KANISA SI UPINZANI

MAKALA HII ILITOKA KWENYE GAZETI LA RAI 2005.

KANISA SI UPINZANI!

Ninakubaliana na hoja ya Askofu Kilaini, kwamba kanisa si upinzani. Huu ni ukweli ambao ni vigumu kuupinga, hasa katika nchi yetu ya Tanzania. Inawezekana katika nchi nyingine kanisa likalazimika kuwa upande wa upinzani maana kuichia serikali isiyotenda haki kuendelea kutawala ni dhambi isiyokuwa na msamaha. Kanisa ambalo linafuata mafundisho ya Yesu Kristu wa Nazareti, ni lazima kwa nyakati tofauti lijikute linaunga mkono wapinzani. Ujumbe wa kristu ni wa kutetea wanyonge, maskini, wanaoonewa, na kwa bahati mbaya serikali nyingi si za wanyonge wala masikini. Hata hapa Tanzania imeanza kuwa vigumu kwa mtu masikini kuingia Bungeni au katika uwanja wa kuiongoza nchi. Ukitaka kuwa mbunge ni lazima uwe na pesa, ukitaka kuwa rais wa nchi ni lazima uwe na pesa. Nguvu ya pesa ikizidi na pesa ikawa na dhamani kuliko binadamu, haki haiwezi kutendeka. Na haki ikipotea, ni lazima kanisa lisimame kupinga, kama lisiposimama, linakuwa limeshindwa kazi yake kama linavyoshindwa kule Larin Amerika. Hii ikitokea basi chumvi inakuwa imeishiwa uchumvi wake, linalobaki ni kuitupa njiani ili ikanyagwe na kila mpita njia!

Hali ya siasa inavyoendelea hapa Tanzania, inawezekana siku moja kanisa likawa upande wa upinzani. Itafikia mahali wanyonge hawatakuwa na mtetezi katika Bunge la Tanzania – hali hii ikijitokeza ni lazima kanisa kusimama na kutetea wanyonge, linataka lisitake ni laima lisimame upande wa wapinzani!

Kwa upande wetu hapa Tanzania ni bahati kabisa kwamba kanisa si CUF, si Chadema, si TLP au chama kingine cha upinzani. Ingawa kuna ukweli mwingine kwamba vyama vya upinzani vina wanachama ambao ni waumini wa makanisa mbali mbali hapa nchini. CUF, ina wanachama Wakristu. Mheshimiwa Lwakatare, ni mkristu na anatoka katika familia ya kikristu kweli kweli. Willbrod Slaa wa Chadema ni mkristu na ni mwanateolojia. TLP, Mheshimiwa Mrema ni Mkristu hodari. Kanisa halina chama lakini lina waumini wa vyama mbali mbali. Pamoja na ukweli huu ningependa kumkumbusha Askofu Kilaini, kwamba kanisa si CCM! Na kwamba ipo siku CCM, itakuwa chama cha upinzani! Hivyo haina maana kuonyesha kuunga mkono chama kimoja kwa vile kiko madarakani. La msingi ni kujiwekea mambo ambayo ni ya muhimu na yakuheshimiwa na vyama vyote. Ikiwa ni CCM, ije na sera zake, lakini isiguse mambo ambayo ni moyo wa taifa letu. Ikija CHADEMA, ije na sera zake lakini isiguse mambo ambayo ni moyo wa taifa letu. Ikija CUF, ije na sera zake, lakini isiguse mambo ambayo ni moyo wa taifa letu nk.

Moyo wa Taifa letu ni maslahi yetu. Katika makala iliyopita nilihoji juu ya maslahi ya taifa letu. Bado ninasubiri majibu. Haiwezekani tuwachague viongozi bila kutambua maslahi ya taifa letu. Haiwezekani kuwachagua viongozi bila kuwapima jinsi walivyoyalinda na kuyatetea maslahi yetu siku za nyuma.

Moyo wa taifa letu ni watu wake. Leo hii watu hawa wanashambuliwa na gonjwa hatari la UKIMWI. Wale wanaotaka kuingia kwenye madaraka wamepambana vipi na gonjwa hili?

Moyo wa taifa letu ni utajiri wetu. Hawa wanaotaka kuingia madarakani wameutunza vipi utajiri wetu. Walihakikisha kwamba kila Mtanzania ananufaika na utajiri huu? Je, kama walishindwa kutetea utajiri wa nchi yetu kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita, wataweza kuutetea kwa kipindi cha miaka mitano ijayo?

Moyo wa taifa letu ni uzalendo wa watu wake. Uzalendo huu upo? Watu wanafanya kazi kwa kujituma au wanakula rushwa na kupora mali ya taifa.

Sina hakika kama kuna mtu hapa Tanzania, anayetaka kanisa liwe upinzani au liunge mkono vyama vya upinzani, ingawa kufanya hivyo si dhambi. Hakuna anayetaka Askofu awe CUF, CHADEMA au TLP. Askofu ni kiongozi wa wote, wezi, maskini, matajiri, wadhambi, watakatifu, wanasiasa na wasiokuwa wanasiasa, vijana, wazee na wasiojiweza. Lawama zinazosikika zina hoja za msingi:

Wakati CCM ikijiandaa kufanya mkutano mkuu ili kumpata mgombea urais Kanisa liliandaa sala. Maaskofu, wachungaji na waumini walikusanyika kusali na kuiombea CCM, ili impate mgombea aliye bora. Kwa vile Tanzania ni nchi ya kidemokrasia inayoongozwa kwa mfumo wa vyama vingi tulitegemea sala kama hiyo iendeshwe kuviombea na vyama vingine ili vimchague mgombea aliye bora. Sala hii hadi leo hii hatujaisikia! Hii inaleta picha kwamba kwa upande wa kanisa, mkutano mkuu wa CCM, ndio ulikuwa uchaguzi mkuu wa kumchagua Rais wa Taifa letu. Kwanini basi watu wasianze kuwa na wasiwasi kwamba kanisa ni CCM? Linaunga mkono CCM, Au kwamba kanisa linavipiga vita vyama vya upinzani? Kupinga kitu si lazima kusimama jukwaani na kusema. Hata matendo peke yake yanatoa picha kamili. Kama kanisa haliviombei vyama vya upinzani kwa nini tuamini kwamba linavipenda na kuviunga mkono?

Hoja nyingine ni kwamba Viongozi wa kanisa wanasema kwamba Kikwete, ni chaguo la Mungu. Kwa maneno mengine chaguo la CCM, ni chaguo la Mungu! Hivyo ndivyo walivyoona na inawezekana ni ukweli. Wasi wasi wa vyama vya upinzani na watu walio makini na kulipenda taifa letu, wanauliza kama Kikwete ni chaguo la Mungu, hawa wagombea wengine tisa ni chaguo la nini? Chaguo la shetani? Ukweli ni kwamba wagombea wote ni chaguo la Mungu. Ni imani yangu kwamba hata na Mheshimiwa Kikwete, anafahamu kabisa kwamba wapinzani wake ni chaguo la Mungu. Bila kuwa chaguo la Mungu, ni nani atasimama? Maaskofu hawalijui hili? Nina mashaka!

Askofu, ambaye ni kiongozi wa ngazi ya juu katika kanisa. Askofu anayesimama badala ya Kristu, na maaskofu wengine wanasimama badala ya Mungu, akishatamka kwamba mgombea Fulani ni chaguo la Mungu, waumini wa kweli si watamwamini? Huku si ni kuingilia uhuru wa mtu wa kumchagua kiongozi anayempenda? Kiongozi atakayekuwa amempima kwa vigezo yake, kama vile uzalendo, mchango wake katika kuliendeleza taifa letu, kisomo chake na uelewa wa mambo ya kitaifa na kimataifa. Lakini Askofu, akishatamka kwamba mgombea ni chaguo la Mungu, mjadala unakuwa umefungwa. Wewe utakuwa ni nani kwenda kinyume na matakwa ya Baba Askofu? Kilio cha kila Mtanzania ni kwamba uchaguzi uwe wa huru na haki. Lakini kwa mtindo huu wa shinikizo la viongozi wa kanisa ni vigumu kusema kwamba uchaguzi utakuwa wa huru na wa haki.

Ninafikiri yule atakayefanikiwa kuchaguliwa kuwa rais wa taifa letu, atafurahi na kujivuna kama atakuwa amechaguliwa kwa uchaguzi ulio huru na haki na hii nampatia imani kwamba anakubalika na kupendwa. Akishinda kwa shinikizo itakuwa ni kinyume.

Lakini mbaya zaidi ni hii dhambi ya ubaguzi ya kuwatenga watu katika makundi. Kwamba wapo ambao ni chaguo la Mungu. Dhambi hii ndiyo inayozaa wateule, watakatifu, makabila bora na uchafu mwingine unaoendana na dhambi ya ubaguzi. Dhambi hii ndiyo inayozaa tabia ya kuwatenga watu katika makundi ya sura nzuri na sura mbaya. Watu wanaweza kupigana hadi kupoteza maisha kwa vile kundi moja lina sura nzuri na kundi jingine lina sura mbaya. Maneno haya yamesikika kwamba vyama vingine vimewasimamisha wagombea wenye sura nzuri, wenye mvuto na vyama vingine vimesimamisha wagombea wenye sura mbaya. Utafikiri sura ya mtu ina lolote katika utendaji kazi wake. Hata hivyo sura nzuri na mbaya zinafanana vipi? Ni kigezo kipi kinapelekea mtu kuwa sura nzuri?

Kauli kama hizi za Fulani ni chaguo la Mungu, Fulani ana sura ya mvuto ni lazima zishikiwe bango. Si kauli za kuleta maendeleo katika taifa letu. Ni kauli za kuleta ubaguzi na kuchochea mtengano katika jamii yetu. Ni bora kuwapima watu kwa kutumia vigezo vya utendaji kazi wao kuliko kuwapima watu kwa kufuata sura zao!

CCM, imefanya mambo mengi mazuri, sina haja ya kuyataja maana yanatajwa kila siku. Lakini pia kuna mambo mengine ambayo haikufanya vizuri. Watu wanalalamika jinsi utawala wa CCM ulivyoshindwa kuendesha vizuri zoezi zima la uwekezaji, ubinafsishaji, soko huria na mfumo mzima wa utandawazi. Inawezekana Viongozi wa kanisa hawayaoni haya. Haiwezi kushangaza kwamba hawayaoni maana wanaishi maisha yaliyo tofauti kabisa na wananchi wa kawaida. Hawana shida ya chakula, hawana shida ya makazi, hawana shida ya usafiri hawana shida ya matibabu – sadaka inaendelea kuja, iwe imepatika kwa njia za haki au kinyume chake wenyewe hawana habari.

Inawezekana pia viongozi wa kanisa hawaoni hatari iliyo Zanzibar. Kwa vile hawataki kuwa upande wa wapinzani wanaona hali ni shwari. Wanajifanya kuwa vipofu. Hali hii inaweza kuwa imeficha unafiki mkubwa. Unafiki wa kanisa wa miaka mingi wa kuunga mkono serikali yoyote ile iliyo madarakani. Serikali isiyogusa maslahi ya kanisa!

Kama kanisa linataka kuwa chumvi ya Tanzania, basi lishiriki kikamilifu katika harakati za kuwafundisha watu kutambua maslahi ya nchi yetu. Kanisa litetee uhai wa watanzania. Kanisa liwasaidie watanzania kuwahoji wagombea. Kwa vile kanisa lina mizizi hadi vijijini, liwaandae wananchi kuwachagua wawakilishi. Kanisa lisaidie kuwafundisha wananchi watambue ni nini maana ya mwakilishi. Watambue kwamba mvuvi hawezi kuwa mwakilishi bora wa mkulima na kwamba mtu anayeishi mjini hawezi kuwa mwakilishi mzuri wa mtu wa kijijini.
Jambo linalosikitisha ni kwamba, badala ya kanisa kujadili mambo muhimu kuhusiana na uchaguzi, linajishughulisha na mambo madogo. Mfano badala kukupoteza muda kutangaza kwamba kanisa si upinzani, kanisa lingejadili mbinu za kuwapata viongozi bora watakaoshughulikia mambo ambayo ni changamoto kama UKIMWI. Ugonjwa huu unatishia uhai wa watanzania. Hatuwezi kuongelea kutetea maslahi ya watanzania kabla ya kuongea kulinda uhai wa watanzania. Ni nani kati ya wagombea kumi wa urais analifahamu vizuri na ataweza kulishughulikia vizuri swala la ugonjwa wa UKIMWI. Tunajua wazi jinsi viongozi wa kanisa wamekuwa mstari wa mbele kukwamisha juhudi za kuzuia maambukizo ya virusi vya UKIMWI. Ni mgombea gani hataogopa kuwaelezea maaskofu ukweli juu ya ugonjwa huu. Kama yupo, basi huyo ndio anastahili kuliongoza taifa letu. Bila watu, taifa haliwezi kuwa taifa tena. UKIMWI, anakwenda kasi ukielekea kulifyeka taifa zima. Kupona kwetu ni kuwachagua viongozi wenye upeo na uzalendo.

Na,
Padri Privatus Karugendo.

0 comments:

Post a Comment