JUKWAA LA KIJAMII LA KIMATAIFA

MAKALA HII ILITOKA KWENYE GAZETI LA TANZANIA DAIMA JUMAPILI 2006

JUKWAA LA KIJAMII LA KIMATAIFA NI KITU GANI?

Kongamano la Jukwaa la Kijamii la Kimataifa,
limemalizika Bamako Mali tarehe 23 mwezi huu. Jukwaa hili limewavuta watu zaidi ya elfu 25 kutoka pande zote dunia. Ni jukwaa lililojadili mambo mbali mbali yanayosonga Dunia ya tatu, kama Vita, utandawazi, njaa, UKIMWI nk., Wale wanaofuatilia habari
wanajua kwamba kongamano kama hili limefanyika Brazil
na Mumbai-India. Na kwamba mwaka kesho kongamano kama
hili litafanyika Kenya na Tanzania.

Kuna ushahidi wa kutosha kwamba watanzania walishiriki
kwenye kongamano la Mumbai- India. Na watanzania hawa,
wengi wao walitoka kwenye ASIZE, zisizo za kiserikali.
Kongamano la Bamako, pia lilikuwa na watanzania.
Pamoja na ukweli huu, bado kuna shaka kama watanzania
wanajua maana ya Jukwaa hili na umuhimu wake.

Maana yake ni nini? Ni kwamba watanzania wakirudi
nyumbani baada ya kushiriki kwenye makongamano haya,
wanakaa kimya! Kila mtu na kamhogo kake! Hawafanyi jitihadi ya kusambaza habari
kupitia vyombo vya habari - au kwa njia nyingine ni
kwamba ASIZE, zisizokuwa za kiserikali, zina uvivu au
upofu wa kushirikiana na vyombo vya habari.

Jukwaa hili lilianzishwa mwaka 2001, kupingana na
jukwaa la matajiri, lililofanyika Uswiss-Davos.
Mataifa tajiri, wafanyabiashara wakubwa na mabwana wa
utandawazi, walikutana kujadiliana mbinu mpya za
kuendelea kuwanyonya mataifa masikini. ASIZE zisizo za
kiserikali, wanaharakati wa haki za binadamu na watu
binafsi wanaojali ustawi wa binadamu wote waliamua
kuanzisha jukwaa la watu waliopembezoni, jukwaa la
maskini. Jukwaa hili linajulikana kwa jina la "World
Social Forum" au "WSF". Ni nafasi ya pekee ya watu
waliopembezoni, watu wanaonyonywa na kunyanyaswa, watu
wanaobaguliwa kijinsia, kukutana na kujadiliana na
kutumia kila njia kushinikiza Jukwaa la matajiri
"World Economic Forum".

Mfano jukwaa la Bamako, limefanya maandamano makubwa kupinga kile kinachofanywa na Ufaransa kwa Waafrika. Maandamano haya yalionekana kwenye vyombo mbali mbali vya dunia nzima na ujumbe utakuwa umefika.

Jukwaa hili ni muhimu sana na kila raia wa dunia ya
tatu ni lazima alifahamu vizuri. Kuna mashirika mengi
yasiyokuwa ya kiserikali yanayojinadi kuwatumikia
watu. Kufuatana na takwimu za TANGO, kuna mashirika
zaidi ya 600, yaliyo chini ya uratibu wa TANGO.
Mashirika haya yamesambaa Tanzania, nzima. Hivyo
hakuna sababu yoyote watanzania wasiwe na habari juu
ya Jukwaa la Kijamii la Kimataifa. Vinginevyo
mashirika haya yameshindwa kazi yake na ni bora
yasiendelee kuwepo!

Inashangaza kuona hata na Jukwaa, ambalo ni la
Tanzania moja kwa moja, halifahamiki kwa watanzania.
Kitu kama mchakato wa Helisinki, hakifahamiki vizuri.
Mchakato wa Helisinki, umezaa Jukwaa la Kijamii la
Kimataifa-Tanzania, na Jukwaa la Kijamii la Kimataifa
-Finland. Jukwaa hili linaitwa Citzen Grobal
Platform,CGP. Ni wangapi wanajua juu ya jukwaa hili.

Mwaka kesho Mchakato wa Hlisinki, ujulikanao kama
Helisinki-Dar, utakuwa na Jukwaa Dar-es-Salaam. Hili
kongamano kubwa ambalo litayakutanisha mataifa mengi.
Hadi leo watanzania wameandaliwa vipi kushiriki katika
kongamano hili? Ni jukumu la nani? TANGO pamoja na
CGP, wana habari tangia mwaka jana kwamba kongamano
hili la Helisinki-Dar, litafanyika Dar, ni kiasi gani
wamewafahamisha watu kuhusiana na kongamano hili?

Ni wangapi wanaofahamu malengo ya mchakato wa Helisinki ulioanzishwa na Rais Mkapa na Rais wa Finland, kwa lengo la kujadili utandawazi? Na kwamba Rais wetu wa sasa hivi Mheshimiwa Jakaya Kikwete na Waziri wa Mambo ya nje wa Finland, walikuwa watendaji wakuu wa mchakato huu?

Rais Kikwete, amekazania sana suala la majadiliano na Jukwaa la majadiliano katika hotuba zake- je ni wangapi wanajua kwamba uzoefu wake katika Jukwaa la Kijamii la Kimataifa la Tanzania na Finland, umemsaidia sana kupata upeo na umuhimu wa majadiliano na hasa majadiliano yanapokuwa kwenye jukwaa huru lenye kukaribisha mawazo ya watu mbali mbali?

Kuna Tanzania Social Forum, itafanyika mwaka huu mwezi wa tatu, ni watanzania wangapi wanafahamu juu ya Jukwaa hili la Tanzania na umuhimu wake? Ni jukwaa la viongozi wa mashirika, au ni jukwaa la kijamii. Sasa hivi kuna mabishano kati ya serikali na viongozi wa dini kuhusu matumizi ya kondomu. Wananchi wameandaliwa kiasi kutoa maoni yao juu ya jambo hili kwenye jukwaa la kijamii. Jukwaa hili ni huru, ni mahali ambapo mtu anaweza kusimama na kusema maoni yake bila kuwa na woga kukamatwa na polisi au kutengwa na viongozi wa dini.

Kuna tatizo la ajira kwa vijana. Je vijana hawa wameandaliwa vipi, ili watoe kilio chao kwenye jukwaa la kijamii la taifa? Wanawake wanaonyanyaswa, watoto yatima, watoto wa mitaani, wenye virusi vya UKIMWI nk., ni vipi wanaandaliwa? Yale mashirika yanayojinadi kuwatumikia, ni kiasi gani wanawaandaa ili wao wazungumze juu ya matatizo yao kwenye jamii yetu na kwenye Jukwaa la dunia nzima?

Mbali na kongamano la Helisinki-Dar, kuna Jukwaa la
Kijamii la Kimataifa(World Social Forum), litakalo
fanyika Kenya. Ni watanzania wangapi wana habari juu ya
Jukwaa hili? Je, watu wanajua kwamba jukwaa ni la kila
mtu, awe mwanaharakati, awe kwenye mashirika yasiyokuwa
ya kiserikali, awe mwanasiasa, awe katika madhehebu ya
dini au awe mfanyabiashara. Kila mtu ana haki ya
kushiriki kwenye jukwaa la kijamii, kutoa maoni yake,
kusikiliza maoni ya wenzake au kuuza bidhaa zake. Kila
mtu ana nafasi katika Jukwaa.

Mfano Bamako, kikundi cha ngoma kilitoka Burundi, kilicheza ngoma za Burundi na kutoa ujumbe wa amani kwa dunia nzima. Ngoma zile kubwa za Burundi, zilibebwa kwa ndege hadi Bamako. Hivyo hivyo hata za wasukuma, Wagogo, Wahaya na wasanii wa Bagamoyo, zinaweza kubebwa hadi Bamako, au Nairobi Kenya.

Hivyo ni matumaini kwamba majukwaa ya Dar na Kenya,
yatapata watu wengi kutoka vijijini na mijini. Itakuwa
aibu watu wasafiri kutoka nchi za mbali kuja Dar na
Kenya, wakati wenyeji wamelala usingizi wa pono bila
kujua linalotendeka. Itakuwa ni aibu watu watoke mbali
kuja kuuza bidhaa zao Dar na Kenya, wakati wenyeji
hawana soko la kuuza bidhaa zao. Itakuwa aibu watu
watoke mbali kuja kujadili matatizo yao, wakati
wenyeji hawana sehemu au jukwaa la kujadili matatizo
yao.

Helisinki-Dar, na Jukwaa la Kijamii la Kimataifa
litakalofanyika Kenya, ni kipimo cha kuyachuja
mashirika yasiyokuwa ya kiserikali, ni wakati wa kuona
ni mashirika yapi yanasimamia sauti zilizopembezoni.
Ni wakati wa kuyaona mashirika yanayowasiliana na watu
wa chini kule vijijini. Ni wakati wa kuona umuhimu na
ufanisi wa TANGO. Kwa vile kuna mashirika mengi yaliyo chini ya uratibu wa TANGO, basi ni jukumu la TANGO, kukumbusha, kusukuma na ikibidi kuyawajibisha mashirika yaliyo chini yake ili yajitokeze na kuwaandaa watu kwaajili ya majukwaa haya yaliyo mbele yetu.

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment