UTAMADUNI WA AMANI

MAKALA HII ILITOKA KWENYE GAZETI LA RAI 2005Utamaduni wa Amani


Watu wengi wanaamini kwamba Tanzania ni nchi yenye utamaduni wa amani. Wengine wanakwenda mbali na kuiita Tanzania kuwa ni “Kisiwa cha Amani”. Ninakumbuka, siku za nyuma kidogo kusoma makala ya mwandishi Ndesanjo Macha, juu ya upana wa neno amani. Katika makala hiyo mwandishi alijitahidi kutofautisha amani na kutokuwepo kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe. Mfano mtu anapoilinda amani kwa mtutu wa bunduki, hiyo inakuwa si amani. Hata kama hakuna vita vya wenyewe kwa wenyewe, kitendo cha kutumia bunduki kulinda amani, si dalili za amani! Au mtu anapojaribu kuilinda amani kwa kumwaga damu ya mtu mwingine, hiyo inakuwa si amani. Ndesanjo, aliendelea kuielezea amani, mfano, kwamba hata kama hakuna vita, amani inaweza kupotea. Mtu, asipokuwa na kipato cha kutosha, amani yake inaweza kupotea, mtu asipokuwa na chakula amani yake inaweza kupotea, mtu asipopata tiba, amani yake inaweza kupotea, mtu asipopendwa au akutumiwa kama chombo cha starehe, amani yake inaweza kupotea nk.

Hoja nzito ya Ndesanjo, ilikuwa kwamba kama Tanzania, kuna amani, si kwamba imejengwa na mtu mmoja au kikundi cha watu, itakuwa imejengwa na watanzania wote. Hivyo utamaduni wa amani utakuwa umejengwa na watanzania wote. Kuna tabia iliyojengeka hapa kwetu, kwamba kuna watu ambao ni hodari wa kujenga utamaduni wa amani na wana mbinu nzuri za kuidumisha amani. Hili ni jambo ambalo Ndesanjo, alilitilia mashaka, na mtu yeyote anayeishi Tanzania, atalitilia shaka. Utamaduni wa amani, haujengwi na mtu wala kikundi – unajengwa na jamii nzima.

Suala kubwa ambalo limekuwa likinisumbua kichwa changu ni namna utamaduni katika jamii unavyojengeka na kuwa sehemu ya maisha. Wataalam wa sayansi ya jamii wana namna yao ya kulielezea jambo hili. Kwa uelewa wangu mdogo mimi ninafikiri utamaduni ni mazoea ya kawaida ambayo yamezoeleka katika jamii. Kitu kinafanywa kikiwa na sababu zake kinaendelea kufanywa kwa muda mrefu halafu kinazoeleka ndipo baadaye kinakuwa utamaduni wa jamii ile.

Mfano watu siku hizi wanapojadili suala la ukwepaji wa kodi nchini wanataja sababu nyingi sana. Moja ya sababu wanazotaja ni kwamba watanzania hawana utamaduni wa kulipa kodi. Au kwa namna nyingine kwamba watanzania wana utamaduni wa kukwepa kodi. Swali linalokuja ni je watanzania hawa wanazaliwa wakiwa wakwepa kodi? Au wanakulia katika mfumo ambao kodi inakwepwa halafu nao wanakuwa sehemu ya jamii hiyo? Sababu nyingine zinazotajwa ni pamoja na viwango vikubwa vya kodi, uwezo wa mamlaka husika kumkamata mkwepa kodi, faini ndogo kama utashikwa, walipa kodi kutojua ni nini kodi yao inafanya na nyinginezo. Sababu hizi kwa mtazamo wangu ndio hujenga utamaduni wa kutolipa. Kama faida za kukwepa kodi ni kubwa au gharama za kuikwepa ni ndogo kwa nini mtu asikwepe kodi? Huyu anakwepa, yule anakwepa, anayekuja kwenye biashara anakwepa, baada ya hapo utamaduni wa kukwepa unajengeka. Watanzania wanakuwa, kiutamaduni, ni wakwepa kodi. Hivyo ndivyo utamaduni unavyojengeka katika jamii. Yanaanza kama mazoea, polepole yanaota mizizi na kukubalika kama utamaduni.

Nimeanza na mfano wa kodi ili nijenge hoja ya utamaduni wa amani. Amani haiji tu kama wana wa Israeli walivyokuwa wakishushiwa mana (Angalau Biblia ndivyo inavyosema). Amani ya kweli hujengwa, hujengwa na watu. Ili iwepo amani ya kweli ni lazima kila mtu kushiriki, kila kikundi kushiriki, kila mtu aguswe, kila mtu atosheke na kila mtu aamini kwamba jamii yake inamtendea haki. Mbegu ya amani inapandwa mapema kwenye vichwa vya watoto, wanakuwa nayo. Wanachukia vurugu, wanachukia unyanyasaji, wanapenda kuishi palipotulia. Tukishindwa kuijenga mapema madhara yake tutayaona. Miaka ya karibuni tumeshuhudia jinsi ambavyo tumeshindwa kuwalea watoto wetu katika kuwajengea utamaduni wa amani. Kwanza nikiri kwamba siku hizi watoto wanapendwa sana na wazazi wao. Atakachotaka atapewa. Si ndio upendo huo?

Nitazungumzia madoli ya bunduki. Kama kuna kitu ambacho kinaanza kuwaharibu watoto mapema leo hii ni haya madoli yenye mfano wa bunduki. Mtoto ananunuliwa bunduki ili achezee kama mpira au kalamu ya kuchorea. Mtoto anakulia kwenye mazingira ya kujua kazi za bunduki. Anaichezea wazazi wanafurahia anavyolenga, wanacheza pamoja. Siku hizi wanatengeneza madoli makubwa kabisa vile vidogo wameona haziwafundishi vurugu vizuri. Baada ya kununuliwa bunduki, mtoto anaanza kutazama sinema za vurugu. Zenye mapigano ya ajabu zinazotumia bunduki zinazofanana na alizonunuliwa na wapendwa wazazi wake. Anakuwa akipenda hizo sinema. Baada ya muda baba atanunua silaha ya kweli ataiweka ndani. Wapenzi watoto wetu wataiona. Kitakachotokea kitaeleweka baadaye.

Majuzi, kule Marekani tumesikia jinsi mtoto wa sekondari alivyochukua silaha na kuwaua watu si chini ya tisa, wakiwemo waalimu, wanafunzi na mlinzi. Hii ilitangazwa sana kwa vile ilihusisha watu wengi. Habari za namna hiyo kwa wale wanaofuatilia habari ni za kawaida, nadhani kama ya kuua mtu mmoja au wawili hiyo siyo habari mpaka wawe wengi. Hawa watoto hawakuzaliwa wakiwa watu wa namna hiyo wamekuzwa katika utamaduni nilioeleza hapo juu. Walipendwa na wazazi. Wakanunuliwa madoli. Wakaachwa watazame sinema za kuua kadri wanavyopenda. Baba alivyonunua silaha akaiacha popote au alimshirikisha mwanaye kuinunua na kumwonyesha ilipo akasahau kwamba alishamfundisha matumizi tangu akiwa mdogo. Wanapoudhiwa na wenzao wanakimbilia kwenye kifaa rahisi cha kuwamaliza maadui zake pamoja na yeye mwenyewe. Huko ndiko tunapokwenda.

Wachina wanazidi kutengeneza bunduki kwa ajili ya watoto wetu wapendwa, wanakuja kutuuzia kwenye maduka ambayo yametapakaa kila mahali. “Maduka ya kuuza madoli”. Hizi ndizo athari za mfumo wa kufungulia kila kitu. Athari moja kubwa sana ya mfumo wa kibepari ni kwamba haujali ni namna gani fedha zinapatikana. Ubepari hauna maadili ndio maana ukiwa na kilabu cha usiku ambacho watu hutembea uchi kufurahisha wateja si mbaya. Asubuhi watafuata kodi yao. Hawajali ni namna gani fedha inapatikana hata kama kwa gharama ya kuua maadili ya taifa. Kwao si suala zito. Suala ni pesa. Hili nimelijadili kwa kirefu katika makala yangu ya juma lililopita. Labda niongeze tu kusema kwamba mfumo wa ubepari, ambao tunaelekea kuukumbatia kwa sasa, hauwezi kutusaidia kujenga utamaduni wa amani. Mfumo unaojali faida , ni vigumu kujenga amani – kwa njia moja ama nyingine ni lazima mfumo huu utumie bunduki kulinda amani na mali! Penye bunduki, hakuna amani! Tukiangalia ukweli ulivyo na yale yanatokea kila siku katika dunia yetu.

Ndivyo hivyo tamaduni zinavyojengeka huanza watoto wakiwa wadogo, wanakuwa na hisia kama hizo mpaka ukubwani halafu tunajiuliza imekuwaje. Utamaduni wa kuwaona watu weupe au watu wa mataifa mengine ni wa maana kuliko weusi kwa mfano unaanzia mbali. Mtoto anapozaliwa anapewa jina la Kizungu au la Kiarabu. Wakristo wanampa jina la ubatizo wanaita jina la “Kikristo.” Waislamu wanampa jina wanaita la “Kiislamu.” Sijui kama kuna majina ya Kikristo na ya Kiislamu hapa duniani. Haya ni majina ya Kizungu na ya Kiarabu tu.

Baada ya kumpa jina ambalo halimhusu ananunuliwa mwanasesere wa Kizungu. Anaambiwa huyo ni mtoto wake ampende kweli. Anapewa mifano inayopendeza kwamba ni mzuri kama huyo mtoto mwanasesere wa Kizungu. Anaanza kuabudu Uzungu anaona kila jema ni la Kizungu. Kinachoendelea baada ya hapo tunajua. Kila jambo zuri ni la Kizungu. Chakula kizuri ni cha Kizungu. Tunda kubwa ni la Kizungu. Mtoto au mtu mzima msafi aliyevaa mavazi mazuri kapendeza kama mzungu lakini inzi mkubwa si wa Kizungu!

Mtoto anakuwa, anaanza shule. Shule nzuri ni ile inayofundisha Kizungu. Bila Kizungu wewe si kitu. Wanajazwa historia iliyopindishwa katika vitabu vilivyoandikwa na Wazungu. Tunaanza kulemazwa fikra tangu tunavyokuwa wadogo. Tunakuwa hivyo hivyo mpaka tunazeeka tunaabudu Wazungu. Kujiamini kunakwisha kabisa. Hata kama unajua kitu kuliko mzungu unaogopa unadhani anajua zaidi. Ndivyo tunapoanza na kuendelea mpaka uzeeni. Mzungu, Mzungu, Mzungu. Hii nadhani ndiyo sababu kubwa ya matatizo ya Afrika. KUTOJIAMINI. Huamini chochote cha kwako kama ni chema kuliko cha Kizungu.

Watoto wanaona jinsi tunavyoshindwa kuendesha mambo yetu wenyewe mpaka tusaidiwe na Wazungu kufanya maamuzi. Utamaduni huu wa kutojiamini ukikua na kusimika mizizi unaweza kuvunja amani kwa njia moja ama nyingine.

Nimetoa mfano wa watoto kuangalia sinema za vita na vurugu. Lakini pia siku hizi watoto wetu wanashuhudia jinsi bunduki zinavyotumika kulinda amani, bunduki zinavyotumika kutoa roho za binadamu katika harakati za kulinda na kudumisha amani! Hii inajengeka kwenye vichwa vya watoto wetu. Pole pole wataanza kujiuliza juu ya maana ya amani kulindwa na bunduki. Watauliza juu ya maana ya damu kumwagika katika harakati za kulinda amani. Watajenga utamaduni wa kulinda amani kwa kutumia mtutu – wataamini kwamba bila mtutu amani haiwezi kujengeka.

Ni kweli Tanzania kuna amani kwa vile hakuna vita. Lakini si lazima vita ndipo amani ipotee. Kujenga nyumba na kujifungia “gate” si dalili za amani, kujenga nyumba na ikazungukwa na walinzi wenye bunduki si dalili za amani. Ipo mifano mingi inayoonyesha kwamba pamoja na Tanzania, kuishi miaka mingi bila kuwa na vita ya wenyewe kwa wenyewe, amani yetu iko mashakani. Kuna mambo mengi ya kufanya kwa pamoja kama taifa ili utamaduni wetu wa amani uendelee kudumu.

Tuache tabia ya kuwanunulia watoto wetu midoli ya bunduki na kuwafundisha vurugu. Vinginevyo watoto wetu watatuliza siku moja kwa kutumia bunduki tunazonunua kuwalinda wao, mali zetu na amani yetu. Vitu vya watoto vya kuchezea ni vingi. Wakililia bunduki waambie ni mbaya wataelewa. Ninakuhakikishia watoto wanaelewa, tatizo hatuwasiliani nao. Na hili limekuwa ni tatizo sugu katika jamii yetu inayojiweka kifua mbele kuwa kisiwa cha amani wakati watoto wetu hawana amani. Mambo mengi yanawachanganya na tatizo kubwa ni kukosekana kwa mawasiliano kati yao na wazazi. Nina mifano ya watoto wa miaka mitatu ambao wanakataa kuona mdoli wa bunduki wanasema si nzuri. Wakiona ule usanii wa mieleka wanaacha kuangalia luninga, hawataki vurugu. Wakiona picha za ngono wanazima luninga, wakitatizwa na jambo wanauliza na huo ndo mwanzo wa kujenga utamaduni wa amani kwa mtoto.

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment