TUSIWASHINIKIZE VIONGOZI WA SERIKALI IJAYO
Wakati tunaelekea uchaguzi mkuu, yameanza kujitokeza
mambo ya kushangaza. Watu wengine wameanza kuunda
serikali. Na wengine wameanza kuiwekea mashinikizo
serikali ijayo ili iwapatie madaraka watu wanaowapenda
wao wenyewe. Wapo ambao wanakwenda mbali kiasi cha
kuanza kupanga orodha yote ya mawaziri, kuanzia
waziri mkuu hadi wakuu wa wilaya. Ingawa jambo hili
si baya, maana kila chama kina watu wake ambao
kinaamini wanaweza kuchukua nafasi mbali mbali katika
serikali endapo chama hicho kitafanikiwa kuiongoza
dola. Ila si sahihi jambo hili kufanyika au kupangiwa
kwenye pombe, mitaani, kwenye bao na vijiweni. Ni
imani yangu kwamba kila chama kina utaratibu wa
kufanya kazi kufuatana na misingi kilichojipangia na
maadili yanayoendana na utamaduni wa nchi yetu na hasa
kwa kuiheshimu katiba ya nchi yetu. Ni lazima chama
kinachoshinda na kufanikiwa kuiongoza serikali, kikae
chini na kuwachunguza vizuri wanachama wake ambao
wana uwezo wa kusaidiana na rais kuliongoza Taifa.
Nchi nyingine ambazo Uzalendo ndio kitu
kinachotangulia, hata kabla ya mapenzi ya Chama,
anaweza kuchaguliwa mtu yeyote hata kama ni wa chama
cha upinzani au hana chama, ili asaidiane na rais
kuiongoza nchi. Kinachoangaliwa ni uzalendo, kipaji,
elimu na uwezo wa kufanya kazi kwa kujituma.
Mbaya zaidi, na hili ndilo linalo kera na kuleta
wasiwasi ni pale watu wanapoanza kuiwekea mashinikizo
serikali itakayoingia madarakani Oktoba mwaka huu.
Juzi tu amesikika Waziri Mkuu Frederick Sumaye,
akisema kwamba serikali ijayo isimtupe Mheshimiwa
Magufuli, ambaye sasa hivi ni waziri wa ujenzi. Na kwa
kusema hivyo, basi ni sawa na kusema, kwamba CCM ndio
chama kitakachoshinda. Maana sisi hatujajenga
utamaduni wa serikali inayotawala kukubali kumchagua
mtu wa Chama cha upinzani kuwa waziri. Sina hakika
kama CUF ua CHADEMA wakishinda wanaweza kumchagua
Magufuli. Nina mashaka, kama Mheshimiwa Sumaye,
anaposema serikali ijayo impatie kazi Magufuli, ana
TLP au NCCMageuzi kichwani mwake. Atakuwa anaifikiria
CCM tu. Itakuwa ni shinikizo kwa Mheshimiwa Jakaya
Kikwete.
Ombi kama hili, maana tumezoea kwamba mtu mkubwa
akiomba kitu inakuwa ni amri, linaleta wasiwasi na
mashaka makubwa. Huku ni kutaka viongozi watakaoingia
madarakani kufanya kazi kwa mashinikizo, watalazimika
kuwachagua watu kwa mashinikizo. Na kwa upande huu ni
kutaka Mheshimiwa Kikwete, kwa upande wa CCM, endapo
ataingia Ikulu, aanze kufanya kazi, walao kwa siku za
mwanzoni kwa mashinikizo. Hili si jambo zuri. Ni
lazima utamaduni huu upigwe nyundo kubwa.
Sote tunajua kwamba Magufuli, amefanya kazi nzuri.
Hakuna anayeweza kubisha kwamba barabara zimejengwa,
nyumba za serikali zimeuzwa, meli ziendazo kasi
zilizuiwa kupita kwenye barabara zetu, ili
zisiharibike. Meli, hizi sasa hivi ziko Kisumu,
zikisubiri kuelekea Mwanza. Labda barabara za Kenya,
ni imara zaidi, au walipenda pesa kuliko kuangalia
usalama wa barabara zao. Magufuli, amefanya mambo
mengi mazuri. Hakuna asiyekumbuka kile kituo cha
mafuta cha Mwanza, ambacho kilivunjwa kwamba kilikuwa
barabarani, lakini hadi keshokutwa kituo hicho
hakikuwa barabarani. Magari ya serikali hayatumiki
ovyo tena, yote hayo ni kwa juhudi za mheshimiwa sana
Magufuli.
Yawe mazuri au mabaya, lakini yote aliyoyafanya
Magufuli, kwenye Wizara ya ujenzi, hakuyafanya peke
yake. Hili ndilo jambo ambalo tunapaswa kulizingatia.
Angekuwa na watendaji wabovu asingefika mbali. Ana
waziri mdogo wa ujenzi, ana Katibu mkuu na waandamizi
wengine. Makatibu wakuu walio wengi wanafanya kazi
usiku na mchana na sifa zote wanabeba mawaziri! Kama
ni sifa, si haki zimwendee Magufuli peke yake na kama
ni lawama si haki zimwendee Magufuli peke yake. Wizara
nzima ilikuwa ikifanya kazi. Kama ni kuwaombea kazi
basi wote wa Wizara ya Ujenzi, waombewe kazi kwenye
serikali ijayo.
Magufuli, anaweza kurudi au kutorudi serikalini. Uwezo
anao, lakini si Mtanzania peke yake ambaye anaweza
kufanya kazi hii. Tuna watanzania wengi wenye uwezo na
uzalendo. Kwanini uamuzi wa yeye kurudi au kutorudi
tusiwaachie viongozi wa serikali ijayo?
Sina tatizo lolote na Magufuli, lakini ninaona
tunataka kujenga mfumo wa Usultani katika nchi
inayoongozwa na Demokrasia. Lakini mbaya zaidi ni
kujenga tabia ya kutowaachia viongozi kuongoza.
Tunataka kujenga utamaduni wa Rwanda ya Habyalimana wa
Akazu. Yaani wale walio kwenye Akazu ndio hao
watakuwa mawaziri miaka nenda rudi. Rais Habyalima,
aliendesha nchi kwa kuisikiliza Akazu na matokeo yake
tunayajua sote. Utamaduni huu ni mbaya kabisa na ni
lazima tuupige vita.
Rais ajaye, ni lazima awe na uhuru wa kuitengeneza
serikali yake jinsi anavyotaka. Anaweza kuwabadilisha
mawaziri wote na kuweka wengine wapya. Hakuna mtu
aliyezaliwa kuwa waziri. Na ili mtu awe Mtanzania
mwema na mzalendo wa kweli si lazima awe waziri. Hadi
leo hii tunao watanzania wengi wanaochangia maendeleo
ya nchi yetu lakini zi mawaziri.
Inashangaza kabisa kwamba hakuna mtu au kiongozi wa
juu kabisa serikalini aliyejitokeza kuikemea kauli ya
Mheshimiwa Waziri Mkuu. Yeye mwenye ametangaza kwamba
ameachana na siasa. Nina imani ataendelea kuwa
Mtanzania mwema na mzalendo. Sasa kama yeye anaacha
siasa, kwa nini anataka kuacha mashinikizo nyuma yake?
Kwa nini hataki viongozi watakaoingia madarakani
wafanye kazi kwa uhuru bila ya mashinikizo?
Nchi hii ina watu wangapi wanaofanya kazi kufa na
kupona lakini hakuna mtu hata mmoja anayewataja wala
kuwasifia? Kama Magufuli, ameweza kujenga barabara,
basi kuna watu waliofanya kazi nzuri ya kukusanya
kodi. Mbona hao tusiwasifie? Hoja yangu ni kwamba
hakuna mtu anayefanya kazi peke. Ni lazima mtu
asaidiane na watu wengine.
Hata hivyo wakati huu si wa kuanza kuwaombea watu
kazi. Ni wakati wa kujadili sera za vyama vya siasa.
Je, sera hizi zinalenga kuleta maendeleo katika taifa
letu? Je ni sera zinazotekelezeka? Je, hawa watanzania
wanaopiga kelele na kuzisukuma sera hizi wana umri gani
katika taifa letu na kwa umri huo wamelifanyia nini
taifa letu. Si kwamba mtu akiingia madarakani ndipo
atakuwa mbunifu au kuanza kufanya kazi kufa na
kupona. Ni lazima mtu kumpima kwa yale aliyoyafanya
siku za nyuma. Ni wakati wa kuwahoji wagombea wote
wanaotaka kuingia Bungeni. Je wanaingia Bungeni,
kuwawakilisha akina nani? Ukweli ulio wazi ni kwamba
wabunge wengi hata na Magufuli akiwemo, si wakazi wa
kudumu katika majimbo yao. Ukweli wenyewe ni kwamba
Magufuli, ni mwenyeji wa Dar-es-Salaam, kuliko alivyo
mwenyeji wa Chato. Matatizo ya Chato, hayawezi kumgusa
kama yale ya Dar-es-Salaam. Umeme, ukikatika
Dar-es-Salaam, utamgusa kuliko ukikatika wa chato, Maji
yakikatika ya Dar-es-Salaam, itamgusa kuliko yakikatika
ya Chato, ambayo hata hivyo hayapo! Muhimbili,
madaktari wakigomba, itamgusa kuliko wakigoma wa
Chato, ambao hata hivyo watu wa Chato waliowengi
wanashindwa kuwafikia. Baraba za Dar-es-Salaam zikiwa
na mashimo zitamgusa zaidi kuliko zile za Chato na
Nyamilembe. Kama shule za Dar-es-salaam zitakuwa mbaya
itamgusa sana, maana itamlazimu kuwapeleka watoto wake
nje ya nchi kwa gharama kubwa. Kwa mantiki hii,
Magufuli anaweza kuwa mbunge wa maana zaidi
Dar-es-salaam kuliko Kule Chato anakopita bila
kupingwa, ambako ingawa watu amewapelekea umeme,
hawana uwezo wa kuulipia!
Haya ndio mambo ya kukaa chini na kuyajadili. Kwanini
watu wa mjini watake kuwa wawakilishi wa vijijini?
Kwanini walimu watake kuwa wawakilishi wa madaktari?
Kwanini mkazi wa Mbezi, atake kuwa mwakilishi wa mtu
wa Manzese? Haya ndiyo mambo ya msingi ya kujadiliana
nyakati kama hizi. Ni wakati wa kujiuliza kwamba wale
wanaotaka kuingia Bungeni wanayafahamu matatizo na
matumaini ya watanzania? Wanaifahamu katiba yetu?
Wanafahamu uwakilishi ni nini? Kuingia Bungeni, si
kwenda kuimba au kuonyesha mitindo ya mavazi. Ni
kwenda kuwashirikisha maoni na matakwa ya wananchi.
Ni imani yangu kwamba Mtu kama Waziri Mkuu, ambaye ni
kiongozi wa ngazi ya juu katika taifa letu ndio
angekuwa msitari wa mbele kuongoza majadiliano kama
haya. Majadiliano ya kutaka kulijenga taifa letu.
Lakini anapoacha kujadili haya na kuanza kuwaombea
watu kazi, inasikitisha na kukatisha tamaa.
Ni bora tuwaachie viongozi wanaokuja uhuru wa kufanya
kazi na kuwateua watu watakaowaona wanafaa. Tusianze
mchezo mchafu wa kuwawekea mashinikizo ya
kuwalazimisha kuwachagua watu ambao sisi tunafikiri
wanafaa kwa manufaa yetu binafsi. Waswahili wanasema
Kizuri kinajiuza na kibaya kinajitembeza.
Na,
Padri Privatus Karugendo.
0 comments:
Post a Comment