BARUA YA WAZI KWA MAREHEMU KAINAMULA

MAKALA HII ILITOKA KWENYE GAZETI LA RAI 2006

BARUA YA WAZI KWA MAREHEMU GOSBERT RUTABANZIBWA KAINAMULA.

Mpendwa marehemu Kainamula. Nilitamani kukuandikia barua hii mwezi wa tano mwaka jana baada ya kura za maoni za CCM. Bahati mbaya nilishambuliwa na kigugumizi cha mikononi na sababu kama tatu hivi zilifunga akili yangu. Si kwamba niliacha kufikiri, lakini nilishindwa kabisa kuyaweka chini kwa maandishi yale niliyoyafikiri.

Sababu ya kwanza iliyoifunga akili yangu ni kwamba nilikuwa na mashaka kama kweli huko ulipo kuna uwezekano wa kusoma barua. Ingawa hadithi ya Aliyeonja pepo inatupatia matumaini kwamba huko maisha yanaendelea kwa njia nyingine ambayo ni bora zaidi, mfano kwamba huko hakuna kuoa na kuolewa, hakuna tajiri na masikini, hakuna mwenye taabu, kila kitu ni raha tupu, lakini wengi wetu ni kama Thomas, bila kuona kuamini ni vigumu. Nimekuwa nikisoma barua ambazo watu mbali mbali wamekuwa wakimwandikia marehemu Mwalimu Julius Nyerere. Labda hii ingekuwa sababu tosha ya kunishawishi kukuandikia. Lakini pia sikuwa na uhakika kama wewe na Mwalimu Nyerere, mko sehemu mmoja. Kwa vile yeye atatangazwa mwenye heri, basi yeye yuko mbinguni. Nilifikri ikitokea wewe uko motoni, usalama wa barua yangu kukufikia bila kuungua ni mdogo.

Sipendi kuamini kwamba uko motoni, lakini ninajua fika kwamba ulikuwa na dosari ndogo ndogo za kukufungia milango ya mbinguni. Kitulizo changu ni kwamba kazi za kujitolea ulizozifanya kwenye shirika la Msalaba Mwekundu (Red Cross), kwenye ngazi ya Wilaya, Mkoa na Taifa, zinatosha kukufungulia milango ya mbinguni. Ulijitolea kiasi kikubwa na kuliongoza shirika la Msalaba Mwekundu katika Wilaya ya Karagwe. Pia ulichangia kiasi kikubwa katika uongozi wa Mkoa wa Kagera na Taifani. Mbali na kazi za Red Cross, ulionyesha upendo mkubwa kwa watu. Kama Mwenyezi Mungu, hakuona mema yako na kuamua kuangalia dosari ndogo ndogo ulizokuwa nazo, basi wa kuiona Mbingu ni wachache sana. Kasoro ulizokuwa nazo ni zile zinazowakumba binadamu wote ambao wameumbwa kwa ukamilifu. Dosari hizo mtu wa kuzikwepa ni yule mwenye sifa ya marehemu! Wapo wachache wenye kufanikiwa kuzificha kasoro hizi macho pa watu, wanafiki ambao kwa kufanikiwa kufanya hivyo wanajiona ni bora kuliko wengine na wanakuwa mahakimu wa wengine, lakini hawawezi kufanikiwa kuficha lolote mbele za Mwenyezi Mungu. Ninabaki kujituliza kwamba Mungu, alizifumbia macho kasoro ndogo na kuangalia mema yako mengi.

Sababu ya pili iliyonifanya nichelewe kuandika barua hii ni kwamba mara baada ya kura za maoni za CCM, zilizompitisha rafiki yako wa Karibu Mheshimiwa Jakaya Kikwete, Freeman Mbowe, wa CHADEMA, alitangaza kugombea kiti cha urais kupitia chama chake. Unaukumbuka urafiki na undugu wangu na Mbowe. Siwezi kukana uhusiano huo. Pia siwezi kukana kutofahamu uwezo, uzalendo na ukomavu wa kisiasa wa rafiki yangu Mbowe. Wengine wanasema ni mchanga katika siasa, wengine wanasema ni mhuni kwa vile anaendesha biashara ya “Nights Clubs”. Wengine wanasema yeye ni pandikizi la CCM, kwa vile baada ya Tume ya uchaguzi kumtanga JK, kama mshindi, Mbowe, alimkumbatia. Yalisemwa mengi, lakini kwa watu kama mimi ambao tuko karibu naye, bado tuliamini kwamba kijana huyu ni hazina kubwa katika taifa letu. Hivyo Kikwete upande mmoja na Mbowe, upande mwingine kilikuwa ni kigugumizi tosha.

Sababu ya tatu iliyochelewesha barua hii ni kwamba wakati wa uchaguzi mkuu TEMCO, ilinipatia kibarua cha kuwa mwangalizi wa ndani. Nilipangwa Mkoa wa Mtwara. Kazi yangu ilikuwa kuangalia na kutoa ripoti TEMCO, hivyo TEMCO, ndio wasemaji wakuu. Nisingeweza kukuandikia wakati huo ingawa nilikuwa na mengi ya kukushirikisha. Mfano umasikini wa mkoa wa Mtwara, ni kitu kilichoisimbua roho yangu hadi leo hii. Mbaya zaidi ni kwamba wakati wa kampeni, pesa nyingi zilitumika. Wagombea walionyesha kuwa na pesa nyingi za kutisha. Kwamba walikuwa na pesa si swali, lakini ni wapi pesa hizi zilipatikana miongoni mwa watu maskini hivyo ni swali gumu hata kwa Mheshimiwa Jakaya Mlisho Kikwete. Lakini kwa vile Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini, ameteuliwa kuwa Waziri wa Nchi- Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Mheshimiwa Jakaya Kikwete, atakuwa na jibu. Tumpatie muda. Ni imani yangu kwamba watu wa Nanyamba, waliomkataa mama huyu mbele yake watafurahi kusikia jibu hilo.

Pamoja na sababu hizo tatu ni kwamba nilianza kusahau kukuandikia kama nisingetembelea Karagwe wakati wa mwaka mpya. Nikiwa Karagwe, kumbukumbu zilikuja, na hasa baada kukutana na ndugu na jamaa zako. Nilipokutana na Sabi Rwazo, mtu anayeipenda CCM kuliko maisha yake, mtu anayeitumikia CCM bila kusubiri shukrani. Mtu ambaye kwa miaka mingi amekuwa msingi wa uhai wa CCM katika Wilaya ya Karagwe na mkoa mzima wa Kagera. Sabi Rwazo, ambaye pamoja na mapenzi ya CCM, hana chuki yoyote ile na wapinzani, mtu wa watu, nilishindwa kujizuia kujadili juu yako wewe Marehemu Gosbert Rutabanzibwa Kainamula.

Lakini hasa nimesukumwa na habari nilizozisikia Karagwe, kwamba Mheshimiwa Jakaya Kikwete, alimkumbatia baba yako Mzee Kainamula “Mfalme wa Nyuki”, kwa furaha kubwa wakati wa kampeni zake mjini Kayanga. Nimesikia, alimwambia baba yako kwamba wewe ulikuwa rafiki yake mkubwa. Ni ishara kwamba mtu huyu ana kumbukumbu. Hii ni ishara nzuri kwa kiongozi.

Nimeandika kukujulisha kwamba Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, ni Rais wa Tanzania. Binafsi simfahamu kwa karibu Mheshimiwa Kikwete. Kumfahamu kama vile ninavyomfahamu kwa karibu Mheshimiwa Freeman Mbowe. Wewe mwenyewe unafahamu jinsi nilivyomfahamu Mheshimiwa Jakaya Kikwete, kupitia watu mbali mbali. Nilimfahamu kupitia kwako, kupitia wanamtandao na ndugu zangu waliobahatika kufanya kazi naye kwa karibu.

Nilipoandika makala ya Fisadi na Mwenye Virusi ni nani zaidi, niliandika kwa kupinga dhana nzima ya kuwanyanyapaa watu wenye UKIMWI. Kwangu niliona bora kuongozwa na mtu mwenye virusi kuliko fisadi. Ingawa huu ulikuwa ni uvumi ulioenezwa kwa nia ya kumdidimiza Jakaya Kikwete, nilisimama upande wake si kwa vile ni mtu niliyemfahamu kwa karibu au kuwa rafiki yangu kama alivyokuwa rafiki yako. Nilisimama kutetea haki!

Ninakumbuka miaka mitatu iliyopita tukiwa tumekaa “Farida CafĂ©” Kanyanga- Karagwe, ulinielezea juu ya ndoto za Jakaya Kikwete, kuwa rais wa Tanzania. Ingawa nilikuwa na habari za Jakaya Kugombea Urais wa Tanzania mwaka 1995, sikufahamu kwamba mtu huyu alikuwa na ndoto hii kwa muda mrefu. Hili jambo la pekee kidogo na ni la Afya kwa Taifa letu. Mtu mwenye ndoto hama hii ni lazima awe makini, mzalendo na mwenye upeo mkubwa. Uliniambia kwamba miaka ya nyuma mkiwa Tabora, Jakaya alikudokezea juu ya nia yake ya kutaka kuwa kiongozi wa Taifa la Tanzania. Na ukaongezea kwamba siku hiyo ikifika basi a wewe utakuwa mkuu wa Wilaya! Siku hiyo sasa imefika. Jakaya ni Rais! Bahati mbaya wewe ni marehemu! Wilaya yako, ni nani ataiongoza? Ni kweli ungekuwa Mkuu wa Wilaya, maana inavyoelekea Jakaya, hana tabia ya kuwasahau rafiki zake, na hasa rafiki wachapakazi kama ulivyokuwa wewe Kainamula. Amemteua rafiki yenu Lowasa, kuwa Waziri Mkuu na kusimama kidete kutetea uchaguzi wake kwamba si urafiki bali ni kwa vile Lowasa, ni mchapa kazi. Watu wengi waliotegemea jambo hili walijitahidi kumkatisha tama kwa kuandika juu ya uhusiano wao kwenye magazeti na kwenye mikutano isiyokuwa na mwenyekiti wala katibu, lakini Jakaya, hakuyumba!

Mpendwa Marehemu Kainamula, wewe ulikuwa mtu wa kwanza kunifunulia uwezo wa Jakaya. Uliniambia kwamba Jakaya ni mzalendo wa kweli, ni mchapa kazi, si mtu wa kupendelea rushwa, mtu wa watu, mtu wazi na kwa kutaka kuwa mwaminifu kwa maneno yako, ulisema kwamba yeye ni Nyerere wa pili! Hotuba yake ya kulifungua Bunge, ilionyesha jinsi ulivyomfahamu vizuri Jakaya. Sasa hivi hotuba hiyo ni gumzo. Mbali na ujumbe mzito uliokuwa kwenye hotuba hiyo, ni ule uwezo aliouonyesha wa kutoa hotuba ndefu bila kusoma, kuzivuta na kuzigusa hisia za watu, kucheka yeye mwenyewe na kuwachekesha wale wanamomsikiliza kama alivyokuwa akifanya baba wa taifa. Pia ameonyesha hali ya kujisimamia kama alivyokuwa Mwalimu. Ile namba yake ya kusema mara kwa mara “ Tusilaumiane mbele ya safari” imeonyesha kwamba hana ndugu wala rafiki kwenye kazi.

Ninakumbuka uliniambia kwamba tatizo pekee ulilolifahamu kwa Jakaya, ni kutofuata muda. Kwamba alikuwa na tabia ya kuchelewa kwenye mikutano na sehemu mbali mbali. Lakini pia ulimtetea kwamba tatizo kubwa ni hali yake ya kutaka kumlizisha kila mtu. Kwamba anapenda kumaliza tatizo moja kabla ya kuanza jingine, anapenda kumsikiliza mtu hadi mwisho bila kumkatisha tama kwa kumwambia kwamba ana ahadi na watu wengine. Kwa njia hii alishindwa kufuata muda. Lakini kwa vile sasa ni Rais, muda wake utapangwa na hatakuwa na uhuru wa kumlizisha kila mtu kama alivyokuwa amezoea.

Mbali na yale uliyonielezea kuhusu Jakaya, nilipata pia bahati ya kukutana na wanamtandao wakati wa mchakato wa kura za maoni. Swali langu kubwa kwao lilikuwa ni je kama Jakaya, asipotitishwa na CCM, atajiunga na vyama vya upinzani. Waliniambia kwamba ukitaka kukosana na Jakaya, uliza swali hilo. Hakutaka kulisikia, maana aliamini asilimia miamoja kupitishwa na chama chake. Wanamtandao hawa walinisaidia kumfahamu zaidi Mheshimiwa Jakaya Kikwete.

Ninapokuandikia barua hii tayari amemaliza kuwateua mawaziri. Majina mengi ni mapya, lakini wengi wao ni wanamtandao, hivyo utakuwa unawafahamu. Namba ya wanawake imeongezeka kuliko wakati wa utawala wa hamu zilizopita. Na wengine wachache ni wazee wetu wa siku nyingi kama Mungai, Muramba na Mzee Kingunge. Baraza lenyewe ni kubwa. Mawaziri na manaibu mawaziri jumla inakuja watu 60! Kwa mtindo wa zamani, hayo ni mashangingi mapya 60, bila kutaja mengine. Serikali iliyomakini, idadi hiyo si kubwa, lakini kwa mtindo wa kuonyesha ufahari na ukubwa wa uwaziri, ni hatari ambayo kila mtu anasubiri kwa hamu miujiza ya Jakaya. Tumpe muda!

Kuna mambo mengi mapya katika serikali ya Jakaya. Mfano Ofisi ya Waziri Mkuu ina naibu Waziri anayeshughulikia Maafa na Kampeni Dhidi ya Ukimwi. Hili limeonyesha umakini wa Jakaya. Maana kama kweli tunataka kupamba na ugonjwa huu wa hatari ni lazima kuonyesha kwa matendo. UKIMWI, ni adui mkubwa wa taifa letu. Unawachukua watu ambao wangelisaidia kulijenga taifa letu.

Jakaya, ameitisha mjadala wa kitaifa. Ameonyesha wazi nia ya kutaka kujenga Jukwaa la majadiliano. Mtu kama mimi ni lazima nifurahi sana, maana nimekuwa nikipigia kelele Jukwaa la majadiliano. Ni vigumu nchi yoyote ile kupata maendeleo ya kweli bila kuwa na jukwaa la majadiliano. Na nitakuwa mtu wa kwanza kuingia uwanjani:

Nimeiangalia kwa makini serikali ya Mheshimiwa Jakaya Kikwete. Sikuona vizuri anapotaja maadili ya vijana wetu. Nilitegemea jinsi Maafa na kampeni dhidi ya Ukimwi, ilivyopatiwa Naibu waziri, basi na kwa upande wa Elimu, maadili ya vijana wetu yangempata Naibu waziri. Hali ilivyo sasa hivi ni kwamba tunawatelekeza vijana wetu. Tunawaachia vijana wetu kutafuta msimamo wao juu ya maadili, na hasa juu ya uhusiano wa msichana na mvulana. Hakuna mwongozo unaoeleweka wa kuwaongoza vijana wetu katika bahari ya mahusiano. Zamani tulikuwa na vitabu kama Mvulana Je, na Msichana je,- Mheshimiwa Willbrod Slaa, Mbunge wa Karatu, ni kati ya watu waliokuwa wameshirikia kuviandaa vitabu hivi. Siku hizi vitabu hivi havisikiki tena. Mbaya zaidi ni kwamba kile kizazi ambacho ndicho kingepanga mfumo mzuri wa kuwaongoza vijana, ndicho kinachochea maadili mabaya kwa vijana wetu. Badala ya kuwasaidia vijana wetu kuongelea na kulivuka salama dimbwi la mapenzi wanawasaidia kuzama na kuangamia! Inakuwa vigumu kupambana na UKIWMI, inakuwa vigumu kutengeneza familia bora ambazo zinaweza kuwa msingi wa taifa imara. Tunawaachia vijana wetu kuliona tendo la ndoa kama kitu cha kawaida, kitu cha starehe, burudani, biashara, silaha ya kushinda mitihani kwa wasichana nk., tunashindwa kuwafundisha utakatifu wa tendo hili, umuhimu wa tendo hili na hasa jinsi tendo hili linavyoweza kukomaza na kuendeleza uhusiano wa mtu na mtu, jinsi tendo hili linavyoweza kusaidia kujenga familia bora ambazo zinaweza kuwa msingi wa taifa lililo imara. Ingawa ni mapema sana kusema, lakini kwa muundo wa serikali inaonyesha kwamba hata na kwa mtu makini kama Jakaya, swala hili la malezi ya vijana bao limetupwa kando!

Nimekuandikia mengi, bila kuwa na uhakika kama utapata nafasi ya kuyasoma na kunijibu. Lengo langu kubwa lilikuwa kukujulisha kwamba, kama ulivyoniambia, miaka mitatu iliyopita, sasa hivi Jakaya Mrisho Kikwete, ni Rais wa Tanzania. Sina shaka kwamba yeye sasa hivi ni tumaini la taifa letu. Akifanya vizuri nitakujulisha, akifanya vibaya nitakulalamikia! Ni bahati mbaya kwamba wewe uliikimbia nafasi yako ya Ukuu wa Wilaya. Unafikiri angekupatia Wilaya gani? Tabora mjini? Mungu, ailaze roho yako mahali pema peponi.

Na,
Padri Privatus Karugendo.

2 comments:

Unknown said...

Padri Priva.

Kwaza kabisa napenda kukusalimia.
Pili nimesoma kwa furaha na heshima kubwa barua yako ya wazi kwa mkubwa wangu Gozbert Kainamula.
Napenda kukushukuru kwa barua hii japo muda umeidha pita lakini kwangu mimi barua hii ni mpya.

Johannes Bingasheki Rwazo.
The Netherlands.

Anxto said...

Samahani VP naweza kupata hiyo makala ya mwaka 2006

Post a Comment