MWALIMU MKUU

UCHAMBUZI HUU WA KITABU CHA MWALIMU MKUU ULITOKA KWENYE GAZETI LA RAI 2005.

MWALIMU MKUU!

Nimesoma kitabu! Zamu hii si “The Da Vinci Code” cha Dan Brown na wala si “Blindness” cha Jose Saramago, au Makuhadi wa Soko Huria, cha Profesa Chachage. Nimesoma, Mwalimu Mkuu, riwaya iliyoandikwa na Paschally Mayega, Mtanzania! Kawaida mtu ukisoma kitabu, unatamani na wengine wakisome. Inawezekana kitabu hiki kimesomwa na wengi? Kimetolewa 2003,mimi nimekiona mara ya kwanza mwaka huu mwezi wa saba! Labda mimi niko nyuma ya wakati! Ni wangapi wamekisoma kitabu hiki cha Mwalimu Mkuu?

Mwandishi wa kitabu hiki bwana Paschally Mayega, ni rafiki yangu wa muda mrefu ambaye urafiki wetu ulianzia kwenye maonyesho ya vitabu yanayofanyika kila mwaka. Ni ajabu kwamba mimi na Paschall Mayega, hatujakuta sehemu nyingine zaidi ya kwenye maonyesho ya vitabu! Magomvi yangu na yeye tunapokutana ni kwamba niache kuandika juu ya kanisa. Kwamba mambo ya kanisa yabaki ndani ya kanisa: “Kanisa, lisiloishi ndani ya jamii?”. Huo ndio msimamo wangu. Kama kanisa liko nje ya jamii, nitaufunga mdogo wangu! Kila tukikutana ni mabishano hadi marafiki zetu wengine wakafikiri mimi na yeye ni maadui! Mwaka huu nimekutana na Mayega, Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam, kwenye maonyesho ya vitabu wakati wa Kongamano la Kimataifa la Kiswahili. Zamu hii hatukubishana! Alinikaribisha kwa furaha kwenye banda lake la vitabu na kunipatia zawadi ya kitabu chake cha Mwalimu Mkuu. Aliniomba nikisome na kumpatia maoni yangu. Nimekisoma na kumpatia maoni yangu kwa njia ya barua pepe. Ni kitabu kizuri. Ni changamoto. Ingawa kuna ndugu zetu watanzania wanaozipuuzia riwaya, kwa mfano kama ile ya “The Da Vinci Code”, riwaya kama ya Mwalimu Mkuu, si ya kusomwa na kutupwa pembeni wala kapuni!

Ingawa riwaya hii ni nzuri, mimi binafsi sikupenda kuandika makala juu yake. Niliogopeshwa na mwisho wake, inaishia katika kumwaga damu ya watu wengi. Sipendi vita! Ninachukia aina yoyote ile ya umwagaji damu hata kama inabeba nembo ya ukombozi. Kumwaga damu ni kuyapoteza maisha, na maisha yakishapotea hayarudi! Sipendi kuamini kwamba nchi yetu imeishiwa na watu wenye busara, hekima na uzalendo kiasi cha kulitelekeza taifa letu kwenye dimbwi la damu. Bado nina imani kwamba tunaweza kutanzua matatizo yetu kwa njia ya amani. Kama hizi ni ndoto, ninyoshewe kidole!

Kwanini basi sasa ninaandika makala juu ya Mwalimu Mkuu? Ninaandika baada ya kusikiliza hotuba ya Mheshimiwa Freeman Mbowe, aliyoitoa wakati akikubali kuteuliwa na Chama chake cha CHADEMA, kugombea urais wa Taifa letu la Tanzania, katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu. Freeman, anasema Taifa letu limemwagiwa mafuta ya taa. Kwamba panahitajika kichaa mmoja kuwasha moto. Kwamba wale wanaoishi Mbezi, Oysterbay na Mikocheni watajikuta Ubungo na kuungana na wenzao wa Manzese, wakielekea kwenye makambi ya wakimbizi Kibaha!

Inatisha! Hotuba ya Mheshimiwa Freeman Mbowe, haina tofauti na maoni yaliyo kwenye riwaya ya Mwalimu Mkuu! Maoni haya hayatofautiani na yale ya Profesa Lipumba, mheshimiwa Mbatia, Profesa Chachage na wengine wanaojali!

Sina sababu yoyote ile ya kuuwekea mashaka uzalendo wa Mbowe, uwezo wake mkubwa wa kuchambua mambo, uelewa wake mkubwa, busara na hekima. Amekuwa mbunge wa Hai, sifa zake zinasikika nchi nzima. Ni Mwenyekiti wa chama ambacho watu walio wengi wanaamini kwamba ni chama makini. Ni mfanyabiashara asiyetiliwa shaka, Hakwepi kodi! Hatujasikia kashifa yoyote juu yake. Hivyo akitamka kitu si kama kasuku, anakuwa amekifanyia kazi.

Kama rafiki yangu Mayega, anaota ndoto za mchana kwenye riwaya yake ya Mwalimu Mkuu, haiwezekani Freeman, Lipumba, Mbatia,Chachage na watu wengine wanaojali waugue ugonjwa ule ule wa kuota ndoto za mchana kwa wakati mmoja! Ni lazima kuna kitu! Kuna jipu au kichomi katika taifa letu la Tanzania.

Utangulizi wa riwaya ya Mwalimu Mkuu, unasema hivi:
“Kama nitasema kweli tupu siku zote KUNA UBAYA GANI? Msema kweli ni mpenzi wa Mungu. Hapendezi mbele ya binadamu wenye roho mbaya. Hukimbiwa hata na marafiki zake wenye roho nyepesi. Nikipatwa na mkosi kama huo sitawaonea wivu watu wawezao kudumu na marafiki zao wote siku zote. Siwezi kuikana kweli kwa kuogopa upweke wa muda, Nikanyimwa ushirika wa milele unaotazamiwa kutokea baada ya kushindwa kwa uongo.

“ Riwaya hii ni ya kubuni. Hata nchi inayosimuliwa katika riwaya hii haipo ni ya kufikirika tu. Hivyo ikiwa itatokea baadhi ya majina yaliyotajwa katika riwaya hii kufanana na majina halisi ya miji, vitu au watu waliopo hiyo ni bahati mbaya tu na wala haikukusudiwa kwani kama nilivyosema mwanzo riwaya hii ni ya kubuni tu.”

Inawezekana kabisa riwaya hii ni ya kubuni. Lakini inaongelea Taifa letu. Hata kama ni kufanana tu, wahusika watakuwa na uhusiano wa karibu na watanzania. Majina yanayotumika kwenye riwaya hii yamefanana sana na yale tunayoyafahamu: Tibaijuka, anayetajwa kama Dada Tibaijuka!, Jakaya, anayetajwa kama Kaka Jakaya, Lyatonga, Pombe, Salim,Edward, Makamba,Azimio la Kijenge, Azimio la Mji Mkongwe,Mama Shamim,Sajenti Freeman,Luhigo, Tendwa, Hakimu Barnabasi, Luhanga,Jamuhuri Ya Muungano, Mwadilifu Freeman wa Hai, nk. Haiwezekani kuna nchi nyingine yenye kufanana na Tanzania, kiasi hiki!

Riwaya ya Mwalimu Mkuu, inahusu mapambano kati ya Mwalimu Mkuu Ngowe Boniface, wa Shule ya Msingi Kumwitu akisaidiwa na wanafunzi na wananchi dhidi ya mwekezaji Mzauzi Bw.Frederick de Witts, anayekingiwa kifua na kulindwa na Serikali.

Frederick de Witts alikuwa mgeni aliyekuja nchini kuwekeza. Katika kuwekeza kwake alijenga kiwanda. Kiwanda cha kusindika minofu ya mbu na wadudu wadogowadogo kama sisimizi. Kiwanda hiki kilijengwa katika chanzo pekee cha mto Luzi. Mto ambao ulikuwa pekee katika eneo hilo kwa maji ya kunywa, kuoga na kazi nyingine. Pia mto Luzi, ulikuwa ndio tegemeo la wananchi kwa ajili ya uvuvi wa samaki wa kitoweo na biashara. Kiwanda hiki kilijengwa jirani kabisa na Shule ya Msingi ya Kumwitu. Moshi uliotoka katika Kiwanda hicho mara nyingi uliifunika kabisa shule ile na sehemu za makazi ya wananchi. Mara kadhaa ilibidi masomo yasimamishwe na wanafunzi kutoka nje shauri ya Moshi kujaa madarasani. Nje pia kulikuwa na moshi. Mafuta na kemikali zilizotoka katika kiwanda hicho zilitupwa katika mto Luzi na hivyo kusababisha uharibifu mkubwa wa mazingira.

Wananchi wa zehemu hiyo waliathirika kiafya, waliugua kikohozi kisichopona kutokana na moshi wa kiwanda, ngozi zao zilibabuka nk. Mwalimu Mkuu, alitaka kiwanda hicho kifungwe. Serikali, na hasa mawaziri waliokuwa wakipokea rushwa kutoka kwa msauzi, walitaka kiwanda hicho kiendelee!

Mwandishi anaonyesha vizuri mawasiliano mabovu kati ya Mwekezaji na Rais wa nchi, na kati ya Rais na wananchi wake. Mwekezaji anatoa rushwa ya kumpelekea Rais, ili kumziba mdomo. Rushwa hiyo inaishia kwenye mifuko ya Waziri wa viwanda na Waziri Mkuu. Rais, anapata taarifa nzuri kwamba kiwanda ni kizuri na kinaleta faida kwa taifa, wakati kiwanda ni hatari kwa maisha ya wananchi. Malalamiko yanapozidi, Rais, anataka kukitembelea kiwanda. Waziri mkuu na waziri wa viwanda, wanamshauri msauzi kufunga kiwanda chake kwa muda, hadi rais atakapomaliza ziara yake. Msauzi anakataa kufunga kiwanda:

“Nimekubali kuwapeni ninyi mali ya kila aina ili nifanye shughuli zangu bila bughudha. Unaponiambia nifunge kiwanda changu unataka mimi nikueleweje? Niliwaambia sisi wawekezaji ni mtandao. Hao wenzangu nitawaambia nini? Nilishaambia kuwa Rais yupo na sisi, wewe unakuja kuniambia upuuzi? Mwalimu Mkuu atawashindaje wakati yeye hana jeshi, hana mamlaka yoyote. Sema nyinyi mnataka kuniletea kujua. Ukitaka kunijua mimi ni nani uliza nchi jirani. Wote walioleta mchezo huu unaoleta hawapo Duniani. Ohoooooo! Mnataka kucheza na moto……kamwambie huyo Waziri Mkuu wako na wenzio wote kuwa upuuzi wenu huu haukubaliki. Kitaondoka chochote hata matumbo au mapafu yenu lakini mimi nitabaki na kiwanda changu. Nimekuja hapa kuishi na si vinginevyo.” (Uk 47).

Mwandishi wa riwaya, anaonyesha jinsi jitihada za Mwalimu Mkuu na wananchi, za kukifunga kiwanda hicho kwa amani zinashindikana. Rushwa, na mawasiliano mabovu kati ya Rais, Waziri Mkuu, Mawaziri, mwekezaji na wananchi utawala mbovu inasababisha Mwaimu Mkuu, wanafunzi na wananchi kutumia nguvu kukifunga kiwanda cha msauzi. Kama ilivyo kwa mapambano yoyote yale ya ukombozi wa umma, nguvu ya wananchi inashinda. Msauzi anashindwa na serikali inashindwa lakini baada ya kumwaga damu nyingi.

Nimejaribu kufupisha, lakini kitabu cha Mwalimu Mkuu, kinaelezea mambo mengi yanayotokea katika jamii yetu, mambo ambayo bila hekima, busara na uzalendo wa kweli, atatokea mwendawazimu mmoja, kama anavyosema Freeman Mbowe, na kuwasha moto maana nchi nzima imemwagiwa mafuta ya taa!

Kwanini tufike huko? Kwanini tusikae chini kama taifa na kuyapitia haya mambo yanayoleta utata kama uwekezaji? Tunashuhudia magomvi hadi vifo kati ya wananchi na wawekezaji kwenye machimbo ya madini. Wananchi wanalalamika kwamba machimbo hayana faida nao. Kama hawezi kuuza nyanya zao, ndizi zao, maziwa yao nk., kila kitu kinatoka Afrika ya kusini, kwa nini wasilalamike? Kama mwenye mali, mwananchi, hana pesa ya kumpeleka mtoto shule wala kununua dawa, wakati mwekezaji anaishi Dar-es-Salaam, na kufanya kazi kila siku Kahama, ana uwezo wa kusafiri kila siku kwa ndege, kwa nini mtu hata kama hakusoma, asitilie shaka uwekezaji?

Kuna mambo mengi ya kuhoji juu ya uwekezaji. Wananchi wanapiga kelele, lakini hakuna anayejitokeza kutoa majibu. Mifano inayotolewa ni ujenzi wa barabara ambazo zilizo nyingi hazipiti kwenye sehemu za machimbo na maeneo mengine ambayo wawekezaji wamesimika mizizi. Mfano mwekezaji wa pori la Kimisi, wilayani Karagwe, anamnufaisha vipi mwananchi aliyehamishwa ili kumpisha mwekezaji? Ujambazi unaendelea kwenye pori hilo, hata juzi watu wameuawa na kuporwa mali zao! Ujenzi wa Barabara za lami unaihusu vipi Karagwe, wilaya isiyokuwa na barabara hata moja ya lami? Karagwe, inazalisha Kahawa nyingi. Kahawa zinaingiza pesa za kigeni, lakini…… kuna kitu, kama si jipu ni kichomi!

Hadi leo wananchi wa Igoma na Kisesa,Mwanza, wanaendelea kuathirika na harufu mbaya inayotoka kwenye viwanda vya kusindika minofu ya samaki. Kwa vile viwanda hivi ni vya wawekezaji hakuna anayesema, watu wanaendelea kuathirika na mazingira yanaharibika!

Kuna ugomvi mkubwa kati ya wavuvi wadogo wadogo na wawekezaji wa viwanda vya kusindika minofu ya samaki. Ugomvi huu unasababisha mambo mengi: mauaji, uvuvi haramu, wananchi kushindwa kumudu bei ya samaki nk. Bila busara na hekima, ugomvi huu unaweza kuelekea kwa Mwalimu Mkuu!

Baadhi ya watu wanaunga mkono sera nzima ya uwekezaji. Baadhi wanapinga! Hawa wanaopinga hawapingi uwekezaji, bali wanapinga jinsi uwekezaji unavyoendeshwa, mfano kujenga kiwanda kwenye makazi ya watu, kuchimba madini yetu na kutuachia mashimo na watu wachache kunufaika na uwekezaji.

Wananchi walio wengi hawajui faida na hasara za uwekezaji. Wanachokiona ni moshi unaoathiri afya zao, ni harufu mbaya inayotoka kwenye viwanda, ni maisha bora na ya starehe ya wawekezaji, ni kutozwa kodi kubwa, ni kuzuiwa kuingia ziwani kuvua kwa vile ziwa ni la wawekezaji, ni kuzuiwa kuwinda kwa vile misitu yote ni ya wawekezaji. Ni kuzuiwa kutumia uwanja kwa vile mwekezaji ameukarabati. Haya na mengine yasipopata maelezo ya kina, yakifanyiwa mzaha, ni kweli Mwalimu Mkuu, wanafunzi na wananchi watapambana na kushinda!

Kwanini tufike huko? Na kwa nini tusifike huko kama hakuna jitihada zinazofanyika ili kuliepusha taifa letu na janga la kumwaga damu? Kama Mayega, anaandika uongo kwa nini tusimnyoshee kidole na kumsuta? Kama Freeman Mbowe, anasema uongo, kwa nini tusimnyoshee kidole na kumsuta? Amesema bungeni, tumemsikia, ameandika makala nyingi na sasa analihutubia taifa zima, mbona hakuna anayejitokeza na kusema Mbowe ni mwongo? Kwanini wananchi wasimwamini na kumfuata? Kama Profesa Chachage, anaandika uongo katika Makuwadi wa Soko Huria, mbona asijitokeze msomi mwingine akaadika kitabu cha harusi na sherehe ya Soko Huria? Kukaa kimya ni kukubali ukweli?

Wahaya wana msemo: “Akataizile bwankya, kaija bwaigolo”. Tafsiri isiyo ya rasmi ni: Jambo lisipotokea asubuhi, kuna uwezekano wa kutokea jioni.

Tunapoelekea uchaguzi mkuu, tusifanye mzaha. Kila Mtanzania ni muhimu na ana la kuchangia! Uhai wa Tanzania, uko mikononi mwa kila Mtanzania!

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment