MISAADA YA NJE

MAKALA HII ILITOKA KWENYE GAZETI LA RAI 2005

Misaada ya Nje itamaliza Matatizo ya Afrika?

Siku za nyuma kidogo nilijadili juu ya udaku. Nilisema kwamba badala ya wasomi wetu kusoma udaku, wasome na kujadili mambo mbali mbali yanayolihusu taifa letu, Afrika na dunia nzima kwa ujumla. Msomi mmoja amenitumia ujumbe kwenye simu yangu ya mkononi kwamba mimi nimepitwa na wakati, maana magazeti ya udaku, siku hizi yana hoja nzito. Labda huyu alitaka ninunue na kuchangia magazeti haya. Nimeyasoma, sioni tofauti. Bado ni udaku kwa maana ya neno udaku. Na bado udaku huu una mvuto kwa wasomaji wengi. Nimeshindwa kuziona mada motomoto katika magazeti haya ya udaku kama zile za kizazi kilichotutangulia cha kupigania uhuru wa bara letu.

Kizazi kilichotutangulia kilipigania uhuru. Kizazi chetu kina jukumu la kupigania uhuru wa uchumi na kuzikomboa fikra zetu. Mfano mada kama hii ninayojadili leo: Misaada ya Nje itamaliza matatizo ya Afrika? Ndizo mada ambazo wasomi wetu wangekuwa wanazijadili na kuziweka katika lugha ya kawaida ili wananchi wazifahamu vizuri na kuweza kuwahoji viongozi wanaotaka kuchaguliwa kuziongoza nchi za Afrika. Maana kama kiongozi wa nchi hana upeo wa uchumi wa taifa lake, Afrika na dunia nzima, tutakuwa sasa hivi tunaandaa balaa jingine kama lile la utumwa na ukoloni! Na tukubali tusikubali, historia itatuhukumu tu!

Misaada ya nje kwa nchi zinazoendelea limekuwa ni suala lenye utata mkubwa kupindukia. Wakati wa Mkutano wa nchi tajiri duniani maarufu kama G8 uliofanyika Uskochi Julai Mwaka huu, lugha ilikuwa ni kuongeza misaada ya nje kwa nchi masikini sana. Hili halikuwa pendekezo la Tony Blair peke yake na wala si jipya. Ukiangalia malengo ya Milenia, utekelezaji wake unategemea kwa kiasi kikubwa misaada toka nchi zilizoendelea, ukiangalia kinachoitwa NEPAD wanasema ili mkakati utekelezeke watahitaji mabilioni ya dola toka nje.

Nadharia ya misaada ya nje na ukuaji wa uchumi kwa nchi zinazopokea misaada hiyo limekuwa ni swala tata na la muda mrefu. Kuna maelfu ya machapisho duniani yenye kuelezea mchango wa misaada kwa ukuzaji uchumi. Hadi sasa hakuna hitimisho au makubaliano ya pamoja kwamba misaada ya nje hukuza uchumi, pengine bado hakujapatikana zana za kutosha kutafiti mchango wa misaada katika ukuaji wa uchumi.

Kwa mtazamo wangu Waafrika wengi kwa ujumla, walifurahia na kushangilia sana pale mkutano wa G8 ulipohitimishwa kwa kuongeza misaada lukuki katika bara la Afrika. Kwanza kabisa inabidi tujue kwamba misaada si sadaka tuu ; kuna malipo yake baadaye iwe ni moja kwa moja au kupitia njia nyingine. Misaada hii pia huwapatia watoaji mwanya wa kwenda katika nchi zinazopokea ili kula fedha zao wenyewe. Katika misaada wanayokupa, asilimia kubwa sana hutumiwa na wao wenyewe na pili misaada haijengi uwezo wa nchi inayopokea kuongeza uwezo wa uzalishaji au kuwekeza katika teknolojia sahihi. Misaada ingekuwa inajenga uwezo wa kuzalisha bidhaa kwa ajili ya kuuza nje kwa mfano tungetarajia kwamba urari wa malipo ya nje kuimarika kutokana na ongezeko la bidhaa zetu nje lakini halisi si hivyo. Mramba katika bajeti yake ya mwaka 2005/2006 anasema kwamba urari wa malipo ya nje umekuwa mzuri kwa sababu nyingine ikiwemo misaada ya nje ambayo imeongezeka zaidi ya mara tatu pamoja na misamaha ya madeni. Mara nyingi misaada ya nje huwa na ajenda maalum pengine si lengo la watoaji kumaliza au kupunguza matatizo yako, wanajua watapata nini kama malipo.

Misaada kwa tafsiri pana ambapo mara nyingine ni pamoja na mikopo hutolewa kwa lengo la watoaji kutumia fedha zao wanavyotaka na matokeo yake misaada mingi haiwafikii walengwa. Mashirika ya Oxfam na Action Aid katika taarifa yao waliyotoa mwezi Februari mwaka huu kwa mfano, wanasema kwamba ni moja ya tano tuu ya misaada ya nje huwafikia wanaohitaji sana. Taarifa pia inasema kwamba asilimia 40 ya misaada hiyo hutumika kuagiza bidhaa kwa bei za juu toka nchi wahisani pamoja na gharama za washauri waelekezi ambao hutoka katika nchi zao. Taarifa hiyo ilizilaumu moja kwa moja Marekani kwa kuwa kinara wa nchi zinazotumia zaidi ya asilimia 70 ya misaada kwa kuzilipa kampuni zake. Taarifa hiyo pia ilisema kwamba Senegal katika mwaka 2003 iliwapokea wageni si chini ya 50 toka Benki ya Dunia nadhani kufuatilia miradi yao wanayofadhili huko. Angalia wageni 50 wa nini? Wanakula fedha hizo hizo walizotoa katika miradi hiyo na huu unaweza kuwa mkopo. Kwa hivyo wana wa nchi ya Senegal watalipa gharama zote hizo. Pia majuzi kulikuwa na habari za matumizi ya mamilioni ya fedha za misaada katika nchi ya Malawi kutumika kwa ajili ya malazi ya wanaoitwa wafadhili kwenye hoteli kubwa. Hii ndiyo hali halisi.

Misaada pia huja na masharti makali sana ambayo wakati mwingine inashindikana kutimiza, huja na watu wao wanaoitwa wataalamu. Jambo la muhimu sana la kuelewa hapa ni kwamba kama utapewa msaada wa Shilingi 100, halafu shilingi ishirini zikatumika kumlipa mshauri mwelekezi toka Ulaya, shilingi 40 zikatumika kuagiza vifaa halafu 10 zikatumika kulipa mishahara kwa wataalamu wao, unabaki na shilingi 30 ambazo kati ya hizo kuna kama 15 zitatumika kwa shughuli za utawala na unabaki na 15 ambazo ndizo zinatarajiwa kuleta maendeleo. Hakutapatikana maendeleo kupitia misaada kwa minajili hii. Jambo moja la wazi hapa ni kwamba kunahitajika njia nyingine ya kumsaidia Mwafrika misaada si suluhisho hata kidogo. Kama kweli tunataka msaada uwe suluhisho ni lazima ulenge katika kukuza uwezo wa ndani wa kuzalisha ili kuweza kukuza ajira na kuongeza wingi wa bidhaa zinazouzwa nje, kwa maana hiyo kitakachosaidia ni kuhakikisha kwamba kiasi kikubwa cha fedha zinazotolewa kama misaada kinatumika kwa nchi inayopokea na si kutumiwa na wenyewe. Tusitarajie kwamba wanatupa misaada ili waweze kutatua matatizo yetu watatumia matatizo yetu kumaliza ya kwao.

Sasa hivi usione tunajisifu kupata misaada mingi, hata hizo nchi wahisani zinashindana kuitoa kwa vile wanajua watapata malipo yao kwa njia moja au nyingine. Majuzi gazeti la Guardian la Uingereza liliandika habari iliyokuwa inasema kwamba mikakati ya nchi za magharibi ya kusaidia Afrika ni aina mpya ya upigianiaji wa bara la Afrika kama ulivyofanyika karne ya 19. Kwa mujibu wa habari hiyo, wakati kila nchi ikijikomba kwa nchi za Afrika, makampuni makubwa ya nchi za magharibi yanawekeza na kuiba kwa kasi rasilimali za Afrika sijuhi ni lini watakaa tena kugawana Afrika, safari hii sijuhi itakuwa wapi. Sidhani kama ni Berlin!! na mgawanyo hautakuwa kama ule wa karne ya 18 utakuwa wa kisayansi zaidi hasa ikizingatiwa kwa sasa tunawakaribisha wenyewe. Kwa wale wasomaji wa vitabu wanaweza kusoma kitabu kiitwacho: Lords of Poverty kilichoandikwa na mwandishi Graham Hankock. Ni kitabu kizuri kinachoonyesha jinsi wamagharibi wanavyotumia umasikini wetu kujitajirisha.

Mantiki hii ya fedha za misaada ikiwepo mikopo kutumika na watoaji wenyewe inazalisha maswali mengi sana na hasa inavyokuwa mkopo. Kama umekopa shilingi 50 ambazo utaanza kuzilipa baada ya miaka kumi na tano kwa mfano, na kiasi kikubwa cha fedha hizo zisitumike kwa walengwa basi ujue utalipa fedha zote pamoja na riba wakati wewe kama mkopaji umetumia asilimia kama 10 au 15 nyingine zimetumika na wao wenyewe. Hapo hatujaweka uwezekano mkubwa wa matumizi ya ovyo yanayofanywa na sisi tunaoipokea. Inapofikia hapa ndipo baadhi yetu tunahoji uhalali wa kusamehewa madeni ambayo hatujui yalitumikaje. Je tunataka tusamehewe madeni tuliyotumia hovyo nikimaanisha watoaji na wapokeaji ili tukopesheke, tupate fedha nyingine na kuzitumia hovyo? Kwa kweli ni lazima wanaojiita wanaharakati wahoji suala hili si kuandamana kusamehewa madeni yaliyoishia kwenye matumbo ya wachache ili kukopa tena na kuishia kwenye matumbo hayohayo. Tusipofanya hivyo tutakuwa tunacheza mchezo wa kujificha na kutafuta.

Mikopo ya masharti nafuu inayokopwa leo na kuanza kulipa baada ya miaka 15 au 20 tujue wengi wetu ambao ni watu wazima kiasi hatutakuwepo kuilipa. Watalipa watoto wetu, kama haitatumika vizuri tutakuwa tunafanya dhambi ya mauti kwa kizazi kijacho. Kwa mfano fedha zilizokopwa na Serikali ya Tanzania kwa ajili ya mpango wa elimu ya msingi, ni lazima tujue watoto hao hao ndio watakaozilipa, kwa hivyo ni lazima zitumike kwa lengo hilo kama zitaishia kuimarisha vitambi vya wachache sasa pamoja na mabwana wa Benki ya Dunia basi tutakuwa tumeshindwa hata kuheshimu uhasiri wa kizazi kilichopo kufanya maandalizi kwa kizazi kijacho, kizazi kijacho kitalipa fedha zilizotumika hovyo na baba zao. Hii itakuwa ni dhambi ya ajabu sana. Nchi zilizoendelea kama Amerika, zinaandaa maisha bora ya vizazi vijavyo, na maisha bora ya sasa ya nchi zilizoendelea ni matokeo ya maandalizi ya vizazi vilivyotangulia. Waliwatumia mababu zetu kuwaandalia watoto wao na wajukuu zao maisha bora. Walitumia rasilimali kutoka Afrika, kutengeneza maisha bora ya vizazi vilivyofuata. Sisi tunafanya kinyume, tunataka kuishi maisha ya neema, kwa kuandaa Jehanamu kwa vizazi vijavyo. Wale tunaowaita wenzetu, wanaotupatia misaada, wanajua ukweli huu, lakini ukimwamsha aliyelala, utalala mwenyewe!

Kwa ujumla misaada si mwahamsini wa matatizo ya Afrika hasa ukizingatia kanuni hizi za wenyewe kula fedha zao. Cha muhimu zaidi ni kwa Waafrika kusukuma zaidi kuongezeka mchango wake wa biashara kimataifa. Takwimu zilizopo zinaonyesha kwamba mwaka 1948 mchango wa Afrika katika biashara ya kimataifa ukiondoa Afrika ya Kusini ulikuwa asilimia 5.3 ikilinganishwa na asilimia 1% mwaka 2002 japo Afrika ina asilimia 12 ya idadi ya watu duniani. Kama Afrika ingeweza kuongeza angalau asilimia moja tuu ya mchango wa biashara ya kimataifa ingeweza kupata kiasi cha Dola za kimarekani bilioni 70 ikilinganishwa na dola bilioni 13 zinazotolewa kama msaada wa maendeleo kwa mwaka. Lakini kutokana na mfumo wa biashara uliopo kwa sasa haitawezekana kirahisi Afrika kuongeza huo mchango. Pili ruzuku kubwa inayotolewa na nchi za dunia ya kwanza kwa wakulima wake ni kikwazo kikubwa kwa nchi za Afrika kushindana. Kwa mfano, nchi hizi hutoa ruzuku ya dola bilioni 300 hivi kwa mwaka hii ni zaidi ya mara sita ya misaada inayotolewa kwa nchi changa.

Unaweza kuona jinsi siasa za biashara za kimataifa zinavyofanya kazi. Kuwapa misaada kwao ni heri kubwa kuliko kulegeza masharti ya biashara. Inaonekana pia kwamba wakati wa ukoloni Afrika ilikuwa ikifanya biashara kubwa zaidi kuliko Afrika huru sasa. Lakini hata kama nchi zinazoendelea zikilegeza masharti ya biashara bado ni nchi chache sana Afrika zitakazofaidika moja kwa moja. Hali za nchi za Afrika ni mbaya kabisa. Ukiangalia kwa mfano mpango wa AGOA na EBA bado haijaweza kufaidisha nchi nyingi sana kwa kuwa hakuna miundombinu ya uzalishaji bidhaa. Kinachotokea ni kuwaita wawekezaji toka nje ambao nao wana mambo yao. Hakuna mwekezaji atakayekusaidia kuendelea wewe badala ya kuandaa maisha ya baadaye katika nchi yake. Ukiona yanayotokea Lesotho ambapo Wachina wengi waliwekeza katika viwanda vya nguo sasa inasikitisha, viwanda vinafungwa kwa kuwa Wachina sasa wanapunguziwa kwa lazima soko lao la bidhaa za nguo Ulaya na Marekani.

Matatizo ya Afrika ni makubwa si rahisi kama wengi wanavyofikiri kwamba yatatatuliwa na Wazungu. Hapana ni lazima tuyatatue wenyewe. Ni lazima tuonyeshe dunia ni nini tunaweza kufanya, ni kitu gani kipya tunachoweza kuleta duniani. Bila kuwa na kitu kipya ambacho kitakuwa na soko jipya tutapiga hadithi tuu. Tutahubiri na kuwaachia Wazungu walete maendeleo wagharimie mipango ya maendeleo. Hayo maendeleo hayatakuja naapa!. Ni lazima tusafishe nyumba zetu pia. Rushwa, matumizi mabaya ya fedha za umma, misamaha ya kodi na utoaji hovyo wa rasilimali zetu ni lazima vipigwe vita kwa kasi zote na sisi wenyewe. Hawa Wazungu wanapopiga kelele za utawala bora wanajua fika kabisa ni vigumu mabadiliko kuletwa na kelele hizo au kuletwa kwa kunyimwa misaada. Kuzilazimisha serikali kufuata misingi ya utawala bora si jukumu la wahisani. Ni la kwetu wenyewe. Tukiamua leo tunaweza.

Ni maoni yangu kwamba haya ndio wasomi wetu wangekuwa wanajadili. Sina uhakika kama kweli haya yanajadiliwa kwenye magazeti ya udaku. Haya ndio kingekuwa kipimo cha viongozi wetu. Wale wanaotaka kuwa wabunge, wanayafahamu haya na wanaweza kusimama kuyatetea? Wale wanaotaka kuwa marais wa taifa letu wanayafahamu haya? Wanafahamu kwamba misaada ya nje haiwezi kusaidia kulijenga taifa letu? Je wale wanaotaka kuwa viongozi wa taifa letu wana mikakati ya kuiandaa Tanzania ya vizazi vitatu hadi vinne mbele yetu? Bila mikakati hii, hatuna uhalali wa kuendelea kuishi!

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment