PARCED EARTH

UCHAMBUZI HUU WA KITABU CHA PARCHED EARTH ULITOKA KWENYE GAZETI LA RAI 2005.


“PARCHED EARTH”

Nimesoma kitabu! Kama nilivyosema kwenye makala zilizopita, ni kwamba mtu ukisoma kitabu unatamani na wengine wakisome. Ni ugonjwa ule ule wa kutaka kushirikiana na wengine. Mfano anayevuta sigara, hawezi kuvuta bila ya kushirikiana na mvutaji mwenzake. Mtu anayekunywa pombe, hawezi kufurahi bila kushirikiana na mnywaji mwenzake, hivyo hivyo anayesoma vitabu hawezi kufurahi bila kushirikiana na wasomaji wenzake. Ingawa bado kuna ukweli ambao ninashawishika kuukubali kwamba watanzania hatusomi vitabu. Tamasha la vitabu mwezi huu Jijini Dar-es-Salaam, lilipambwa na watoto wa shule, watu wazima walikuwa si wengi. Hivyo bado kuna haja ya mtu anayesoma kitabu chochote kile chenye mafundisho ya kuielimisha jamii yetu kusimama juu ya paa la nyumba na kutangaza kwamba amesoma kitabu!

Kitabu nilichokisoma zamu hii si The Da Vinci Code wala Mwalimu mkuu. Nimesoma “Parched Earth”, riwaya iliyotungwa na Mheshimiwa Mama Elieshi Lema. Ingawa kuna watu wanaobeza umuhimu wa riwaya, ukweli utabaki pale pale kwamba riwaya ni Jukwaa la kufundishia na kuielimisha jamii. Riwaya umekuwa ni mchango mkubwa wa kuharakisha maendeleo katika nchi zote zilizoendelea. Ningekuwa na pesa, ningenunua kitabu hiki cha “Parched Earth” na kukitoa zawadi kwa vijana wote wa Tanzania na hasa wasichana. Kwa vile sina uwezo wa kuwanunulia wasichana wa Tanzania, kitabu hiki, ni bora nisimame juu ya paa la nyumba na kutangaza kwamba nimesoma kitabu ambacho kinafaa kwa vijana wanaoelekea katika kujenga familia na kuijenga nchi yetu ya Tanzania. Nina imani ujumbe huu utafika na wahisani watajitokeza na kununua kitabu hiki na kukisambaza kwa vijana wa taifa hili!

Wakati wa tamasha la vitabu lililofanyika mwezi huu jijini Dar-es-Salaam, nilikutana na Mheshimiwa Mama Elieshi Lema, mwandishi wa kitabu cha “Parched Earth”. Nilimpongeza kwa kazi yake nzuri ya kuielimisha jamii kupitia riwaya ya “Parched Earth”. Nilipendekeza kwake kwamba riwaya hii ingefaa kutumika kwenye sekondari na vyuo. Alinijulisha kwamba inatumika Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam. Lakini kwa maoni yangu ni bora kabisa ingetumika hata sekondari maana riwaya hii imesheheni yale yasiyofundishwa popote, imesheheni yale ambayo kwa kawaida kila mtu anaachiwa kuongelea apendavyo. Wale wanaofanikiwa kuongelea vizuri, wanafanikiwa kuvuka – wenye bahati mbaya wanazama au wanaendelea kuogelea bila kufikia mwisho.

Bahati mbaya wale wanaoogelea hadi mwisho, hawako tayari kuelezea uzoefu wao na kutoa mbinu walizozitumia kufanikiwa. Haitoshi kumwambia mtoto asizini, haitoshi kuwazuia vijana kufanya mapenzi, bila kuwapatia mwongozo na uzoefu wa kupambana na nafsi zao, bila mwongozo wa maisha ya kiroho ya kuweza kuweka kando mvuto wa kimwili na kuangalia ndani ya nafsi ya mtu, heshima ya mtu, furaha ya mtu, mema na mabaya ya mtu. Maana uzuri wa mtu si umbo lake, bali ni yale ya ndani yanayomfanya kuwa mtu, ni matendo yale yanayomtofautisha na wanyama wengine.

Kijana anayekua, anayesoma sekondari au chuo, hawezi kufahamu ukweli huu bila mwongozo, bila kuelekezwa. Ukweli ni kwamba hadi leo hii hapa Tanzania hatuna mwongozo wa vijana kuhusiana na mahusiano ya mtu na mtu, na hasa watu wa jinsia tofauti. Ni lazima kijana apate uzoefu kwa wale walioupitia ujana, ni lazima apate uzoefu kwa wale waliovutiwa na maumbile ya nje wakaishia kuzama badala ya kuongelea na kuvuka. Ni lazima apate uzoefu kwa wale waliovutiwa na maumbile ya nje, lakini wakaenda zaidi ya hapo na kuyatafuta yale ya ndani, na walipoyapata wakayavumilia na kuyapenda sambamba na maumbile ya nje.

Riwaya ya “Parched Earth” inavunja tabia hii ya uchoyo wa mafanikio. Kwa upande mwingine inavunja tabia ya kuyafunika matatizo na kujenga utamaduni wa unafiki. Riwaya hii inaelezea maisha ya msichana Doreen Seko, aliyelelewa kijijini, akapata elimu na kufanikiwa kuwa mwalimu. Doreen, kama walivyo watanzania wengi, anakumbana na changamoto ya mfumo dume na mahusiano ya kimapenzi. Safari ya kimapenzi kuanzia utotoni, utu uzima na hatimaye kumpata mchumba aliyefunga naye ndoa na matatizo yaliyojitokeza kwenye ndoa hadi akawa na mpenzi mwingine nje ya ndoa, ni somo zuri sana kwa vijana wanaoachiwa kuongelea bila mwongozo katika mahusiano ya kimapenzi.

Maisha ya Doreen, yanaonyesha ukweli aliokuwa akiuongelea Marehemu Askofu Christopher Mwoleka, aliyekuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Rulenge (1969-1997) kwamba mwanadamu anaishi kwa kufungua pazia. Kwamba mtu anapofungua pazia la kwanza anafikiri amepata ukweli. Baada ya muda anagundua kwamba mchezo ulio jukwaani si ukweli autafutao. Basi analazimika kufungua pazia jingine, hivyo hivyo baada ya muda analazimika kufungua pazia jingine. Kwa maoni ya marehemu Askofu Mwoleka, ni kwamba mwanadamu anaishi katika mchakato mzima wa kufungua mapazia hadi anapokutana na muumba wake! Mfano mzuri ni maisha ndoa. Mtu anapofunga ndoa, anafikiria amefikia mwisho wa mahusiano, lakini baada ya muda, kama ilivyotokea kwa Doreen, anagundua kwamba kufunga ndoa si mwisho, bali analazimika kufungua pazia jingine katika maisha yake. Maana, unapofunga ndoa, sanasana unakuwa umevutiwa na uzuri wa maumbile ya nje. Yale ya ndani, tabia ya mtu, malengo ya mtu, nia ya mtu kuingia katika maisha ndoa, unakuwa huvifahamu. Wengine wanaoa ili waheshimike katika jamii, wengine wanaoa ili wapate wasaidizi katika nyumba, wengine wanaoa ili kupanua ukoo, hivyo mtoto wa kiume ni muhimu kwao nk.

Doreen, alifunga ndoa na Martin, na walipendana kweli. Lakini kwa vile Doreen, alizaa mtoto msichana na kuchelewa kumzalia Martin, mtoto mvulana, mapenzi yao yalipungua. Mchezo uliokuwa jukwaani haukuwa na mvuto tena kwa Martin! Pazia jingine likafunguliwa kwa Doreen na Martin. Wakati Doreen, alitamani kumpata mtu wa kumpenda, kumkubali na kumjali, mtu aliyeugusa moyo wake, Martin, alitamani kumpata mtu mwenye mvuto, lakini pia wa kumzalia mtoto wa kiume! Doreen, alianza kuonja uchungu wa kuwa kwenye ndoa na Martin, akatafuta mpenzi mwingine nje ya ndoa. Au kwa maneno mengine, mtu wa kumzalia mtoto wa kiume, si mapenzi bali ni kutafuta kitu kwa mtu! Uchungu au upweke wa Doreen, ukazaa uhusiano nje ya ndoa kati yake na mwanamme mwingine aitwaye Joseph. Huyu Joseph, ingawa alikuwa tajiri, aliachwa na mke wake, kwa sababu alishindwa kutambua kwamba alichokihitaji mke wake si mali bali upendo wa kweli.

Changamoto anayoitoa Mama Elieshi Lema, katika riwaya hii ni swali la kawaida: je, Mwanamme anahitaji nini kutoka kwa mwanamke na mwanamke anahitaji nini kutoka mwanamme. Na je ni mazingira gani yanaweza kumfanya mwanamke atambue anachohitaji mwanamme, na ni mazingira gani yanaweza kumfanya mwanamme atambue anachohitaji mwanamke.

Inawezekana hili ni swali la kawaida. Lakini tukiingia kwa undani hili linaweza kuwa swali kubwa ambalo halina jibu katika maisha yetu ya kawaida. Tuna mifano mingi ambapo wa kinamama wanaachwa na mabwana zao kwa vile hawakuzaa watoto wa kiume. Je, hicho ndicho wanaume wakitakacho kwa wanawake? Wapo pia akina mama wanaoachwa kwa vile hawakuzaa. Je wakitakacho wanaume ni watoto tu? Upendo wa mahusiano ni watoto?

Katika riwaya, upendo wa Doreen na Martin, unapungua pale Doreen, anaposhindwa kumzalia Martin, mtoto wa kiume. Inawezekana Martin, alimpenda Doreen, kwa lengo la kumzalia mtoto mvulana? Je, mtoto mvulana ndo angejenga uhusiano wa kweli, uhusiano wa kudumu kati ya Doreen na Martin? Jinsi riwaya inavyokwenda, si mali, kabila wala elimu vinavyosababisha uhusiano mbaya kati ya Doreen na Martin. Doreen ni wa Moshi na Martin ni wa Mbeya, lakini tofauti ya mila na desturi si kikwazo, bali ni pale Doreen anaposhindwa kuzaa mtoto mvulana, kana kwamba tatizo hilo ni la mwanamke peke yake!

Joseph naye ni mtu mwenye pesa nyingi na mali, lakini aliachwa na mke wake. Mwandishi, anaonyesha jinsi Joseph, alivyokuwa akitoa zawadi nyingi kwa mke wake. Lakini mwanamke, hakupenda mali, alipenda kitu kingine, alipokipata nje ya ndoa, alikimbia na kuziacha mali zote nyuma yake!

Somo kubwa katika riwaya ya Parched Earth, ni uhusiano wa Joseph na Doreen. Joseph ndoa yake imevunjika, baada ya mke wake kukimbia. Na Doreen, ana matatizo kwa vile mme wake anapenda nje ya ndoa. Watu hawa wawili wanakutana si kwa kuvutwa na maumbile ya nje. Shida zinawaunganisha. Wanapendana na kufundishana mambo mbali mbali. Mfano Joseph, anamfundisha Doreen, uchoraji. Kwa njia hii wanapata nafasi ya kukaa pamoja na kuongea mambo yaliyo rohoni, wanafunuliana mioyo yao, kwa pamoja wanashirikiana kuufukuza upweke kwenye mioyo yao. Pazia linapofunguliwa, wanatambua kwamba wanaweza kuhusiana, kupendana na kusaidiana bila hata ya kufanya tendo la ndoa! Wanagundua kwamba mvuto wa maumbile ya nje si wa muhimu sana. Ukweli kwamba Doreen, aliweza kumpata mtu wa kumsikiliza na kushirikiana naye yale yaliyo moyoni mwake, ulibadilisha maisha yake. Ukweli huu ulimpatia nguvu za kumvumilia mme wake aliyekuwa anapenda mwanamke mwingine nje ya ndoa. Pia uvumilivu wa Doreen, unayabadilisha maisha ya Martin!

Ujumbe wa Mama Elieshi Lema, katika riwaya hii, kama nilivyoelewa mimi ni kwamba uhusiano wa mtu na mtu, na hasa uhusiano wa mwanamke na mwanamme, si jambo la kuachiwa hivi hivi kila mtu akafanya apendavyo. Ni swala la kiroho linalohitaji mfumo wa kijamii. Si mfumo dume, unaowafanya wanawake kuwa vyombo vya kuzaa watoto wa kiume au kufanya kazi za kumfurahisha mwanaume, bali mfumo unaohimiza uhusiano unaolenga kuunganisha nyoyo za watu zaidi ya kuunganisha miili ya watu!

Mfumo ambao unaweza kusaidia kuwafundisha vijana wetu juu ya uhusiano, juu ya kupenda na kupendwa, juu ya kuoa na kuolewa na juu ya kujenga familia zilizo bora. Vijana wakisoma “Parched Earth”, wakapata nafasi ya kujadiliana na kubadilishana mawazo na kusikiliza uzoefu wa wazee waliowatangulia, inaweza kusaidia kutoa mwanga katika maisha yao.

Mfano, vijana wakiyaangalia maisha ya Doreen, wakalinganisha na maisha yao ya sasa. Wanaweza kugundua uongo ulio katika upendo wa kuvutiwa na mwili, upendo ambao mara nyingi unadumu kwa muda mfupi.

Kwa vyovyote tunataka tusitake, hali ilivyo sasa hivi ni lazima tuwe na vitabu kama hiki cha “Parched Earth”, ni lazima tukae na vijana wetu na kuwaelekeza jinsi ya kuogelea na kuvuka kwa salama. Ni lazima tutoe uzoefu wetu wa mahusiano, uwe uzoefu wa mafanikio au wa kushindwa, lakini ni lazima tutoe uzoefu wetu, ili pale tulipokosea sisi vijana wetu wasikosee. Pale tulipofanya vizuri vijana wetu watuige.

Mama Elieshi Lema, ameonyesha mfano mzuri wa kutuandikia riwaya ya “Parched Earth”. Ni bora kila mzazi angemnunulia mtoto wake kitabu hiki. Kama wazazi hawana nafasi ya kuongea na watoto wao, riwaya hii itaongea badala yao. Si lengo langu kukipigia debe kitabu hiki, bali ni kuupigia debe ujumbe mzito ulio katika riwaya hii iliyotukuka.

Na.
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment