TUSOME ALAMA ZA NYAKATI

MAKALA HII ILITOKA KATIKA GAZETI LA RAI 2006.

TUSOME ALAMA ZA NYAKATI.

Sipendi makala hii kuiita Barua ya wazi kwa Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania, nafikiri si busara na ni kutokuwa na heshima kuwaandikia waheshimiwa viongozi wa Kanisa barua ya wazi. Hivyo basi makala hii ninaiandika kwa unyenyekevu mkubwa na kwa kupima kila neno nitakalolitumia. Ninajua vizuri umuhimu na ushawishi wa maaskofu katika Jamii yetu. Nimesita sana kuandika makala hii, lakini nimesukumwa na ukweli kwamba ni lazima tusome alama za nyakati. Tukishindwa, Tukumbushane si dhambi na wala si kushambuliana, si chuki wala kinyongo – kukumbushana ni jambo muhimu sana katika jamii yoyote ile. Wengine wakikumbushwa jambo wanakuwa mbogo, maana kuna utamaduni kwamba kuna watu wasiokosea. Lakini kwa jambo linalohusu uhai wa mwanadamu, ni lazima kukumbushana hata kama inaelekea kutoa picha ya tabia mbaya, tabia ya kutokuwa na heshima kwa viongozi. Ningependa kukumbusha kwamba:

Ni lazima tuipongeze serikali yetu kwa kusimamia maamuzi yenye utata kwa faida ya watanzania walio wengi. Na kweli hii ni kazi ya serikali. Serikali ni lazima iangalie faida ya wengi na hasa jambo linalogusa uhai wa watu wake. Serikali yoyote ile inayojali uhai wa raia ni Serikali ya kupongezwa na inakuwa inatekeleza wajibu wake mkubwa. Msimamo wa serikali wa kupinga tamko la Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, ni la kupongezwa. Bila kuwa na nia ya kuonyesha aliyeshinda au aliyeshindwa maana nia ni kujali uhai wa watanzania. Kwa kutosoma alama za nyakati, maaskofu walitoa tamko la kupinga mpango wa serikali wa kufundisha matumizi ya kondomu kwenye shule za msingi. Serikali imekataa kukubaliana na maaskofu na itaendelea na mpango wa kuwafundisha watoto wa shule za msingi juu ya matumizi ya kondomu.

Ni wajibu wa serikali kutoa elimu kwa watu wake. Matumizi ya kondomu ni elimu muhimu sana maana inagusa uhai wa wananchi wote bila ya ubaguzi. Hakuna aliye huru mbele ya ugonjwa wa UKIMWI, labda yule anayeishi mwezini, na kufuatana na tamko la Maaskofu wetu, labda watoto wafundishiwe Mwezini, lakini kwa yoyote aliye kwenye jamii ya watu wa hapa duniani, hawezi kukwepa kushambuliwa, kwa kutaka yeye au kwa kutotaka. La msingi ni kujikinga kwa maana ya kujikinga, bila porojo, mchezo na unafiki. Hili linahitaji maelezo ya kina, lakini mwenye nia ya kuelewa anaweza kusoma katikati ya mistari.

Sote kwa pamoja ni lazima tusome alama za nyakati. Ukweli ni kwamba watoto wa darasa la tatu wanakuwa wanafahamu kila kitu juu ya tendo la ndoa. Kuna ushahidi wa kutosha kwamba siku hizi watoto wanapata mimba wakiwa na umri wa kuanzia miaka kumi. Hivyo maaskofu wanaposema shule za msingi watoto wana umri mdogo wa kufundishwa matumizi ya kondomu, wanajidanganya na kujifanya vipofu.

Mapadre wa Kanisa katoliki kupitia sakramenti ya kitubio ni ushahidi wa kutosha wa jambo hili. Bila kuingilia siri za kitubio. Ni imani yangu kwamba Padre wote wanafahamu vizuri kwamba tendo la ndoa linaanza katika umri mdogo. Mwanzo mtu akiwa anasikiliza maungamo kwa mara yake kwanza, anaweza kufikiri labda watoto wanatania au hawajui wanachokisema. Lakini huo ndio ukweli kwamba tendo hili linafanyika katika umri mdogo. Kuna vichocheo vingi. Video zimetapakaa sasa hivi kila mahali, kuna magazeti yenye hadithi na picha zinazoonyesha mambo ya ngono. Mtandao nao umesheheni mambo mengi kweli. Mtoto anaanza kujua na kutambua umuhimu wa tendo la ndoa akiwa na umri mdogo!
Hivyo maaskofu wasiongelee kondomu tu, waongelee na video, tv, redio, miziki, magazeti na mambo mengine katika jamii yetu. Waongelee kutengeneza mfumo wa kurudisha maadili bora.

Na tujuavyo ugonjwa wa UKIMWI umejikita sana sana akika tendo la ndoa. Kwa kuona hivyo na kwa vile serikali inajali uhai wa watu wake, ndio maana imepitisha uamuzi wa kufundisha matumizi ya KONDOMU kwenye shule zi msingi. Kinyume na hapo ni kutaka watu waendelee kufa na kuteketeza kizazi chote. Ni heri Serikali imeona hivyo, maana kwa hili sote ni wadau!

Malengo ya Maaskofu wetu ni mazuri. Hakuna anayepinga jambo hili. Sote tunajua kwamba Maaskofu ni lazima wafundishe maadili mazuri na ni lazima wahakikishe tendo la ndoa linabaki kwenye ndoa na ndoa zilizobarikiwa. Hakuna anayeweza kuwapinga wakati wanafanya kazi yao.

Utata unaojitokeza ni kwamba maadili yameanguka. Ni nani wa kubisha? Na dawa yake ni nini? Hatoshi mtu kusema kwamba wasichana wasivae nguo fupi, haitoshi kusema vijana waache vitendo vya ngono, haitoshi kukemea tu panahitajika kazi ya ziada. Kazi ya kuunda mfumo wa kurudisha maadili. Ugonjwa wa UKIMWI unapita kwenye tendo la ndoa ambalo sasa hivi linaonekana kuwa kitu cha kawaida. Tukitaka kuwa wa kweli tendo hili linaonekana kuwa la kawaida kwa watu walio wengi, viongozi wa serikali, viongozi wa dini, vijana hata na watoto wadogo. Je, tufanye nini? Tuache watu waendelee kufa kwa kusisitiza uaminifu, kujinyima na kuacha wakati ni ukweli kwamba haya ni mambo yasiyowezekana. Hapa ni lazima serikali iingilie, tena bila woga. Siku za nyuma serikali ilikuwa na woga wa kufanya maamuzi kama haya. Serikali iliwaogopa sana viongozi wa dini. Lakini woga huu umefikia mwisho maana hata na viongozi wa dini ni kelele tupu. Hawana njia nyingine. Wanabaki kuimba wimbo ule ule wa kwamba wao wanapinga matumizi ya kondomu na kwamba kuruhusu kondomu ni kuruhusu uzinzi, wanabaki pale pale kutaja amri za Mungu, na kutaja vifungu vya Neno la Mungu lakini hawaji na mfumo mzuri wa kurudisha maadili.

Si kweli kwamba mtu akifundishwa kondomu ni lazima aende kufanya tendo la ndoa. Kuna ushahidi wa watu wengi wanaofahamu matumizi ya KONDOMU, lakini hawazigusi, ila wanafahamu kwamba wakati ukifika zinaweza kuwasaidia. Siku za nyuma vijana wote waliomaliza kidato cha sita na vyuo walikuwa wanapitia mafunzo ya Jeshi, walikuwa wanakwenda Jeshi la Kujenga Taifa. Huko walifundishwa matumizi ya silaha. Walifundishwa kushika bunduki na kutumia bunduki. Silaha si kitu kizuri, silaha inatoa uhai wa mtu na kuvuruga amani. Lakini mbona hatukusikia vijana waliotoka Jeshi la Kujenga Taifa, wakitumia bunduki kutoa uhai wa raia, mbona hatukusikia amani inavurugika kwa vile vijana wamefundishwa silaha na mbinu za kupigana. Ujambazi tunaoushuhudia siku hizi haukuwepo wakati vijana walipokuwa wakienda Jeshi la kujenga taifa.

Siri yake ni kwamba. Kulikuwa na mfumo wa kuwafundisha vijana. Serikali iliandaa mfumo wa kuwafundisha vijana silaha na kuwaelekeza ni lini mtu anaweza kutumia silaha. Mafunzo ya Jeshi la kujenga taifa yalikuwa yamepangwa vizuri kwa mbinu nyingi za kumwezesha kijana kuwa raia mwema na kulinda taifa lake. Walifundishwa nyimbo za kimapinduzi na za kujenga uzalendo, walishindiliwa kasumba za kila aina ili walipende taifa lao. Ni mfumo mzuri ulioweza kuwakutanisha vijana wa Musoma, Mwanza, Mtwara, Arusha , Dodoma nk. Ni mfumo ambao ulifundisha kwa matendo.

Tunahitaji mfumo kama huo kuwafundisha vijana matumizi ya kondomu. Ili wasifundishwe uzinzi, bali kujua maana ya kondomu na ni wakati gani mzuri wa kutumia kondomu.

Vinginevyo Maaskofu, wabuni mfumo wa kurudisha maadili kwenye mstari. Wabuni mfumo wa kaufundisha uhusiano wa mtu na mtu, uhusiano wa mtu na jinsia tofauti. Sasa hivi jambo hili halifundishwi na Kanisa limeshindwa kuwaandaa viongozi wa kiroho kwenye mashule na vyuo. Mafunzo ya kiroho yangeanzia kwenye shule za msingi na kuendelea hadi vyuo vikuu. Sasa hivi vijana wanaachiwa kuogelea tu katika mahusiano bila kiongozi wa kiroho. Ni nani anaongoza maisha ya kiroho ya vijana wanaoishi kwenye hosteli kama ile ya Mabibo? Maaskofu wetu wanasema nini juu ya hili?

Kwa maoni yangu, badala ya Maaskofu Kupinga mpango wa Serikali, wangeomba kushirikiana na Serikali. Au kwa namna nyingine wangeitisha Jukwaa la Majadiliano, ili watu wote washiriki na kutoa maoni. Wazazi watoe maoni juu ya kuwalea watoto, serikali ichangie na viongozi wa dini wachangie. Serikali ifundishe matumizi ya kondomu, lakini kanisa iingize mafundisho ya kiroho. Ili hivi vitu viwili viende kwa pamoja. Mtoto afundishwe matumizi ya kondomu, lakini hapo hapo ajue mwongozo na maelekezo kuhusu maisha safi ya kiroho. Endapo ataanguka, maana hakuna shujaa wa hili, basi ajue kwamba ni lazima kujilinda yeye na wale wote wanaomzunguka.

Maaskofu wakazane kutengeneza mifumo ya kufundisha kwa matendo au kufundisha kwa kuonyesha mfano. Yawepo makundi ya watu katika jamii yetu wanaoishi maadili ya kweli. Ushuhuda wa Yesu, ulikuwa vipofu kuona, vilema kutembea na wafu kufufuka. Ushuhuda wa Maaskofu wa Kanisa Katoliki ni upi? Ni kikundi gani katika jamii yetu kinaishi maadili safi, ili watu wajifunze kwa kuona na kwa vitendo. Ni familia gani inawalea watoto katika maadili safi ili na familia zingine zione mfano. Ni ndoa gani inaishi maadili bora ya ndoa ili na ndoa nyingine zione mfano? Maaskofu wangekuwa na wasiwasi na haya zaidi ya kuwa na wasiwasi na vijana kufundishwa matumizi ya KONDOMU. Maana kama kuna mfano, hakuna wa kupotosha!

Mikutano na kutoa matamko si mfumo mzuri wa kuisaidia jamii. Yesu, aliishi na watu, alifundisha kwa matendo, alisafisha miguu ya watu, alijenga jumuiya za mfano. Maaskofu pia ni lazima wafanye hivyo. Wajenge jumuiya za watu, wawe karibu na watu na kufahamu matatizo yao, washiriki kabisa maisha ya watu, wawasafishe watu miguu, kwa njia hii wanaweza kuyagusa matatizo ya watu. Kwa njia hii wanaweza kutengeneza mifumo mizuri ya kubadilisha maadili na kuyapatia sura nzuri. Kwa njia hii wanaweza kufundisha vizuri maisha ya kiroho na hasa uhusiano kati ya mtu na mtu. Kwa kukaa kwenye mikutano na kutoa matamko bila kuyagusa maisha ya watu na kutoa matamko yanayopingana na maisha ya kila siku ya wananchi ni ishara kwamba hawasomi alama za nyakati. Na mtu asiyesoma alama za nyakati daima anabaki nyuma. Mfano ni huu wa kutoa tamko, Serikali ikafumba macho na kusonga mbele. Kwa njia hii mambo mengi yatajitokeza na maamuzi yatapitishwa na tutasonga mbele na kuwaacha Maaskofu wetu umbali mkubwa.

Kwa vile bado tunawahitaji maaskofu wetu, bado tunahitaji uongozi wao, basi ni lazima wasome alama za nyakati na kujitahidi kutembea na jamii. Kama wanavyosema, ni kweli kwamba KONDOMU zipo siku nyingi. Lakini nyakati zinabadilika na mambo mapya yanakuja. Huko nyuma UKIMWI, haukuwepo. KONDOMU, zilitumika kuzuia magonjwa ya zinaa na hasa kusaidia uzazi wa mpango. Leo hii ingawa wengine bado wanazitumia KONDOMU kwa uzazi wa mpango, lakini matumizi ambayo ni muhimu na ya kulinda uhai ni yale ya kuzuia maambukizo ya UKIMWI. Hivyo kuna tofauti, na maaskofu wetu ni lazima walione hili.

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment