa njia mbili tofauti. Walifikiri wanaijenga Tanzania yenye umoja na mshikamano; kumbe mwenzao alikuwa na agenda nyingine. Hakuna mashaka na utendaji kazi wa Lowassa. Hakuna mashaka na uwezo wa Lowassa kuiongoza au kuitawala nchi; huyu ni mtu makini na mwanasiasa kweli kweli; ana wafuasi wengi ndani ya chama na mashabiki wa kutosha nje ya chama. Pamoja na tuhuma zote alizonazo leo hii ukiitisha uchaguzi wa aina yoyote ile ndani ya chama, Lowassa ataibuka mshindi, ndo maana wengine wanafikiri labda anataka kufanya ya Zuma!;  tatizo lake kubwa ni kujiingiza kwenye mnyororo wa uporaji wa mali ya umma; kashfa kama ile ya Richmond na utajiri mkubwa usiokuwa na uwiano na kipato cha mtumishi wa umma unautia doa uzalendo wake. Ni nani ndani ya CCM anaweza kusimama na kumnyoshea mwenzake kidole? Majina yote tunayoyajua na kuyasikia kila wakati yamechafuka! Nani ndani ya CCM ameshinda uchaguzi bila kutumia fedha? Ni nani kiongozi wa CCM anaishi maisha ya kawaida ya wananchi kama viongozi wale wa enzi za Mwalimu?

Nafikiri tatizo kubwa ambalo ni lazima sote tulifanyie kazi ni: Nani atalivusha taifa letu kutoka hapa lilipo? Hiki ndicho kilio kikubwa cha Taifa letu! Ni mtu gani huyu atakayeweza kulirudisha taifa letu katika njia sahihi aliyoiandaa Mwalimu Nyerere? Taifa letu likawa juu ya “Udini”, taifa letu likawa juu ya ukabila na ukanda? Serikali yetu ikawa ya wakulima na wafanyakazi badala ya hali ya sasa hivi ya kutekwa na wafanyabiashara na wenye fedha? Ni mtu gani atakayevunja utamaduni huu kwamba ni lazima Tanzania iongozwe na chama kimoja cha siasa (CCM). Ni mtu gani huyu atakaye vunja utamaduni huu uliyojengeka wa kushughulikia mchakato wa kuingia madarakani badala ya kushughulikia mchakato wa kuleta maendeleo? Tumemaliza uchaguzi mkuu mwaka jana, leo hii watu wameanza mchakato wa madaraka; badala ya kukazania mchakato wa kuleta maendeleo; nguvu zote zinaelekezwa kwenye mbio za kutafuta madaraka. Fedha zinatafutwa kwa nguvu zote kwa lengo la kufanikisha mchakato huu na hiki ndicho chanzo cha mikataba mibovu na fedha chafu na haramu zinazoingizwa kwenye taifa letu.

Sasa hivi makundi yanajengwa na fedha zinatafutwa. Wanaoutaka ubunge wanaanza kujiandaa, wanaoutaka Urais wanaanza kujiandaa. Fitina zinaanza, chuki na wakati mwingine hata maisha ya watu kupotea. Maana hawa wanaotafuta fedha nyingi, wako tayari hata kujiingiza kwenye madawa ya kulevya. Kuna ushahidi wa kutosha kwamba Tanzania ni njia ya kupitishia madawa ya kulevya. Kuingilia mtandao huu wa madawa ya kulevya kwa lengo la kuusimamisha ni kutafuta kifo kama ilivyotokea kwa Amina Chifupa. Wanaofanya biashara hii wanajulikana, lakini hawakamatiki? Rais Kikwete, alitwambia kwamba ana orodha ya majina yote ya mtandao huu wa kuuza madawa ya kulevya, lakini hadi leo hii orodha hiyo haijawekwa wazi. Mtandao huo unaendelea na fedha hizo chafu zinawaingiza watu madarakani.

Ni mtu gani atavunja utamaduni uliojengeka wa kutumia fedha kuingia madarakani? Mtu akachaguliwa kwa uwezo wake na uzalendo wake? Tumejenga utamaduni kwamba wananchi hawawezi kujichagulia mwakilishi wao kwa uhuru bila kununuliwa.

Hili ndio tatizo letu kubwa na hiki ndicho kilio cha taifa letu la Tanzania. Tunaongozwa na fedha badala ya kuongozwa na fikira! Tumepotea njia, tuko gizani na tunahitaji mwanga mpya! Na mwanga huu si kazi ya mtu mmoja. Kikwete peke yake hawezi kuleta mwanga huu, CCM na ukongwe wake haiwezi kuleta mwanga huu peke yake na wala vyama vya upinzani peke yake haviwezi kuleta mwanga huu. Mwanga mpya katika taifa letu la Tanzania ni mradi wa pamoja. Ndo maana watanzania wanataka kuwa na Katiba mpya. Katiba itakayo weka msingi na kuhakikisha Taifa letu linakuwa juu ya “Udini” juu ya Ukabila na Ukanda. Katiba itakayo hakikisha Taifa letu linaongozwa kwa misingi ya  Sheria. Katiba itakayohakikisha kwamba hata mbinu zikifanyika za kumwingiza “zuzu” madarakani. “Zuzu” huyo atabanwa na kuongozwa na Katiba.

Kama tungekuwa na katiba imara isiyokuwa bubu kwa baadhi ya mambo ya msingi kwa nini tuwe na wasi wasi kwamba Kikwete, ana njama za kumwachia Urais Mwislamu mwenzake? Katiba mpya itatusaidia kuondoa fikra potovu kwamba kuna watu waliozaliwa kutawala; Tanzania ina watu zaidi ya milioni 40; miongoni mwao hao watu wengi mmoja tu anaweza kuwa Rais wa nchi kwa kipindi Fulani. Na mtu huyo hakuzaliwa kutawala bali anachaguliwa kufuatana na uwezo wake wa kuongoza na uzalendo wake kwa nchi yake.

Hivyo kazi kubwa iliyo mbele yetu si kulalamika kwamba Kikwete, anawaandaa watu wake. Ni kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha tunakuwa na Katiba mpya kabla ya uchaguzi mkuu wa 2015. Nguvu na fedha ambazo mapacha watatu wanatumia kujisafisha, wazitumie kuhakikisha mchakato wa Katiba mpya unakwenda vizuri. Tutapata mwanga mpya katika taifa letu, tukipata Katiba mpya! Wa kulivusha taifa letu hapa lilipo si mwingine bali ni katiba mpya. Wakumaliza kilio cha watanzania si mwingine bali ni Katiba mpya!

Na,
Padri Privatus Karugendo.


 0 comments:

Post a Comment