ASKOFU MWOLEKA

KUMBUKUMBU HII YA MARAEHEMU ASKOFU MWOLEKA

ILITOKA KWENYE GAZETI LA RAI 2005.


Tarehe 16 za mwezi huu itatimia miaka mitatu ya kifo
cha Askofu Christopher Mwoleka, aliyekuwa Askofu wa
Jimbo Katoliki la Rulenge. Ninakumbuka niliandika
makala ya kumbukumbu ya mwaka mmoja wa kifo chake na
mwaka jana niliandika kumbukumbu ya miaka miwili, sasa
ninaandika ya miaka mitatu, nitaendelea kuandika na
kuandika juu yake kama Mungu, atanijalia kuishi zaidi
maana kuna mengi ya kuandika juu Marehemu Askofu
Christopher Mwoleka, ama niseme yanaandikwa mengi juu
yake. Ukiingia kwenye mtandao ukaandika Mwoleka,
utashangaa utakayosoma juu yake. Yanaandikwa na watu
wa nje na kusomwa na watu nje! Ni ule msemo wa Nabii
hasifiki kwao, au ni uvivu wetu wa kutotaka kuandika
na kusoma?

Mwaka jana nilielezea jinsi Mwoleka alivyokuwa na
mipango ya kuwajengea nyumba bora watu wote katika
Jimbo lake. Jinsi alivyoanzisha kikundi cha ujenzi na
jitihada zake za kutengeneza chokaa na sementi. Bahati
mbaya kikundi hiki cha ujenzi sasa kimesambaratika na
kujiunga kwenye mnyororo wa mambo mengi ya Mwoleka,
yaliyosambaratika baada ya kifo chake.

Kuna watu walionitumia maoni yao baada ya kuisoma
makala hiyo na kusema kwamba Mwoleka, alikuwa na ndoto
zisizo tekelezeka. Mfano kuwajengea watu wote nyumba
bora zilikuwa ni ndoto. Ndio hivyo kila mtu ana ndoto
zake. Wengine wana ndoto za kuwa marais, wengine wana
ndoto za madaraka makubwa, za utajiri nk. Yeye
Mwoleka, alikuwa na ndoto za kuwahudumia watu! Ni
ndoto ambazo kesho na kesho kutwa haziwezi kuleta
vurugu na kuisambaratisha jamii yetu kama zilivyo
ndoto za urais, madaraka makubwa na utajiri wa
kupindukia.

Kwa vile ni miaka mitatu baada ya kifo chake, basi leo
nitaongelea “Utatu”. Namba tatu ilikuwa ni ya muhimu
sana kwake. Alipenda “Utatu”. Theolojia yake ilikuwa ya
Utatu Mtakatifu. Nembo yake ya Uaskofu ilikuwa na
maneno “Ili wawe na Umoja”. Haya ni maneno ya Yesu,
yakitaja umoja wa Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu
roho Mtakatifu. Pia ni maneno yanayoelezea umoja
katika tofauti. Kwamba Baba, mwana na roho mtakatifu ni
tofauti, lakini wanaungana na kuwa kitu kimoja, kwa
vile kila nafsi inaifahamu nyingine vizuri na
kuikubali na kuungana. Kwamba tofauti badala ya
kutenganisha zinaunganisha kama zinavyounganika chanya
na hasi na kutoa kitu ambacho si chanya na wala si
hasi!

Pete ya kiaskofu ya Marehemu Askofu Christopher
Mwoleka, iliyochongwa na Mmakonde, ilikuwa na alama
tatu za umoja. Pete hii ilikuwa ikiwashangaza wengi,
si kwa alama hizi za umoja, bali kwa vile ilikuwa
imechongwa kwa mti badala ya dhahabu, shaba au vito
vingine vya thamani. Kwa mtu mwenye kutafakari na
kuzama katika maisha ya kiroho, pete hii ilikuwa ni
ishara na mwanga wa kufahamu Mwoleka. Pete, ilikuwa
ni ya mti, nyumba yake ya kawaida kabisa, alishiriki
maisha ya kila siku ya watu; kwenda shambani, mtoni,
kujenga nyumba nk, aliishi maisha ya watu na
kuchanganyika nao “Ili wawe na umoja”.

Kama kuna kitu kilicho utafuna muda wa Marehemu Askofu
Christopher Mwoleka, nguvu na akili zake zote ni
kujenga uhusiano wa mtu na mtu. Aliamini kanisa kwamba
jambo hili huwezi kulifanya ukiwa ofisini au kwa
kuhubiri kanisani. Ili kujenga uhusiano wa mtu na mtu,
ni lazima mtu kushiriki kikamilifu kwa matendo.
Aliacha kazi zote za ofisini, aliyahama makao yake ya
kiaskofu na kuishi kwenye mazingira ambayo
yangemruhusu kuhusiana na watu kwa karibu, aliacha
kwenda kwenye mikutano ya kila mara ya maaskofu,
akaweka nguvu zake zote katika kujenga uhusiano wa mtu
na mtu. Alitamani kujenga jumuiya ambayo ingeweza
kuishi maisha ya “utatu”. Uhusiano wa Mungu Baba na
Mungu Mwana, uhusiano wa Mungu Mwana na Roho
Mtakatifu, uongoze mahusiano ya watu.

Mwoleka, aliamini kwamba mtu akifanikiwa kujenga
jumuiya yenye kuishi utatu. Jumuiya ambayo uhusiano wa
mtu na mtu unatangulia kila kitu, mambo mengine ya
kutafuta mali, sheria, kanuni nk. yanajileta yenyewe.

Wanateolojia wenye upeo mfupi, ambao hawazami kwa
undani kwenye maisha kiroho, ambao wanafanya na
kufuata kila kitu kama mashini hawakukubaliana naye.
Hata leo hii bado wanalaumu jinsi Mwoleka
alivyoendesha mambo vibaya, ambavyo hakufuata sheria,
utaratibu, kanuni nk. katika jimbo lake. Wanashindwa
kumwangalia Mwoleka, katia mwanga wa maisha ya kiroho.
Wanashindwa kufahamu kwamba huyu ni mtu aliyekuwa
amezama katika maisha ya kiroho na kutaka kuikomboa
roho kwanza, ili roho iusukume mwili kufanya kazi.
Wanashindwa kufahamu kwamba huyu ni mtu ambaye
hakuambatana na mali, madaraka au uhondo wa dunia hii,
aliambatana na Ufalme wa Mungu. Alitamani Mbingu,
kuliko chochote kile. Aliamini kwamba mfumo wa
uhusiano wa mtu na mtu ukiwa mzuri, watu wakaishi
“utatu” wakawa na “Umoja”, basi Mbingu ni hapa
duniani.

Wanateolojia wanaotafuta umaarufu, wanaotafuta
madaraka, wanaoitanguliza nafsi yao kabla ya wengine,
wanaoangalia udhaifu wa wengine, kabla ya kuangalia
udhaifu wao wenyewe, wasingekubaliana na Mwoleka. Na
haishangazi kwamba hadi leo bado hawakubaliani naye na
wala hawaandiki chochote juu yake. Ukweli ulivyo, hata
wanateolojia wakikaa kimya, miti na mawe vitasimama na
kuandika juu ya Mwoleka!

Wale waliopata bahati ya kuishi naye kwa karibu,
wanafahamu alivyokuwa mtu wa kutafakari, mtu wa sala,
mtu wa kujitesa, mtu wa kupambana na nafsi yake na
mchapa kazi. Alikuwa akisoma vitabu na kuandika usiku
kucha. Kilicho msumbua sana ni uhusiano wa mtu na mtu.
Aliamini kwamba dawa ya matatizo yote ya dunia hii ni
kuunda mfumo utakaoongoza mahusiano mazuri kati ya mtu
na mtu.

Ndiyo maana alielewana na Marehemu Mwalimu Nyerere na
siasa yake ya Ujamaa na Kujitegemea. Wakati maaskofu
wa kanisa Katoliki walikuwa na mashaka na dukuduku juu
ya Ujamaa na Kujitegemea yeye alikuwa ni Askofu wa
kwanza kuishi kwenye kijiji cha ujamaa. Aliona siasa
ya Ujamaa ikilenga katika kujenga uhusiano kati ya mtu
na mtu na kuleta umoja na kushirikiana.

Ndiyo maana alielewana kwa haraka na Jumuiya ya
Integration ya Ujerumani iliyomfanya akutane na
kufahamiana kwa karibu na Kardinali Ratzinger, ambaye
sasa ni Papa Benedict wa kuminasita. Malengo ya
jumuiya hii ambayo ipo hapa Tanzania, ni kushughulikia
uhusiano wa mtu na mtu. Ni jumuiya ya pekee
ninayoifahamu inayofanya jambo hili. Si kwamba jumuiya
hii haizalishi mali na kujishughulisha na mambo
mengine ya kidunia. Ina miradi mingi, lakini uhai wa
jumuiya hii ni uhusiano wa mtu na mtu na mtu na Mungu.
Ni jumuiya yenye wanateolojia waliozama kabisa katika
maisha ya kiroho, wanaofanya kazi usiku na mchana
kuhakikisha maisha yanakuwa na maana na yanakwenda kwa
kuufuata mpango wa Mungu wa maisha ya “Utatu”, maisha
ya umoja. Mfano mzuri ni jitihada za Jumuiya hizi za
kujenga tena uhusiano mzuri kati ya Wajerumani na
Waisraeli. Wameweza kuianzisha jumuiya yao kule
Israeli na kuwafanya wanateolojia wa Ujerumani na
Israeli kukaa pamoja na kujadiliana. Askofu Mwoleka,
alikuwa mshirika mkubwa katika majadiliano haya.

Kati ya jitihada za Marehemu Askaofu Mwoleka za
kujenga uhusiano kati ya mtu na mtu ninayakumbuka
mafungo niliyoyafanya naye pamoja na ndugu yangu Padri
Didas Kasusura. Tulifanya mafungo ya siku 14. Tulikuwa
watatu. Hatukuwa na kiongozi wa mafungo. Tulijiongoza
wenyewe. Mafungo haya tuliyafanyia nchini Rwanda,
kwenye sehemu za Ruhegeri – Remela Ruhondo. Tulibeba
vitabu, tukavisoma na kutafakari. Mada yetu kuu
ilikuwa ni juu ya uhusiano wa mtu na mtu. Baada ya
kutafakari na kusali kwa siku hizo 14, tulipata wazo
la “Ndoa Nyoyo”.
Kwamba ili uhusiano wa mtu na mtu uwe na maana, uzae
natunda, ulete amani, uvunjilie mbali wivu na
mashindano, ujenge upendo wa kweli na kuaminiana na
kuchukuliana ni lazima watu wafunge “Ndoa Nyoyo”
kwanza.

Maana yake ni nini? Tulikuwa na mawazo kwamba ndoa
tulizozizoea ambazo tulizipatia jina la “Ndoa Miili”,
ni kwamba watu wawili wa jinsia tofauti wanafunga ndoa
kwa kuvutiwa na maumbile ya nje na kwa kiasi kidogo
maumbile ya ndani. Mara nyingi maumbile ya ndani
hayavutii na kukubalika. Kama ni wema, haki, huruma
yanavutia, lakini kama ni wivu, uchoyo, uongo na
udhaifu mwingine hayakubaliki. Hata wale walio kwenye
ndoa zetu za kawaida “Ndoa Miili” wakigundua
yasiyovutia ndoa inakuwa mashakani.

“Ndoa nyonyo” ni kumpenda na kuungana na mtu si kwa
kuvutiwa na sura au maumbile ya nje, bali ni kuvutiwa
na ya ndani yote, mema na mabaya. “Ndoa nyoyo” si
lazima iwe ya jinsia tofauti. Inawezekana kabisa ikawa
ya jinsia mmoja. Hana ni lazima kuwa mwangalifu maana
sasa hivi vichwa vya watu vimechanganyikiwa na wimbi
la ushoga na usagaji. Niko mbali na haya ingawa pia si
busara kuyatupa kando na kufumba macho, kumbe yapo
mbele yetu. “Ndoa nyoyo” ni kumpokea mtu jinsi alivyo
na kumkubali. Ni watu wawili kufunuliana nyoyo zao na
kila mmoja akajiweka mikononi mwa mwenzake bila
kuficha lolote. Ni mfano wa mtoto mikononi mwa mama
yake. “Ndoa Nyoyo” ni kama uhusiano uliopo kati ya
Mungu Baba, Mungu Mwana Na Mungu Roho Mtakatifu. Nafsi
tatu zilizoungana kutengeneza kitu kimoja. Ni nafsi
tatu lakini Mungu ni mmoja. Maisha ya Utatu
Mtakatifu.

Wazo hili la “Ndoa Nyoyo” lilikuwa wazi kwetu
watatu;Mwoleka, Didas na mimi. Huu ulikuwa muujiza
mkubwa maana baada ya mazungumzo na majadiliano marefu
tulijikuta tunania pamoja. Baada ya mafungo yetu
tulijawa na hamasa ya kulifundisha wazo hili kwa ndugu
zetu tuliokuwa tukiishi nao katika Jumuiya ya
Mkamilishano. Jumuiya aliyokuwa ameianzisha Marehemu
Askofu Mwoleka, katika jitihada zake za kujenga
uhusiano kati ya mtu na mtu.
Tulifundisha wazo hili kuanzia 1990 hadi 1996
alipostaafu Askofu Mwoleka. Katika kulifundisha wazo
hili, ninaungama wazi kwamba tulifanya makosa ya
kutopima vizuri upeo, uelewa na malezi ya nyuma
waliyokuwa nayo watu tuliokuwa tunaishi nao.
Tulipofundisha “Ndoa nyoyo” wachache walielewa, lakiniwalichanganyikiwa. Wenye nia njema na wenye kutaka
wengi nje na ndani ya Jumuiya ya Mkamilishano

kufahamu waliuliza na kuingia kwenye majadiliano na
Jumuiya ya Mkamilishano. Wenye nia mbaya ambao ni heri
hata kama wasingezaliwa walilipanua jambo hili na
kulipatia picha mbaya. Hali hii ilileta wasiwasi
mkubwa kwenye kanisa Katoliki la Tanzania. Mawazo
yalizagaa kwamba Askofu Mwoleka, anafundisha kinyume
na mafundisho ya kanisa, kwamba hafuati sheria za
kanisa, kwamba anakiuka kanuni na utaratibu. Huu ukawa
mwiba wa kumchoma Mwoleka na kuharakisha kifo chake.

Uvivu wa watanzania, hakuna aliyefanya utafiti
kutafuta ukweli. Wengi, hata na viongozi wa kanisa
wenye akili na uwezo ulio tukuka, waliamini uzushi wa
watu wachache wenye nia na malengo yao binafsi. “Ndoa
Nyoyo” na Jumuiya ya Mkamilishano, kikawa chanzo cha
kufuta historia ya mtu aliyekuwa Askofu wa Jimbo
Katoliki la Rulenge kwa kipindi cha miaka 27 na akiwa
Askofu wa kwanza Mwafrika wa jimbo hilo.

Hata hivyo ukweli utabaki pale pale kwamba huyu
alikuwa ni mtu aliyeishi maisha yake yote akijaribu
kujenga jumuiya inayojali uhusiano kati ya mtu na mtu,
jumuiya inayoishi utatu na kuleta kumoja.

Mtu anaweza kupuuza na kuzibeza jitihada alizozifanya
Marehemu Askofu Christopher Mwoleka, lakini ukweli
utabaki pale pale kwamba ili Kanisa Katoliki liwe na
sura yake, liwe na mvuto ambao umepotea kulingana na
kiliko cha Papa Benedicto wa kuminasita,ni lazima
ziwepo jitihada za wazi za kufufua mfumo wa kujenga na
kuimarisha uhusiano kati ya mtu na mtu, mfumo wa
kujenga na kuimarisha Jumuiya za kuishi “utatu
mtakatifu”, Jumuiya za kujenga umoja: “ Ili wawe na
Umoja”.

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment