RWANDA, WAMETHUBUTU,
WAMEWEZA NA WANAENDELEA KUSONGA MBELE.
Siku za hivi karibuni
hapa kwetu Tanzania tumekuwa na kauli mbiu ya tumethubutu, tumeweza na
tunaendelea kusonga mbele. Ni kauli mbiu ya kutia moyo na yenye ushawishi mkubwa wa ndani na nje
kuonyesha kwamba kama taifa huru tumepiga hatua kubwa. Ni wazi yamefanyika
mengi na mengine yalikufa mapema hata kabla ya kuzaa matunda mengi; siasa ya
ujamaa na kujitegemea, mashirika ya umma, viwanda, usafiri wa anga na wa reli,
lugha yetu ya Kiswahili na mambo mengine mengi aliyokuwa ameyaanzisha Marehemu
Mwalimu Nyerere. Hivyo kusonga kwetu mbele ni jambo linalotia shaka. Wakati
mwingine ni vigumu kuangalia kwa macho na kuyaona yale tuliyoyafanya miaka hamsini
ya uhuru wetu. Si lengo la makala hii kusema kwamba hatujafanya kitu, swali ni
je tunaweza kutembea kifua mbele kwa kauli mbiu hii?
Tunaposema tumethubutu,
tumeweza na tunaendelea kusonga mbele, hatuna viwanda vya kuonyesha kwamba hivi
ni viwanda vyetu, hatuna ndege za kuonyesha kwamba hili ni shirika letu la
ndege, hatuna hospitali nzuri za kuwatibu viongozi wetu, wakiugua
tunawakimbiza Uingereza na India, la
kushangaza zaidi hatuna hata na lugha yetu! Miaka hamsini ya Chuo Kikuu cha
Dar-es-Salaam hotuba zote hata na msherekeshaji walitumia lugha ya kigeni.
Tunaweza vipi kusema tunasonga mbele wakati kwa miaka hamsini wasomi wetu wameshindwa kuiendeleza na
kuisimika lugha yetu ya Kiswahili kuwa na uwezo wa kuelezea mambo yote ya
kimataifa, ya kisiasa, kiuchumi, kisayansi nk. Kwa nini tuendelee kuamini
kwamba tunapotumia lugha ya kigeni tunaeleweka zaidi ndani na je ya nchi yetu?
Kwa nini tuendelee kuamini kwamba lugha za kigeni ndio “Usomi”? Huko ni kusonga
mbele? Au ni kurudi nyuma kwenye ukoloni na utumwa wa kifikira?
Katika makala iliyopita
nilidokeza kwamba Rwanda, wamethubutu, wameweza na wanaendelea kusonga mbele.
Wakati sisi tunaiimba kauli mbiu hii kwa mbwe mbwe zote, wenzetu wa Rwanda
wanaitekeleza kauli mbiu hii kwa vitendo. Safari yetu ya kwenda Kigali, mimi na
Mama Eva Kihwele Mwingizi, tulioiwakilisha TARAFA katika sherehe za kumkumbuka
Marehemu Mwalimu Nyerere, tulipanda Ndege ya Shirika la Ndege la Rwanda
(RwandAir). Shirika hili lenye ndege za kisasa, linafanya safari zake nchini
Rwanda, Bujumbura, Dar-es-Salaam, Arusha, Nairobi, Mombasa, Johannesburg,
Libreville, Brazzaville, Dubai na kwa kushirikiana na mashirika mengine
linafanya safari za London, Amsterdam na Guang Zhou. Tulifurahi kusafiri na
shirika hili na kukubali kwamba Rwanda, wamethubutu, wameweza na wanaendelea
kusonga mbele. Wakati sisi shirika letu la Ndege haliwezi hata kufanya safari
za ndani, Wanyarwanda wanakata anga kuelekea mashariki ya mbali na Ulaya.
Jambo la pili
lililoyavutia macho yetu na kutusukuma kukubali kwa kauli moja kwamba Rwanda
wamethubutu, wameweza na wanaendelea kusonga mbele ni usafi na mpangilio wa
Jiji la Kigali. Jiji hili ni safi na limepangiliwa vizuri. Mwaka wa 2008,
shirika la umoja wa mataifa la makazi, lilipatia Kigali tuzo ya kuwa miongoni
mwa majiji safi Afrika. Mkuu wa wilaya ya Muleba Bi Angelina Mabula,
tuliyeungana naye Kigali kusherehekea kumbukumbu ya kifo cha Mwalimu Nyerere,
kwa kushangaa usafi wa jiji la Kigali alisema
“ Kigali ni safi kiasi kwamba hata na miti inaogopa kudondosha majani”.
Si kwamba miti inaogopa kudondosha majani, bali kuna watu wanalisafisha Jiji la
Kigali usiku na mchana. Mbali na usafi, Kigali ni jiji lenye ndoto za
kutokomeza rushwa, uhalifu, utapiamlo na migogoro ya kiutawala.
Jambo la tatu la
kujifunza ni Rwanda kufanikiwa kuwashirikisha vijana na wanawake kati uongozi
wa nchi. Wakuu wa wilaya, wakuu wa mikoa, mawaziri, wabunge na maseneta umri
wao ni kati ya miaka 30 hadi 45. Wazee wanabaki kuwa washauri, lakini uongozi
wa nchi unakuwa mikononi mwa vijana wenye uwezo wa kukimbia mchakamchaka.
Kufuatana na yale tuliyoyaona na kuyashuhudia, vijana wameisaidia Rwanda kupata maendeleo ya kasi.
Jambo la nne la
kujifunza ni kwamba Kiongozi wao Rais Paul Kagame, ana vision, analipenda taifa
lake, anawapenda watu wake na hana uswahiba . Hana cha ndugu wala mwenzetu.
Yeye anafuata utendaji wa kazi. Watumishi wote wa umma wana mkataba wa kila
mwaka na rais wao. Mwaka unapoanza kila mtumishi anaorodhesha vipaumbele vyake
vya mwaka huo na kufunga mkataba na rais. Mwaka unapokwisha, kuna tathimini, na
nguzo kuu nne za tathimini ni uchumi, utawala bora, huduma za -kijamii na haki,
yule anayepata alama chini ya hamsini basi huyo anakuwa amejifukuza kazi.
Anayevuka juu ya hamsini na kufanya vizuri zaidi anapata zawadi na cheti cha
ushindi na wakati mwingine anapandishwa cheo.
Kutokuwa na uswahiba kumemsaidia Rais
Kagame, kulishughulikia kwa ujasiri mkubwa suala la ardhi. Wale
waliokuwa wamejilimbikizia ardhi kubwa aliwanyang’anya na kuigawa ardhi kwa
Wanyarwanda waliokuwa hawana hata kipande cha ardhi. Ni wazi baadhi ya viongozi
wa Rwanda, hawakupendezwa na hatua hiyo, waliamua kuikimbia Rwanda na kueneza
uongo dunia nzima kwamba Rais Kagame ni dikteta. Kwa upande mwingine, kitendo
hiki cha kuigawa ardhi bila kuangalia cheo cha mtu, bila kufuata uswahiba na bila kufuata undugu kiliongeza sifa
na upendo wa Wanyarwanda kwa Rais Kagame.
Leo hii Tanzania tuna
migogoro mikubwa ya ardhi. Baadhi ya viongozi wameteka ardhi kubwa na wengine
wanapora ardhi ya wananchi. Kuna haja ya kwenda Rwanda kujifunza jinsi
walivyoitanzua migogoro ya ardhi maana
kusema kweli kwa suala hili la ardhi, wamethubutu, wameweza na wanaendelea
kusonga mbele. Kwa kifupi ni kwamba sisi watanzania tuna mambo mengi ya kujifunza
kutoa Rwanda:
Tulipokutana na Waziri
wa Serikali za mitaa Mheshimiwa James Musoni alitwambiwa “ Kufikia Desemba
mwaka huu hakuna Mnyarwanda atakayekuwa akilala kwenye nyumba ya nyasi.
Wanyarwanda wote watakuwa na nyumba nzuri za kisasa zilizoezekwa kwa mabati na
vigae. Hayo ndiyo malengo tuliyojiwekea na kuingia mkataba na Rais wetu.
Yasipotimia, basi mimi na wote walio chini yangu ni lazima tuwajibike kwa
kuacha kazi. Hata hivyo nina imani tutafanikiwa maana tumepiga hatua kubwa”.
Mheshimiwa Musoni aliendelea kutuelezea kwamba “ serikali ikisaidiana na
mashirika yasiyokuwa kiserikali, inahakikisha kwamba kufikia mwaka kesho, kila
Mnyarwanda awe na godoro”. Na kuongezea kwamba “Familia ambazo ni masikini
serikali inazipatia Ng’ombe mmoja wa maziwa ili waweze kuinua kipato na
kuboresha lishe ndani ya kaya. Soko la maziwa liko mlangoni mwa kila kaya,
maana gari la kusomba maziwa linazunguka kila siku kupita kwenye kaya zenye
maziwa”.
Mheshimiwa James Musoni,
alituelezea sheria iliyotushangaza sote ya maji ya mvua: “ tumetunga sheria ya maji ya mvua. Hakuna mtu
anayeruhusiwa kuyaachia maji ya mvua kwenye paa la nyumba yake kutiririka
kwenda kwa jirani yake au barabarani. Kila mtu ni lazima kuhakikisha anayavuna
maji kwenye paa lake ili kuepusha kuleta maafa kwa jirani au mafuriko.
Anayeshindwa kufanya hivyo anawajibishwa kisheria”. Sheria hii ingekuja hapa
Dar-es-Salaam, labda adha ya mafuriko mvua zinaponyesha ingepungua.
Mikutano tuliyoifanya na
wakuu wa wilaya, wakuu wa mikoa na kuongea na watu mbali mbali, tumeambiwa na
kuona wenyewe kwamba Rwanda inapiga hatua kubwa katika maendeleo. Barabara
nyingi zimetengenezwa kwa kiwango cha lami, majengo yamejengwa kwa mpangilio
mijini na vijijini, usafi unazingatiwa mijini, vijijini, barabarani hadi kwenye
kaya. Mazingira yametunzwa kwa kupanda miti na maua. Wanyarwanda wanaweza
kusimama kifua mbele na kusema: Tumethubutu, tumeweza na tunaendelea kusonga
mbele:
Rwanda wameweza
kuzalisha chakula cha kutosha na kubakiza ziada ya kuuza nje. Hii ina maana
wameweza kupambana na janga la njaa ambalo lilikuwa likiisumbua nchi hii kwa
miaka mingi. Wameweza kuwatunza na kuwalinda watoto yatima na wajane,
wamefanikiwa kusimamisha utawala wa sheria na kuiletea nchi yao amani na
utulivu. GDP ya Rwanda inakuwa kwa asilimia saba kila mwaka, na kufikia mwaka
huu kipato cha Mnyarwanda kwa mwaka ni zaidi ya dola 500. Kwa sababu ya amani
na utulivu watalii wameendelea kuja Rwanda, mwaka wa 2010 kiasi cha watalii
666,000 walikuja Rwanda na kuingizia nchi hiyo kiasi cha dola za marekani
milioni 200. Kuna chanzo kingine cha mapato, ambacho sisi kwetu Tanzania
hatujakirasimisha na hadi leo hii hatujui kinaingiza kiasi gani. Wanyarwanda
wanaoishi nje ya Rwanda wanaingiza zaidi ya dola milioni 200 kila mwaka.
Mwaka 2003, Wanyarwanda
waliokuwa wakipata huduma ya maji safi na salama walikuwa asilimia 41, mwaka
huu Wanyarwanda asilimia 80 wanapata maji safi na salama. Mwaka 2000, ni kaya
asilimia 4 ndio zilikuwa na huduma ya umeme, kufikia mwaka huu asilimia 13 ya
kaya zinapata huduma ya umeme.
Chini ya uongozi wa Rais
Kagame, Rwanda imejenga hospitali nzuri na zenye huduma bora. Tuliambiwa kwamba
hata yeye Rais Kagame na viongozi wengine wa kitaifa wanatibiwa kwenye
hospitali hizo. Ni tofauti kabisa na kwetu Tanzania, ambapo hata kama viongozi
wetu wanaumwa mafua wanakimbizwa Uingereza na India. Mwaka 2003 asilia 7 ya
Wanyarwanda ndio walikuwa na bima ya afya, lakini leo hii asilimia 96 ya
Wanyarwanda wana bima ya afya. Mwaka
2000, asilimia 40.6 ya Wanyarwanda walikufa kwa ugonjwa wa malaria, idadi hii
imepungua kufikia asilimia 16 mwaka wa
2009.
Chini ya uongozi wa Rais
Kagame, Rwanda imeweza kujenga shule nyingi na kuziboresha. Tuliambiwa kwamba
hata watoto wa Rais Kagame na viongozi
wengine wa kitaifa, watoto wao wanasoma kwenye shule hizo. Watoto wote wa
Rwanda wanamaliza miaka tisa ya elimu ya msingi. Mpango wa kompyuta kwa kila
mwanafunzi umefanikiwa kiasi kikubwa. Hadi mwanzoni mwa mwaka huu zaidi ya
“laptops” 57,387 zimesambazwa kwenye shule 113 nchi nzima. Vyuo vikuu navyo
vimeongezeka, leo hii Rwanda ina wanafunzi 62,734 kwenye vyuo vikuu idadi
ambayo ni mara 17 ya ile ya mwaka 1993 kabla ya mauaji ya kimbali. Asilimia 44
ya wanafunzi wa vyuo vikuu ni wasichana.
Rwanda hawachangii arusi
kama tunavyofanya hapa Tanzania. Wao wanachangia elimu na miradi ya maendeleo.
Gharama za sherehe za arusi inabaki kuwa ni shughuli ya mtu binafsi; ndugu na
jamaa wanaalikwa, lakini wanajinunulia kinywaji chao na kushiriki na ndugu yao
furaha ya siku kwa gharama ndogo bila kujiingiza kuchangishana mamilioni ya
fedha kama tufanyavyo sisi kwenye vikao vya arusi. Hili nalo ni la kujifunza kutoka Rwanda, maana fedha
tunazochangishana kwenye vikao vya arusi tukiziweka kwenye elimu na miradi ya
maendeleo, tunaweza kusimama kifua mbele na kusema; tumethubutu tumeweza na
tunaendelea kusonga mbele vinginevyo kauli mbiu hii tuwaachie wenyewe!
Na,
Padri Privatus
Karugendo.
0 comments:
Post a Comment