TANZIA HII ILITOKA KWENYE GAZETI LA TANZANIA DAIMA JUMAPILI 2005.
UA LETU LIMEPUKUTIKA!
Dr. Rose Chinkuaile Katesigwa, wa hospitali ya wilaya ya Magu, Mwanza, anapenda kuwatangazia ndugu, Jamaa na marafiki kwamba Ua lililochanua na kupendeza na kuwavutia wengi kwa kipindi cha zaidi ya miaka 89, Ua, lililoipamba Bushangaro, Karagwe na kuwavutia watu wengine wa Bukoba hadi Dar-es-Salaam, Kampala hadi Nairobi na hata nchi za mbali kama Holland, Germany na Uingereza, limepukutika! Kama ndoto, lakini ni kweli kwamba Mzee Paulo Katesigwa Birusya, Ua lililopendwa na kila mtu, aliaga dunia tarehe 6.7.2005 katika hospitali ya Nyakaiga-Bushangaro-Karagwe na kuzikwa tarehe 8.7.2005 kijijini kwake Kibondo. Mamia kwa mamia ya watu walifika kwenye mazishi yake, wakiwemo viongozi wa vyama na serikali, mapadri, masista, watu kutoka vijiji vya mbali na karibu, “Pande na pande” msemo wa marehemu! na wapitanjia!
Madaktari, waganga na wauguzi wa hospitali ya Nyakaiga, walifanya kila waliloliweza kuyaokoa maisha ya Mzee Paulo Katesigwa Birusya, lakini mapenzi ya Bwana yalitimia. Yeye ndiye anayepamba, Ua likapendeza na kuwavutia wengi, lakini saa ikifika yeye mwenyewe ndiye anayewezesha Ua linyauke na kupukutika! Ndio maana Dr. Rose Katesigwa, mtoto wa mwisho kati ya watoto nane walio hai wa Marehemu Mzee Paulo Katesigwa Birusya, aliyeshuhudia jitihada za madaktari, waganga na wauguzi wa hospitali Nyakaiga,walizozifanya kuyaokoa maisha ya marehemu baba yake, jitihada kama zile anazozifanya yeye mwenyewe kwenye hospitali yake ya Magu, kuyaokoa maisha ya watanzania wengine na wakati mwingine wengine wanapona na wengine Mungu anawapenda zaidi na kuwaita kwake; kwa niaba ya familia nzima ya Marehemu Mzee Paulo Katesigwa Birusya, anatoa shukrani zake kwa njia ya Tanzia hii.
Shukrani hizi zinawaendea pia na wote waliofika kwenye mazishi, kuwafariji wafiwa na wote waliotuma salamu za rambirambi na kushiriki msiba huu kwa njia moja ama nyingine. Ni vigumu kumshukuru kila mtu. Shukrani haziozi, maana tanzia hii imechelewa kidogo!
Hivyo tanzia hii, pamoja na kutoa taarifa za msiba huu mkubwa ni ya shukrani. Lakini pia inalenga katika kujenga utamaduni mpya wa kuandika tanzia katika magazeti si kwa waheshimiwa wabunge, mawaziri, maprofesa, mabalozi, maaskofu mashehe, vigogo wenye pesa tu, bali pia na kwa wazee wetu wa vijijini wanaotoa michango mikubwa katika kuliendeleza taifa letu la Tanzania. Ingawa michango ya wazee hawa haionekani wazi, japokuwa wengine ni muhimu sana wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu, wana mchango mkubwa kama ulivyo msingi kwenye nyumba yoyote ile!
Marehemu Mzee Paulo Katesigwa Birusya, alikuwa mmoja wa wazee hawa ambao ni misingi katika jamii. Mzee huyu alikuwa na majina mengi, na kila jina lina umuhimu wake katika jamii . Miongoni mwa majina yake mengi ni:Maganda, Arabika, Robusta na Harambee.
Mzee huyu aliamini kwamba kilimo cha kahawa kinaweza kuchangia maendeleo ya haraka katika jamii ya wanyamo na mkoa mzima wa Kagera. Hivyo aliwahimiza watu kulima kahawa. Kuna aina mbili za kahawa zinazooteshwa Karagwe na karibu sehemu zote za mkoa wa Kagerra. Aina hizi ni Arabika na Robusta. Kaulibiu ya Mzee Paulo Katesigwa Birusya, ilikuwa “ Arabika na Robusta” hadi akabatizwa majina hayo. Ni kweli watu wengi walilima kahawa kwa kumsikiliza, na hivi sasa wanakula matunda ya kaulimbiu ya “Arabika na Robusta”!
Kahawa ambazo hazikukobolewa zinajulikana kwa jina la Maganda. Wakulima wa kahawa wa Karagwe, wana chaguo la kuuza Maganda au kuuza kahawa zilizokobolewa. Zoezi la kukoboa kahawa ni gumu sana, linachukua muda mwingi na pesa nyingi. Kufuatana na bei ya kahawa kuwa ya chini, Mzee Paulo Katesigwa Birusya, aliwashauri watu kuuza Maganda. Wengi walikubali wazo lake, na kumbatiza jina la Maganda.
Marehemu Jommo Kenyatta, aliyekuwa Rais wa kwanza wa Kenya, alikuwa na kualimbiu ya Harambee, katika jitihada zake za kuhimiza maendeleo katika nchi ya Kenya. Mzee Paulo Katesigwa Birusya, aliipenda kaulimbiu hiyo na kuitumia kuwahimiza vijana kufanya kazi. Hakupenda vijana wawe “tanga tanga”. Kwa umri wake wa zaidi ya miaka 89, alikuwa akifanya kazi kwenye shamba lake kila siku ya Mungu. Historia yake ni ya kufanya kazi. Alianza kufanya za kujitegemea akiwa na umri mdogo wa miaka kumi katika migodi ya Tin, kule Kyerwa Karagwe, baadaye alienda kufanya kazi nchini Uganda, kwa kutembea kwa miguu kutoka Karagwe hadi Uganda. Alifanya pia biashara ya kuuza mafuta ya samli aliyokuwa akiyafuata kwa miguu kutoka Rwanda na Burundi. Ingawa hakukuwa na majokofu wakati ule, lakini watu waliweza kubeba samli kwa mwendo mrefu tena kwenye jua kali. Utaalam huo sasa umepotea. Hivyo jina la Harambee, ilikuwa ni ishara ya kuchapa kazi. Alitaka vijana kuchapa kazi, kama wazee walivyochapa kazi.
Ingawa mzee huyu hakuenda shule, ni mzee aliyekuwa na upeo mkubwa wa kufahamu mambo mengi. Alihimiza elimu na kuchangia ujenzi wa sekondari iliyo katika kijiji chake. Ni mzee ambaye hata ungeongelea vita vya Iraq, au juu ya Bush, utandawazi, soko huria, vyama vya kisiasa, angeweza kufuata na kuchangia. Kufuatana na maelezo yake, alisoma hadi darasa la pili. Alizoea kusema “ Iwe shule okandema kake” akiwa na maana ya “ Wewe shule ulinishinda kidogo”. Wazungu waliomtembelea nyumbani kwake walistaajabu uwezo wake wa kufahamu mambo na kuyachambua.
Mzee huyu alipenda kutunza muda na tarehe. Kwenye kalenda kila siku ipitayo alikuwa akiifuta. Hivyo ukiangalia kalenda yake ya mwaka huu, utafahamu ni lini aliugua sana. Hakuna mtu mwingine aliyekumbuka kuendelea kufuta tarehe kama alivyokuwa akifanya yeye. Alipoachia, ndio hapo hadi kufa kwake!
Utamaduni wa karibu sehemu zote za mkoa wa Kagera, ni kwamba akifa mzee wa umri mkubwa wajukuu hucheza ngoma na kufanya utani. Kwa mzee Paulo Katesigwa Birusya, ilikuwa tofauti. Badala ya kucheza ngoma na kufanya utani wajukuu walilia hata kuwazidi baba zao na mama zao. Walilia kiasi cha kumgusa kila mtu hata na yule anayelia mara moja katika maisha yake.
Umri wa Mzee Paulo Katesigwa Birusya, ulikuwa mkubwa, kila mtu alilijua hilo, lakini hakuna aliyetegemea kwamba Ua zuri hivyo, lingepukutika mapema hivyo. Wema, huruma, ushauri, upendo na ukarimu wa Mzee Paulo Katesigwa Birusya, ulifunika macho ya watu kuona ukweli wa afya yake na umri wake. Mawazo ya mke wake Bi Paulina Rutegaisa Katesigwa, yalifanana na ya kijana wake Bwana Karoli Majaliwa, aliyeamini baba yake mkubwa Mzee Paulo Katesigwa, angeweza kuendelea kuishi zaidi ya miaka kumi mbele. Kifo, kilipokuja kama vile mwizi wa usiku, si Majaliwa, Bi Paulina na wala si Renatha George Ramadhani, mjukuu ambaye hata leo hii hakubali kwamba babu yake ni marehemu, walioshangaa na kuumia, ni familia yote, ndugu jamaa na marafiki walishtushwa na kusikitishwa na kifo cha Mzee Paulo Katesigwa Birusya. Kumpe duniani tunapita. Sote ni maua, yanachanua na kupendeza, lakini wakati ukifika yanasinyaa na kupukutika. Kama mizizi ni imara, yatachanua maua mengine. Hivyo ndivyo tunavyoishi kwa matumaini.
Mungu, ailaze pema peponi roho ya mzee wetu Paulo Katesgiwa Birusya,Maganda, Arabika, Robusta, Harambee!
Na
Privatus Karugendo
0 comments:
Post a Comment