MAKALA HII ILITOKA KWENYE GAZETI LA TANZANIA DAIMA JUMAPILI 2005.
WILAYA MPYA KWA MTIZAMO UPI?
Rais Mkapa anamaliza Muda wake na kuondoka zake. Atakumbukwa kwa mengi, mazuri na mabaya. Wengine wamembatiza jina la Mzee wa Utandawazi, Uwekezaji, Ubinafsishaji. Wengine wanamwita mzee wa Kiingereza, kwa jinsi anavyojua kuimudu lugha hii. Hakuna shaka juu ya uzalendo wake na mapenzi yake kwa taifa letu. Wale waliokubaliana na kila alichokifanya watamkumbuka kwa mema. Wale watakaokuwa wa kweli na kuona kwamba kuna aliyofanya mazuri na kuna aliyofanya mabaya watapima. Kama mazuri yatazidi mabaya watafunika mabaya. Kama mabaya yatazidi mazuri yatafunika mazuri. Ingawa binadamu tulivyo, baya moja linaweza kufunika mema hata kama ni elfumoja. Ukweli ni kwamba wanafiki tu ndio watakaosema kila alichofanya ni kizuri. Bahati mbaya namba ya wanafiki, hasa wakati wa kuagana na mtu ni wengi. Watajitahidi kuyafunika mabaya na kuyataja mazuri. Watu kama hawa si msaada kwa maendeleo ya taifa letu ambalo bado ni changa na linahitaji kukua kwa kila hali. Na wale watakaosema kila alichofanya ni hovyo nao hawatamtendea haki. Na si kwamba hawatamtendea haki Rais Mkapa, peke yake, bali hawatalitendea haki taifa letu. Ni ukweli kabisa kwamba yapo mazuri mengi yaliyotendeka wakati wa hawamu hii inayoelekea ukingoni.
Moja ya mambo atakayokumbukwa nayo Rais Mkapa ni kugawa baadhi ya wilaya na kuanzisha mpya. Alianzisha pia mkoa mmoja mpya, mkoa wa Manyara ambao ulileta kelele nyingi na kuonyesha kwamba kumbe watanzania bado tumegawanyika katika makundi madogo ya kikabila. Ilikuwa ni kazi ngumu kupata jina la mkoa na makao makuu. Pia ilikuwa kazi ngumu kuamua mipaka ya mkoa. Yeye mwenyewe na wale wanaokubaliana naye wanajenga hoja kwamba kuanzisha wilaya au mkoa mpya ni kusogeza huduma karibu na wananchi. Hili linawezekana kabisa likawa kweli. Ukiliangalia kwa haraka bila kutafakari, bila kuzingatia maendeleo ya teknolojia na ubora wa miundo mbinu, unaweza kusema kwamba ni kweli, ni kweli kwamba ni kusogeza huduma kwa wananchi. Lakini ukiliangalia kwa undani ni tofauti. Ukweli au uongo wa jambo hili utaeleweka kama tutaweka mizania kwa vigezo vidogo vya kiuchumi. Unapoanzisha wilaya mpya unaunda utawala mkubwa. Unajenga ofisi, unakuwa na Mkuu wa wilaya, mkurugenzi, afisa utawala, afisa mipango, afisa maendeleo na wafanyakazi wengine wengi, hawa wote wanahitaji huduma za kiwilaya, wanahitaji magari, nyumba nk., unanunua vifaa vya ofisi na gharama nyinginezo. Unaongeza gharama za utawala kwa miaka yote itakayodumu ile wilaya. Kwa maneno mengine kuanzisha wilaya ni kuwabebesha wananchi mzigo mzito. Ni kurudisha maendeleo nyumba, badala ya kuyaendeleza. Sote tunajua kwamba katika bajeti ya wilaya, kifungu kikubwa kinatumika kuendesha maofisi, kununua magari, kununua mafuta na matengenezo ya magari.
Ulipoundwa mkoa wa Manyara sababu moja ilikuwa ni kwamba kuna umbali toka katika baadhi ya wilaya hadi makao makuu ya mkoa. Kwanza unaanza kujiuliza? Mkoani wanatakiwa wafuatilie nini kwa kiasi hicho? Kama suala ni la kazi sasa hivi kuna mitandao ya kisasa ya mawasiliano. Cha muhimu ni kuwekeza katika teknolojia sahihi kukwepa safari zisizo za lazima. Ni kujitahidi kujenga barabara ambayo itarahisisha usafiri toka kituo kimoja kwenda kingine. Suala si kuanzisha mkoa na gharama zake kubwa za kiutawala. Zamani ulikuwa ukisafiri toka dar hadi Songea kwa Masaa siyo chini ya 24 kisa barabara. Leo unaondoka asubuhi jioni umefika. Makao makuu ya hayajaamishwa lakini masaa ya safari yamepungua. Teknolojia inavyouwa wala huitaji kufanya safari zisizo za lazima. Suala ni kupima gharama za kuanzisha wilaya mpya au mkoa na kuimarisha miundombinu.
Jambo la kushangaza ni kwambal hata na maeneo ambayo miundombinu ni mizuri, zimeanzishwa wilaya mpya. Mfano kuigawa Wilaya ya Hai, katika wilaya mbili ina maana gani? Mawasiliano kati ya wilaya na wilaya ni mazuri, na umbali kutoka wilaya hadi nyingine ni mfupi. Kwa misingi ya kiuchumi, tukiweka mbali mambo ya siasa, kuitenga wilaya ya Hai, katika wilaya mbili ni hasara tupu. Mtu angetegemea Kyerwa, kuwa wilaya kabla ya Misenyi. Miundo mbinu na mawasiliano ya Kyerwa ni mabaya zaidi ukilinganisha na Misenyi. Hata Chato, ingesubiri, ukilinganisha na Kyerwa. Lakini la kushangaza, Misenyi na Chato zimeitangulia Kyerwa. Kawaida tunasema kwamba Njia za Mungu, si sawa na za Binadamu – labda na njia za Viongozi si sawa na za wananchi!
Kwa nini kila wakati Mkuu wa Wilaya aende mkoani? Kwanini tuwe na mikoa? Kwa nini mambo mengi yasiishie huko huko. Mambo yakaishia wilayani, badala ya kuanzisha mikoa mipya, ikapunguzwa au kufutwa kabisa. Mimi nilidhani katika hali hii ya kupeleka madaraka karibu na wananchi mikoa inafutwa sikuwahi kufikiri kuna mtu ataongeza. Na kila wakati nilikulwa na mawazo kwamba mpango mzima wa Maboresho, wa kupeleka madaraka kwa wananchi ulikuwa na lengo hilo hilo la kufuta mikoa na kuongeza uwezo wa kutenda wa milaya zilizopo na wala zi kuunda wilaya na mikoa mipya. Ukiweza kuimarisha tarafa zako huhitaji kugawa wilaya. Mambo yatamalizwa huko huko. Huitaji kila siku kuchapa miguu kutembelea maeneo. Safari zenyewe zinazofanywa na viongozi ni gharama mno. Kwa mfano rais anapofanya ziara ya mkoa mmoja kwa siku tatu inawezekana gharama zake zikawa sawa na kujenga visima vitatu vya maji katika wilaya. Kukiwa na huduma za msingi kama vile shule, zahanati nakadhalika na kukishakuwa na miundombinu mizuri kama barabara gharama za usafirishaji zitapungua, wanunuzi wa mazao wataweza kwenda kwa kirahisi vijijini kununua mazao na mambo kama hayo. Lakini ukishamweka mkuu wa wilaya na mlolongo wa watu wake pale ni kitu gani watakachofanya kuharakisha hiyo miundombinu? Wengine watasema kwamba ni kuhamasisha wananchi ili kujiletea maendeleo. Ukweli ni kwamba wananchi wanahamasika zaidi katika ngazi za chini kinyume na kuamini kwamba mkuu wa wilaya anaweza kuhamasisha zaidi. Vijiji vingi vyenye maendeleo makubwa vimepata msukumo kutoka kwa wanavijiji wenyewe bila kelele wala bugudha za mkuu wa wilaya.
Hoja inayojengwa hapa ni kule kupanga na kuchagua ni kipi chenye manufaa ya muda mrefu kwa nchi. Nadhani kwa lugha yoyote ile miundombinu kama vile barabara, mawsiliano ya kisasa ni rahisi na uwekezaji wa muda mrefu kuliko kujenga majengo mawili na kumweka mtu unayemwita mkuu wa wilaya na ofisi yenye kugharimu mamilioni kila mwaka. Fedha za utawala zingeweza kutumika kuwekeza katika miundombinu ambayo ingerahisisha mawasiliano badala ya kuendeleza ukiritimba wa safari za kila mara kwendamkoani au makao makuu ya wizara. Sidhani kama kuanzisha wilaya au mkoa mpya kunaweza kuharakisha maendeleo. Kuna wilaya zilizoanzishwa miaka mingi iliyopita lakini hadi leo hazina tofauti na wilaya au makao makuu ya tarafa ambazo kuna mawasiliano mazuri.Wilaya nyingine zilizoanzishwa katika mtindo huu wa kuwazawadia watu wilaya zimekuwa mzigo mkubwa na sehemu nyingine ni aibu tupu, nyingine zina umri wa zaidi ya miaka kumi, lakini zina majengo mabovu na utendaji uziopendeza. Kinachotakiwa kwa sasa ni kuweka mazingira yatakayovutia vitega uchumi (siyo vitega uchumi vya wazungu) na kwa njia hiyo maendeleo yataharakishwa pasi na haja ya kuongeza mlolongo wa kiutawala ambao ni ghali kupindukia. Mkuu wa wilaya, anataka aisha kama mkuu wa wilaya,mkurugenzi anataka aishi kama mkurugenzi. Na viongozi wote wa wilaya wanataka waishi kwenye ngazi yao bila tofauti na viongozi wengine wa wilaya nyingine. Haya yote yanaongeza gharama kubwa na mzigo mkubwa kwa wananchi.
Leo hii kutokana na ukiritimba wa kila kitu kutaka kifanyike katika makao makuu ya uhamiaji tunapoteza mamilioni ya saa za uzalishaji kwenda kupiga foleni kwa ajili ya pasi mpya. Hii inatokea wakati ambapo kuna wimbo wa kuimarisha mamlaka za chini. Kama ukipiga hesabu rahizi ya masaa ambayo yanapotezwa kwa ajili ya kufuata pasi mpya basi inawezekana yamepotea mamilioni ya fedha. Lakini kwa Tanzania nani anayejali? Yote haya yakitokea kuna rushwa ya hali ya juu inaendelea shauri ya ukiritimba huo wakati ambao Serikali inaimba utawala bora.
Nina imani Rais Mkapa, alikuwa na nia njema kwa kuanzisha wilaya mpya, ila kwa mtu yeyote anayeangalia maendeleo ya taifa letu kwa kuzingatia misingi yote ya uchumi, atatilia shaka nia njema ya kuanzisha wilaya mpya. Si nia yangu kumhukumu Rais Mkapa, labda mengi aliyafanya kwa bahati mbaya. Na inawezekana kabisa nia yake ilikuwa ni jema kama yeye anavyosisitiza daima. Kwa vile hili limekwishatendeka, basi iwe fundisho kwa rais anayekuja kuwa makini zaidi na kusitisha zoezi hili kama lilikuwa katika mpango wa kuendelea zaidi. Badala ya kuanzisha wilaya mpya na mikoa, tuboreshe miundombinu.
Na,
Padri Privatus Karugendo
0 comments:
Post a Comment