MWANA MAMA

TATU ABDI JUMA.

Katika safu yetu ya Mwana Mama, leo tunakuletea Tatu Abdi Juma, kutoka Lushoto Tanga. Mama huyu mwenye umri wa miaka 49 alishika nafasi ya tatu katika shindano la Mama shujaa wa Chakula 2012. Yeye ni mkulima na mfugaji. Ana shamba lenye ekari sita, ana ng’ombe 4, kondoo 8 na kuku 20.

Mashindano ya Mama shujaa wa chakula, yameanza kuwaibua wanawake wanaofanya mambo makubwa lakini walikuwa hawajulikani. Ndo maana tunapendekeza mashindano haya yaendelee na yaungwe mkono na wale wote wanaotetea haki za wanawake na kutamani kuona wanawake wanamiliki mali nakutoa mchango katika kuliendeleza taifa letu la Tanzania. Kuna walioanza kuyabeza mashindano haya, lakini sasa inaelekea walikuwa wakijidanganya. Ukweli unajionyeshana sisi sote ni mashuhuda wa ukweli huu. Tulikuwa tunabaki kuimba wimbo wa wanawake wanaweza, wakati kuna wanawake wanaoitekeleza kaulimbiu hii kwa vitendo. Hivyo wale wote wanaotetea haki za wanawake wangebuni mbinu za kuwaibua wanawake hawa na kuacha maneno matupu.Hapana shaka kwamba baada ya mashindano ya mama shujaa wa chakula, kuna mashirika na makampuni yatakayokuwa yameguswa na maisha na jitihada za Tatu Abdi Juma na kutaka kumpatia mtaji zaidi. Na kwa njia hii wanawake wengine watanufaika. Bila shindano hili, mama huyu asingefahamika na juhudi zake zingebaki kijijini kwake na ndani ya familia yake.

Vijijini kuna wanawake wengi kama Tatu Abdi Juma. Wanalima, wanafuga na kufanya miradi mingine ya maendeleo, tatizo ni kwamba hawana masoko ya uhakika wa kuuza mazao yao na bidhaa nyinginezo wanazozizalisha. Ni kazi ya serikali kuliona hili na kulishughulikia. Badala ya kuendelea kuimba wimbo ule ule tuliouzoea wa “Wanawake wanaweza”, zibuniwe mbinu za kuwatafutia wanawake hawa masoko ya uhakika.

Tatu Abdi Juma, analima kilimo cha kisasa, alipata mafunzo kwenye chuo cha Kilimo na mifugo Tengeru na pia alisaidiwa na shirika Oxfam kupata ujuzi zaidi. Analima kilimo cha kumwagilia. Katika shamba lake ana uwezo wa kuvuna majunia 20 ya mahindi kutoka kwenye heka moja. Analima pia viazi mviringo na maharagwe. Kwa vile anafuga kisasa, ana uwezo wa kupata lita 200 za maziwa.

Mama huyu ni mjane na mfano wa kuigwa kwa wanawake wa Lushoto na Tanzania nzima. Kufuatana na utamaduni wa wilaya ya Lushoto, kama ilivyo kwa tamaduni nyingi za Tanzania, ardhi ni mali ya wanaume. Kule Lushoto, wanaitia Shamba la mzee. Na tamaduni za kule mwanaume anakuwa na wanawake wengi zaidi ya watatu. Ni nadra sana kijana mwenye umri wa miaka 30 kuwa na mwanamke mmoja.

Tatu aliolewa akiwa na umri wa miaka 20, kama mke wa pili. Kwa maoni yake mwenyewe ni kwamba wanawake wanatumika kama jembe au trekita la kulimia na kuzalisha mali. Hivyo alitumia muda mwingi akilima kwenye shamba la mme wake. Kwa vile alikuwa kwenye ndoa ya wake wengi, maisha yake yalikuwa magumu pale mme wake alipofariki.

Ndugu na jamaa wa mme wake walimfukuza kwenye ardhi aliyokuwa akilima na kuzalisha chakula. Alinyang’anywa mifugo yake na fedha zake zaidi ya shilingi 600,000. Kwa vile yeye ni mama shujaa, alipambana kupitia serikali za mitaa na hatimaye alifanikiwa kupata nusu ya arithi ya mme wake na kuendeleza kilimo na ufugaji.

Alijiunga kwenye vikundi vya wanawake na kufanikiwa kupata mikopo ya fedha na mifugo. Mafanikio yake ya leo yanatokana na juhudi ya kufanya kazi na kupambana na maisha bila kutegemea msaada na kuomba omba.

Tanzania tuna kasumba ya kufikiri kwamba ili tuendelee ni lazima tupate misaada kutoka nchi za nje. Ukweli ni kwamba tuna utajiri mkubwa. Kinachohitajika ni kufanya kazi na kutengenezewa mifumo mizuri ya kupata mitaji na soko la uhakika.

Na jambo la msingi ni kuhakikisha kila mwananchi ana haki ya kumiliki ardhi. Tunasema kwamba kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania. Hivyo bila watu kumiliki ardhi ni vigumu kilimo kikawa uti wa mgongo. Tumeona mfano mzuri wa mama huyu ambaye kwa kutumia ardhi ameweza kuendesha maisha yake. Ilivyowezekana kwa mama huyu inawezekana pia kwa kila Mtanzania.

Changamoto anayoipata mama huyu ni kutokuwa na vifaa vya kilimo vya kisasa na magomvi ya wakulima na wafugaji. Haya ni matatizo sugu ya Tanzania. Watanzania wengi wanaendesha kilimo cha jembe la mkono na wakulima na wafugaji wamekuwa na migogoro ya ardhi. Wakati wakulima wanahitaji ardhi kulima mazao wafugaji wanahitaji ardhi kutunza mifugo yao.

Tunachojifunza hapa ni kwamba ni muhimu kuwa na sheria inayoruhusu wanawake kumiliki ardhi; kwa vile ndoa za wanawake wengi ni sehemu ya utamaduni wa Mtanzania, basi iwepo sheria ya kuhakikisha kila mwanamke anapata haki katika ndoa yake na hasa haki ya kumiliki ardhi. Jambo la pili tunalojifunza ni kwamba ili kuzalisha na kupata faida kubwa ni lazima kutumia vifaa vya kisasa. Hivyo ni wajibu wa serikali kuwawezesha wakulima kupata vifaa vya kisasa. Tusiendelee kuimba wimbo wa kilimo kwanza, bila kufanya jitihada za kukiendeleza kilimo. Jambo la tatu ni kwamba ili kuondoa migogoro ya wakulima na wafugani ni lazima kupanga vizuri matumizi ya ardhi yetu: Na mipango hii isiwe na upendeleo wa upande wowote. Jambo la tatu la kujifunza ni kwamba kule vijijini wako wanawake wengi kama huyu Mama Tatu, tatizo ni kwamba hawasiki! Hivyo tuwaibue, ili tukomeshe utamaduni wa kulalamika na kuimba nyimbo za wanawake wanaweza!

Na,

Padri Privarus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment