ATATOKEA JASIRI?

MAKALA HII ILITOKA KWENYE GAZETI LA TANZANIA DAIMA JUMAPILI 2005.

Atatokea Jasiri wa Kuamua suala la Makao Makuu?

………Mheshimiwa Spika kabla ya kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mchokonoa Mambo, mbunge wa Uchokozini, naomba nitoe maelezo yafuatayo: Ni kweli kabisa kwamba Serikali iliamua kuamia rasmi Dodoma mwaka 1973. Ni zaidi ya miaka 30 sasa tangu maamuzi hayo yalipotolewa. Kipindi hiki si kirefu sana, japo ukweli ni kwamba kwa mtoto aliyezaliwa mwaka huo sasa naye anaweza akawa na mtoto aliyeanza shule na ambaye anaweza kuchanganyikiwa kabisa kama ataambiwa Dodoma ndiyo makao makuu ya Tanzania.

Serikali imefanya juhudi nyingi kabisa. Kwanza imeanzisha CDA. Lengo likiwa ni kustawisha mji wa Dodoma. Pamoja na kuwa na CDA ambayo mikoa mingine haina bado kasi ya ukuaji wa Dodoma ni ndogo. Yaani hata ile miji ambayo ina manispaa tu bila CDA imekuwa haraka kuliko Dodoma. Kama mtakumbuka pia tulianzisha viwanda vingi vilivyokuwa chini ya CDA lakini kama vingine vimekufa. Vingine vimeuzwa kwa bei ambayo wawekezaji ambao baadhi yenu siku hizi mnawaita waezekaji eti mnadai kwamba hawajajenga chochote wanaezeka tu vile ambavyo tulikwishajenga walipanga wao. Kile kiwanda cha vigae kwa kweli kilikufa kwa sababu ya kushindwa ushindani. Si waheshimiwa wabunge mnajua kabisa nchi yetu ilivyo? Si mara ya kwanza kabisa. Sababu ni kwamba vigae vya nje ni bei nafuu kuliko vilivyokuwa vinazalishwa hapo. Na hii si ajabu kabisa, hata mchele toka Thailand si mnaona ni bei rahisi kuliko wa Kyela? Usafiri Kyela ni mgumu kweli kweli. Ndivyo ilivyokuwa kwa vigae vyetu hapa Dodoma. Na pia kuna hii kasumba ya watanzania kutopenda kabisa vitu vya kwao. Tabia hii Waheshimiwa wabunge hata sisi tunayo. Tena sana. Hata hapa tulipo huwezi kuona aliyevaa nguo iliyotengenezwa hapa nchini. Hata majumbani kwetu tukienda leo kila kitu kitakuwa kimeagizwa toka nje. Hii kasumba sijui itatufikisha wapi. Ukiangalia kiundani kabisa hata sheria na kanuni tunazotumia hapa bungeni si za kwetu ni na nje. Sasa kwa mtaji huu kweli hata hivyo viwanda vingedumu?

Juhudi nyingine ni zile za kukamilisha jengo la Chimwaga. Jengo hili hata hivyo halijakamilika vizuri. Labda kwa kukumbusha tu, Chama Twawala kiliiuzia Serikali jengo hili kabla ya kumalizika na hadi leo Serikali inaendelea kulijenga ili liishe. Lazima nikiri kwamba hatujui hata jengo litatumikaje likiisha kwa kuwa hadi sasa ni mikutano mikuu ya chama Twawala tu ndiyo inafanyikia hapo. Hata hivyo ni lazima nikiri kwamba huenda tukapata namna nzuri ya matumizi yake. Na nyie waheshimiwa wabunge mjitahidi kufikiria namna nzuri ambayo tunaweza kulitumia.

Baada ya maelezo haya sasa nikuambie kabisa kwamba Waziri Mkuu amehamia Dodoma siku nyingi sana. Nasikia wengine mnaguna, lakini ukweli ni kwamba Waziri Mkuu kaishaamia hapa. Mtakumbuka alitangaza ndani ya bunge hili hili. Lakini kama mjuavyo kazi nyingi za Serikali zinafanyika DSM kwa hivyo inabidi wakati mwingi akae huko. Mnajua wazi kabisa kwamba ndiye mshauri mkuu wa rais haitakuwa busara hata kidogo yeye awe hapa na Rais awe Dar es Salaam. Kwa kweli hilo halihitaji mjadala zaidi. Ni lazima tukubali gharama nyingine jamani. Lakini pia Wizara ya TAMISEMI, Maji na Mifugo pamoja na Ushirika na Masoko zimeamia hapa kabisa. Japo mawaziri na maafisa wote wakuu wanakuwa DSM muda mwingi kutokana na sababu zile zile nilizoeleza hapo juu. Serikali inajaribu kubana gharama sana. Wizara nyingine zitakuwa zinahamia taratibu.

Kuna sababu nyingine ambayo hatuwezi hata siku moja kutamka kwamba tutaacha kuamia Dodoma. Unajua tumeshawahakikishia wananchi kwamba nia ya Serikali ni kuhamia Dodoma. Sasa tukibadilisha ghafla, kura za kanda ya kati zote tutazikosa. Nani yuko tayari kukosa kura hizo? Hata nyie wapinzani mnaoguna mnajua wazi kabisa kwamba hamuwezi kutamka hilo kwenye kampeni zenu. Mnajua kabisa mtakosa kura. Mwenye ubavu na asimame kwenye kampeni aseme hatuamii makao makuu.

Wengine mnajua kabisa hata Nigeria iliwachukua miaka mingi kuhama toka Lagos kwenda Abuja. Brazil nao iliwachukua muda. Australia nao pia. Ya kwetu si ajabu. Mnajua kabisa kwamba sisi ni watembeza mabakuli wazuri kwa wafadhili. Na wao wamegoma kuamia hapa. Hivi mnataka serikali ikiamia hapa hiyo asilimia 41 ya bajeti toka kwa wafadhili ifidiwe na nini? Ni lazima tukae karibu nao ili tupenyeze bakuli zetu. Tukikaa mbali ni ngumu. Waheshimiwa ni lazima mkumbuke kwamba nchi yetu ni masikini kwa hivyo msitarajie tukaweza kukaa mbali na wafadhili. Na mnajua wazi kabisa mabalozi na wafanyakazi wa mashirika mbalimbali ya kimataifa hawawezi kuishi mbali na bahari. Kwa hiyo ni lazima tuwasikilize.

Mtakumbuka kwamba tunajenga nyumba 300 kwa ajili ya watumishi wa Serikali. Hii inaonyesha kabisa kwamba tuna nia japo wengine wanadai kwamba hata zile nyumba zilizojengwa na mashirika kama ya NSSF ilichukua muda kupata wapangaji. Ni kweli mji unakua taratibu na sasa tutawalazimisha watu wakae Dodoma hata kama Rais hatakuwa ameamia Dodoma.

Hayo ndiyo majibu ya Mheshimiwa Waziri. Ukishayasoma majibu haya utachanganyikiwa wala si kidogo. Utauliza swali la nyongeza kama mtu wa mtaani. Hivi ukiifungua Dodoma kwa kujenga barabara itakuwaje? Kwa mfano ukaacha hizo ngonjera zote za nyumba za serikali na mengineyo ukaamua kujenga barabara ya Dodoma Arusha, Dodoma Iringa, uone kama Dodoma haitafunguka. Kitakachoendelea hapo ni kwamba Dodoma haitahitaji CDA kuiendeleza. Dodoma haitahitaji waamiaji wa siku za bunge na Mkutano wa CCM kuongeza kipato. Kipato cha Dodoma kitakuwa cha kudumu. Kutakuwa na ongezeko kubwa la shughuli za kiuchumi na jamii. Wananchi wa Dodoma watafaidika na miundombinu kuliko kipato cha mpito cha siku za bunge. Hayo mapesa wanayolipwa maofisa wa Serikali wanaojifanya wamehamia Dodoma kumbe kimsingi wako DSM zingetumika kuboresha miundo mbinu. Kungejengwa huduma za jamii kama chuo kikuu kimoja basi Dodoma ingekuwa kitu tofauti kabisa.

Ngonjera za kukosa kura kwa wananchi wa Dodoma zingeisha. Wananchi wangeona maendeleo ya kweli na dhamira ya kweli kwa kujengewa miundombinu na siyo hadithi za nyumba 300. Huu mtindo wa kudanganya watu sijui utaisha lini. Ngonjera za kwamba kasi inakwamishwa na upungufu wa fedha itaendelea tu lakini ukweli ni kwamba hakuna mwenye nia ya kuishi Dodoma. Huo ndio ukweli. Dodoma kwa sasa haikaliki. Kama hakutakuwa na mpango wa kuifungua Dodoma na kuiunganisha kwa barabara imara na mikoa mingine basi usitarajie mji huo ukue. Tutadanganyana na majibu ya nyongeza ambayo hayatatosheleza milele. Ifike mahali tufanye tathimini ya mradi wa kuhamia Dodoma umefika wapi. Tuache siasa za majukwaani. Mradi gani usiokuwa na tathimini? Tujue tumetumia mabilioni mangapi. Ni mangapi yamebaki kutosha kuhamishia makao hayo. Na chanzo cha fedha ni kipi.

Rais ajaye ni lazima awe na ujasiri wa kufanya maamuzi haya. Awe jasiri kama Ariel Sharon aliyeamua kuhamisha makazi ya walowezi ya Ghaza. Pamoja na ubabe wake bado ninamuona ni jasiri kuliko Waziri Mkuu mwingine yeyote wa Israeli. Kila aliyemtangulia alikuwa anakuwa na kigugumizi cha kufanya maamuzi haya. Ya Tanzania na makao makuu nayo inahitaji ujasiri. Ujasiri angalau wa kusitisha hilo zoezi kwa muda mpaka hapo mambo yatakapokuwa mazuri au hapo ambapo Dodoma itakuwa imekuwa vya kutosha na kuvutia watu kuhamia, au kama ana ubavu ajitose yeye akae Dodoma na tuone wizara ambayo haitahamia huko. Hili la pili ni gumu sana kwa vile mji ule haujawa tayari kupokea watu wote hao. Kama tutapata rais anayeonea fedha za Tanzania huruma atafanya maamuzi ya busara kwa zoezi bandia la kuhamia Dodoma wakati watu wanakaa DSM.

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment