HOTUBA YA RAIS MKAPA NI MUHIMU

MAKALA HII ILITOKA KWENYE GAZETI LA RAI 2005

HOTUBA YA RAIS MKAPA NI MUHIMU

Jana tarehe 30.9.2005, Mheshimiwa Rais Mkapa, alitoa hotuba ambayo karibia ni ya mwisho katika uongozi wake kama Rais wa taifa letu. Amesema kwamba hotuba zake za mwisho kwa taifa ni zile zinazougusa moyo wake. Ameamua kuanza na UKIMWI, ni kweli UKIMWI, unaugusa moyo wake na kuigusa mioyo ya watanzania wote. Alionyesha jambo hili kwa matendo pale alipoutangaza UKIMWI, kuwa ni janga la Kitaifa. Amejitahidi awezavyo kupambana na UKIMWI. Anasema kwa kipindi cha miaka kumi ya utawala wake watu nane kati ya kumi wamepata habari juu ya gonjwa hili hatari. Lakini bado watu wanaendelea kuugua na kufa na walio wengi hawajabadilisha tabia zao. Kufuatana na takwimu, gonjwa hili linaua na kuacha yatima wengi Afrika kusini mwa jangwa la Sahara. Ingawa watafiti wengine wanaonyesha kwamba maambukizo ya virusi vya UKIMWI, yanapungua, kuna ukweli kwamba, utafiti huu ni wa kupotosha, kama anavyosema Bwana Joseph Tumushabe, wa Chuo Kikuu cha Makerere Uganda, kwamba nchi ya Uganda, iliyosifiwa katika kupambana na maambukizo ya virusi vya UKIMWI, maambukizo yameongezeka kiasi cha kutisha. Utafiti wake, haupendwi Uganda, maana unafichua ukweli ambao umefichwa siku nyinyi.

Hotuba ya Rais Mkapa, imeeleza ukweli mtupu juu ya matatizo yanayouzunguka ugonjwa huu: vifo, yatima, unyanyapaa nk. Jambo ambalo mheshimiwa Rais Mkapa, hakutaja, ni utata unaouzunguka ugonjwa huu:
Utata juu ya Ukimwi; Waathirika wakubwa ni Waafrika Maskini

Tangia Robert Gallo, Mwanasayansi kutoka Marekani atangaze kwamba amegundua kuwa virusi vya HIV ndivyo vinavyosababisha UKIMWI zaidi ya miongo miwili iliyopita, kumekuwa na ubishi mkubwa na wa muda mrefu kisayansi. Chanzo cha ubishi huu ni kwanza; ni nini hasa chanzo cha kirusi cha HIV? Wanazuoni wengine wanaamini kabisa kwamba kirusi hiki kilitengenezwa Maabara mnamo miaka ya 1970 wakati wa mapambano makali ya kutafuta tiba ya kansa baada ya Rais Nickson kutangaza vita dhidi ya ugonjwa huo. Wengine wanaamini ni mpango matokeo ya mpango mzima wa vita ya kibaiolojia wa Marekani. Kwamba hizi ni hisia au ni ukweli bado ni kitendawili cha kutenguliwa. Wanasayansi wengine wanadai kwamba kirusi hiki kimetokana na nyani wa kijani wapatikanao Afrika hawa wameshawishi ulimwengu kwa kiasi kikubwa japo kuna kundi ambalo bado linabishana nao. Kwamba kirusi kimetoka wapi si suala tena kwa sababu tunacho kimethibitika kisayansi kuwepo.

Sehemu ya pili ya ubishi wa kisayansi ni kama kinasababisha UKIMWI. Hapa ndio kuna kazi nzito ya kuhakikisha hilo. Mwaka 1984, Gallo alipotangaza ugunduzi wa HIV kila mmoja alijua kwamba baada ya miaka miwili chanjo ingepatikana, wanasayansi wakasubiri watu wakawa na matumaini makubwa sana kwamba ifikapo mwaka 1986 basi tungekuwa tumedhibiti kuenea kwake. Hii ilikuwa kinyume kabisa na walivyobashiri. Leo baada ya miaka zaidi ya miaka ishirini bado hakuna chanjo wala dalili hazipo karibu sana. Baada ya hali hii kudhihirika, ndipo wanasayansi machachari kama vile Peter Duesberg, profesa wa Molecular Biology katika Chuo kikuu cha California Berkely akaanza kupuliza filimbi yake kwamba ana wasiwasi mkubwa na nadharia ya Gallo ya virusi vya HIV kusababisha UKIMWI. Huyu ni Gwiji wa sayansi, alikuwa mtu wa kwanza kutenganisha kirusi cha kansa mwaka 1970. Hoja yake kubwa ni mpaka leo hakuna anayeweza kuhakikisha kutenganisha kirusi cha HIV. Na kama haujaweza kukitenganisha huwezi hasa kudai kwamba kinasababisha UKIMWI moja kwa moja. Hii ni hoja nzito ambayo amekuwa akipambana nayo, kuna wakati hata machapisho yake yalikataliwa katika majarida makubwa ya utafiti. Sasa hivi hata fedha za kufanya utafiti hapati toka serikalini. Kisa ni kuwa na mawazo tofauti.

Ukweli ni kwamba hata baadhi ya wanasayansi waliokuwa wakitembeza nadharia ya HIV kusababisha UKIMWI akiwepo mgunduzi Mwenza wa HIV, Profesa Motegneur kutoka Ufaransa na Gallo mwenyewe wamekuwa wakielekea kukubali kwamba HIV inaweza kuwa sababu moja tu kati ya nyingi zinazosababisha kupunguka kwa kinga mwilini. Suala la msingi hapa ni kwamba kuna uhusiano kati ya HIV na UKIMWI lakini hakuna ushahidi kwamba HIV inasababisha UKIMWI. Kuna tofauti kubwa hapa uhusiano hauna maana kusababisha. Hiki ni kitendawili cha kisayansi ambacho hakijatenguliwa. Wanaopambana kisayansi ni weupe toka nchi za dunia ya kwanza ambapo UKIMWI si tatizo kubwa, ni tatizo la kundi fulani. Kwa mfano utafiti umeonyesha kwamba Ulaya ya magharibi na marekani, UKIMWI ni tatizo la wanaojichoma sindano za dawa za kulevya pamoja na wasenge. Hili ni kundi dogo na lisilo na umaarufu sana. Hapa Afrika ni kwa kila mmoja, vijana wenye nguvu zao na ambao hata pengine hawajui sindano za dawa zikoje. Isitoshe tatizo ni kubwa.

Changamoto kwa wanasayansi wa Afrika ni je kinafanyika nini kutatua mabishano haya yanayofanywa na wanasayansi toka nchi za magharibi? Pamoja na tatizo letu la kila siku la ukata inabidi serikali zetu zifanye chochote. Fedha zetu wenyewe lazima zitengwe kwa tafiti. Tukingoja fedha toka kwa wanaoitwa wahisani hatutazipata kwa lengo la kufanya utafiti, tutapewa za kuhubiri UKIMWI badala ya kutafiti UKIMWI. Wanasayansi wetu wamekuwa wahubiri kuliko watafiti. Kila mmoja anakimbilia kuhubiri na kukusanya takwimu za UKIMWI. Wazungu wanazihitaji sana hizo takwimu ili waweze kukadiria kiasi cha dawa za kupunguza makali ya UKIMWI. Zitakazohitajika katika kipindi cha miaka kadhaa ijayo. Tusipoweza kufanya lolote katika utafiti, UKIMWI utakuwa kama Malaria. Tatizo la Malaria ni la nchi masikini na ndiyo maana imeshindikana kabisa kutengeneza chanjo. Ninaamini ingekuwa ni tatizo la nchi tajiri pengine leo au miaka mingi iliyopita lingekuwa limekwisha. Lakini wapi, tumekaa na malaria miaka yote hii tunanunua dawa toka nchi zao. Ndiko tunakoelekea kwenye UKIMWI tusipotafiti tumekwisha. Tusipotumia wataalamu wetu katika kutafiti na badala yake tukaendelea kuwafanya wahubiri na wakusanya takwimu basi tutaendelea kufa pasi na tegemeo lolote.

Kana kwamba mabishano hayo hayatoshi yameanza mengine. Virusi vipo, kwamba chanzo chake ni kipi hakuna uhakika kamili, kwamba vinasababisha UKIMWI bado hakuna ushahidi wa kisayansi. Sasa wametafuta dawa za kupunguza makali ya tatizo hili. Ubishi sasa ni je dawa hizo ni kweli zinafaa? Hilo limekuwa ni jambo lililoanza kubishaniwa karibuni baada ya wanasayansi kadhaa kudai kwamba dawa za kurefusha maisha zina sumu ya ajabu na pengine zinaharakisha kufupisha maisha ya muathirika. Duesberg kwa mfano anasema Dawa zinazotumika kuzuia maambukizo toka kwa mama kwenda kwa mtoto zinasababisha madhara makubwa kwa mtoto na kwa mama pia na kupunguza nguvu ya kinga ya asili.

Siku za karibuni ameibuka mwanasayansi daktari wa Kijerumani, Matthias Rath ambaye anadai kwamba tatizo kubwa la UKIMWI kwa kila binadamu ni upungufu wa vitamini na virutubisho mwilini. Anasema kwamba asilimia 90 ya binadamu wote kwa ujumla wanakosa aina moja au nyingine ya virutubisho au vitamini. Ukosefu huu unasababisha udhoofu wa mwili na hivyo unapokutana na visababishi magonjwa basi mwili unadhoofu kwa haraka sana. Dr. Rath pia anasema dawa za makampuni ya magharibi za aina zozote zile ni biashara tu humfanya mgonjwa akawa tegemezi kwazo na hivyo kuongeza biashara za kampuni hizo. Dawa za kupunguza makali ya UKIMWI nazo hazina tofauti na nyinginezo. Ni biashara, na kwa vile unatakiwa kuzitumia maisha yako yote basi ni biashara babu kubwa. Badala yake yeye anasisitiza matumizi ya vitamini na virutubisho vinginevyo.

Kuonyesha jinsi vitamini zake zinazofanya kazi, amefanya utafiti kwa kuwapa waathirika vitamini hizo katika eneo moja la watu masikini huko Cape Town. Katika waathirika 18 aliowapatia tiba hiyo wote wakiwa hoi kabisa wamepata nafuu ya ajabu wameweza kurudia kazi zao bila kutumia chochote zaidi ya virutubisho. Baada ya kuona kwamba ameanza kutangaza tiba yake, kundi linalojiita wakereketwa wa dawa za ARVs wameamua kumtundika mahakamani ili aache kutangaza tiba yake. Kesi bado ingali ikiendelea sasa mahakamani. Umoja wa mataifa pia umetoa taarifa ya kulaani matangazo yake na nchini kwake Ujerumani wamezuia matangazo yake la sivyo atalimwa faini ya Euro 250,000. Tatizo ni lile lile, wanaopigana ni mafahali wa nchi za magharibi wanaoumia ni waathirika hoi wa nchi za Afrika. Hapa ndio kuna swali tena zi wapi serikali zetu kuwekeza katika tafiti? Wako wapi wanasayansi wetu angalau kutoa tamko lisilo na uegemezi wa upande mmoja?

Kilicho wazi hapa ni kwamba iwe mvua au jua, iwe masika au kiangazi iwe elininyo, tsunami au kingine chochote, kuna mkono wa biashara. Wazalishaji wa ARV’s watapenda kulinda biashara yao ya dawa wanapata mabilioni kumbuka. Huyu mwingine naye atataka kutangaza tiba yake ya vitamini apanue soko lake. Wanasayansi watafiti nao wana maslahi yao. Kuna ushahidi kwamba kwa sasa wanasayansi wengi wanaotafiti UKIMWI wanafadhiliwa na kampuni za dawa. Wanasayansi wengine pia si kwamba wana usongo sana na kutatua matatizo ya jamii wanataka sifa zao za kitaaluma ziongezeke. Wanataka machapisho yao yaonekane kwenye majarida ya kisayansi, watataka kuitwa guru wa UKIMWI kwa kuandika na wengine kumnukuu watataka kukumbukwa kwa kufanya hiki na kile . Yote haya yakiendelea Waafrika masikini ambao ndio waathirika wakubwa wa tatizo hili wanaendelea kuumia.

Kwa nini sasa umoja wa mataifa na makampuni makubwa ya dawa yawe mwiba mkali kwa utafiti mbadala? Ingebidi umoja huu utafute mbinu za kuweka tafiti hizi pamoja ili zilenge kusaidia jamii kama kweli jamii ndiyo mteja wao, badala yake wamekuwa wakipinga kila jitihada au wazo lililo tofauti na lile la kampuni za dawa. Kuna ubaya gani kukawa na utafiti wa kupunguza sumu iliyopo kwenye ARV’s kwa kuongeza vitamini? Huo ndio utafiti wa maana. Huko ndiko kufanya kazi kwa pamoja. Tukiacha kila mmoja afanye kivyake tutakuwa na tatizo la msingi hapa. Kila mmoja atataka kuonekana guru katika utafiti wake na matokeo yake ni kwamba hakutakuwa na makubaliano hasa pale kundi moja litakapoona maslahi yake ya kibiashara yakipungua.

Kuna wengine ambao ni wahojaji hafifu, watakuuliza, hivi kama dawa hizi ni biashara mbona tunapewa misaada na hizo nchi tajiri? Hili tatizo la uelewa wa siasa za misaada ya nje. Cha kuelewa hapa hakuna cha bure kila shilingi unayopata ya bure inaweza kuzaa mara tatu au nne. Unapopewa msaada wa dawa kama hizi za kutumia maisha yako yote ujue kwamba hutapewa msaada huo mpaka mwisho. Utapewa sehemu tu serikali au wewe mwenyewe utatakiwa kununua kiasi kingine baadaye. Usidhani kwamba hizo dawa hutengenezwa kwa gharama kubwa kiasi hicho. Kiasi utakachonunua kinatosha kurudisha gharama na faida yao. Hata kama hutalipia kwenye dawa, utanunua mashine, utanunua silaha, utanunua ndege ya Rais na kadhalika. Mahesabu yanakatana humo humo. Isitoshe, nyingi ya dawa hizo hutengenezwa kwa kutumia rasilimali na pengine miti shamba toka Afrika. Hili suala la misaada ya nje litakuwa mada inayojitegemea. Kwa sasa nakuacha ukijua hakuna bure. Umeshalipa au utalipa kwa njia moja au nyingine. Kama si wewe watoto wako watalipa. Wenzetu wana mipango ya muda mrefu hawafikirii karibu kama sisi, hawatafuti umaarufu wa matumbo yao kwa kipindi cha miaka mitano, wana ajenda za miaka mingi.

Kuna haja kubwa kwa serikali kuwaenzi wanasayansi wetu, gharama za tafiti ni kubwa, lakini si kwamba haziwezekani. Kuna haja ya tiba asilia kuimarishwa, kutafitiwa. Ni lazima jitihada za kuungisha tiba asilia na za kisasa zifanywe. Hapa lazima ujue ukitegemea pesa za misaada hutakaa uzipate hata siku moja nani anayetaka kupoteza soko lake? Kila mmoja anataka fedha, kila mmoja anataka kwake kuwe kuzuri kuliko kwako. Kila binadamu ni mchoyo, huo ndio ukweli na asili ya binadamu. Usitarajie mzungu aje atatue matatizo yako, sanasana atatumia matatizo yako kutatua ya kwake. Hawa Wazungu ni matajiri wa umasikini. Wanatumia umasikini wetu kujitajirisha. Hakuna cha kufanya, bila kutafuta fedha za tafiti na kuacha kudhalilisha wanasayansi wetu kwa kuwafanya wahubiri na wakusanya takwimu badala ya watafiti. Tusipowatumia tumekwisha Wazungu watakuja na dawa zao na kutufanya nguruwe
wa majaribio na kutuuzia dawa zao zenye sumu ya ajabu zinazotengenezwa kwa kutumia miti yetu wenyewe.

Ni lazima tumpongeze Rais Mkapa, kwa juhudi alizozionyesha kupambana na GONJWA, hili, lakini pia tukumbuke kwamba bado kuna kazi kubwa. Badala ya kuendeleza malumbano ya kutumia au kutotumia kondomu, badala ya kunyosheana kidole cha uzinzi na unyanyapaa, badala ya kasumba ya uaminifu na kujinyima, ni bora kukaa chini kama taifa na kupanga mipango imara ya kupambana na Gonjwa hili na hasa huu utata unaolizunguka gonjwa hili.

Na,
Padri Privatus Karugendo.

1 comments:

Unknown said...

wewe mtumishi wa mungu nakuheshimu sana hua unanifungua akili sana na makala zako asante
Padri Privatus Karugendo.

Post a Comment