UCHAGUZI NI KITU MUHIMU TUSIUCHEZEE!

MAKALA HII ILICHAPISHWA KWENYE GAZETI LA RAI 2005

UCHAGUZI NI KITU MUHIMU TUSIUCHEZEE!

Kwa mtu yeyote yule anayelitakia mema taifa letu la Tanzania, ni lazima aheshimu zoezi zima la uchaguzi mkuu. Mwenye sifa za kupiga kura ni lazima apige kura kwa uhuru bila kununuliwa na bila vitisho vya aina yoyote ile.

Kupiga au kupigiwa kura ni haki ya kila raia. Humpa fursa mwenye umri wa kuanzia miaka 18 na kuendelea kuwachagua wawakilishi wao katika ngazi mbalimbali. Hii ndio nafasi pekee ambapo watu wanaweza kuamua nani ataliongoza taifa na ni nani atawawakilisha bungeni na katika serikali za mitaa.

Kupiga kura au uchaguzi ni njia ya kuwashirikisha wananchi katika utawala wa nchi. Kuwashirikisha wananchi katika utawala wa nchi ni haki ya kimsingi ambayo imesimikwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Haki hii pia imeainishwa katika Sera na Sheria mbalimbali za nchi. Hili ni jambo ambalo ni lazima liwe wazi kwa kila mwananchi, na kama ikitokea kwamba halifahamiki vizuri, serikali iliyo madarakani, haiwezi kukwepa lawama – na ni lazima iwe agenda ya kwanza ya serikali itakayoingia madarakani.

Ushiriki wa wananchi ni msingi wa demokrasia na utawala bora. Hii ina maana kwamba kila mwananchi ana haki ya kushiriki katika kuamua jinsi gani nchi itawaliwe. Mwananchi ana haki ya kuweza kushiriki ama moja kwa moja au kwa kupitia kwa viongozi waliowachagua. Na kama mwananchi anashiriki kupitia kwa viongozi aliowachagua, ni lazima awachague wale anaoamini kwamba wana uwezo wa kumwakilisha vizuri.

Ushiriki wa moja kwa moja wa mwananchi katika masuala ya utawala unathibitika pale ambapo mwananchi mwenyewe hugombea na kuchaguliwa katika uchaguzi huru na wa haki. Ushiriki usio wa moja kwa moja wa mwananchi huthibitika pale ambapo mwananchi huchagua viongozi wao kuwawakilisha. Hivyo, wanaochaguliwa huwawakilisha wananchi hao katika kutunga sheria na kuandaa bajeti na mambo mengine ya kiutawala.

Hivyo uchaguzi mkuu unaokuja, kuna wananchi watakaoshiriki katika utawala wa nchi yetu kwa kuchaguliwa wao wenyewe na wengine watashiriki kwa kuwachagua hao wawakilishi. Hivyo kila mwananchi aliye na miaka 18 na kuendelea ana haki ya kushiriki kikamilifu.

Viongozi wanaochaguliwa kwenye uchaguzi huu ni Rais wa nchi, Makamu wa Rais, wabunge na madiwani. Rais na Makamu wake pamoja na wabunge huchaguliwa siku moja. Madiwani huchaguliwa kama inavyokuwa kwa wabunge; ila ni katika ngazi ya kata. Madiwani huwakilisha kata zao katika Halmashauri za Wilaya/Manispaa/Jiji.

Viongozi hawa wanaochaguliwa wanafanya kazi kwa niaba ya wananchi katika vyombo vya maamuzi kama Bunge, Halmashauri za miji, Manispaa au wilaya ,vijiji na mitaa. Kwa vile wanafanya kwa niaba ya wananchi, ni haki ya wananchi kuwahoji viongozi wao pale mambo yakienda kinyume na matarajio yao.

Wabunge ni viongozi wakuchaguliwa ambao wana nafasi nzuri sana ya kusikiliza mahitaji ya wananchi na kuyawakilisha bugeni kwa utekelezaji. Wabunge ni kiungo muhimu kati ya wananchi na Serikali Kuu. Wananchi wanatakiwa kuwasiliana nao pale wanapohitaji kuwasilisha matakwa yao serikalini. Hivyo mbunge ni lazima awe mtu mwenye karama ya kusikiliza, uelewa na kuyafahamu vizuri mazingira ya watu anaowawakilisha.

Wabunge wa kuchaguliwa ni wajumbe wa Halmashauri za wilaya watokako. Njia mojawapo ya kuwapata wabunge ni wakati wa vikao vya Bunge au wakati wako kwenye vikao vya Halmashauri watokako. Ni wajibu wa wananchi kukutana na mbunge wao na kuwasilisha maoni yao kwake, ili yeye ayafikishe Bungeni.

Madiwani kama wabunge, huchaguliwa ili kuwakilisha matakwa ya wananchi katika mabaraza ya Halmashauri. Madiwani huhudhuria vikao vya Halmashauri vinavyofanya maamuzi ya kupitisha Sheria ndogondogo au kupendekeza sera Fulani. Vilevile, wanaweza kutumiwa katika ushawishi ili kuvutia upande Fulani wa utungaji wa sheria au sera kwa sababu hufanya kazi katika ngazi ya Wilaya na wanayajua sana matatizo yanayowakabili watu waishio nao.

Hivyo uchaguzi mkuu si kitu cha kuchezea au kufanyia mzaha. Ni kitu cha kufanyika kwa makini maana ni wakati wa kuchagua wawakilishi wa wananchi. Ni wakati wa kuchagua viongozi wa kuliendesha taifa letu kuanzia vijijini, tarafani, wilayani, mikoani hadi taifani. Ni jambo la msingi wananchi kulifahamu hili na wagombea kulifahamu pia. Si kwamba tunawachagua wafalme au watawala. Tunawachagua wawakilishi na viongozi! Tunawachagua watu wenye uwezo wa kuwakilisha, wenye uwezo wa kuyasikiliza matatizo ya wananchi na kuyachambua na kuyawakilisha kwa ufasaha. Hili linahitaji elimu, karama, busara na uzalendo wa hali ya juu, maana ni kutafuta kutumikia na wala si kutumikiwa. Ingawa wabunge wetu wanapenda tuwatambue kama “Waheshimiwa”, ukweli ni kwamba waheshimiwa ni wale wanaowatuma kuwawakilisha. Uwakilishi ni kutafuta kutoa mchango katika maendeleo ya taifa, kuliko kutafuta kuchuma na kujiendeleza mtu binafsi. Ni kazi ngumu kuwachambua watu na kumpata yule anayefaa kuwawakilisha wananchi. Ni kazi ambayo haina uhusiano na sura ya mtu, umbile, kabila au kipato chake; awe ana nyumba au hana nyumba ,awe ana shamba au hana shamba, awe ana gari au hana gari, awe ana ndoa au hana ndoa, la msingi ni kuangalia utendaji, ushirikiano, elimu, karama, uelewa na uwezo wa kuchambua mambo mbali mbali, kujituma na uzalendo.

Mwakilishi wa watu na hasa Mbunge, ni lazima atoke miongoni mwa watu anaowawakilisha. Ni lazima ayajue matatizo yao na kuyagusa. Kama jamii ile ni ya wavuvi, basi naye awe mvuvi, kama ni jamii ya wafugaji, basi naye awe mfugaji, kama ni watu wa vijijini, basi naye awe ni mwanakijiji. Kama watu wake hawana maji, naye awe anaguswa na hilo, kama hawana barabara, naye awe anaguswa na hilo, kama hawana hospitali, naye awe anaguswa na hilo, kama hawana chakula naye awe anaguswa na hilo, kama hawana shule naye awe anaguswa na hilo. Lakini, kama mwakilishi anawawakilisha watu wenye matatizo ya maji wakati yeye hana tatizo hilo, wana matatizo ya hospitali wakati yeye na familia yake wanatibiwa nje ya nchi, wana tatizo la shule wakati watoto wake wanasomea nje ya nchi, hawezi kuwa mwakilishi mzuri.

Ingawa uchaguzi ni zoezi gumu na wakati mwingine linaleta matukio mabaya kama magomvi, rushwa na kupakana matope, lakini kazi ngumu ni baada ya uchaguzi. Baada ya kuwapata viongozi na wawakilishi ndio kazi kubwa inaanza. Maana ni lazima wananchi na viongozi wao wawasiliane. Hiki ni kitu kigumu sana na kimekuwa kikikwamisha maendeleo siku za nyuma. Tulivyozoea kule nyuma ni kwamba baada ya uchaguzi, mawasiliano kati ya wananchi na viongozi hukatika. Pesa zinazotolewa wakati wa kampeni hazionekani tena baada ya uchaguzi. Ngoma, nyimbo na pilau havipatikani tena. Unyenyekevu wa wagombea wakati wa uchaguzi unakwisha. Viongozi wanakuwa juu kabisa, wanakuwa watawala, Na wananchi wanakuwa chini kabisa, wanakuwa watawaliwa. Badala ya mambo kuanzia chini kwenda juu, yanaanzia juu na kuja chini! Katika dunia ya leo ya demokrasia na utawala bora, hapa ndipo panapogomba. Lengo kubwa la uchaguzi wa viongozi wa kuwawakilisha wananchi ni kutaka mambo kutoka chini kwenda juu! Na hili linawezekana kukiwa na mawasiliano kati ya wananchi na viongozi wao.

Kuwasiliana na viongozi ni njia ya kuwasiliana ili kuzungumza tatizo kwa nia ya kuvumbua au kuzungumzia mipango ya maendeleo; au hata kujadili mbinu na mikakati. Katika nchi inayofuata misingi ya demokrasia watu wote wana haki ya kuwasiliana na viongozi, na ni jukumu la viongozi kuwa tayari kukutana na wananchi. Wananchi wanapaswa kutafuta njia ya mawasiliano na kubadilishana mawazo na viongozi wao wanao wawakilisha katika ngazi mbalimbali za Serikali. Namna nyingine za mawasiliano, hasa kwa viongozi wa juu ni kwa njia ya uwakilishi. Yaani, wananchi wanawasiliana na viongozi walio karibu nao kama wabunge kwa matarajio kuwa watapeleka ujumbe wao kwenye ngazi za juu ili kushughulikiwa.

Mawasiliano yanaweza kufanyika kwenye mikutano ya vijiji ambapo wananchi wanaweza kuuliza maswali au kujadili maswala mbalimbali na viongozi wa Serikali za mitaa au wabunge.

Mawasiliano mengine yanaweza kufanyia kupitia kwenye vikundi wakilishi: kwa mfano vikundi vya akina mama vinaweza kuomba fursa ya kuongea na viongozi wa vijiji, kata, au wilaya kwa nia ya kuongea matatizo na maswala ya maendeleo na utatuzi. Au kwa kuandika maelezo ambayo yatasainiwa na wananchi wengi. Maelezo hayo yatakuwa na madai ambayo wananchi wanataka watendewe na viongozi au wananchi wanaweza kuandika barua kuomba fursa ya kuongea na kiongozi. Au kwa kutumia vyombo vya habari. Hii ni pamoja na kuandika makala, barua kwa mhariri, habari kuhusiana na jambo maalum linalohitaji kushughulikiwa . Njia nyingine ya mawasiliano na viongozi ni radio na luninga.

Kuchaguliwa na kuchagua kiongozi si hoja kubwa. Ni haki ya kila mwananchi kuchagua na kuchaguliwa. Hoja ni je unachaguliwa kufanya nini na unachagua ili iwe je? Hoja ni mgombea kutambua kwamba anatafuta kuchaguliwa ili kuwawakilisha wananchi. Si kutekeleza matakwa yake bali, bali ni kutekeleza matakwa ya wananchi waliomchagua. Hoja ni mwananchi kutambua kwamba anamchagua mtu wa kumwakilisha. Hivyo ni lazima awe makini na kupima kwa makini ni mtu gani ana sifa ya kumwakilisha vizuri. Hoja nyingine ni kwamba ili kumwakilisha mtu ni lazima pawepo na mawasiliano na ushirikishwaji.

Kwa vile uchaguzi wa mwaka huu unaendeshwa wakati Serikali ikiendesha zoezi la maboresho lenye lengo la kuyapeleka madaraka kwa wananchi. Ni imani yetu kwamba zoezi zima la uchaguzi litakwenda vizuri. Na baada ya uchaguzi tutashuhudia uwajibikaji wa hali ya juu. Viongozi wanaochaguliwa na wananchi na kuwajibika kwa wananchi wanaweza kuchochea kasi ya maendeleo. Tunaambiwa kwama nchi zote zilizoendelea ni zile zinazoheshimu uchaguzi wa haki na huru. Ni nchi ambazo wananchi wanaujua wajibu wao na viongozi wanajua wajibu wao. Nchi zilizoendelea zinadumisha mawasiliano kati ya wananchi na viongozi na kuzingatia dhana nzima ya ushirikishwaji.

Pamoja na kuelekeza nguvu zetu katika maandalizi ya uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu, ni wajibu wetu pia kuandaa mazingira mazuri ya yale yatakayofuata baada ya uchaguzi mkuu.

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment